Home Makala Wanaoitaka ripoti ya IMF hawatutakii mema

Wanaoitaka ripoti ya IMF hawatutakii mema

2101
0
SHARE


Joseph Mihangwa

NASHINDWA kabisa kuwaelewa wote. Watanzania kwa wasio Watanzania, wanaotaka Serikali iruhusu kutolewa hadharani kwa taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) juu ya hali ya na utekelezaji wa sera za kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu kipindi cha mwaka wa fedha uliopita, tukifahamu kwamba kwa uhusiano wa IMF na nchi za dunia ya tatu kama yetu ni sawa na uhusiano wa Fisi na Mwanakondoo.

Natamani kutwanga hedi yeyote anayetaka kutusogeza karibu na IMF tukijua ni sera za Shirika zilizofilisi nchi na dira ya maendeleo kutufikisha hapa “jehanamu” tulipo, lakini narudi nyuma kuogopa vijana wa Kangi Lugola kunidaka kwa kosa la kupigana hadharani.

Nabaki kuumia bila machungu, nikijihoji:  hivi nani katuroga Watanzania; kwamba, kama mwaka 1978 Mwalimu Nyerere aliwatimua Mitume wa IMF walipofika kumuuzia sera zao dhidi ya sera zetu za kiutu, usawa na ubinadamu, hawa Mitume wa kuumba leo wanataka kutuambia nini?.

Sera za pacha wawili-IMF na Benki ya Dunia [WB] zimeshindwa na kufukarisha nchi si yet utu popote zilikojaribiwa na sasa zinapigwa vita dunia nzima, iweje sisi tulilie kupimwa kiuchumi kwa sera za Mumiani hao na mawakala wa ukolonio-mamboleo?.

Juhudi zote za Serikali ya sasa inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ni kuinua uchumi na maisha ya Mtanzania kwa kuasi sera za mumiani hao, iweje leo kuna miongoni mwetu wanaotaka juhudi hizi zichafuliwe kwa njia ya picha na taarifa ambayo haitashabihiana na mazingira, dira ya maendeleo na Tanzania tunayotaka?. Kama kuna msomi yeyote anayeshabikia jambo hili, basi, huyo ni mmoja wa mamluki na wakala wa ubeberu wa kimataifa anayestahili kufungwa jiwe shingoni na kutoswa baharini kuepusha dhoruba chomboni kwa “laana” yake.

IMF ni Mtume wa nguvu za giza asiyepaswa kuchekewa. Tumepeleka wapi ujasiri wa kukemea pepo mchafu huyu uliotupaisha hadhi na heshima kimataifa kama Taifa lenye kuongozwa kwa sera za usawa, utu na haki za binadamu?. Historia inatuambia nini juu ya “Injili” ya IMF?.

Zaidi kidogo ya karne moja iliyopita Wazungu, waume kwa wake, walijimwaga kupenya ndani ya bara la Afrika kwa jina la Ukristu kutafuta walichokitaka.  Kwa azma kubwa na bila ya kujali maisha yao na hofu ya kutojua kilichokuwamo ndani ya “bara hilo la giza”, walivumilia magonjwa na adha mbali mbali ili kuleta “mwanga wa imani [ya Kikristu] na ustaarabu” kwa watu, kama walivyodai, waliokuwa “nusu ya wanyama”, waliogubikwa na umasikini, “ushamba” na imani potofu.

Mafanikio ya Wazungu hawa [inavyodaiwa], yalikuwa ni “kuvumbuliwa kwa nchi mpya”, ambazo mwanzoni zilijulikana kwa wenyeji tu, kuletwa kwa sayansi ya kisasa, ustaarabu, magonjwa mapya na elimu ya Ki-Magharibi.

Ingawa walikuja kwa jina la kueneza dini, lakini ukweli walikuwa sehemu ya nyenzo za ukoloni barani Afrika, kama walivyokuwa wavumbuzi, wafanyabiashara, na wanajeshi wavamizi. Hawa wote, licha ya kuwa mawakala wa ukoloni mkongwe, ndio pia waliofungua milango kwa mfumo wa uchumi wa kinyonyaji wa kikoloni.

Katika kipindi cha miaka 58 ya uhuru wetu, kumeibuka dini mpya inayohubiriwa na kizazi kipya cha “Wamisionari” wapya wa Ulaya, na imeenea kwa kipimo cha mapana na marefu ya taifa letu.  Wakati hapo zamani imani ilikuwa juu ya Kristu na ukombozi, lakini chini ya dini mpya, imani ni “maendeleo” chini ya mwavuli wa utandawazi; na njia ya ukombozi ni misaada kutoka nje.

Wakati zamani tulifundishwa kusali:  “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, utupe leo mkate wetu wa kila siku, utusamehe makosa yetu, utuopoe maovuni”; leo tunafundishwa kusali:  “Baba yetu uliyeko huko Amerika na Ulaya; jina lako litukuzwe, utandawazi wako uje, ufalme wako utawale, kama ilivyokuwa enzi za ukoloni, utupe leo dola [fedha] yetu,  misaada na ushauri kwa maendeleo yetu; tufundishe kuwa wanyenyekevu na watiifu kwako; tupe nguvu za kuwashinda wanaopinga sera na utamaduni wako; njoo bwana ututawale, milele na milele – Amina”.

Wamisionari wa zama hizi ni Mashirika ya kimataifa chini ya Mtandao wa Bretton Woods, yakiwamo Benki ya Dunia [WB] Shirika la Fedha la Kimataifa  [IMF], Shirika la biashara la Kimataifa [WTO], Shirika la Chakula duniani [FAO] na mengineyo yaliyozikaba koo chumi za nchi za dunia ya tatu.

Kwa hadaa tupu, lengo la “Wamisionari” hawa, kama wanavyodai, ni kuziinua nchi hizi kutoka katika dimbwi la umasikini kwa njia ya misaada na ufadhili, kuzipa utamaduni wa Kimagharibi na kuzielimisha juu ya namna ya kutajirika na kujikomboa kiuchumi.

Zamani, tulifundishwa jinsi ya kuutua mzigo wa dhambi kwa njia ya toba; sasa tunaambiwa kuutua mzigo wa deni ni kwa njia ya misaada kutoka nje na kulipia madeni ya zamani.

Kama ilivyokuwa zama za karne zilizopita, Afrika, pengine kuliko eneo lingine lolote la dunia ya tatu, limebakia uwanja wa mazoezi ya kupiga shabaha kwa shughuli za “Kimisionari”.  Kwa nini?

Ni Cecil Rhodes, Mbeberu mahiri wa ukoloni wa Kiingereza, aliyetoboa siri ya Umisionari huu mwaka 1895 aliposema, “Ili kuwaepushia Waingereza milioni 40 vita ya umwagaji damu ya wenyewe kwa wenyewe, sisi mabingwa wa ukoloni, lazima tupate maeneo na ardhi mpya kuweza kuwahamishia huko watu wetu wa ziada; na pia tuweze kujipatia masoko kwa bidhaa tunazozalisha Viwandani na katika migodi.  Ukitaka kuepuka vita ya wenyewe kwa wenyewe, lazima uwe M-beberu”.   [Nukuu hii ni kutoka kitabu cha V.I. Lenin, “Imperialism:  The Highest Stage of Capitalism”]

Ni kwa mtazamo huu kwamba, dunia ya ubepari mkongwe, hasa nchi zenye Viwanda maarufu kama G.20, hazilali usingizi kwa kukuna bongo kufikiri kwamba, kama nchi masikini kama Tanzania zitaachwa kujifia hivi hivi kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayozikabili, “Wamisionari” hao wapya watakosa waumini wa kuwaimbia sala na soko la bidhaa zao.

Kwa hiyo dawa inayopikwa ni ya kuwainua walioanguka japo kwa kuwafanya waimbe utukufu wa Umisionari huo, kuwashika mkono watembee japo kwa kuchechemea, kuwanywesha uji usio na lishe wapate nguvu kidogo kuubeba mzigo wa deni, na kuwachoma sindano ya ganzi kuuwa maumivu kwa mzigo mzito wanaobebeshwa, waendelee kuitikia “Amina”.

Ubeberu, kwa mujibu wa Lenin, hauna maana tu ya unyakuaji wa nchi ya wengine unaoweza kufanywa na mataifa yenye nguvu; au kudhibitiwa kwa uchumi wa nchi na mataifa ya kigeni.  Ubeberu ni pamoja na wafadhili kuhodhi hatamu za tafsiri halisi ya maendeleo ya nchi inayofadhiliwa.

Injili ya Wamisionari wapya inatueleza kuwa, sisi tu masikini kwa sababu tumekosa maarifa na mwelekeo, na hivyo lazima tuisikie Injili ya “ukombozi”.  Tunaambiwa, tujikane kila siku eti kwa kuwa hatufai kitu; utajiri wetu ni takataka, ila tu pale unaposhikwa na wageni.  Angalia wanavyotusema:  Lester Thurow, katika kitabu chake “Head to Head” anasema, “Afrika haiwezi kuwa Mmbia katika uchumi wa dunia kwa sababu bara hili ni takataka tu zinazopaswa kutupwa na kuoza.  Kama Mungu angekupatia bara hili uwe mmiliki wake kiuchumi; njia pekee ya busara ni kulikataa na kumrudishia [Mungu] bara lake”.

Injili hii, inayotaka tujikane wenyewe na utu wetu, inaweza kufananishwa na sehemu ya Injili ya Wamisionari wa kale, yenye kutupoza tusipambane:  “Heri walio masikini maana ufalme wa mbingu ni wao; Heri wenye huzuni, maana hao watafarijika; Heri wenye njaa, maana watashibishwa” [Matayo 5: 3-10].  Kwa vipi na mpaka lini tutaendelea kuimba “Heri” hizi?

Kenichi Ohmae, katika kitabu chake “The Borderless World: Power Strategy in the Interlinked Economy”, anahubiri kwa kusema: “Katika dunia ya leo, matakwa ya taifa hayana maana tena kama yalivyo matakwa ya kiuchumi yasiyojua mtu”.

Hapa tena, Wamisionari wapya hawataki tujitegemee wala kutetea maslahi ya taifa.  Harakati zozote zinazolenga kuwaamsha wazalendo kudai haki zao au kujinasua kutoka kwenye unyonyaji na ukandamizaji, huchukuliwa kama dhambi mbele ya “Mungu” huyo mpya; na kwamba, wanaofanya hivyo ni mashetani, wapinzani wa injili ya utandawazi na Wakomunisti.

Kama Waisraeli mateka huko Babeli, walivyolazimishwa kumtii na kumwimbia Mungu katili wasiyemjua, nasi tunalazimishwa kutii masharti ya IMF na WB kwa sala ifuatayo:  “Dhambi nilizotenda sizijui; makosa niliyotenda siyajui; Nioshe mungu wangu [IMF/WB] dhambi zangu nisizozijua; hata kama ni kubwa sabini mara sabini”.  Waafrika tuna dhambi gani hata tulazimike kupiga magoti  kwa IMF na WB, kuomba toba kwa kushindwa kwa uchumi wetu unaovurugwa na miungu hao hao?.

Injili hii mpya inaweza kufananishwa na Injili ya kale inayowaonya wanaojijali:  “Yeye aipendaye nafsi yake, ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu [wa utandawazi] ataisalimisha” , [Yohana 12: 35].

Tofauti na Wamisionari wa kwanza, waliokataza kukopesha kwa riba kwa kuagiza:  “Tendeni mema, na kukopesha; msitumaini kupata malipo [riba] na thawabu yenu itakuwa nyingi” [Luka 6:35]; Wamisionari wa leo wana kiu ya mali, biashara na faida  [Paul Kennedy:  Preparing For the Twenty First Century, tulivyoeleza hapo juu].

Tujiulize:  Kuna ukweli gani kwamba nchi tajiri [the G.8] na za Viwanda [G. 20] zinafadhili nchi masikini kwa moyo mweupe, ukizingatia jinsi zilivyopora, na zinaendelea kupora na kutorosha utajiri wa nchi masikini, tangu enzi za Wamisionari wa kwanza?  Nani anamdai nani, kati ya nchi tajiri na nchi masikini?

Ukweli, nchi masikini ndizo zinazozidai nchi tajiri; lakini kwa kuwa tumefundishwa kujikana wenyewe na kufumbwa macho kwa njia ya “heri” tatu, haya yote hatuyaoni, tumepofushwa sisi na viongozi wetu, hatuna wa kutumulikia njia.

Chukua mfano tu wa Amerika, taifa lenye nguvu na tajiri kuliko yote duniani:  utajiri wake unatokana na unyonyaji wa jasho la mababu zetu waliochukuliwa utumwa kutoka Afrika enzi za biashara ya watumwa; wakafanyishwa kazi za suluba katika mashamba makubwa ya Mamwinyi, chini ya mazingira magumu ambayo ni Mwafrika pekee aliyeweza kuyamudu.

Hata biashara ya watumwa ilipopigwa marufuku kufuatia mapinduzi ya Viwanda, ni  Waafrika hawa, au mababu zao, waliohenyeshwa kwa uzalishaji Viwandani, chini ya mazingira magumu.  Utajiri huu ndio umeiwezesha Marekani kukwea juu ya nchi zote zilizoendelea, kiuchumi na kijeshi.

Jiulize:  kama bidhaa za Viwanda zinazoletwa katika nchi zetu zingeweza kuzungumza; kama mashine na mitambo yote ingesema, kama teknolojia ya nje na huduma kutoka nchi zilizoendelea zingesema; kama ubaranganyaji wa kalamu, kati ya nchi hizo na watawala wetu ungesema jinsi tunavyoibiwa; kama tungezinyang’anya nchi zilizoendelea yote haya na mengine zinayopata kutoka nchi masikini, bila ya shaka yoyote zingegeuka kuwa “omba omba” kama tulivyo sisi hivi leo.

Ni ukweli usiopingika kwamba nchi za dunia ya tatu ni soko kuu la bidhaa za dunia ya kwanza kwa shinikizo, kiasi kwamba hata bidhaa zisizofaa, au zile zisizoendana na mahitaji sahihi kwa maendeleo ya watu wetu, hutupwa kwetu kwa nguvu; kazi ya kuamsha hamasa na uchu mpya wa kuzinunua hufanywa kwa shuruti, na kwa kuwatumia watu wetu hao hao wanaodai kutuongoza.

Kwa mfano, nani anahitaji nywele za bandia, vichubua ngozi na bidhaa kama hizo zisizo mantiki kwa jamii ya Kiafrika?  Nani anahitaji mfumo wa demokrasia na uchumi wa Ulaya, badala ya ule wa Kiafrika-Ujamaa?

Fanya hesabu kuona faida nchi hizo zinayopata kutoka soko la nchi masikini; utaona kwamba kile kinachoitwa “mikopo” au “misaada” kutoka nchi tajiri ni tone tu toka ndani ya bahari.  Ni sehemu tu ya kile tunachoporwa kwa mkono wa kulia na “kufadhiliwa”  kwa mkono wa kushoto.

Angalia jinsi mfumo wa kibiashara wa Kimataifa ulivyo; unaziwezesha nchi tajiri kununua mali ghafi [pamba, kahawa, korosho] madini na mazao mengine kwa bei ya chini kutoka kwetu, lakini kinyume chake, zinauza kwetu bidhaa zake kwa bei ya juu mara dufu kama njia ya kutukomoa.  Kile kidogo tunachopata kwa kuuza bidhaa zetu huisha kwa kununua bidhaa chache [za bei ya juu] kutoka nchi hizo.

Zaidi ya hayo, nchi tajiri zinalinda soko la bidhaa zake kwa kutoa ruzuku kwa wazalishaji wake, lakini tunapotaka kufanya hivyo kwa watu wetu, IMF na WB wanang’aka:  “Mnapotaka misaada yetu, msilinde soko la bidhaa zenu, wala msitoe ruzuku”.  Ukweli ni kwamba, Injili ya WB na IMF si ya ukombozi, bali ni ya kutupeleka Jehanamu.

Hili linaloitwa “deni la nje”, si deni halali, na ni vyema nchi masikini zikaungana kutaka lifutwe, ikizingatiwa kwamba nchi hizo tajiri hazijaweza kufidia kikamilifu utajiri ziliopora na zinazoendelea kupora kutoka nchi masikini. Kwa upande mwingine, vikundi vya wajanja wachache kutoka nchi zinazotoa misaada, kwa kushirikiana na wazalendo wachache [wanaojiita wasomi na wanasiasa], ndio wanaotumbua fedha za misaada hiyo; lakini wanaolipa deni ni wakulima na wafanyakazi.