Home Habari Mihadarati iligharamia Dola ya Uingereza Karne ya 19

Mihadarati iligharamia Dola ya Uingereza Karne ya 19

2082
0
SHARE


NA HILAL K SUED

Wanazuoni wengi wa Kiingereza wa historia kuhusu iliyokuwa Dola yao yao wamekuwa wakikwepa kuandika ukweli mmoja – kwamba Dola yao hiyo ilyozagaa maeneo mengi duniani ilikuwa ikiendesha biashara kubwa na ya mafanikio makubwa ya dawa za kulevya (mihadarati na bangi).

Katika karne ya 19 Uingereza ilipigana vita viwili vya bangi (Opium Wars) dhidi ya China katika mkakati wa kuilazimisha kuingiza nchini humo dawa za kulevya kwani ilionekana kuwa na soko kubwa kutokana na idadi yake kubwa ya watu.

Mihadarati hii ilizalishwa India na kusafirishwa kupitia kampuni yake ya kibiashara iliyoitwa British East India Compay (BEIC) hadi China. Na baadaye, mwaka 1857 kazi hiyo ilifanywa na serikali yenyewe ya kikoloni ya India ili kupata fedha za kugharamia bajeti za majeshi na makoloni yake katika maeneo ya Kusini na kusini mashariki mwa Asia.

BEIC ilianzisha ‘ubalozi’ nchini China ambayo kazi yake kuu ilikuwa kuwafundisha vibarua wa China kuwa tegemezi kwa mihadarati ili kujenga soko la bidhaa hiyo na hivyo kulifanya taifa la nchi hiyo kuwa la wavuta bangi.

Tabia hii ilikuja kuzimwa na utawala wa Kikomunisti wa Mao Zedong katika miaka ya 60 alipoanzisha Mapinduzi ya Kitamaduni (Cultural Revolution) ambayo pamoja na mengine lengo kubwa lilikuwa kukomesha uvutaji bangi.

Mwanazuoni Muastralia Carl A. Trocki anaandika kwamba bila kuwepo faida kubwa sana iliyotokana na mauzo ya mihadarati, huenda Dola ya Kiingereza isingekuwepo duniani.

Katika karne ya 20 ‘Dola ya Marekani’ (American Empire) nayo kwa kiasi fulani ilijiingiza katika biashara kama hiyo hiyo ya mihadarati.

Hata hivyo ‘Dola’ hii ya Marekani ni tofauti kubwa na ile ya Uingereza karne moja nyuma kwa sababu hii haikuwa na makoloni ya moja kwa moja iliyokuwa ikiyatawala. Ilikuwa inajieneza duniani katika ushawishi hasa wakati wa Vita Baridi (Cold War) kupinga itikadi ya Kikomunisti na baadaye kutokana na kupambana na kinachoitwa Uisilamu wa msimamo mkali.

Kwa mfano, inadaiwa kwamba biashara ya mihadarati nchini Afghanistan imeongezeka maradufu tangu uvamizi wa Marekani nchini humo mwaka 2001. Kufuatana na takwimu za Umoja wa Mataifa biashara hii haramu ina thamani ya Dola za Kimarekani 65 bilioni kila mwaka. Afghanistan inazalisha asilimia 92 ya mihadarati ya aina ya opium – na inakadiriwa tani 3,000 za mihadarati hiyo husafirishwa kutoka nchi hiyo kila mwaka.

Inadaiwa mtandao wa biashara hii ulikuwa unalindwa na vigogo akiwemo Ahmed Wali Karzai, mdogo wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo – Hamid Karzai. Kufuatana na ripoti ya gazeti la New York Times, Ahmed Karzai alijiongezea udhibiti wake wa biashara hiyo kwa msaada wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) ili tu kuwaangamiza washindani wake katika biashara hiyo.

Aidha inadaiwa kwamba kuongezeka kwa biashara hiyo baada ya uvamizi wa Marekani kulitokana na harakati za CIA kurejesha biashara nono ya bidhaa hiyo iliyojulikana kama Golden Crescent Opium Trade – biashara iliyokuwapo wakati shirika hilo la CIA lilipokuwa linatoa msaada kwa wapiganaji wa Kiisilamu (Mujahideen) waliokuwa wakipambana na wavanizi wa Urusi ya Kisoviet katika miaka ya 80 na 90.

Biashara hiyo iliongeza mihadarati hiyo iliyokuwa ya bei nafuu kwa watumiaji katika mitaa ya miji ya Uingereza na Marekani na hivyo kuyaharibu maisha yao – huku faida kubwa ya haramu ikipatikana.

Inadaiwa kwamba sasa hivi fedha za kuendesha harakati za mapambano ya vikundi vya Alqaeda na Taliban dhidi ya Marekani na utawala wa Kabul zinatokana na uzalishaji wa mihadarati. Wanafahamu wazi kwamba wakikiondoa chanzo hicho cha fedha vikundi hivyo vitaangamizwa.

Hivyo kuliko kuyaharbu mashamba ya mihadarati hiyo na kuwalipa wakulima fedha kama fidia, Marekani inayalinda mashamba hayo na kuwaruhusu wakulima kuuza bidhaa hiyo na hivyo kuendelea kwa Marekani kupambana na vita bandia duniani kote – vita wanayojua hawatashinda.

Na fedha ambazo Marekani, kupitia CIA zinazopatikana katika biashara hii hutumiwa kupambana na biashara hiyo kusini magharibi ya nchi hiyo, katika mpaka na nchi ya Mexico.

Kuanzia mapema 2007 kumetokea vifo vya watu zaidi ya 6,800 vilivyotokana na biashara ya mihadarati ya vikundi (drug cartels) vya Mexico, vikundi ambavyo vimekuwa vikijiingiza hadi katika mitaa ya miji ya Marekani. Na hili ndiyo sababu moja inayomfanya Rais Donald Trump kutaka kujenga ukuta kati ya nchi yake na Mexico.

Unafiki wa namna hii wa Marekani pia ulionyeshwa na mtangulizi wa Trump – Barack Obama pale alipomtuhumu Rais mpya (wakati huo) wa Ufilipino – Rodriguez Duterte kwa kuwapiga risasi na kuwaua washukiwa wa utumiaji wa mihadarati nchini kwake.

Kwa tawala za Marekani huu ni unafiki tu. Mwishoni mwa miaka ya 80 wakati wa Urais wa George H Bush katika kile kilichoitwa ‘Bush Wars’ nchini Colombia, rais huyo alituma vikosi nchini humo kupambana na wazalishaji na wafanyabiashara wa mihadarati (aina ya cocaine). Askari hao walikuwa wakiwaua washukiwa wa biashara hiyo na kuchoma nyumba na mashamba yao.