Home Maoni Wastafu EAC waendelee kukumbukwa

Wastafu EAC waendelee kukumbukwa

2630
0
SHARE

TUNAKIPONGEZA kitendo cha Rais John Magufuli cha kumzawadia Rubani Peter Mapunda fedha pamoja na kutambua mchango wake kwa taifa hili.

Kitendo chake cha kutorosha ndege aina ya Boeing kutoka uwanja wa ndege wa Kenyatta, Kenya, na kuileta Dar es Salaam ni cha kishujaa na kizalendo.

Pamoja na kwamba, uongozi wa lililokuwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAA), uliamuru kwamba ndege zote zirudishwe makao makuu Nairobi, Kapteni Mapunda, kwa vile alikuwa ndiye rubani wa ndege hiyo, akafanya uamuzi wa haraka — kuirusha ndege hiyo Tanzania.

EAA, pamoja na mashirika mengine kama vile la reli (EARC) ilikuwa inamilikiwa na nchi tatu zilizounda Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya awali (EAC) na wakati wa tukio hilo kulikuwa na kusigana kimtizamo wa kisiasa katika Jumuiya hiyo hadi kusababisha kuvunjika mwaka 1977.

Msigano mkubwa ulikuwa kati ya Kenya na Tanzania, Kenya wakiamini kwamba wao ndio walikuwa wanaiendesha EAC, wakati haikuwa kweli. EAA kwa mfano, ilikuwa na viwanja vingi vya ndege ndogo ndogo nchini Tanzania kuliko Kenya na Uganda.

Kwa upande wa reli kadhalika, Tanzania ilikuwa na mtandao mpana wa reli — Mwanza, Kigoma-Dar es Salaam, Dar-Tanga – Moshi hadi Arusha, lakini makao makuu ya Shirika la Reli Africa Mashariki (EARC) yalikuwa Nairobi. Ni katika mazingira hayo, Kapteni Mapunda akaamua kurudisha ‘kiduchu’ nyumbani—alikuwa amehamasika.

Kitendo cha Rais Magufuli kumkumbuka Kapteni Mapunda, hata kama asingempa fedha, kinatosha kumpa faraja kwamba Taifa bado linamuenzi. Mapunda sasa aingizwe kwenye kundi la watu mashujaa, walioweka maslahi ya taifa mbele.

Bila shaka Kapteni Mapunda si Mtanzania pekee aliyeweza kutenda matendo ya kishujaa, tunaamini wapo wengine ambao nao kwa nafasi na maeneo yao waliweza kuisaidia nchi kutopoteza mali za EAC.

Aidha wapo wastaafu wa iliyokuwa EAC iliyovunjika mwaka 1977, kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wanasotea mafao yao. Mafao hayo yalitokana na mgawanyo wa mali na madeni ya EAC yalikabidhiwa serikali za kila nchi za Jumuiya kuwalipa wastaafu hao.

Mwaka 2005 Serikali ilikubali kuwalipa, lakini ilifanya hivyo si kwa kiwango na kikotoo kilichokuwa kimeaanishwa na Tume iliyopewa jukumu la kugawanya mali za EAC, wakati serikali za Kenya na Uganda ziliwalipa wastaafu wao kwa kiwango stahiki.

Wengine wamefariki bila kupata mafao yao, wengine bado wapo, ni wazee na maisha yao ni ‘choka mbaya’. Ni wazee waliolitumikia Taifa letu katika mashirika, idara na taasisi zingine zilizokuwa chini ya EAC kama vile Shirika la Reli (EARC), Shirika la Bandari (EAHC), Shirika la Posta na Simu (EAPTC), Idara ya Ushuru wa Forodha (EA Customs) na mengine.

Tunamwomba Rais Magufuli, kwa moyo ule ule uliomwona Kapteni Mapunda, aliangalie kwa huruma suala la wazee wastaafu wa iliyokuwa EAC. Wazee hawa ndio waanzilishi wa mashirika ya huduma nchini mwetu baada ya kuvunjika kwa EAC, walifanyakazi kwa uzalendo mkubwa na kuwaaibisha waliokuwa wanasema wao ndio Jumuia.

Sio siri tena kwamba mafao ya watumishi hao ambayo walitakiwa wayapate, yalihodhiwa na Serikali kwa kuwa wakiingia katika utumishi wa umma na Serikali ikatumia fedha zile kwa kazi ya kitaifa vile vile.

Awamu zote zilizopita, tunadiriki kusema kwamba hazikuwatendea haki wastaafu hawa. Tunaomba Serikali hii ya awamu ya tano, ifanye tofauti — iwalipe wazee hao na imalize suala hili ambalo linaitia doa Tanzania — kwamba haiwathamini wazee walioitumikia kwa moyo mkubwa na uzalendo.

Wazee hawa warudishiwe matumaini ya kuimba tena: Tanzania, Tanzania Nakupenda kwa Moyo wote kama anavyoimba Kapteni Mapunda sasa!