Home Makala Viongozi Afrika na ushindani wa kubadilisha katiba

Viongozi Afrika na ushindani wa kubadilisha katiba

2477
0
SHARE

Rais Alpha Conde wa Guinea.

HILAL K SUED

Imekuwa kama vile ushindani wa namna fulani vile – au pengine ni lana aliyoiteremsha Mungu Mwenyezi kwa bara hili. Lakini vyote viwili tafsiri ni moja – linapokuja suala la demokrasia Barani Afrika ni sawasawa na “tupa kule.”

Hakika inashangaza kuona viongozi Barani humu hawaoni, au kama wanaona, hawataki kabisa kujifunza yanayowapata viongozi wenzao wanaokuwa na uchu wa kurefusha vipindi vyao vya utawala zaidi ya vile vilivyowekwa na katiba za nchi zao.

Sasa hivi aliyeibuka na uchu huo ni Rais wa Guinea, Alpha Conde aliyeingia madarakani 2010 kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano bila kuongeza – kwa mujibu ya katiba ya nchi hiyo.

Kwa vile muda wake wa miaka 10 unamalizika mwaka huu tayari ameshaanza figisu za kutaka kuendelea kukaa madarakani – anapendekeza kubadilisha katiba y alum wezesha kugombea urais tena. Na sasa imekuwa mtindo – itapendekezwa kwamba badala ya miaka mitano iwe miaka saba na mabadiliko haya yaanze na yeye – hivyo atawale tena kwa miaka 14 mingine.

Haya si ya kutunga – yamefanyika kwa Paul Kagame, Pierre Nkurunziza na Yoweri Museveni kuhusu katiba za nchi zao. Wa mwisho kabisa wiki iliyopita tu ni Abdel-fattah al-Sisi wa Misri.

Waliokuwa marais wa Sudan na Algeria nao walikuwa katika michakato ya kujiongezea muda wa kutawala lakini wananchi wamewashtukia na kuwatolea nje – ‘nje’ kwa maana halisi.

Kuhusu Guinea – nchi ya Afrika Magharibi ambayo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi barani humu pamoja na utajiri mkubwa wa madini imekuwa na historia ya hovyo kiutawala. Katika nusu karne ya kwanza tangu kujipatia uhuru nchi hiyo ilitawaliwa na madikteta wawili – Ahmed Sekeu Toure na Lassana Conte, kila mmoja miaka 25, na wote wawili hao vifo ndiyo viliwaondoa madarakani.

Baada wa huyo wa pili kufariki mwaka 2008 nchi ikachukuliwa na jeshi lakini miaka miwili baadaye katiba ya kiraia ikapitishwa na Alpha Conde akashika urais. Anataka kuwapiku watangulizi wake Sekeou Toure na Lassana Conte.

Halafu uchu wa namna hii hauna umri, hivyo hatuwezi kusema watu kama akina Pierre Nkurunziza (Burundi) au Joseph Kabila (DRC) kutokana na ujana wao ndiyo pekee wangependa kukaa madarakani kwa muda mrefu zaidi.

Mwaka 2012, akiwa na umri wa miaka 86, aliyekuwa rais wa Senegal kuanzia 2000 Abdoulaye Wade alitaka kubadilisha katiba ili aendelee kugombea kwa kipindi kingine cha tatu cha miaka sita. Wananchi wakamtolea nje – nje kwa maana halisi.

Ajabu ni kwamba Wade aligombea urais wa nchi hiyo mara nne kuanzia 1978 na kushindwa kila mara, na alipoupata mwaka 2000 akatamani uwe urais wa milele.

Na kuna wengine huwa hata hawakumbuki au hawajali yaliyotokea kwa watangulizi wao wakati wanabadilisha katiba ili kuwaongezea muda madarakani. Kwa mfano, baada ya takriban miaka 30 ya utawala wa kikandamizi wa Hosni Mubarak, Wamisri walisema inatosha na wakaja juu kwa wingi katika maandamano ya kumtaka aondoke. Lakini sasa wamerudi kule kule.

Sote tunakumbuka maandamano ya 2011 ya kila siku ya halaiki ya watu katika Medani ya Tahriri (Tahrir Square) jijini Cairo, maandamano ambayo wananchi wengi walipoteza maisha katika mapambano na vikosi vya serikali. Baada ya Mubarak kusalimu amri na kung’atuka (na baadye kukamatwa) wengi tulitarajia kwamba ndiyo ulikuwa mwisho wa udikteta nchini humo. Lakini wapi – “ufarao” kamwe hawawezi kutoweka Misri.

Sasa hivi mwingine unainyemelea nchi hiyo – na eti kwa ridhaa ya wananchi. Wiki iliyopita rais wa sasa Abdelfattah alSisi aliyetumia jeshi kupora urais kutoka kwa mtangulizi wake Mohamed Morsi – rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, naye kafanya mabadiliko ya katiba ya kuondoa ukomo pamoja na kuongeza urefu wa vipindi hivyo akitaka atatawala hadi 2034. Na si hilo tu, mabadiliko hayo ya Katiba pia yanampa mamlaka rais katika michakato ya mahakama na pia jeshi kuingilia masuala ya utawala.

Na inadaiwa wananchi kupitia kura ya maoni iliyofanywa kwa spidi ya zimamoto, wameridhia ‘ufarao’ huo mwingine, miaka saba tu baada ya kufanikiwa kwa tabu kuuondoa ‘ufarao’ waliokuwa nao.

Halafu eti huyu mtu miezi kadha iliyoita alipewa uenyekiti wa umoja wa Afrika (AU) kwa kipindi cha mwaka mmoja – na hivi majuzi aliendesha kikao cha kamati ya umoja huo kuiadabisha Sudan – kwamba akina alBashir lazima wakabidhi madaraka kwa raia. AU nayo! Siku hizi imepoteza mwelekeo kweli kweli!

Katika nchi nyingi Barani humu kubadilisha katiba huwa rahisi pengine kuliko kwa mtu kubadilisha shati. Nchi kama Marekani ni nadra sana watu hata kufikiria kubadilisha katiba ya nchi kutokana na mchakato wake kuwa mgumu sana. Lakini Barani humu Katiba hubadilishwa – hasa kwa lengo la kuondoa ukomo wa vipindi vya utawala kutokana na takwa la yule aliye madarakani.

Lakini mara nyingi yeye huwa hatamki hivyo – ni kazi ya wapambe – hawa ni jamii hatari ya wakubwa wanaomzunguka rais na pia watu wengine anaowatuma kiaina ‘kupima joto’ au kufanya kampeni za kichini chini kuonyesha kwamba “wananchi wengi bado wanampenda, kafanya mengi makubwa” na blah blah nyingine nyingi.

Lakini pia hutokea kwamba marais hung’ang’ania madarakani kwa hofu ya kile kitakachompata akiondoka – hasa kutokana na “madhambi” aliyoyatenda. Hapo huwa hata haamini yoyote miongoni mwa maswahiba wake kisiasa kumuachia madaraka.

Baada ya miaka 38 madarakani, aliyekuwa rais wa Angola – Edouardo dos Santos hatimaye aliachia ngazi mwaka juzi (2017) na kumuachia swahiba wake wa karibu – aliyekuwa waziri wa ulinzi Joao Lourenco na hivyo kujihisi atakuwa salama nje ya madaraka.

Lakini haikupita muda rais mpya aliyeahidi kupambana na ufisadi kikweli kweli alianza kazi hiyo kwa kuigusa familia ya rais aliyemtangulia. Haikupita mwaka Jose Filomeno dos Santos, mtoto wa kiume wa dos Santos alitiwa mbaroni kwa tuhuma za ufisadi na utakatishaji fedha. Aidha binti wake wa kike Isabella dos Santos naye aliwekwa katika uchunguzi kuhusiana na utoroshaji fedha.

Hii inathibitisha kitu kimoja – kwamba iwapo kiongozi mpya ataingia madarakani na gia ya kupambana kwa dhati na ufisadi, basi ni vigumu vita hiyo kumuacha rais aliyetangulia, pamoja na familia yake. Ni vigumu sana.