Home Afrika Mashariki Hatua za haraka zichukuliwe kuiokoa EAC

Hatua za haraka zichukuliwe kuiokoa EAC

4158
0
SHARE

Rais Pierre Nkurunzia wa Burundi.

HILAL K SUED

Mapema mwa miaka ya mwanzo ya Milenia hii aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) Amanya Mushegga wa kutoka Uganda aliwahi kusema kwamba iwapo Burundi na Rwanda zingekuwa zimeruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ile ya zamani na kwamba Jumuiya hiyo isingeachiwa kuvunjika mwaka 1977, matatizo ya kikabila yasingeweza kujitokeza katika nchi hizi mbili na kwamba hata mauaji ya kimbari ya Rwanda kamwe yasingetokea mwaka 1994.

Lakini kauli hiyo ilikuwa ni ya kufikirika tu kwani mwaka 2007 Rwanda na Burundi zilijiunga na Jumuiya (ya sasa) lakini bado hii haijasaidia kutuliza migongano ya kikabila na ya kisiasa ndani ya nchi hizo, hususan Burundi.

Na sasa hivi badala ya kujiunga katika Jumuiya kwa nchi hizo mbili ili kutatua migogoro yao ya kikabila na mingineyo, Burundi ndiyo inatajwa sana kuwa huenda ikawawa ndiyo kichocheo, au tuseme chanzo cha kuvunjika kwa Jumuiya hii ya pili ya nchi hizi za ukanda wa mashariki mwa Bara la Afrika, baada ya ile ya kwanza kuvunjika miaka 41 iliyopita. Bila shaka sasa hivi Mushegga anaweza kutoa neno kuhusu kauli yake ile ya mwaka 2002.

Tatizo safari hii lilianzia mwaka 2015 pale Rais Pierre Nkurunziza alipochaguliwa kuongoza muhula wa tatu wa urais, muhula ambalo ulileta utata mkubwa kuhusu uhalali wake na hivyo kuibua ghasia kubwa yakiwemo maandamano na jaribio la kutaka kupinduliwa na jeshi wakati akiwa mkutanoni nchini Tanzania.

Hali hii tete ya Burundi iliivuta ndani nchi ya Rwanda, nchi ambayo Rais wake Paul Kagame ndiye alibebeshwa lawama la jaribio hilo la mapinduzi na hivyo kuzorotesha mahusiano baina ya nchi hizo mbili ambazo zilikuwa zinatawaliwa kama nchi moja na Ubeligiji kabla ya kuzipa uhuru mapema miaka ya 60.

Hali hii pia ilisababisha kuahirisha, mapema mwezi huu, kwa mkutano wa 20 wa Viongozi Wakuu wa nchi za Jumuiya mjini Arusha, huku Burundi haikuhudhuria kabisa. Hata huo mkutano uliosogezwa ili ufanyike Desemba 27, nao pia umefutwa.

Katika hali hii ni vyema ifahamike Mkataba uliounda Jumuiya hiyo na vipengele vyake kabla ya kuanza kufikiria uvunjikaji wake. Mkataba huo uliotiwa saini mwaka 1999 unelezea waziwazi vyombo vikuu vinayounda Jumuiya hiyo na majukumu yake.

Mkutano wa viongozi wakuu (EAC Summit) ndiyo chombo cha juu kabisa, na ndiyo dereva wa injini ya Ushirikiano wa nchi hizi (East African Integration) na hatimaye kuuundwa Shirikisho la Kisiasa (Political Federation). Chombo hiki husaidiwa na Baraza la Mawaziri (Council of Ministers).

Wajumbe wa viongozi wakuu (EAC Summit) huchagua, miomgoni mwao, mwenyekiti wake, (sasa hivi ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda) ambaye hushika wadhifa kwa kipindi cha mwaka mmoja na huzunguka kwa zamu.

Mkutano wa viongozi wakuu hufanyika angalau mara moja kila mwaka, na maamuzi yake hutokana na maelewano, isipokuwa tu labda itokee kwamba kuna nchi mwanachama inayofikiriwa kusimamishwa uanachama au kufukuzwa.

Kila nchi mwanachama inatakiwa itume mkuu wake wa nchi kwenye mkutano wa viongozi wakuu (EAC Summit), au mwakilishi mwingine yeyote ili shughuli za mkutano huo ziweze kufanyika. Burundi inalifahama vyema hili, na ndivyo zilivyofanya Rwanda na Sudan ya Kusini kwa mkutano ule uliofutwa. Nchi hizi zilikuwa zimetuma mawaziri kama wawakilishi wa marais wao. Burundi haikutuma mwakilishi yeyote.

Mzozo huu hauna afya kabisa kwani Mkataba wa Jumuiya umeweka wazi mfumo kwa nchi wanachama kusuluhisha migogoro miongoni mwao. Kwanza ni mgogoro baina ya Burundi na Rwanda, kwani hili ni siala la ndani linalohusu uhai wa Jumuiya.

Pili ni kwamba Mkataba wa Jumuiya hauzifungi moja kwa moja nchi zilizo huru. Matakwa ya sheria za kimataifa huibuka baada ya kuridhia kwa nchi husika ambayo inatakiwa ieleze waziwazi kwamba inafungamana na sheria hizo.

Mkataba wa Jumuiya unaruhusu nchi mwanachama kujitoa kutoka Jumuiya hiyo iwapo Bunge lake litaridhia hivyo kutokana na kukubaliwa kwa theluthi mbili ya Wabunge wote wanaostahili kupiga kura, na baadaye hati ya kimaandishi ya azma ya kujitoa ipelekwe kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya.

Tatu Mkutano wa Viongoziu wakuu (EAC Summit) una uwezo wa kuisimamisha nchi mwanachama kwa kushindwa kwake kufuata masuala ya kimisingi ya Jumuiya, pamoja na kushindwa kutimiza wajibu wake wa michango kwa Jumuiya kwa kipindi cha miezi 18.

Nne, Mkutano Mkuu una uwezo wa kuifukuza nchi mwanachama kutokana na kukiuka kwa mara kwa mara kwa malengo na misingi mikuu ya Mkataba wa Jumuiya baada ya kuipa notisi ya miezi 12.

Wadadisi wa mambo wanaona kwamba ni vyema kwa viongozi wakuu wa nchi za Jumuiya wakalishughulikia suala hili ili kuiokoa Jumuiya kutokana na mgogoro ambao unaanza kuonyesha sura mbaya.

Ni muhimu kwa Mwenyekiti wa sasa wa Viongozi hao wakuu – Rais wa Uganda Yoweri Museveni – kutumia uzoefu wake ili kuziweka kwenye mstari nchi za Burundi na Rwanda,  kwani yeye pia ndiye alihusika sana katika kuzifungulia njia nchi hizo kujiunga katika Jumuiya.

Kimtazamo, Jumuiya hii ni muungano wa watu, hivyo si vyema ukaharibiwa kutokana na tofauti zinazojitokeza miongoni mwa Viongozi wa Mkutano Mkuu (EAC Summit). Wananchi wa nchi hizi wana haki ya kufaidi matunda ya Jumuiya kutokana na ushirikiano wao kibiashara na kijamii.

Vinginevyo Jumuiya hii ya sasa nayo inaweza kwenda na maji kama ilivyokuwa ile ya awali miaka 41 iliyopita, na ambayo ilivunjika kutokana na sababu hizi hizi, mtatizo yaliyotokana na tofauti miongoni mwa viongozi wakje wakuu, na si wananchi.

Na hakuna haja ya kusema hapa Jumuiya hii ya sasa haifikii hata robo moja ya ile ya awali katika masuala ya ushirikiano. Mbali na kuendesha kipamoja mashirika ya kutoa huduma kama vile usafiri wa reli, ndege, shughuli za posta na simu na uendeshaji wa bandari, pia kulikuwapo mahakama moja ya rufaa kwa nchi zote tatu – Court of Appeal for East Africa – na uendeshaji wa kipamoja taasisi kadha nyingine kama vile za utafiti wa malaria, uvuvi na uthibiti wa wadudu waharibifu wa mimea.

Ilikuwa ni kazi ngumu kuvunja jumuiya yenye mshikamano kama ule, lakini siku zote wanasiasa si watu wa kuchezea hata kidogo. Matarajio ya wengi yalikuwa ni kwa Jumuiya hiyo kukua, siyo kufa. Lakini ilikufa!