Home Makala DRC inaangamia mikononi mwa mawakala wa ubeberu

DRC inaangamia mikononi mwa mawakala wa ubeberu

2116
0
SHARE


JOSEPH MIHANGWA

JAMHURI ya Watu wa Kongo (DRC) ni nchi yenye historia ya mitafaruku ya kisiasa, kiuchumi, ubeberu na usaliti wa watawala unaochafua amani ya nchi na kimataifa.  Ilianza na Mfalme Leopold wa Ubelgiji kati ya mwaka 1877 – 83 alipotuma wapelelezi kuchunguza utajiri wa nchi, na baada ya kuridhika na kilichomo, mwaka 1883 alijitangazia kunyakua nchi hiyo kama Koloni huru kwa jina la “Congo Free State” (Nchi huru ya Kongo).

Hatua hiyo ya Mfalme Leopold ilichochea mashindano kwa nchi zingine za Ulaya kujitangazia Makoloni Barani Afrika na kuzua kile kilichoitwa “Kinyang’anyiro cha kunyakua makoloni Afrika” (Scramble For Africa) nusura ziingie vitani kugombea Makoloni. Ndipo mwaka 1884/85 zilipokaa mezani mjini Berlin, Ujerumani kuelewana misingi na namna ya kuigawana Afrika (Portion of Africa) kama kipande cha mkate huku Mfalme Leopold alikwishaweka kwapani Kongo.

DRC ilipata uhuru wake kutoka Ubelgiji Juni 30, 1960 chini ya Waziri Mkuu Mzalendo, Patrice Emery Lumumba ambaye mwaka 1961 alipinduliwa na Kanali Joseph Desire Mobutu kwa msaada wa Ubelgiji na Marekani (CIA) zilizotaka kuendelea kudhibiti na kupora utajiri wa nchi hiyo kwa mwavuli wa Ukoloni mamboleo chini ya ubeberu wa kimataifa, Mobutu akiwa kama Mkuu wa Serikali, na Rais wa kupachikwa asiye Mtendaji, Joseph Kasavubu, wakiwa mawakala wa ubeberu huo. Lumumba aliuawa kwa amri ya Ubelgiji na Marekani Januari 17, 1961 wakimwita “Mbwa kichaa, wakala wa Ukomunisti asiyestahili kuishi”.

Kuanzia hapo, DRC imekuwa kitovu cha vita baridi barani Afrika kati ya nchi za ubeberu wa Kimagharibi zikiongozwa na Marekani na nchi za Kisoshalisti za Mashariki zikiongozwa na Urusi huku mzimu wa Lumumba ukizidi kuitafuna.

Kwa kipindi chote hadi alipochukua madaraka mpiganaji nguli wa vita vya Msituni, Laurenti Desire Kabila, Mobutu aliitawala DRC kama wakala wa Marekani kulinda maslahi ya Taifa hilo lenye nguvu za kijeshi na kiuchumi duniani, lenye kufukarisha nchi changa kwa njia ya uporaji wa rasilimali na kwa ubabe wa kivita.

Mobutu baada ya kuchokwa na Marekani kwa udikteta uliopitiliza na kuchoka kwa mwili na akili, mwaka 1997 taifa hilo la kibeberu liliwatumia Viongozi wababe wa vita ukanda wa Maziwa Makuu, Majenerali Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, kupandikiza maasi nchini, kumpindua Mobutu na kupandikiza mtu wao, Laurent Desire Kabila kutawala nchi kwa maslahi yao nay a ubeberu wa Kimarekani.

Vivyo hivyo, Laurent Kabila alipositukia ubabe wa Kagame na Museveni uliobana uhuru wake wa kujiamlia mambo ya nchi na kuanza kuchukua hatua dhidi ya ubabe huo, aliuawa hima kwa usaliti wa ndani na nafasi yake kuchukuliwa na pandikizi lingine la Kagame na Museveni  la Kinyarwanda na mpwa wa Kagame, Hypollite Kanembe ambaye pia ni mtoto wa kufikia wa Kabila kwa mke wa kurithi wa marehemu Christopher Kanembe [Mnyarwanda] mwaka 1977 mama Marcelline Mukambukye; hivi kwamba, Hypollite, kwa msaada wa Mjomba wake na mteule wa Kagame katika mapambano dhidi ya utawala wa Mobutu nchini Kongo, Kanali James Kabarebe, aliweza kuingizwa Jeshini kwa mafunzo kupambana na Majeshi ya Mobutu na washirika wake.

Kwa shinikizo la Kagame, Kabarebe ndiye aliyekuja kuwa Mkuu wa Majeshi ya DRC ya Laurent Kabila kwa cheo cha Jenerali; na akawezesha pia kupandishwa cheo mpwa wake Hypollite Kanembe, kuwa Meja Jenerali na Mkuu wa Jeshi la Ardhini na Usalama Jeshini na alianza kufahamika kwa jina la Joseph Kabila kufuatia kifo cha Laurent Kabila kwa maandalizi ya kuchukua mamlaka ya nchi Januari, 2001.

Kama Mobutu alikuwa Wakala wa ubeberu wa Kimarekani, na Laurent Kabila aliyemwondoa madarakani Mobutu alikuwa pandikizi na wakala wa wababe wa vita Kagame na Museveni; vile vile, kama Hypollite Kanembe aliyejulikana baadaye kama Joseph Kabila na kuitawala DRC kuanzia mwaka 2001 – 2019 kufuatia kifo cha Laurent Kabila, alikuwa pandikizi la Kagame na Museveni; basi, hapana shaka kwamba Laurent Kabila na Joseph Kabila walikuwa mawakala wa ubeberu wa Kagame na Museveni nchini Kongo, sawa tu na Mobutu alivyokuwa wakala wa ubeberu wa Kimarekani nchini humo kwa zaidi ya miongo mitatu. Je, Rais mteule mpya, Felix Tshisekedi, aliyeapishwa kushika madaraka Januari 24, ni wakala wa nani?.

Tunaelezwa, Rais aliyeondoka madarakani, Joseph Kabila, alipendelea kuona rafiki yake wa Chama chake, Emmanuel Shadari akirithi nafasi yake lakini umma wa Kikongo ukakataa kwa kumnyima kura kwa mshangao wa Kabila dakika za mwisho. Kisha, haraka haraka, akamshika mkono Felix Tshisekedi ambaye hakupewa nafasi sana zaidi ya Martin Fayulu ambaye umma wa Kikongo unaamini ndiye alikuwa mshindi, lakini akashindwa kimiujiza, hatua inayozua mtafaruku wa kisiasa nchini humo hadi sasa. je, kuna matumaini yoyote kwa amani kurejea Kongo baada ya miaka 58 ya machafuko tangu kifo cha Patrice Lumumba?. Kuna ishara zipi kuonesha hivyo?.

Hebu tuangalie kwa kifupi jinsi uwakala wa Mobutu wa Marekani na Ubelgiji ulivyoua demokrasia nchini na jinsi pia ubeberu mpya wa wababe wa vita, Kagame na Museveni, ulivyochafua amani DRC kuwawezesha kupandikiza wateule wao, na kama Felix Tshisekedi ni Rais huru kuweza kurejesha amani DRC. Tutakayoona yatatufikirisha pia namna Kiongozi wa Kiafrika anavyoweza kuingia madarakani kwa kauli mbiu ya kuvutia, na muda si mrefu kugeuka kuwa Mwanasiasa mnyama wa kutupa na adui wa demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria kwa kilio cha kwikwi na kusaga meno.

Aliponyakua madaraka ya Urais kutoka kwa Rais Joseph Kasavubu mwaka 1965 na kuwa Rais Mtendaji, Jenerali Mobutu alitoa sababu za kufanya hivyo: kwamba, “Wanasiasa wameiteketeza nchi kiuchumi na kijamii kwa uchu wa kujaza mifuko na matumbo yao, na hivyo kuiweka rehani kwa ubeberu wa kimataifa”. Siku hiyo, Mawaziri wanne wa Serikali iliyopinduliwa walihukumiwa kifo na Mahakama ya kijeshi, na siku mbili baadaye walinyongwa mbele ya umati wa watu 50,000. Huu ulikuwa ukatili wa pili wa aina yake uliofanywa na Mobutu, kufuatia ule wa kuuawa kikatili kwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo, Patrice Emery Lumumba mwaka 1961 na Shirika la Kijasusi la Marekani [CIA], wakati huo Mobutu akiwa Mkuu wa Jeshi na Kiongozi wa Serikali ya kimajimbo na Kasavubu akiwa Rais asiye na mamlaka kwa shinikizo la Ubeogiji na Marekani.

Mobutu alikuwa wakala wa Shirika la Kijasusi la Marekani – CIA nchini Kongo ambapo lilimgharamia mafunzo ya Uandishi wa Habari kumwezesha kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, na alibakia hivyo hata baada ya kujiteua Rais mwaka 1965.