Home Tukumbushane Kukosekana kwa adhabu kali hakutamaliza ufisadi

Kukosekana kwa adhabu kali hakutamaliza ufisadi

2327
0
SHARE


HILAL K SUED

Nimejaribu sana kutafuta tafsiri sahihi kwa Kiswahili ya neno la Kiingereza “deterrence” – kwa neno moja lakini sikufanikiwa.

Tafsiri ya karibu niliyoipata ni “kuzuia makosa yasitendeke (au yasirudiwe), ingawa pia kuna neno “ukali” lakini hili zaidi ni kwa matumizi ya kijumla tu.

Mtunzi vitabu na mcheza sinema wa Marekani mapema karne iliyopita aliwahi kutoa nukuu moja kuhusu neno hili:

“Kuzuia makosa yasitendeke ni namna ya kusimika woga kwa mtu yoyote anayetaka kutenda jinai ili asiitende jinai hiyo.”

Na wanazuoni katika fani za jinai na adhabu wanasema hakuna adhabu yenye nguvu kamilifu ya kuzuia makosa yasitendeke kwa lengo kwamba yasitendeke. Lakini pia wanasema, ni vyema kuwepo kwa hii “deterrence” kuliko kutokuwepo kwake – yaani fikiria jamii isiyokuwa na kanuni za adhabu kwa wakosaji..

Lakini pia suala zima hili linazungukia suala jingine la utoaji au uwepo wa haki ambao msisitizo wake uko katika maeneo mawili: kuitoa kwa hiari (distribution) au kuitoa kama malipo na/au kisasi kwa mabaya mtu aliyotenda (reattribution).                            

Eneo hili la pili ndilo linahusisha utoaji wa adhabu kwa lengo la kutoa tahadhari kwa wengine au kuwaridhisha wengine ambao waliathirika au wanaofuata sheria. Lakini yote mawili haya, pamoja na kuwepo au kutokuwepo kwa uhuru wa mahakama huliweka suala zima la ‘haki’ kutizamwa kwa karibu sana na jamii.

Wiki iliyopita gumzo kubwa liliibuka katika vyombo vya habari na katika mitandao ya jamii kuhusu suala ambalo limekuwa kama fasheni kuanzia miaka ya karibuni – la maafikiano baina ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na baadhi ya washtakiwa wanaokabiliwa na kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kukubaliana malipo ya mabilioni kama faini na hatimaye kuachiwa huru – bila ya kupitia mchakato wa sheria unaosimamia utoaji haki.

Akichangia mjadala Bungeni wiki iliyopita wa hotuba ya bajeti ya Tamisemi na Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Umma na Utawala Bora), Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema DPP hukubaliana na baadhi ya washtakiwa ambao ama hulipa faini, kupunguziwa adhabu au kufutiwa mashtaka. Alihoji DPP anafanya hivyo kwa sheria ipi na fedha hizo zinakwenda wapi.

Pia alihoji kuwapo alichodai utamaduni wa ofisi ya mwendesha mashtaka kukamata watu, ambao alidai haijulikani iwapo ni kutokana na jinai halisi au za kubambikizwa, lakini baadaye, Zitto alidai – watu wale wanakubaliana na ofisi ya DPP na kulipa pesa na kesi hiyo inakwisha.

Naye Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa kambi Rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akichangia hoja hiyo hiyo alidai kwa sasa inaonekana kama kesi za utakatishaji fedha ni mkakati mpya wa kukuza mapato ya Serikali.

Hoja yangu kuu katika makala hii siyo suala la mapato kwa serikali, bali linajikita zaidi katika suala zima la utoaji haki. Kama hayo yanayodaiwa kufanywa na DPP hayapo kisheria basi kuna hatari kubwa ya wananchi kuonewa na kujikuta wakinung’unika kimya kimya. Na hakuna haja ya kusema hapa kwamba utaratibu huu unaathiri vita dhidi ya ufisadi kwani “maafikiano” na DPP siyo njia ya haki ya utoaji adhabu – ingawa unaweza kuwa unatumika nchi nyingine kama vile Marekani. Lakini iwapo ni muhimu, basi uwepo kisheria.

Halafu isitoshe utaratibu wa aina hii unaondoa ile dhana nzima ya “deterrence” niliyozungumzia hapo juu – kwamba kuna wengine wanaweza kujiingiza katika jinai kubwa kubwa kwa kujua kwamba kamwe hataenda jela (kitu kinachohofiwa na watenda jinai wengi) – si ataingia tu “maafikiano” na DPP? Atalipa baadhi tu ya pesa kutokana na zile alizoiba/alizofisidi basi mambo yanaisha.  

Halafu isitoshe, kwa kuwa uwepo wa “utaratibu” wa namna hii haupo wazi kwa kila mwananchi kuufahamu, basi wapo baadhi ambao walitenda makosa kama hayo na kuhukumiwa kwenda jela, tena kutokana na makosa madogo madogo tu kama vile wizi mdodo mdpgo wa mali ya umma, rushwa ndogo ndogon, ukwepaji kodi n.k. na iwapo wangelijua, nao wangependa kuingia “maafikiano” na DPP ili waondokane na mateso ya kukaa gerezani.

Vinginevyo ielezwe wazi kabisa kwamba nchi hii inayo mifumo ya aina mbili ya utoaji haki – kwa wale wenye fedha nyingi ambao ni wachache katika jamii na wanaotumia kalamu zaidi katika jinai zao – na hawa wengine walio wengi.

Lakini suala la kuwapo kwa taratibu mbili za utoaji haki halikuanza katika awamu hii ya utawala. Katika awamu ya kwanza ya Rais aliyetangulia (Jakaya Kikwete) kuliibuka kashfa kubwa ya uchotaji wa fedha kutoka akaunti ya fedha za kigeni (EPA) ya Benki Kuu (BoT).

Mapema Agosti 2008 Kikwete alilihutubia Bunge lilikowa linaketi Dodoma na katika hotuba yake alitoa muda wa miezi miwili (hadi kufikia 31 Oktoba mwaka huo) kwa waliochukuwa fedha za EPA kuzirejesha la sivyo watapelekwa mahakamani.

Katika hotuba yake hiyo aliwaita watu hao kuwa ni ‘watu waliochukua au waliolipwa hela kutoka BoT’ na alikwepa kutumia neno “wezi” kwani ushahidi wote uliokuwapo ni kwamba walikuwa wezi tu kwani hawakustahili kulipwa hela hizo.

Hata hivyo serikali iliikazania sana ile azma yake kwamba jitihada kwanza zielekezwe katika kuzirejesha hela zilizoibiwa kuliko kuwapeleka mahakamani watuhumiwa.

Na tuliona namna baadhi ya watuhumiwa hatimaye walivyofikishwa mahakamani na usiri mkubwa uliogubika ‘urejeshwaji’ wa hizo fedha zilizoibiwa. Kutokana na usiri huu ambao hadi leo mantiki yake haijawekwa wazi na serikali, wengi walishuku iwapo hela kweli zilirejeshwa kama ilivyodaiwa.

Watu walihoji pia iwapo utaratibu wa “rejesha hela ulizoiba usiende jela” ungekuwapo kwa kila mtu, wafungwa wangepungua sana katika magereza yetu.

Aidha Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 ilikuja mapungufu kadha. Kwa mfano sheria hiyo haitoi tafsiri (definition) halisi ya neno ‘ufisadi’ (corruption) katika utangulizi wake wa tafsiri ya maneno na vifungu mbali mbali vya maneno (Intepretation of General Clauses).

Pili sheria hiyo inatoa ulaini wa adhabu kwa watakaopatikana na hatia, kwani imeweka chaguo (option) la faini kwa mahakimu na majaji – kwamba wanaweza kutozwa faini au kwenda jela wasipoweza kulipa faini, au vyote viwili. Mtu kafisidi mabilioni, halafu anapigwa faini – si atatumia kiasi kidogo tu cha hela hizo hizo alizofisidi kulipa hiyo faini? “Derrence iko wapi hapo?

Hii haiwezi kumaliza ufisadi nchini, kwani haiweki ukali (deterrence) wowote. Wanaokumbuka, mwaka 1972 utawala wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ulipitisha sheria iliyoitwa Minimum Sentences Act – Sheria yha Viwango vya Chini vya Hukumu.

Sheria hii ilitamka kwamba iwapo mtuhumiwa wa makosa ya rushwa na wizi wa mali ya umma atapatikana na hatia, basi hakimu au jaji anayesikiliza kesi hiyo analazimishwa kumpeleka jela kwa kipindi kisichopungua miaka miwili, bila ya faini yoyote.