Home Makala AU haiko tayari kuumaliza mgogoro wa kisiasa Sudan

AU haiko tayari kuumaliza mgogoro wa kisiasa Sudan

1379
0
SHARE
Sudanese President Omar al-Bashir addresses the parliament about national dialogue talks, on October 19, 2015 in Khartoum. AFP PHOTO/ ASHRAF SHAZLY (Photo credit should read ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images)


NA MOSES NTANDU

Jumuiya za kiuchumi na za kisiasa barani Afrika zikiwemo IGAD na COMESA zikiongozwa na Umoja wa Afrika (AU) zina nafasi kubwa sana kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Sudan.

Wiki iliyopita nilijadili masuala kadhaa kuhusu mgogoro wa Sudan ikiwa ni pamoja na mkakati wa serikali ya nchi hiyo kukabiliana na hali tete ya kisiasa inayoendelea kulikabili taifa hilo.

Katika muendelezo wa mjadala huu leo nitaangazia ukimya unaoendelea kutoka kwa jumuiya za kisiasa na maendeleo barani humu katika kutatua mgogoro huo ambao unaonekana kama mdogo lakini ukiendelea kukomaa kila uchao.

Pamoja na mambo mengine zikiwemo hatua kadhaa ambazo serikali ya nchi hiyo inaendelea kuzichukua ili kuweka mambo sawa bado juhudi hizo pekee hazitoshi ikiwa jumuiya za kiuchumi na kisiasa ambazo taifa hilo la Sudan ni mwanachama zikiendelea kukaa kimya.

Suala kubwa hapa tunaloweza kujiuliza ni nini dhima kubwa ya Jumuiya hizi katika mataifa wanachama katika hali kama hii inayoendelea nchini Sudan? Toka vuguvugu hili la maandamano na kelele za hapa na pale kuanza nchini humo na kusababisha kupotea kwa maisha ya wananchi kadhaa wasio na hatia bado hakuna jumuiya yoyote iliyojitokeza hadharani kusaidia katika kutatua changamoto hiyo ya kiuchumi na kisiasa nchini Sudan.

Umoja wa Afrika (AU) ni jumuiya mama inayopaswa kuwa kinara katika hili si tu kusema jambo lolote bali kuratibu na kuhakikisha kuwa taifa hili linakuwa katika hali ya amani na utulivu. Naamini kuna hatua kadhaa wanazozichukua ili kupata suluhisho la kudumu kwa taifa hilo lakini ukimya katika kutatua mgogoro huo bado ni tatizo pia.

Tunapaswa kuona na kusikia matamko na maonyo kadhaa yakitoka kwa jumuiya hizi ambazo kwa kiwango kikubwa hilo ndio jukumu lao. Sio tu kusubiri mambo yaharibike na kuanza kupeleka vikosi vya majeshi kwenda kutafuta amani wakati sasa kuna uwezekano wa kuidhibiti hali hiyo.

AU inapaswa kujitokeza hadharani na kusema waziwazi na kushirikiana na jumuiya nyingine ikiwemo jumuiya ya soko la pamoja la ukanda wa Afrika Mashariki na Kaskazini (COMESA) pamoja na Mamlaka za pamoja za kiserikali za Maendeleo kwa ukanda wa nchi za pembe ya Afrika (IGAD) kwa pamoja wanalo jukumu kubwa sana katika kutatua mgogoro huu.

Mahusiano ya jumuiya hizi ambazo taifa la Sudan ni mwanachama hayapaswi kuishia katika mashirikiano ya kimaendeleo tu ama pale tatizo kama hili linapokuwa kubwa na tayari likiwa lemeleta madhara makubwa ndipo wajitokeze kutafuta suluhu.

Methali isemayo kuzuia ni bora kuliko kuponya hapa inapaswa kutamalaki katika kutatua mgogoro huu ambao tayari umesha leta madhara kadhaa kwa taifa hilo ambapo vifo kadhaa vimeripotiwa kutokana na mgogoro huu ambapo vifo hivyo vimewakumba raia wasio na hatia na watumishi kadhaa wa serikali ambao wanaonekana kuwa maadui wakubwa wa raia nchini humo.

Jumuiya hizi zina nafasi kubwa hasa ya ushawishi wa kisiasa na hata kiuchumi jambo ambalo ndilo chimbuko kubwa la mgogoro unaoendelea nchini humo. IGAD na COMESA wakishirikiana na Umoja wa Afrika kujitokeza hadharani na kushughulikia mgogoro huu hakika suluhu ya kudumu itapatikana.

Kwa hali ya mambo ilivyo nchini Sudani kwa sasa kunahitajika sana uwepo wa sio tu matamko bali kuwepo kwa mikakati mahsusi na ya moja kwa moja kwa jumuiya hizi kujitokeza kutafuta suluhu kwa taifa hili mwanachama wa jumuiya zote hizo.

Ukimya huu wa jumuiya hizi unaleta maswali mengi yanayozua utata wa nini dhima halisi ya jumuiya hizi kwa mataifa wananchama wake hasa yanapoibuka matatizo kama haya au ndipo msemo ule wa “kufa kufaana” unajidhihirisha hapa?

Wakati huo huo serikali ya taifa hilo wiki iliyopita ikiwa ni muendelezo wa kutafuta suluhu ya mgogoro huo imekuwa ikijaribu kuimarisha uchumi wake kwa kufungua mpaka wake na taifa la Eritrea mpaka uliofungwa takribani mwaka mmoja sasa.

Mpaka huu unaelezwa kwamba kwa muda mrefu umekuwa ukitumika kufanya biashara za magendo ya bidhaa nyingi kutoka nchini Sudan kwenda Eritrea.

Inaelezwa kuwa kwa kufungua mpaka huu walau wananchi wa Sudan waliopo katika maeneo ya Mpaka huo na serikali yao ya Sudan watanufaika kwani kumekuwa kiwango kikuwa cha uhitaji wa bidhaa kutoka nchini Eritrea ambapo kwa takribani mwaka mmoja sasa wamekuwa wakikosa mapato baada ya mpaka huo kufungwa.

Ikiwa kutakuwa na mpango mkakati wa pamoja wa jumuiya za maendeleo za kikanda pamoja na serikali ya Sudan kuwa sikivu na kushirikiana kwa pamoja hakika mgogoro huu unaoendelea katika taifa hili utakuwa ni nhistoria.

Rais wa taifa hilo Omar Hassan Al Bashir akiwa ziarani katika mji wa Kassala uliopo mpakani hapo alisema “Tumeamua kufungua mpaka huu ili kuongeza fursa za kiuchumi ambazo zitatumiwa na wananchi wetu kuboresha maisha yao kwa kufanya biashara huru na sio za magendo kama ilivyokuwa hapo awali”

Utayari wa serikali na jumuiya hizo unahitajika sasa kwa kiwango kikubwa sana ili kulinusuru taifa hilo kuingia katika majanga makubwa kwani bila tahadhari hizo lolote linaweza kujitokeza.

Mwandishi wa Makala haya ni mwandishi na mtafiti kutoka katika Kituo cha Afrika cha Mahusiano ya Kimataifa (ACIA) nchini Tanzania, anapatikana kwa simu namba 0714 840656 pia kwa baruapepe mosesjohn08@yahoo.com

MWISHO