Home Makala Wabunge wa kuteuliwa, mawaziri wanamwakilisha nani?

Wabunge wa kuteuliwa, mawaziri wanamwakilisha nani?

1066
0
SHARE

JOSEPH MIHANGWA

Unasikia kupitia vyombo vya habari kwamba Mbunge wa jimbo lako la uchaguzi kateuliwa kuwa Waziri; unafurahi kwamba “mwenzenu” kaukata.  Unaiangalia Katiba ya nchi na kugundua kwamba nafasi ya Waziri ni sehemu ya mhimili wa Utawala ambayo Kikatiba haipashwi kuchanganywa na mhimili wa Bunge [Ibara ya 4].  Unajihoji kutaka kujua kama kwa uteuzi huo jimbo lako bado lina mwakilishi Bungeni au la.  Na kama ni Waziri Mbunge, anamwakilisha nani?.

Haujapita muda, unasikia tena kupitia vyombo vya habari kwamba Rais kamteua rafiki yako mwingine kuwa “Mbunge wa kuteuliwa”, bila hata yeye kutarajia.  Haamini masikio yake kwa kuwa alikuwa hajawahi kufikiria hata kugombea au kuwaza kuwa Mbunge.  Lakini potelea mbali, anajipongeza kwa uteuzi wa kazi ambayo hajaiwazia wala kuitamani.

Hapo tena moyo unadunda, unapojihoji kutaka kujua kama kweli hiyo maana yake ni uwakilishi, rafiki zako hawa wawili wanamwakilisha nani, au mhimili gani Bungeni?. 

Unaitazama tena Katiba ya nchi, unaona uteuzi huu umefanywa kukidhi matakwa ya mteuzi, yaani Mtawala. Ingawa Wanasheria watakwambia kwamba sehemu ya Utangulizi [Preamble] ya Sheria yoyote haihesabiwi kama ni sehemu muhimu ya Sheria hiyo, lakini unaendelea na msimamo wako kwamba sehemu hiyo ni muhimu [katika Katiba] kwa sababu inaelezea na kufafanua misingi na madhumuni ya kutungwa kwa Sheria hiyo, hapa kwa maana ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977. Unauangalia Utangulizi wa Katiba hiyo na kusoma: “Na kwa kuwa [misingi ya Katiba hii] yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake husimamiwa na bunge lenye Wajumbe waliochaguliwa na linalowakilisha wananchi…”

Unabaini kuwa, kumbe Serikali yetu inapashwa kusimamiwa na Bunge lenye Wabumge waliochaguliwa kuwakilisha wananchi pekee, na si kuwakilisha utawala. Unazidi kujiuliza, “Kwa kuwa rafiki yako si Mbunge wa kuchaguliwa, je, huyo ni Mbunge halali au ni Mbunge kivuli?.  Anamwakilisha nani?”

Unatafiti kujua mtindo huu wa Bunge kuwa na Wabunge wasiowakilisha watu ulitoka wapi hapa nchini.  Unabaini kuwa hata ule UTANGULIZI wa Katiba ya Uhuru [The Independence Constitution] ya 1961 na Katiba ya Jamhuri [The Republican Constitution] ya 1962, unafanana na utangulizi wa Katiba ya sasa, lakini enzi hizo hapakuwa na uteuzi wa mlolongo wa Wabunge kama ilivyo sasa.  Unabaini kwamba uteuzi huu una lengo la kulipunguzia Bunge nguvu ili sauti ya wananchi izamishwe na sauti ya Wabunge wanaoitika kwa mhimili wa utawala!.

Unabaini pia kwamba, mtindo huu ulipoanza mwishoni mwa miaka ya 60, ulipata upinzani mkubwa Bungeni, pale Mbunge wa Iringa Kusini, Mheshimiwa Chogga aliposema: “Mheshimiwa Spika, siafiki mtindo huu wa uteuzi wa Wabunge; siuamini hata kidogo mtindo huu.  Inapotokea mtu mmoja kumteua mwingine [kuwa Mbunge], anayeteuliwa lazima afuate na akubali yote ya aliyemteua. Nani asiyejua usemi kwamba “amlipaye mpiga zumari ndiye huchagua wimbo”?.  Alihoji.  [Soma Hansard, Julai 12, 1968]

Unaendelea kujiuliza, Bunge ni nini?  Mbunge ni nani?  Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kuiangalia kwa kifupi tu nafasi na mantiki ya Bunge katika Serikali staarabu na ya kidemokrasia. Mwanafalsafa wa Kifaransa, Baron Montesquieu, aliwahi kuandika katika Kitabu chake kiitwacho, “The Spirit of Laws” [1748] kwamba, katika Serikali yoyote yenye demokrasia ya Kiliberali, kuna nguzo au Mamlaka kuu tatu:  Bunge, Utawala na Mahakama.

Anafafanua kwamba, kazi ya Bunge ni kutunga Sheria zinazoongoza nchi na Watawala, ambapo kazi ya Utawala ni kutekeleza Sheria hizo [ikiwa ni pamoja na Katiba]; bila ya hiari. Chini ya mantiki hii ni kwamba, katika nchi ya kidemokrasia, Serikali madarakani [Utawala] inakuwapo kutekeleza Sheria na matakwa ya Bunge [ibara 34 (2) na 64 (1)], ambapo Mahakama zinakuwapo kutoa haki [kwa kutumia Sheria za Bunge] bila ya woga au upendeleo [ibara 13 (3)]

Mtindo huu wa Serikali kuwajibika kwa Bunge katika kutenda kazi zake unafuata mfumo wa Bunge wa Westminster tuliorithi kutoka Uingereza. Ni kwa mantiki hii pia kwamba, Desemba 11, 1961, siku mbili tu baada ya Uhuru, Bunge la Tanganyika huru chini ya mfumo huu, lilizinduliwa na mwana wa Mfalme wa kiume wa Uingereza, [Prince] Philip kwa niaba ya Malkia Elizabeth wa II, na Tanganyika ikapokelewa kuwa mwanachama wa Jumuia ya madola hadi leo.

Chini ya mfumo huu wa Kibunge, kila Waziri aliwajibika kwa Bunge kuhusu kazi za Wizara yake; nao Mawaziri katika ujumla wao, waliwajibika kwa Bunge na kwa Mkuu wa nchi kuhusu sera kuu za Serikali.  Utaratibu huu unapaswa kuzingatiwa hadi leo.

Naye Gavana [baadaye Rais] alipashwa kufuata ushauri wa Baraza la Mawaziri na ushauri wa wengine waliotambulika kisheria.  Leo, Rais hawajibiki kufuata au kukubali ushauri wa mtu au chombo chochote anapotekeleza shughuli zake za Serikali [Ibara ya 37 (1)].

Enzi hizo, Miswada ya Sheria, ilichambuliwa na kujadiliwa kwa kina Bungeni bila ya uoga.  Waziri Mkuu na wenzake hawakufanya mzaha Bungeni, Spika vivyo hivyo, hakuwa ndumila kuwili kwa hoja za Wabunge.  Nayo Serikali iliwajibika Kikatiba na kikweli kweli kwa Bunge, tofauti na ilivyo sasa.

Pius Msekwa, Mtanzania mweusi wa kwanza kushika wadhifa wa Katibu wa Bunge mwaka 1962, anakiri katika kitabu chake “Towards Party Supremacy” [1977], kwamba “Bunge la uhuru liliheshimika kwa Watawala na kwa wananchi kwa ujumla, sio tu kama chombo cha kutunga Sheria, bali pia kama taasisi ambayo watu, kupitia wawakilishi wao, walitumia haki yao ya kutoa mawazo na maamuzi yaliyogusa maisha yao na uongozi wa nchi”.

Anasema, “Chini ya mfumo huu, Chama cha Siasa hakipewi nafasi ya kuingilia au kufifisha kazi na madaraka ya Bunge”.

Kazi ya Mahakama kwa upande wake, ni kutafsiri sheria, kuziba au kusahihisha mapungufu ya Sheria, kuzuia matumizi mabaya ya Sheria kwa watawala; na kwa Mahakama kuitumia Sheria bila woga bila kuingiliwa na mhimili mwingine.

Mfumo huu wa mhimili mmoja wa Serikali [Bunge, Utawala au Mahakama] kutoruhusiwa kuingilia utendaji kazi wa mhimili mwingine huitwa “Mgawanyo wa Madaraka”.  Huu ni msingi mkuu wa dhana ya Utawala wa Sheria, demokrasia na utawala bora. Montesquieu, katika kitabu chake anabainisha kwamba, haki na uhuru wa mtu mmoja utakuwa hatarini iwapo mtu mmoja huyo ataachiwa kutekeleza mamlaka yote, yaani Kutunga Sheria, Kuzitekeleza, kuzitafsiri na kuhukumu.

Mwandishi bingwa katika Sheria ya Katiba A. Dicey, anabainisha kwamba, Bunge ni chombo cha kutunga Sheria; ni mhimili mkuu katika Serikali yoyote, kama tulivyokwishaeleza hapo juu, kwa sababu Bunge ndilo linalotunga Sheria za kusimamia utawala na kuongoza nchi.

Kwa sababu mihimili ya Utawala na Mahakama inaundwa na kuendesha shughuli kwa Sheria za Bunge, umuhimu huu wa Bunge dhidi ya mihimili mingine kwa misingi ya demokrasia na Utawala bora hujulikana kama “Ukuu wa Bunge” [Parliamentary Supremacy].

Ukuu wa Bunge unasimama kwa miguu miwili; kwanza, kwamba hakuna jambo ambalo Bunge linashindwa kufanya.  Inasemekana katika kutekeleza wajibu wake, “Bunge laweze kufanya kila kitu isipokuwa uwezo wa kumfanya mwanaume kuwa mwanamke, na mwanamke kuwa mwanaume”.  Pili, ni kwa nafasi yake, Bunge halina mshindani.

Tusije tukapotea njia juu ya lengo la makala hii; sasa turejee kwenye swali letu la awali: Je, Mbunge anapokuwa Waziri anamwakilisha nani?

Mbunge ni mwakilishi wa watu Bungeni chini ya dhana ya Utawala kwa njia ya uwakilishi,

[representative democracy]

kwa kuwa ni haki ya mwananchi kushiriki katika shughuli za Serikali.  Mbunge kama mwakilishi wa wananchi anawajibika kwa waliomchagua na si kwa Serikali, kwa maana ya mhimili wa Utawala.

Waziri, kama sehemu ya mhimili wa Utawala, anawajibika kwa Rais na ni mtetezi wa Utawala [Serikali] Bungeni; kwa hiyo hawezi kuihoji Serikali hata kwa kero alizotumwa kuhoji na waliomchagua; akifanya hivyo atakuwa amekiuka miiko ya kazi yake na atafukuzwa Uwaziri [Ibara ya 53 (2)]. Mpaka hapo, haihitaji kukuna kichwa kufahamu kwamba, Mbunge anapoteuliwa kuwa Waziri, anakoma kuwa mwakilishi, wala hawajibiki tena kwa wananchi waliomchagua.  Hiyo ni sawa na kusema kwamba jimbo “lake” linakuwa halina mwakilishi.

Uteuzi wa Mawaziri, pamoja na ule wa “Wabunge wa kuteuliwa”, ni kuteka nyara demokrasia ya Bunge kwa kujaza “Wabunge” bungeni wasiowakilisha wala kuwajibika kwa wananchi. Udhaifu huu upo pia kwa nafasi ya Spika wa Bunge. Tunaambiwa Spika lazima awe Mbunge au mtu yeyote mwenye sifa ya kuwa Mbunge na atokane na Chama cha siasa.  Kwa nini atokane na Chama cha siasa wakati Bunge si chombo cha siasa bali kinachotetea Katiba ya nchi?.  Kwa nini iwe hivyo wakati Katiba ya nchi si Katiba ya Chama cha siasa?.

Demokrasia haina Chama cha siasa.  Sharti la Spika kuwa atokane na Chama cha siasa ni uzushi na ndicho chanzo cha malumbano ya Kisiasa na Uchama usiotakiwa Bungeni unaoua umakini wa Wabunge na Bunge.

Mtindo wa kuwateua Wabunge kuwa Wenyeviti wa Mashirika au asasi za umma ni ugonjwa mwingine sugu unaodhalilisha hadhi ya wabunge licha ya kwamba mtindo huu ni kinyume cha Katiba ya nchi, inayolitaka Bunge kuwa msimamizi wa Serikali katika utekelezaji sera, na si Serikali kusimamia Bunge.

Itawezekanaje kwa Mbunge ambaye wakati huo huo ni Mkuu wa asasi ya umma, kuweza kuiwajibisha asasi anayoiongoza na Watendaji wake?  Yote haya yanaonyesha jinsi tabaka la watawala lilivyopania tangu enzi za uhuru, kufifisha harakati za wananchi za ujenzi wa demokrasia ya kweli.

Dhana ya “Mgawanyo wa Madaraka” ndiyo hati miliki pekee ya utawala bora, Demokrasia na Utawala wa Sheria kwa wananchi.  Lakini, pamoja na kuipenyeza dhana hii katika Katiba yetu [Ibara ya 4], sambamba na kuridhia Mkataba wa Kimataifa juu ya wa Haki za Binadamu [Bill of Human Rights], vioja vya demokrasia vinavyojitokeza sasa, kama kile cha malumbano na kutishana kati ya Mawaziri na Wabunge Bungeni; vinaonyesha jinsi tunavyoimba Utawala bora kama Kasuku, na kuugeuza bango la kuvutia misaada kutoka kwa wafadhili wakati utawala bora haupo.

Maendeleo ya nchi hayaji kwa njia ya vitisho na matumizi ya vyombo vya dola; bali huletwa na watu kwa kuwashirikisha katika maamuzi ya kitaifa, badala ya kuwafanya watazamaji tu wa “mchezo wa kuigiza” nje ya uzio.

Watashiriki vipi katika maamuzi ya kitaifa wakati wawakilishi wao – Wabunge wamewahama na kujiunga na tabaka la Watawala kama Mawaziri; wamegeuka “ndumila kuwili” wapate kula matunda ya uhuru, wananchi wakipiga miayo?

Watashiriki vipi wakati Bunge lao limelemewa mzigo wa Wabunge wa kuteuliwa bila ya ridhaa yao,  wasiowakilisha matakwa yao wala kuwajibika kwao?.

Ili demokrasia kwa njia ya uwakilishi iwe na maana kwetu, kuna haja ya kuipitia upya dhana nzima ya demokrasia ya Uwakilishi na Utawala bora, sio kwa mantiki tu ya kupunguza ukubwa wa Bunge na hivyo gharama kwa nchi, bali pia kuimarisha demokrasia na uwakilishi wa kweli wa wananchi ndani ya Bunge.