Home Tukumbushane Nani mwenye mwarobaini wa ajali za barabarani?

Nani mwenye mwarobaini wa ajali za barabarani?

3041
0
SHARE

HILAL K SUED

Kuna mateso ya aina mbili katika barabara zetu. Wakati barabara za mikoani zinazidi kuwaangamiza wanaozitumia – abiria na watembea kwa miguu pia, zile za mijini, hasa jiji la Dar es Salaam zinaendelea kuwapa adha watumiaji wake kupitia misongamano ya magari na kujaa maji wakati wa vipindi vya mvua – hali zinazowakera sana.

Tofauti kati ya aina mbili hizi za mateso iko katika ‘kasi.’ Kwa barabara za mikoani ni mwendo wa kasi ambao umekuwa unatwaa roho za binadamu, wakati kwa barabara za jiji la Dar es Salaam ni ule mwendo wa konokono ambao unatoa bughudha kubwa kwa watumiaji na watu wengine pia.

Na katika hali zote mbili hizo mamlaka husika pamoja na jitahad wanazofanya hazionekani kuwa na suluhisho la kudumu isipokuwa uwingi wa ahadi na maneno, maneno, maneno… Je inawezekana changamoto hizi zinaeleza mengi kuhusu tabia yetu inayosababishwa na magari haya yatembeayo?

Tuchukulie hili la mwendo kasi wa magari. Tangu yalipovumbuliwa, magari yamekuwa yakihusishwa na mwendo kasi – yaani mbio za magari. Ilikuwa mwaka 1895 pale mashindano ya kwanza ya mbio za magari yalifanyika, wakati magari yalikuwa katika hatua za mwanzo tu za kuendelezwa na kuboreshwa.

Hivyo basi kuanzia mwaka huo, magari na mwendo kasi vimekuwa vitu ambavyo haviwezi kutenganishwa – kama vile lugha ya mitaani isemavyo – daima ni spidi tu kwa kwenda mbele. Matokeo yake ni athari kubwa kwa maisha ya binadamu na mali.

Hii inatokana kwa sababu binadamu wanaabudu sana kwenda kasi wakiwa ndani ya magari wakiyaendesha. Ni kitu bado hakijaeleweka kwa nini ikawa hivyo, pamoja na tafiti nyingi kufanyika. Muitaliani Enzo Ferrari, bingwa wa zamani wa mbio za magari aliwahi kunena: “Mbio za magari ni ulevi mkubwa ambao mtu anajitolea kila kitu, bila kujali, bila kusita.”

Aidha angalia ukweli huu pia: – kwa nini siku zote dereva aliye nyuma yako anaonekana kama vile yuko kwenye mashindano ya mbio za magari na yule aliye mbele yako anaonekana kama vile anatalii tu?

Kwa mtu yoyote mwenye akili timamu, ajali nyingi za barabarani zinazotokea siku hizi na kusababisha vifo lazima zinaibua swali: Kunani katika sekta ya uchukuzi? Kwa nini ajali hizi zinaongezeka – kwa idadi na vifo na kwamba inaonekana hakuna hatua zozote zinachukuliwa kwa dhati kutatua kadhia hiyo?

Miezi kadha iliyopita Rais John Magufuli alimbadilisha waziri wake wa ndani, Mwigulu Nchemba, baada ya kumtuhumu, pamoja na mengine, kushindwa kusimamia suala la ajali za barabarani, suala ambalo liko chini ya wizara yake.

Hatua hiyo ilikuja baada ya ajali mbaya ya barabarani kuua zaidi ya watu 20 mkoani Mbeya. Hata hivyo haikumalizika wiki ajali nyingine ikatokea huko huko Mbeya na kuua watu wanne.

Sasa pamoja na kuwepo kwa waziri mwingine ajali bado zinaongezeka kama vile ile iliyoua watu 19 Mkoa wa Songwe jirani na Mbeya wiki mbili zilizopita. Isitoshe chini ya waziri huyu mpya ajali zinazohusu magari ya serikali na taasisi zingine za umma zimekuwa zikiongezeka na kusababisha vifo vya watumishi wa umma.

Hii inaonyesha kwamba kupambana na ajali za barabarani ni suala lenye changamoto kubwa na nyingi na si la kumtwishia lawama mtu mmoja. Na historia katika miongo ya karibuni jinsi nchi hii imekuwa inapambana na janga hilo inathibitisha hili.

Kwa mfano mwanzoni tu mwa miaka ya 90 serikali ilipiga marufuku kwa mabasi ya abiria kutembea usiku – kuanzia saa 2 hadi alfajiri. Kama basi bado liko barabarani na imefika saa 2 usiku dereva anatakiwa aliegeshe mahali salama hadi alfajiri ndiyo aendelee na safari yake. Marufuku hii ipo hadi leo lakini haijaweza kumaliza ajali za barabarani – na kusema kweli ziliongezeka – tena mchana kweupe. Sasa hivi kuna wito mpya wa kuruhusu mabasi hayo kusafiri usiku pia.  

Jitihada ya nyingine ya serikali iliyofuatia ilikuja katikati ya miaka ya 90 pale serikali ya Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa ilipoanzisha ulazima kwa magari yote ya abiria (yaani mabasi) kufungwa vifaa maalum vya kudhibiti kasi ya mabasi hayo – yaani ‘vidhibiti mwendo” – (speed governors).

Ulazima huu ambao ulilenga kupunguza ajali za barabarani kuhusu mabasi ya abiria pia ulihusu mabasi ya ‘daladala.’ Kwa kifupi ni kwamba kwa mabasi ya kwenda mikoani kifaa kilitakiwa kudhibiti spidi kutozidi kilomita 80 kwa saa – yaani hata dereva akikandamiza kiongeza-mwendo (accelerator) hadi mwisho.

Na kwa daladala spidi isizidi kilomita 50 kwa saa. Ili zoezi hili kuwa na baraka za kisheria, Sheria ya Usalama Barabarani (Road Traffic Act) ya mwaka 1973 ilirekebishwa.

Zoezi hilo lililokuwa na nia njema lilianzishwa kwa kishindo lakini hatimaye lilipotea kimya kimya kwa sababu mbali mbali – kubwa iliyotajwa ni kwamba hakukuwepo na utafiti wa kutosha kabla ya serikali kuja na maamuzi hayo.

Sababu nyingine – kama ilivyo ada kwa mazoezi mengi ya kitaifa yanayotajwa kuwa ni ya ‘nia njema’ au/na kwa masilahi ya taifa na watu wake, harufu ya ufisadi ilikuwapo, kwani wamiliki wa mabasi hayo ndiyo walilazimika kugharamia kwa kuvinunua kwa bei kubwa – hadi sh 500,000/- (wakati ule) kwa kila kifaa na kwamba kwa kuwa vilikuwa vinaagizwa kutoka nje — awali aliteuliwa muagizaji mmoja tu wa kuvileta nchini na kuvisambaza kwa bei aliyopanga yeye.

Hivyo kulikuwa na madai kwamba watu fulani ‘wapiga dili‘ ndiyo walioliuzia serikali wazo hilo, na watendaji serikalini wenye maamuzi wakaingia kichwa kichwa. Zoezi hili halina tofauti sana na lile la mashine za EFD (electronic fiscal devices) ambazo hapo awali wafanyabiashara walilazimishwa kununua kwa bei kubwa na ambalo pia ilitajwa kulikuwapo waagizaji wa mashine hizo waliotaka kutengeneza pesa.

Wamiliki wengi wa mabasi walishindwa kuvinunua kutokana na bei, lakini pia hata wale waliuomudu iliwalazimu kusimamisha shughuli zao ili wakayapaleke mabasi yao yakakae foleni kungojea kufungiwa vidhibiti mwendo na hivyo kuleta adha kubwa kwa wasafiri wa jijini hapa.

Ajabu moja ni kwamba eti kwa kuona adha hii kwa wakazi wa Dar es Salaam, serikali iliruhusu magari ya aina ya pick-up kusaidia kubeba abiria – na wengi walihoji busara iliyotumika katika uamuzi huu kwa sababu pick-up hizo si kwamba hazikuwa salama kubeba abiria, bali pia nazo hazikuwa na vidhibiti mwendo.

Aidha haikupita muda ikaja kugundulika kwamba vidhibiti mwendo vile ambavyo pamoja na ‘ubora’ wake kuthibitishwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) havikuwa na ubora wowote kwa lengo lililokuwa limekusudiwa. Ingawa viliweza kudhibiti spidi zinazotakiwa, lakini vifaa hivyo havikuwa na kinga ya kutochokonolewa (tamper proof) na madereva/wamiliki wa mabasi. Hivyo vilikuwa vinachokonolewa sana na kuharibu lengo zima la vifaa hivyo.

Hali hii ya uchokonoaji wa vidhibiti mwendo ilisambaa sana kwani baadaye mamia ya polisi wa usalama barabarani (traffic police) walikuwa na kazi moja kubwa – ya kukamata mabasi ambayo vidhibiti mwendo vyake vilikuwa vimechokonolewa na hivyo kuzalisha mwanya mwingine wa rushwa kwa polisi wa usalama barabarani na matokeo yake ni kwamba ajali za mabasi ziliongezeka badala ya kupungua.

Hata hivyo wengi walihoji busara iliyotumika ya kulazimisha vidhibiti mwendo kwa mabasi ya abiria tu – na si kwa magari ya aina nyingine ambayo pia hutumia barabara hizo hizo.

Walisema hata kama mabasi yatakuwa yamedhibitiwa spidi kwa kuwekewa vifaa hicho – je magari mengine yanayotumia barabara hizo hizo kama vile malori na magari mengine madogo madogo ambayo yanaweza kuhusika katika kusababisha ajali mbaya kwa mabasi yenye vidhibiti mwendo?

Baada ya kufa kwa zoezi la vidhibiti mwendo serikali ikaja na zoezi jingine la kufunga vifaa maalum ‘tachometer’ kwenye mabasi makubwa, vifaa ambavyo vilikuwa vinaweka kumbukumbu ya safari na uendeshaji wa basi husika kati ya mji (kituo) mmoja hadi mwingine – kama vile muda iliyotumia ikiwa njiani na kama ilisimama mahala popote na iwapo ilizidisha spidi inayokubalika.

Vifaa hivyo hukaguliwa na polisi wa barabarani kila kituo na hivyo kujua iwapo dereva alizidisha spidi na kuchukuliwa hatua. Hata hivyo vifaa hivyo havikuonekana kuleta ahueni katika ajali za barabarani na baadaye serikali ikaanzisha zile tochi

zinazoshikwa mikononi na polisi wa usalama barabarani na zilihusu magari yote. Hawa polisi husimama sehemu fulani fulani barabarani na mara nyingi katika sehemu wasionekana kiurahisi na madereva wa magari.

Huzielekeza ‘tochi’ zao kwenye mabasi yanayopita barabarani na kurekodi spidi yanayokwenda na kupeleka taarifa kituo cha pili ili madereva wanaokwenda spidi zaidi ya ile iliyowekwa washugulikiwe kisheria.

Lakini pamoja na jitihada zote hizi bado ajali za barabarani zinazosababishwa na mabasi yanayokwenda kasi zinazidi kuongezeka kila siku. Kwa hiyo tunarejea pale pale – tatizo kubwa zaidi linatokana na hulka, au tabia ya waendesha magari.