Home Makala Kimataifa Charles Njonjo- waziri katika baraza la kwanza Kenya aliye hai

Charles Njonjo- waziri katika baraza la kwanza Kenya aliye hai

2754
0
SHARE

>>Alipenda kukumbatia mila na desturi za Wazungu na kudharau Waafrika

HILAL K SUED NA MITANDAO

Wakati Kenya imeadhimisha (Desemba 12) miaka 55 tangu ipate uhuru wake, bado yupo hai Mjumbe mmoja wa Baraza la kwanza kabisa la mawaziri – Charles Mugane Njonjo – au “Sir Charles” – jina alilopachikwa kutokana na tabia yake ya kupenda kutukuza sana, na yeye kuzifuata mila za Wazungu, hususan Waingereza – kama vile kuvaa suti za mistari mistari miembamba (pin-striped suits) wanazopenda kuvaa Waingereza mashuhuri.

Njonjo alizaliwa mwaka 1920 wakati nchi ya Kenya ndiyo inabadilishwa na kuwa koloni la Uingereza, na baba yake, Chief Josiah Njonjo, alikuwa mshiriki mkubwa wa wakoloni wa Kiingereza. Charles Nonjo umri wa miaka 98 saSA HIVI na anaishi mji wa Kabete kaskazini mwa Nairobi – hivyo kupachikwa cheo cha “Duke of Kabeteshire.” “Duke” ni cheo cha watawala wa maeneo ya Uingereza yanayoitwa ‘Shire’ – kama vile Cheshire, Hampshire, Wiltshire nk.

Inadaiwa alikuwa anawaona Waafrika kuwa ni watu ambao hawajui, au wasioweza kitu chochote ukilinganisha na Wazungu. Kuna stori moja (isiyothibitishwa rasmi) kuhusu yeye kwamba alikuwa hapandi ndege yoyote ambayo rubani wake ni Mwafrika – lazima rubani awe Mzungu.

Inaelezwa siku moja alikuwa anasafiri kutoka London kuja Nairobi na wakati yupo uwanja wa ndege wa London Heathrow aliuliza nani rubani wa ndege yake. Wahudumu wa pale walimjibu kuwa ni “Captain Rogers” – akachekelea kwa furaha.

Ndege ilipofika uwanja wa Nairobi na abiria kuanza kutoka kwenye ndege mlangoni alikuwapo kasimama Mwafrika mmoja kavaa nguo za ki-rubani na kujitambulisha kwamba yeye ndiyo “Captain Rogers” na kumpa mkono kila abiria aliyetoka akiwaambia bila shaka walifurahia safari yake.

Njonjo (ambaye hana facebook account) aliteuliwa katika Baraza kwanza kabisa la mawaziri mwaka 1963 kama Mwanasheria Mkuu, na ni miongoni mwa watu walioshika wadhifa huo kwa kipindi kirefu zaidi na pia alikuwa mwenye mamlaka makubwa.

Wakati anateuliwa katika wadhifa huo, alikuwa ni miongoni mwa Waafrika wachache sana waliokuwa wanamiliki magari – alikuwa anaendesha gari lake mwenyewe kutoka Kabete hadi ofisini kwake Nairobi kila siku.

Aidha inadaiwa wakati wa chakula cha mchana, ilikuwa kawaida yake kutembea bila viatu katika Ikulu ya rais Jomo Kenyatta huku akipiga champagne.

Mwanasiasa mwingine wa zamani wa Kenya aliye bado hai ni Daniel arap Moi – rais wa pili wa Kenya ingawa yeye hakuwamo katika Baraza la kwanza la mawaziri.

Kama vile kwa watu wa ukoo wa Moi, watu wa ukoo wa Njonjo wameishi umri mrefu. Baba yake Chief Josiah Njonjo alikuwa hai akiwa na umri wa miaka 86 wakati Tume ya Uchunguzi iliyoundwa mwaka 1984 kuchunguza uhusika wake katika jaribio la kupinduliwa rais Moi mwaka 1982. Wakati wa uchunguzi huo Njonjo alikuwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba na Mbunge wa Jimbo la Kikuyu.

Dada zake Njonjo pia wamefaidi umri mkubwa wakati yeye mwenyewe bado anaonekana akisafiri kuja Nairobi karibu kila siku kuangalia biashara zake za kifamilia ambazo zimeenea katika mabenki, bima, usafiri wa anga, huduma za afya, ufugaji, kilimo, ununuzi na uuzaji majumba na biashara za ununuzi na uuzaji wa hisa katika masoko ya hisa. Ni miongoni mwa mabilionea wa kutupa nchini Kenya.

Nini siri ya umri wake mkubwa? Inadaiwa ni katika lishe. Watu wake wa karibu wanasema chakula chake cha asubuhi ni kikombe kimoja cha chai na vipande viwili vya mkate. Chakula cha mchana na jioni ni matunda na mboga kwa wingi. Iwapo utamualika kwenye nyama choma, basi ujue utazila mwenyewe.

Tangu aondoke serikalini baada ya Tume ya Uchunguzi dhidi yake ya mwaka 1984 alijiteremsha chini hadi pale rais Moi alipomteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma ya Idara ya Wanyamapori.

Lakini katika kipindi cha urais wa Jomo Kenyatta, Njonjo alikuwa mtu mwenye mamlaka makubwa sana katika serikali na agizo lake lilikuwa sheria. Idara ya upelelezi – CID – ilikuwa ni sehemu ya ofisi yake ya Mwanasheria Mkuu hivyo aliweza kuanzisha uchunguzi dhidi ya mtu yoyote yule. Tofauti na sasa, wakati ule CID walikuwa na mamlaka ya kumtia mtu mbaroni hata kumuua mtu kwa risasi.

Kwa kutumia kalamu yake tu, Njonjo aliweza kuifuta kampuni yoyote na kuwafukuza kutoka nchini raia wa nje. Aidha alikuwa anatia saini hati za kumuweka mtu kizuizini nyumbani kwake au pia kuwaachia wafungwa.

Mamlaka haya makubwa yalimfanya kuwa na maadui wengi – hususan miongoni mwa viongozi wenzake serikalini, isipokuwa watu kama Makamu wa Rais Moi, Waziri wa Fedha Mwai Kibaki, Waziri Msaidizi G.G. Kariuki, Mkuu wa Utumishi wa Umma (Civil Service) Jeremiah Kiereini, Waziri wa Kilimo Bruce McKenzie na mkuu wa Usalama (Itelligence) James Kanyotu.

Hata hivyo mara nyingine mamlaka haya makubwa yalileta matokeo tofauti. Rais Kenyatta alipofariki Agosti 22 1978, Njonjo, akiwa kama Mwanasheria Mkuu alizuia jaribio la kundi lililoitwa “Mt Kenya Mafia” waliodhamiria kubadilisha katiba ili kumzuia Makamu wa Rais Daniel arap Moi kuwa rais.

Hatua hii iliokoa uongozi wa Moi ambayo pia ilimhakikishia Njonjo kufaidi madaraka makubwa hadi mara nyingine kumfanya awabwatukie wanadiplomasia kwamba “hii ni serikali yangu…”

Hata hivyo watu hawa wawili (Moi na Njonjo) walikuja kukosana miaka mitatu baadaye wakati Njonjo akiwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba alipotupwa moja kwa moja katika pipa la taka la kisiasa baada ya kutuhumiwa kuhusika katika jaribio la kumpindua Moi mwaka 1982 lililofanywa na askari wa kikosi cha anga. Alizikana tuhuma hizo na Rais Moi alimsamehe kabla hata Tume ile ya uchunguzi kumaliza kazi yake.

Kuanguka kisiasa kwa Njonjo kwa kiwango fulani kilisababishwa na mwanasiasa mwingine mashuhuri aliyekuwa anaibukia, Nicolas Biwott aliyefariki Julai mwaka jana.

Njonjo, pamoja na kusifiwa kuiokoa Kenya kutoka mgogoro mkubwa wakisiasa alipozuia ubadilishaji wa katiba ili Moi asipate urais, pia analaumiwa kwa vitendo vyake vingine hasi kwa muonekano wa nchi yake lkakini hasa kwa nchi za nje.

Anadaiwa kuukumbatia utawala wa Wazungu wachache wa Afrika ya Kusini (apartheid), utawala wa Wazungu wa Rhodesia na wakoloni wa Msumbiji na Angola wakati nchi zingine za Afrika zilikuwa katika jitihada za kuzikomboa kutoka tawala hizo. Kuhusu uhusiano na Makaburu, uhusiano wa Kenya na Afrika ya Kusini huru umekuwa unalegalega hadi leo.

Njonjo pia anatajwa kuhusika katika kuchochea kuvunjika kwa jumuiya ya kwanza ya Afrika ya Mashariki mwaka 1977. Ilidaiwa kwamba wakati ilipotangazwa kwamba Jumuiya hiyo imevunjika rasmi, Njonjo alifanya sherehe kubwa nyumbani kwake wakila na kunywa usiku kucha.

Katikati ya miaka ya 70, katika kipindi ambacho uhusiano baina ya Kenya na Uganda haukuwa mzuri, Njonjo alihusika katika mazungumzo ya siri na serikali ya Israel, mazungumzo ambayo inadaiwa ndiyo yalifanikisha ile Operation Entebbe – uvamizi wa vikosi vya Israel wa ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa (Air France) iliyokuwa na abiria 248 ambayo ilikuwa imetekwa na wapiganaji wa Kipalestina na kupelekwa uwanja wa ndege wa Entebbe, Uganda, wakati wa utawala wa Idi Amin.

Serikali ya Kenya iliruhusu uwanja wake wa Nairobi kutumika na vikosi vya uokoaji wa Israel kama kituo cha kutokea katika kuwavamia wapiganaji hao wa Kipalestina na kuokoa abiria wote waliokuwa wanashikiliwa kama mateka.

Kuhusika kwa Njonjo katika kufanikisha Operation hiyo baadaye kulithibitishwa na Njonjo mwenyewe katika mahojiano na mwanahistoria Sail David alipokuwa katika matayarisho ya kitabu chake “Operation Entebbe” kilichotoka 2015