Home Uhondo wa Siasa Lowassa na Chadema ni kama Ngasa na Simba

Lowassa na Chadema ni kama Ngasa na Simba

3272
0
SHARE

HONORIUS MPANGALA

WAKATI taifa letu likiwa limeelekeza macho na masikio katika kitongoji cha Kipawa kupokea mwili wa marehemu Rugemarila Mutahaba, ambaye amefariki dunia huko nchini Afrika kusini kwa matatizo ya figo, na huko Mahakamani ya Rufaa jijini Dar es salaam Jaji akaondoa zuio la hati ya kunyimwa dhamana kwa kuwapa ahueni Chadema, Mwenyekiti wao Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime, Ester Matiko kuwa na nafasi ya kurudishiwa dhamana zao wakati kesi ya msingi ikiendelea, likajitokeza tukio kubwa la kisiasa likihusisha chama cha CCM.

Kwa kawaida akili za watu wengi zikiwa huko Kipawa, Mahakamani pamoja na mwendelezo wa minyukano ya maneno ya kejeli na matusi huko mitandaoni kwanini Diamond hajaenda msibani (ingawaje baadaye alikwenda kwenye msiba), akaibuka mtu mmoja akiwa na jambo ambalo linawahamisha watu uelekeo. Mtu huyo ni Edwasrd Lowassa.

Jina la Edward Lowassa ni kubwa sana kisiasa nchini. Yeye amewahi kuwa waziri mkuu kwa miaka miwili, mbunge wa muda mrefu wa jimbo la Monduli mkoani Arusha, na mwanasiasa ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali katika baraza la mawaziri na utumishi wa umma.

Katika siasa kila mwanasiasa anakuwa na jina la utani, ambapo Lowassa huitwa “Mamvi” kutokana na nywele zake, pia anaitwa mwana “Boys II Men’ kutokana na uswahiba wake na rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete. Majina ya utani au makundi ya utani ni mambo ya kawaida, kwahiyo jina hilo kubwa pia linakuwa na watani wake.

Kuna wengine wamesema eti Lowassa amekosea ‘timing’  ya kutangaza muda wa kurudi CCM, lakini kwangu mimi naliona jambo hilo kama njia mojawapo ya kupunguza ‘kiki’ kali ambayo ingeleta mjadala mzito kwa pande zote mbili. Pia kuiweka ‘kiki’ hiyo katikati ya majonzi, ni kupunguza msongamano wa habari za kisiasa.

Niendelee kwenye hoja yangu. Suala la Edward Lowassa kuhama chama kutoka Chadema kwenda CCM ambako wengi tunaamini amerejea nyumbani kwake, ambako alijengwa kifalsafa na itikadi  kuliko ile aliyokwenda kujiunga nayo.

Hamahama ya wanasiasa tangu mwaka 2015 hadi leo hii kwa kweli haiwashangazi tena wanasiasa. Kuna wabunge wamehama upinzani na kwenda CCM, kisha wakateuliwa kugombea nyadhifa zao na kuwa wabunge tena kwa tiketi ya chama kipya.

Sasa turejeshe kumbukumbu nyuma, je unakumbuka jinsi Lowassa alivyoondoka pale CCM? Ilikuwa Julai 12 mwaka 2015, tukio hilo nina imani liliwapa shida watu wa Chadema kumnadi kutokana na zile skendo walizokuwa wanamtuhumu nazo bila ushahidi. Na katika maisha yake ya upinzani nadhani Lowassa amepata kuona namna gani wapinzani wanaishi na anafahamu namna gani chama dola wanaishi.

Kwenye mchezo wa soka kuna maneno kama ‘deal done’. Sisi wapenzi wa soka unapofika usajili wa wachezaji huko barani Ulaya tunafurahi sana kwani tunaamini usajili umekamilika. Hata kwenye siasa iko hivyo hivyo kuwa wapo wana CCM wameshangilia kukamilika kwa usajili huu wa Lowassa.

Sasa kwa kurejea kwa Lowassa pale mtaa wa Lumumba (makao makuu madogo ya CCM) ni kitu ambacho wengi wataona kama hakuna alichoiathiri Chadema. Hata hivyo napenda kuwakumbusha kuwa matokeo ya Lowassa kuhama Chadema hayako sasa ila kuanzia kwenye boksi la kupigia kura yataonekana dhahiri na kujua kama ameacha madhara au amewaachia faida.

Wakati Lowassa anasajiliwa na Chadema binafsi nilikuwa najiuliza vipi akiwa kiongozi hawezi kufanya Joyce Banda wa Malawi kwa kuhama chama akiwa kiongozi? Ikumbukwe Joyce Banda alikuwa Makamu wa Rais, ambaye alikihama chama tawala cha DPP na kuunda chama kingine lakini Katiba ilimruhusu kuendelea na cheo chake. Malawi ni tofauti na Tanzania, katiba yetu haiimpa mshindi wa diwani, ubunge, urais nafasi ya kuhama na cheo chake.

Binafsi kurejea kwa Lowassa chama tawala nilitehemea na tukio lake linafanana na lile la mchezaji Mrisho Ngassa. Wakati Mrisho Ngassa akiwa fiti kweli kweli, Yanga wakaamua kumuuza na kwenda klabu ya Azam FC kwa dili la milioni 58.

Ngassa akiwa klabu ya Azam FC, akafanya kituko ambacho wengi walijiuliza aliwaza nini. Ngassa alipewa jezi ya Yanga na mashabiki wa timu hiyo, naye akaivaa na kuibusu nembo ya Yanga. Kuona hivyo Azam FC wakachukua uamuzi wa kumuuza kwa mkopo kwenda klabu ya Simba.

Ngassa alihusishwa na Simba kwasababu tu imani ya mashabiki kuwa Mzee Khalfani Ngassa aliwahi itumikia klabu hiyo. Kikukweli Azam FC walilazimisha tu ule mpango. Ngassa ni shabiki haswa wa Yanga. Akiwa Simba, wengi waliamini muda wowote anaweza kurudi Yanga kuliko Azam.

Imani ya wapigakura iliyokuwa kwa Edward Lowassa ni kubwa. Ni kama vile Wanayanga walivyoamini kuwa Mrisho Ngassa ni mtu wao na aterejea wakati wowote. Na kwa CCM nao waliamini na sasa wamempokea Lowassa akitokea Chadema.

Licha ya kusaini mkataba na klabu ya Simba lakini Mrisho Ngassa akawachanganyia mafaili wapenzi wa Simba na kwenda kusaini tena Yanga. Ni vigumu kumtenganisha Mrisho Ngassa na klabu ya Yanga, hata Simba walifahamu suala hilo. Ila walimsainisha kwa kutaka kukomeshana kati ya Azam, Simba na Yanga.

Kwa mzingira yaleyale wafuasi wa vyama vya siasa wakampokea Edwad Lowassa, wakadeki barabara lami ili Lowassa apite, wakazungusha mikono kuimba wimbo wa mabadiliko, lakini leo ameamua kufanya kama Mrisho Ngassa na Yanga yake.

Ilikiwa ni kama anawaigizia tu kufanya harakati za kwenda Chadema na Leo amerejea tena. Lowassa na Chadema ni kama Mrisho Ngassa na Simba, ni vitu ambavyo haviwezekani moyoni ila utaaminishwa machoni.

Waliodeki lami wameachwa solemba kama wale waliojitokeza wakati wa mapokezi ya kumpokea Mrisho Ngassa akikea klabu ya Azam FC kwenda Simba. Wakapiga naye picha na gari aliyokuwa amenunuliwa. Leo hii Lowassa yuko CCM na Ngassa yuko Yanga. Heshimu moyo huwa unaweza kukupa furaha ukasahau shida zilizopo duniani.

Haya mambo ya usajili hayahitaji hasira waweza kujikuta unakuwa sehemu ambayo hukutarajia kuwepo.Katika Siasa hakuna soka, ila kwenye soka siasa ipo. Na haiwezi kutoka katika hilo ndipo unapokuta nembo ya klabu ya Real Madrid ina kofia ya Mfalme na kiongozi wa taifa la Hispania, ama nyakati za aliyekuwa waziri mkuu wa Italia Silvio Belsucon akitamba na klabu yake ya Ac Milan.0753 449254