Home Makala Muswada wa Vyama vya Siasa ni majanga

Muswada wa Vyama vya Siasa ni majanga

3261
0
SHARE

Balinagwe Mwambungu

Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa unaokusudiwa kupelekwa bungeni kusomwa kwa mara ya pili, umeelezwa kwamba ni muswada wenye nia mbaya ya kuua vyama vya upinzania nchini Tanzania.

Namshangaa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mtungi, msomi mwenye uwezo mkubwa wa kutafsiri sheria, kuwa hayaoni mambo ambayo wananchi, viongozi wa makundi mbalimbali, wakiwamo wanasheria na viongozi wa siasa wanayapinga. Jaji Mutungi  yeye anatetea kwamba ni muswada mzuri.

Inawezekana kwamba muswada huu ulishushwa kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa bila kushirikishwa. Kama ofisi hiyo ilisjirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na wakakubaliana kwamaba maudhui yaliyomo katika muswada huo ni sahihi, basi kuna kila sababu ya kuamini kwamba walikuwa wanafuata maelekezo.

Ukiangalia mwenendo wa siasa hapa nchini tangu mwaka 2016, pamekuwapo na nia ya kuvunja nguvu ya wapinzani na kuwanyamazisha. Toka mwanzo imetumika nguvu kubwa ya kuuzima upinzani—kwa kukataza vyama vya upinzani visifanye siasa. Baada ya kelele nyingi, amri hiyo ikarekebishwa kwa kauli kwamba ni Wabunge wa kuchaguliwa ndio wanaruhusiwa kufanya mikutano ya siasa katika majimbo yao. Lakini ni marufuku kwa Wabunge hao kuwaalika viongozi wa vyama vyao au Wabunge wa chama husika kujumuika nao, ili kupeana nguvu katika kutangaza mikakati na sera za vyama vyao.

Ilitamkwa kwamba viongozi wa vyama, wanaruhusiwa kufanya mikutano ya ndani, lakini nayo imeleta mkanganyiko. Polisi wamekuwa wakiizuia kwa visingizio mbalimbali. Kuna tukio ambapo uongozi wa kitaifa wa chama cha upinzani, ulizuiwa kufanya kikao kilichoandaliwa kwa muda mrefu kwa maelezo kwamba Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, alikuwa anafanya ziara kwenye mkoa huo wa Geita.

Hivi sasa kuna sauti mbili tu ambazo zinasikika—sauti ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Dk. Bashiru Ally na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli. Wengine wote wamenyamazishwa, wengine wako rumande na wengine wanahangaika na kesi mahakamani.

Kama kwamba hii haitoshi, sasa Serikali imeamua kuvipumzisha vyama vya upinzani kisheria—kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Upinzani. Kama utatua bungeni jinsi ulivyo na kupitishwa na Wabunge wa CCM, basin chi yetu itakuwa imeingia katika ‘new dark epoch’—mwanzo wa kipindi kipya cha giza.

Ni jambo la kushangaza sana—kwamba nchi za wenzetu hupitisha sheria zenye tija—hazitungwi kwa ajili ya chama au kundi fulani, ndio maana hatusikii kwamba sheria zao zinarekebishwa, kubadilishwa  au kufutwa mara kwa mara.

Frederick Chiluba akiwa mpinzani mkubwa wa Rais Dk. Kenneth David Kaunda, alipinga sana sheria inayompa madaraka rais kumweka mtu kizuizini bila maelezo, na bila kumfikisha mahakamani. Lakini alipoingia madarakani  mwaka 1991 kupitia chama chake cha Movement for Multi-party Daemocracy (MMD), mpaka anaondoka mwaka 2002, hakuifuta sheria hiyo. Badala yake akaitumia sheia hiyo hiyo kumweka kizuizini mwanzilishi wa taifa la Zambia, Dk. Kaunda.

Jambo la kujifunza hapa ni kwamaba, viongozi walio madarakani sasa, wajue kwamba hawata tawala milele, ingawaje Dk. Mashiru, msomi na mchambuzi, yeye anasema (arrogantly) kuwa chama cha kuiondoa madarakani CCM, bado hakijazaliwa! Iko siku, sheria hizi mbovu ambazo zinatungwa kwa kuwalenga wapinzani, zitajatumika kuwadhibiti wao pia.

Ninachokiona hapa ni kwamba muswada huu haukutungwa kwa nia njema. Nakubaliana na Askofu Benson Bagonza, kwamba Muswada huu sio wa Marekebisho, ni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, bali ni muswada wa Msajili wa Vyama.

Askofu Bagonza, alitoa uchambuzi mzuri alipokuwa akiongea hivi karibuni kwenye Mdahalo wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ambao uliandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Alibainisha kuwa sehemu kubwa ya muswada huo, inaongelea haki za Msajili, mamlaka yake.

“Muswada huu hauongezi thamani ya vyama vya siasa, unaongelea thamani ya juu ya vyama, unapunguza thamani ya uwepo wa vyama,” alisema.

Alisema kuwa muswada huo unamwondoa Msajili kwenye uhalisia na kumpa hadhi ya kimalaika kwa kutamka kwamba asiweze kushitakiwa. Akaongeza kuwa muswada huo unaongeza idadi ya watu wenye kinga (kutoshitakiwa pale wanapofanya makosa).

Maana yake nini? Maana yake kwamba mbali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutaongeza kikundi cha watu wenye kinga, ambao watafanya makosa yamakusudi (kukomoa), kwa vile wanakinga ya kisheria.

Hili naliunganisha na kauli ya Rais Magufuli—kwamba askari polisi, wakijeruhi au kuua mtu wakiwa kazini, wasishitakiwe, jambo ambalo linapingwa na wanasheria. Nani asiyejua kwamba polisi ni coersive—chombo cha mabavu? Unawapaje polisi immunity (kinga), kwa mfano!

Mfano mbaya

Jambo jingine ni kwamba musada huo, kama alivyosema Askofu Bagonza, kwa ujasiri mkubwa, unampa Masajili mamlaka ya kuingilia haki za wengine (sets a bad precedence). Anaonya kwamba muswada huu kiachwa upite, una hatari ya kujenga mawazo ya vyombo vingine (vya usalama), kuingilia haki za watu—haki ya kuabudu, uhuru wa kufikiri (freedom of conscience), uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuandika na kuchapisha.

Aidha imeelezwa kwamba bila kuangalia kwa makini, usipokuwapo umakini, muswada huu unampa madaraka mwenyekiti wa chama kilicho madarakani, kuongoza vyama vingine, kupitia kwa waziri mwenye dhamana na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Hii inatokana na kipengere ambacho kinatamka kwamba waziri husika ndiye mwenye wajibu wa kutunga kanuni za uendeshaji wa vyama vya siasa—visivyo vyake. Kwa mujibu wa Sheria mama (Katiba), hakuna waziri ambaye hatokani na chama.

“Waziri ili awe waziri, lazima atokane na chama fulani, haiwezekani akawa waziri anayetokana na vyama vyote,”.

Waziri unamtwisha mzigo wa kudhibiti (control) vyama vingine visivyo vyake, utakuwa uhuru wa dhamiri utakuwa umeingiliwa,” anatanabaisha Askofu Bagonza.

Kwa jinsi muswada huu ulivyo, kama nilivyosema awali, hauna nia njema ya kuleta mustakabali wa kisiasa (political harmony) na utashi wa kisiasa. Nia yake, ukisoma toka mwanzo, ukalinganisha na hali halisi ya kisiasa ilivyo hivi sasa nchini, utafikia tamati kwamba ni muswada wenye lengo baya—kufuta (stifle) juhudi  zotezilizofikiwa na kuimarisha mfumo wa vyama vingi—kujenga demokrasia na kuendesha nchi katika misingi ya utawala wa sheria.

Hakuna mahala popote duniani, nisahihishwe kama nimekosea—ambako sheria inampa (indirectly) mamlaka mwenyekiti wa chama kilicho madarakani—kuvitawala  vyama vingine kupitia kwa waziri au msajili wa vyama vya siasa. Hakuna.