Home KIMATAIFA S. Arabia yachukizwa kuchaguliwa wabunge wa Kiisilamu nchini Marekani

S. Arabia yachukizwa kuchaguliwa wabunge wa Kiisilamu nchini Marekani

1056
0
SHARE

HILAL K SUED NA MITANDAO

Mapema wiki hii jarida moja linaloandika habari za sera za Mambo ya Nje ya Marekani liitwalo “Foreign Policy Magazine” lilikuwa na kichwa cha habari: “Saudi Arabia yatangaza vita dhidi ya wanawake wawili Waisilamu ambao ni Wajumbe katika Baraza la Wawakilishi la Marekani.”

Habari hiyo hiyo iliendelea kueleza kwamba tawala za falme katika nchi za Kiarabu zinatumia ubaguzi wa kitaifa na habari za uongo kukemea wanasiasa wanaobadilisha historia nchini Marekani.

Wanawake hao wawili ambao ni kiini cha propaganda cha Saudi Arabia ni Rashida Tlaib – Mmarekani mwenye asili ya Palestina ambaye katika uchaguzi mdogo mwaka jana alishinda kiti cha Uwakilishi katika jimbo la Uwakilishi la Michigan 13; na Ilhan Omar, Mmarekani mwenye asili ya Somalia aliyeshinda kiti kama hicho kutoka Jimbo la Minnesota 5.

Lakini ukweli ni kwamba wahafidhina wengi wa kibaguzi nchini Marekani pia walichukizwa kwa kuchaguliwa wanawake hawa wawili wa Kiisilamu katika Baraza lao la Wawakilishi – na mitandao ya kijamii ilijaa kejeli na chuki dhidi ya wanawake hao.

Lakini swali kubwa la kujiuliza ni kwanini mamlaka za Saudi Arabia, au hata zile zingine za Kifalme miongoni mwa nchi za Kiarabu au hata nchi za Kiisilamu ambazo kuishi kwao kunatagemea sana usaidizi wa nguvu za kijeshi za Marekani – zianzishe ugomvi dhidi ya Wabunge hawa wawili wanawake ambao Wamarekani wenyewe waliwachagua pamoja na Uisilamu wao?

Wadadisi wa mambo wanasema badala ya kutoa shutuma dhidi ya wawili hawa, mamlaka za Saudi Arabia, kwa mfano, zingepaswa kuwapongeza, kwani mamlaka hizo ndiyo “Mlinzi wa sehemu mbili takatifu za Kiisilamu” hapa duniani na hivyo huwa tayari kuwalinda Waisilamu wote popote duniani.

Kufuatana na jarida hilo tajwa, wasomi, watu wa vyombo vya habari na wanasiasa wengine walio karibu sana na tawala za kifalme za Ghuba zimekuwa zinawashambulia vikali Rashida Tlaib, na mwanaume mwingine Abdul El-Sayed (ambaye alishindwa katika kinyang’anyiro cha kuwania Ugavana wa Jimbo la Michigan) kwa kusema kwamba ni wafuasi wa kisirisiri wa chama cha Udugu wa Kiisilamu (Muslim Brotherhood), chama kilichopigwa marufuku nchini Misri na ambacho kinapingana na sera za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kukua kwa chama hicho nchini Marekani kama ni chama hatari kilifuatia kipindi kifupi cha utawala wa Rais Mohammed Morsi wa chama hicho nchini Misri mwaka 2012-13.

Hii ilikuwa baada ya wimbi lililoitwa “Arab Spring” – la mabadiliko ya tawala yaliyoanzia Tunisia, kufuatiwa na Misri na Libya ambapo taweala za Misri (baada ya kupinduliwa kwa Morsi), Bahrain, Syria, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zilikiona chama hicho kama ni adui wao mkubwa.

Na kwa sababu Hamas (chama ambacho kinadhaniwa kuwa ni tawi la Muslim Brotherhood) hata Israel ilijiunga katika kundi hilo la Kiisilamu wanalodai linatumia siasa katika kujikweza.

Wadadisi wa mambo wanasema kutokana na umbumbumbu wa kimakusudi, tawala hizi zinadhani zitapunguza nguvu ya wapinzani wao kwa kukionyeshea kidole chama cha Muslim Brotherhood kama ndiyo chanzo.

Hata hivyo inadaiwa kwamba Ilhan Omar kwa mfano amekuwa mpinzani mkubwa wa sera za Saudi Arabia na hivi karibuni aliishutumu nchi hiyo kuhusu kujiingiza kwake kule Yemen, na mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Kashoggi.