Home Maoni Usalama wa raia ajenda muhimu 2020

Usalama wa raia ajenda muhimu 2020

1704
0
SHARE

MARKUS MPANGALA

MATUKIO mbalimbali ya kupotea watu, kutekwa nyara, kuokotwa maiti kwenye mifuko katika fukwe za bahari, mito na maeneo mbalimbali, ni miongoni mwa mambo yanayowatisha wananchi na ambayo bila shaka yatanguruma kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, ikiwa ni hoja ya kulinda usalama wa raia na mali zao kando ya ajenda ya uchumi, afya, elimu, mawasiliano na uchukuzi.

Kuibuka kwa matukio ya kupotea watoto wadogo katika mazingira ya kutatanisha kabla ya kukutwa wameuawa, yanayotokea mkoani Njombe na sasa yameingia Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu, ni kielelezo cha hoja ya usalama wa raia na mali zake kuwa miongoni mwa ajenda kuu inayoweza kutumika kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Hakuna chanzo kimoja cha mauaji hayo, lakini miongoni mwake ni imani za kishirikina ambazo zinadaiwa kukithiri miongoni mwa wanajamii nchini Tanzania.

Mathalani, wakati wa sakata la mauaji ya watoto mkoani Njombe, Mkuu wa Operesheni Maalumu za Jeshi la Polisi, Liberatus Sabas alikaririwa na vyombo vya habari akisema hatua ya awali idadi ya watuhumiwa ilikuwa imefika 27, ambapo msako ulikuwa ukiendelea na walifikishwa mahakamani.

Katika saka hilo hilo, Diwani wa Kata ya Lamadi wilayani Busega, mkoani Simiyu, Laurent Bija, aliliambia gazeti la la Mtanzania toleo la Februari 13 mwaka huu, “Hofu ni kubwa kwa wananchi wangu, hata mimi mwenyewe maana nimelazimika kuwakataza watoto wangu wa kike wawili kwenda kanisani au kutembea, lakini shuleni nawasindikiza asubuhi,” alisema Bija.

Kauli ya diwani huyo ni ishara ya wazi ya wananchi kuishi kwa hofu kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka 2020. Njombe ni mkoa ulioko Nyanda za Juu Kusini, ukiunganishwa na mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Songwe, Iringa na Rukwa.

Licha ya baadhi ya watuhumiwa kukamatwa kutokana na mauaji ya watoto, bado tishio hilo linaendelea kuathiri maeneo mengi nchini na kuibua mjadala wa usalama wa raia.

Matukio ya kupotea baadhi ya watu katika mazingira ya kutatanisha na vifo vya baadhi yao, ni miongoni mwa mambo yanayoonesha dhahiri kuwa suala la ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao linatishiwa. Katika hali ya kawaida wananchi watakuwa na hoja ya usalama wa familia zao na mali zao, huku wanasiasa wakitakiwa kuwashawishi wananchi kuwa chaguo sahihi la usalama wao.

Miongoni mwa waliopotea na kutekwa nchini ni Bilionea Mohammed Dewji (mwaka 2018), mwanamuziki Ibrahim Musa almaarufu kwa jina la Roma Mkatoliki (mwaka 2017), Msaidizi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Benard Saanane (Novemba 18 mwaka 2016), mwandishi wa habari Azory Gwanda, mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Samson Josiah (almaarufu kama Super Sami), pamoja na mauaji ya viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi takribani 40 katika eneo la Kibiti mkoani Pwani, ambao walishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana.

Vilevile mnamo Desemba mwaka 2016, kuliokotwa miili ya watu 7 katika kingo za mto Ruvu, Kijiji cha Mtoni, Kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Matukio haya yanajenga dhana kuwa suala la usalama ni tete kwa sasa, jambo ambalo linaleta hoja ya uchaguzi kwa wanasiasa na kuliangalia kama suala nyeti ambalo litapigiwa upatu kwenye mikutano ya kisiasa uchaguzi ujao.

Ingawaje ajenda ya shughuli za uchumi inadaiwa kuchukua nafasi kubwa, lakini suala la usalama wa raia kwa namna yoyote, litakuwa kipaumbele cha vyama vingine katika mazingira ya sasa.

Ni dhahiri kwamba watu wanaingiwa na hofu juu ya watoto wao, ndugu, jamaa, marafiki, majirani zao na wenyewe, iwe kupotea au kutekwa, hivyo kuwa na uwezekano wa kuathiri shughuli za uchumi kuwa si sehemu salama ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya wananchi wengi ni wakulima na wafugaji.

Kwa mfano, Mkoa wa Pwani unatajwa kuwa wa kimkakati ambapo una viwanda vingi vinavyozalisha bidhaa mbalimbali zinazotumika nchini. Hivyo basi, matukio ya mauaji na kupotea watu yanapotokea katika mkoa huo, yanatajwa kuathiri shughuli za uchumi na kuwatia hofu wawekezaji wenye viwanda, pamoja na wale wanaotarajiwa kuleta viwanda vipya latika mkoa huo.

Hali kadhalika Mkoa wa Simiyu unatajwa kupanda kwa kasi katika chati ya utekelezaji wa sera ya viwanda nchini, ukiwa na viwanda vya maziwa, nyama na chaki, lakini matukio ya mauaji ya watoto yanautia doa Mkoa huo na kuongeza wasiwasi miongoni mwa Watanzania.

Vyama vya siasa vinaweza kutumia ajenda ya usalama na kuwaeleza wananchi kuwa shughuli zao za uchumi na kujipatia pato, zinadhoofishwa na hali ya usalama duni, hivyo kuwaomba wawapigie kura na kushinda, ili waweze kulinda usalama wa raia, kama nilivyoeleza mwanzoni kuwa miongoni mwa masuala yatakayochukua nafasi kubwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Katibu wa Mwenezi na Mawasiliano wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amemwambia mwandishi wa makala haya: “Usalama wetu ni jambo la kuzingatia sana ili kuondoa mashaka kila nyanja, uchumi, jamii na siasa. Pia, hasa katika utekelezaji wa wajibu wa jamii katika ulinzi na usalama. Kwa sababu uwezo wa vyombo vya dola una mipaka bila jamii inayoshiriki kukomesha.”

Mwandishi amemuuliza kiongozi huyo iwapo chama chake kinatarajia kutumia suala hilo kama ajenda ya uchaguzi mkuu 2020, naye alisema: “Usalama kwa ujumla wake ni ajenda ya lazima.”

Kwa muktadha huo, suala la usalama wa raia na mali zao pamoja na usalama wa wawekezaji na rasilimali zao, ni jambo ambalo linagusa kila kona ya maisha ya wananchi.

CCM ambacho kimepewa dhamana ya kuunda serikali tangu mwaka 2015, kinawajibika moja kwa moja kuhakikisha na kuisimamia serikali yake kuwalinda wananchi. Vilevile serikali inatakiwa kutambua kuwa matendo yanayochafua taswira ya nchi, ni yale ambayo yanafumbiwa macho.

Ni rahisi kuvilaumu vyama vya upinzani ambavyo vinatarajiwa kutumia ajenda hiyo kuomba ridhaa ya wananchi na kukipaka matope CCM na serikali, kushindwa kuhakikisha usalama wa raia. Kama CCM na serikali yake havijisafishi kwa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na za wawekezaji, ni nani watamlaumu zitakapoibuliwa wakati wa uchaguzi mkuu ujao?