Home Michezo Kimataifa Hii hapa ‘top four’ EPL 2018-19

Hii hapa ‘top four’ EPL 2018-19

2301
0
SHARE
LONDON, ENGLAND - APRIL 14: manager Pep Guardiola of Manchester City reaction during the Premier League match between Crystal Palace and Manchester City at Selhurst Park on April 14, 2019 in London, United Kingdom. (Photo by Sebastian Frej/MB Media/Getty Images)

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

KILA timu imebakiza mechi mbili tu kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya England na ukiacha vita ya ubingwa, uhondo mwingine ni kuziwania nafasi nne za juu ‘top four’, ambapo Tottenham, Chelsea, Arsenala na Manchester United zinatoana jasho.

Tottenham wanaoshika nafasi ya tatu, nyuma ya Liverpool na Manchester City, wana pointi 70, wakiwa wameiacha mbili Chelsea iliyokaa nyuma yao. Arsenal ni wa tano kwa sasa lakini wakiwa na pointi zao 66, moja pungufu ya walizonazo Mashetani Wekundu.

Wakati msimu huu ukielekea ukingoni, Man City na Liverpool zimeonekana kuwa kwenye kasi ya ajabu, zikiwa zimeshinda mechi zote tano zilizopita. Katika idadi hiyo, Chelsea wameshinda mbili, wakati Arsenal na Man United kila moja imeambulia ushindi wa mchezo mmoja.

City, Liverpool nani bingwa?

Liverpool wako nyuma kwa pointi moja dhidi ya Man City. Vijana wa Pep Guardiola watakuwa nyumbani kuwakabili Leicester City na wiki moja baadaye watafunga safari kuwafuata ‘wabishi’ Brighton.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Leicester, ambao Man City walikuwa ugenini, mbele ya mashabiki 32,312 wanaoujaza Uwanja wa King Power, waliambulia kichapo cha mabao 2-1.

Brighton hawakuweza kuizua Man City mzunguko wa kwanza kwani walikwenda Etihad na kuondoka na kichapo cha bao 2-0, wafungaji wa siku hiyo wakiwa ni Raheem Sterling na Sergio Aguero.

Liverpool wao watakuwa ugenini mwishoni mwa wiki hii kucheza na Newcastle, timu ambayo waliitandika mabao 4-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza. ‘Majogoo’ hao wa Anfield watafunga pazia la Ligi Kuu England msimu huu kwa kukwaruzana na Wolves, ikikumbuka kuwa mchezo wa kwanza Jurgen Klopp na vijana wake walishinda mabao 2-0.

Hivyo basi, kuna uwezekano mkubwa wa bingwa wa msimu huu kuamuliwa na mechi za mwisho, Mei 12, siku ambayo Man City na Liverpool zitakuwa viwanjani kusaka pointi tatu mbele ya Brighton na Wolves.

Vita ‘top four’ itakwishaje?

Tottenham walishindwa kujihakikishia nafasi ya tatu baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa West Ham mwishoni mwa wiki iliyopita, kikiwa ni kichapo chao cha kwanza tangu walipoanza kuutumia uwanja wao wa nyumbani.

Hivi sasa, ni pointi mbili tu zinazowatofautisha na Chelsea inayoshika nafasi ya nne, hivyo pengo lingefikia tano endapo tu wangeifunga West Ham, hasa baada ya Blues kudondosha pointi mbili mbele ya Mashetani Wekundu katika mchezo mwingine uliochezwa katika Uwanja wa Old Trafford.

Arsenal wao, licha ya kuwa nafasi ya tano, wakiwa wamepoteza mechi nne kati ya tano walizoshuka dimbani katika siku za hivi karibuni, bado wana nafasi top four kwani wanahitaji pointi nne tu kuwafikia Tottenham wanaoikamilisha ‘top three’.

Ni kweli vijana wa Unai Emery wamepoteza hali ya kujiamini baada ya kutandikwa mabao 3-2 na Crystal Palace lakini ushindi dhidi ya Brighton katika mchezo ujao pale Emirates unaweza kuwaingiza top four.

Man United wakiwa nafasi yao ya sita, ni pointi tatu wanahitaji kuwafikia Chelsea wanaoikamilisha orodha ya timu nne za juu, hivyo lazima wazifunge Huddersfield na Everton ili kuyaweka hai matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Ratiba ikoje?

Kwa mujibu wa ratiba ya mechi mbili kwa kila timu, Tottenham imebakiza Bournemouth (ugenini) na Everton (nyumbani), wakati Chelsea inayowapumulia ina Watford (nyumbani) na Leicester (ugenini). Huku Arsenal ikikabiliwa na Brighton (ugenini) na Burnley (ugenini), Man United itakumbana na Huddesrfield (ugenini) na Cardiff City (nyumbani).