Home Makala Mjadala Tume Huru ya Uchaguzi kaa la moto

Mjadala Tume Huru ya Uchaguzi kaa la moto

1224
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia mkutano wake na wandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita, kiliezea nia yake ya kutaka kuwapo Tume Huru ya Uchaguzi itakayosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani hapo mwakani.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdallah Safari, suala hilo ni mikononi mwa mambo yaliyojadiliwa na Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Profesa Safari anadai kuwa suala hilo limejadiliwa kwa kina na kuona kuwa kuna haja ya kuboresha Tume ya Uchaguzi ili kuhakikisha kunakuwapo na uchaguzi huru na wa haki.

Kupatikana kwa tume hiyo kunahusisha kubadilisha baadhi ya vifungu vya Katiba vinavyohusiana na tume na kubadilisha sheria za uchaguzi ikiwamo ile ya mwaka 2002.

Profesa Safari anabainisha kuwa chama chake kimeazimia kuandaa rasimu ya kuboresha Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na sheria zake zote, na kwamba itakapokuwa tayari, itajadiliwa na Kamati Kuu ya chama hicho kwa kina na kuiwasilisha kwa wadau wote wa demokrasia kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili ufanyike mjadala wa kitaifa.

“Tukubaliane kuwa sheria hizo zinarekebishwa kuhakikisha mshindi wa kweli anatangazwa iwe rais, mbunge au diwani,” anasema Profesa Safari.

Kauli ya Chadema imetolewa siku moja tangu Mahakama Kuu ya Tanzania itupilie mbali pingamizi la Serikali dhidi ya kesi ya kikatiba ya kupinga wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Kesi hiyo iliyofunguliwa na Bob Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika kesi hiyo, namba 6 ya mwaka 2018, Wangwe anapinga wakurugenzi halmashauri za wilaya, miji na majiji, kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya NEC. Wakurugenzi wote ni ni wateule wa Rais John Magufuli kwa sasa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.

Kwa uamuzi huo wa Mahakama, kesi hiyo sasa itaendelea kusikilizwa, ili kutoa uamuzi wa kuwaacha au kuwaondoa wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Hii ni mikasa michache kati ya mingi ambayo imewahi kutolewa na wadau mbalimbali wakidai mabadiliko ya NEC, ili kuhakikisha kunakuwapo na uwanja ulio sawa kwa wagombe wa vyama vyote vya siasa.

Kitendo cha wandau wa masuala ya siasa kuendelea kudai mabadiliko ya Tume ni kiashiria tosha kwamba kuna kasoro ambazo wanaona ni vema zikaondolewa, ili kuondoa misigano miongoni mwa wadau—hususan  vyama vya siasa, ambavyo mara zote huonesha kutofurahishwa na mwenendo wa Tume katika chaguzi mbalimbali.

Katika mazingira ambayo rais, na mwenyekiti wa chama kimojawapo cha siasa, ambaye wakati mwingine huwa ni mgombea katika uchaguzi husika, sio rahisi kwa chama kuamini kuwa haki inatendeka kweneye chaguzi husika, hata kama inaonekana kutendeka.

Miongoni mwa wadau ambao wamewahi kutoa mapendekezo ya kupatikana Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ni pamoja na Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA).

Wanapendekeza kufanyika marekebisho katika baadhi ya maeneo, ikiwamo kupatikana kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo muundo wake utaakisi majukumu yake, kwa kuwezesha kuwapo kamisheni itakayoongoza Tume hiyo katika utendaji kazi wake, na kuwajibika kwa mambo yote ya kisera na kimaamuzi, pamoja na kuundwa kwa sekretarieti ya Tume itakayokuwa chini ya Mkurugenzi wa Tume, kama mtendaji mkuu.

Kutokana na rais anayekuwa madarakani, kuwa miongoni mwa wagombea katika uchaguzi, au anakuwa kiongozi wa chama kimojawapo cha siasa ambacho kinasimamisha mgombea, wanashauri kupunguzwa kwa mamlaka ya rais ya uteuzi, tofauti na sasa ambapo mamlaka yote ya uteuzi yako chini yake.

Jukata wanapendekeza kuwa mchakato wa kuwapata makamishna wa NEC, utangazwe, ufanyike usaili, kisha majina hayo yafanyiwe mchujo na kupatikana majina 20, yatakayopelekwa kwa rais ambaye atapendekeza majina tisa yatakayopelekwa bungeni kufanyiwa uchambuzi, kujadiliwa na kisha yawasilishwe tena kwa rais ili amteue mwenyekiti wa Tume hiyo.

Baada ya uteuzi huo wa Rais atayawasilisha majina hayo kwa Jaji Mkuu ambaye atayatangaza na kuwaapisha makamishna wa Tume. Pia rais atamteua Mkurugenzi wa Tume kutokana na majina mawili yatakayopelekwa kwake na Tume ya Uajiri wa Umma kutokana na mchakato huru na wa wazi wa uajiri.

Kupitia utaratibu huu, Mkurugenzi wa NEC ndiye atakuwa mtendaji mkuu wa Tume hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi na Katibu wa Kamisheni ya Tume (Board).

Njia hii inaweza kupunguza kwa kiasi fulani, malalamiko dhidi ya Tume, kwa sababu mchakato wake utakuwa umepitia mchakato wa kawaida wa uajiri, na kupunguza nafasi ya uteuzi kwa rais ambaye kwa namna moja, au nyingine, angeweza kumteua mtu asiyekubalika na wengi, hivyo kujenga taswira kuwa amemteua kwa maslahi yake binafsi au ya chama chake.

Katika mazingira ya sasa ambayo wasimamizi wengi wa mchakato wa uchaguzi ni wateule wa rais, hakuna chama kitakachokubali kushindwa kwa haki, hata kama kinatambua kuwa haki imetendeka. Na ikumbukwe kuwa haki siyo tu inapaswa kutendeka, ila pia inapaswa kuonekana imetendeka.

Wenye mamlaka pia wanapaswa kukubali kuwa sio tu yanatakiwa kufanyika marekebisho katika Tume, bali marekebisho makubwa katika mfumo wote wa siasa nchini, ili kuwezesha ustawi wa mfuomo wa deokrasia ya vyama vingi ambao Taifa limekubali kufuata.

Ni vema ikafahamika kuwa, tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, hakuna mabadiliko makubwa yaliyofanyika kisera na kimuundo, bali mabadiliko yaliyofanyika yalilenga kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Njia sahihi ya kufanya mabadiliko ya kimfumo na kimuundo, yalipaswa kufanyika kupitia Katiba Mpya, lakini hilo halikufanyika na hakuna matumaini ya kufanyika sasa, kwa sababu Rais Magufuli mwenyewe amekiri hadharani kuwa licha ya kutambua kuwa wananchi wana hamu kubwa ya kupata Katiba Mpya, kwake mchakato huo sio kipaumbele chake.