Home Latest News Milango kwa wanawake kuitawala dunia imefunguka

Milango kwa wanawake kuitawala dunia imefunguka

6637
0
SHARE
Theresa May

NA TOBIAS NSUNGWE,

UPEPO wa kisiasa unavyoendelea hivi sasa duniani umenifanya nisiamini tena msemo umsemao mwanamke akiwezeshwa anaweza. Sasa nimebaini wanawake wakifanya juhudi na kuungwa mkono na jamii, wanaweza bila ya kuwezeshwa na mtu yeoyote.

Hivi sasa wapo wabunge wengi wanawake wanaowakilisha majimbo.

Mwaka 2006 nchi ilipata Waziri wa kwanza mwanake wa Fedha, Zakia Meghji. Hii ni nafasi kubwa sana. Mama huyu alishika wadhifa huo hadi mwaka 2008. Baadae Saada Mkuya akawa mwanamke wa pili kushika nafasi hiyo mwaka 2015.

Tanzania imepata kuwa na Spika wa Bunge mwanamke, Mama Anna Makinda (68). Mama huyu ambaye amekuwapo kwenye siasa za ushindani kwa miaka 40 alishika wadhifa huo kati ya mwaka 2010 na 2015. Kabla ya hapo alikuwa Naibu Spika na amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Waziri katika wizara kadhaa.

Februari mwaka 2007 nchi lipata heshima kubwa katika siasa za kimataifa baada ya Dk. Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Msomi huyo pia amewahi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Sasa tunae Naibu Spika mwanamke kijana kabisa, Dk. Tulia Ackson (40) ambaye nyota yake inang’ara pamoja na changamoto za hapa na pale ikiwamo kutokubalika na baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzania wakiwamo wanawake!

Tangu wanawake waanze kupigania kupata nafasi kubwa katika nafasi za uongozi wa juu, pengine mwaka jana ndio ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa wanaharakati wa maendeleo ya wanawake.

Mama Samia Suluhu Hassani (55) aliteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea mweza wa Dk. John Magufuli. Hatimaye historia iliandikwa pale alipoapishwa kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke Novemba 5, mwaka jana baada ya CCM kushinda uchaguzi mkuu.

Bado mapambano yanaendelea ili kutimiza ndoto ya baadhi ya watanzania kuona rais au waziri mkuu mwanamke siku zijazo.

Katika bara la Afrika jirani zetu Malawi walipata rais mwanamke, Joyce Banda ambaye alidumu toka April 7, 2012 hadi Mei 31, 2014 aliposhindwa katika uchaguzi mkuu dhidi ya rais wa sasa Peter Mutharika. Mama Banda alichukua hatamu za urais baada ya kifo cha Bingu wa Mutharika ambaye kabla ya hapo alihudumu kama makamu wake.

Hivi sasa Liberia inatawaliwa na rais mwanamke, Ellen Johnson-Sirleaf aliyechukua madaraka hayo toka Januari 16, 2006. Ndiye rais wa kwanza mwanamke katika bara la Afrika. Afrika imepata kuwa na viongozi wengine wanawake kama Catherine Samba-Panza wa Afrika ya Kati na Waziri Mkuu wa Senegal, Aminata Toure .

Bara la Ulaya pia limekuwa na viongozi wanawake kama, Dalia Grybauskaite wa Lithunia, Atifete Jahjaga wa Kosovo, Kolinda Grabar-Kitarovic wa Crotia na Tarja Halonen wa Finland. Ujerumani na Uingereza imekuwa na viongozi wanawake ambao ntawataja baadae.

Asia ni maarufu kwa kuwa na viongozi wanawake. Kati ya mwishoni mwa miaka ya 1970 na 1984 India ilikuwa na Waziri Mkuu mwanamke, Indira Ghandi. Huyu ni mmoja wa wanawake waliokuwa na nguvu wakati wa vita baridi ya dunia katika ya nchi za magharibi na mashariki. Waziri Mkuu wa Bangladesh ni mwanamke Sheikh Hasina Wajed. Aliingia madarakani mwaka 2009.

Kwa sasa rais wa Korea Kusini ni mwanamama Park Geun-hye (64) aliyeingia madarakani baada ya kushinda urais mwaka 2013. Baba yake alikuwa pia rais wa nchi hiyo kati ya mwaka 1963 na 1979.

Hadi mwezi uliopita Brazil ilikuwa inatawaliwa na rais Dilma Rousessef mwanamama ambaye wanasiasa wenzake wamemfanyia ‘figisu’ ili atoke madarakani kwa kisingizio cha kuwa na kesi ya kujibu kuhusu matumizi mbaya ya madaraka yake. Aliingia Ikulu ya Brazil kwa mara ya kwanza Januari 1, 2011.

Amerika ya Kusini ina akina mama wengine maarufu kama aliyekuwa rais wa Argentina, Christina Fenandez de Kirchener ambaye aliingia madarakani mwaka 2007.  Michelle Bachelet ni mwanamke mwingine anayeiongoza Chile. Argentina, Chile na Brazil ni maarufu sana kwa mchezo wa mpira wa miguu duniani.

Pengine wanawake wenye nguvu sana duniani wakatoka Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na sasa huenda dunia ikashuhudia rais wa kwanza mwanamke wa nchi kubwa yenye nguvu za kiuchumi na kijeshi yaani Marekani.

Dunia inafuatilia kwa makini mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa Marekani na mambo yanayoendelea Uingereza baada ya Brexit.

Wabunge wa chama kinachotawala cha Conservative tayari wamempitisha mama Theresa May (59) kuwa kiongozi wa chama hicho na hivyo sasa ndiye Waziri Mkuu baada ya mpinzani wake mama  Andrea Leadsom (53) kujitoa.

May aliyeapishwa Jumatano ya tarehe 14 Julai anaziba pengo la linaloachwa na Waziri Mkuu anayeondoka David Cameroon aliyetangaza kujiuzulu kufuatia nchi yake kupiga kura ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya maarufu kama ‘Brexit’.  Wakati May alitaka Uingereza ibakie Umoja wa Ulaya, Leadsom alipiga kampeni nchi yake ijitoe. Hivi sasa viongozi wa Conservative na Labor wana kazi kubwa kuziunganisha pande mbili za ‘Brexit’

Siku chacke kabla ya kutangaza kujitoa, kampeni za Leadsom ziliingia dosari baada ya kunukuliwa akisema kuwa yeye ni bora zaidi kuchaguliwa kuingoza Serikali ya Uingereza kuliko May kwa kuwa ni mama na ana watoto. Kumbuka May hakujaliwa kupata mtoto ingawa ana mume aitwae Philip. Kauli ya Leadsom imeshutumiwa vikali na wafuasi  wa May wanaomwona mpinzani wao kama ni mtu anayebagua baadhi ya watu katika jamii. Hata hivyo Leadsom amesikitishwa na namna kauli yake ilivyochukuliwa na vyombo vya habari. Leadsom hatimaye alitangaza kumuunga mkono May huku akidai nchi inahitaji kiongozi mwenye uzoefu. May alikuwa Waziri wa Mambo ya ndani.

May anakuwa Waziri Mkuu wa pili mwanamke katika historia ya Uingereza. Wa kwanza alikuwa Margaret Thatcher aliyeingia madarakani mwaka 1977 na kuondoka mwaka 1990. Kama alivyokuwa Thatcher, May anatajwa kuwa mwanamama shupavu.

Rais wa ufaransa Francois Hollande naye anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mwanamama Marine Le Pen ambaye ni rais wa chama cha upinzani cha Front National. Mwanamama huyo amesema ataitumia kura ya maoni ya Uingereza dhidi ya Umoja wa Ulaya kuwashawishi Wafaransa kumpigia kura mwakani. Mwendelezo wa mashambulio ya kigaidi nchini humo unazidi kumweka njia panda Hollande na hivyo kumpa mwanya Le Pen.

Tayari Ulaya ina mwanamama mwenye nguvu kubwa ambaye ni Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (62) aliyechukua uongozi tangu Novemba 2005.  Yeye alipendelea Uingereza ibaki Umoja wa Ulaya. Ni mama ambaye hakujaliwa kuzaa ingawa amewahi kuolewa na Ulrick Merkel mwaka 1972 na kutalikiana mwaka 1982. Hivi sasa anaishi na mume mwingine anayeitwa Joachim Sauer ambaye hapendi kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Ni wazi chama cha Democrat kitamchagua Hillary Clinton (68) kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumanne ya Novemba 4, mwaka huu. Mwanamama huyo amemshinda Bernie Sanders kwenye kura za maoni ndani ya chama chao na  sasa anajiandaa kupambana na Donald Trump wa Republican.

Mume wa Hillary, Bill Clinton alikuwa rais wa 42 wa Marekani kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 2001. Wana mtoto mmoja aitwae Chelsea.

Alipoulizwa anachukuliaje kwa Trump kushinda kura za maoni ndani ya Republican, Rais Barack Obama alisema ‘sisi tumefurahi’ akimaanisha timu ya Democrat ina matumaini kwamba wananchi wa Marekani watamchagua Hillary na kumnyima kura Trump kufuatia kauli zake nyingi zenye utata.

Hata hivyo Trump anaugwa mkono na wananchi wengi nchini humo hasa wanaotaka kuchagua rais ambaye hajawaji kuwa mwanasiasa. Wapinzani wa Hillary wanadai yeye ni sehemu ya watu waliwasababishia taabu wananchi kwani alishiriki kutunga sera zinazodaiwa kuwa mbovu.

Hata hivyo mwamko wa wapiga kura hasa wanawake ni mkubwa sana. Dunia inasubiri kuona rais wa 45 wa Marekani. Baadhi ya wananchi wanataka kuingia katika historia ya kuona rais mwanamke wa Marekani akipatikana katika wakati wa kizazi chao. Hakika utawala wa wanawake unakaribia duniani. Miongoni mwa mataifa makubwa tayari tunaye Merkel wa Ujerumani na May Waziri Mkuu wa Uingereza na Le Pen huenda akaja kushinda urais Ufaransa.

Dunia inasubiri kuona rais wa 45 wa Marekani. Hillary atakamilisha ufalme wa wanawake duniani iwapo atachaguliwa kuwa rais mwezi Novemba na kuapishwa kama ilivyo desturi Januari 20, 2017.

Hakika wanawake wanaelekea kushika hatamu za uongozi duniani. Sasa itakua ukienda London unakutana na May, Berlin unapokewa na Merkel na Paris unakaribishwa na Le Pen wakati ukitua Washington unakaribishwa na Mama Hillary. Patakuwa hapatoshi!!