Home Makala Tumejiandaaje kuwasaidia waliokabiliwa na majanga?

Tumejiandaaje kuwasaidia waliokabiliwa na majanga?

3389
0
SHARE

INAWEZEKANA kabisa zipo sababu kubwa na za msingi kabisa za kwanini Rais John Magufuli, Rais wa wanyonge na mtetezi wa maskini hajaonekana kuzungumza na taifa na sehemu kubwa ya nchi ambayo imekuwa kwenye mshtuko kufuatia tetemeko la ardhi lililopiga Kagera na kurindima sehemu kubwa ya Kaskazini Magharibi mwa nchi yetu.

Sababu hizi zinaweza kuwa ni za msingi kabisa na zenye maana endapo zitatolewa na watu wote wenye fikra huru wakaweza kukubaliana nazo.

Kuna sababu hata hivyo ambazo zikitolewa – kama zitatolewa – zitawafanya watu waangaliane mara mbilimbili kama wanaozitoa hizo sababu wanazitoa wakifikiria watu wote hawana uwezo wa kufikiri au wanajaribu kulazimisha wasifikiri.

Baadhi ya sababu ambazo haziwezi kutolewa na kwa kweli hazipaswi kutolewa ni kama “hili ni suala la viongozi wa chini, siyo suala la Rais” au “mbona Waziri Mkuu (Kassm Majaliwa) alishaenda na suala la maafa liko chini ya yake”. Sababu nyingine ambazo hazipaswi kutolewa au hata kujaribiwa kutolewa ni kama kuamua kusema “lilikuwa janga la kawaida tu hawakufa watu wengi”.

Wenye kutoa sababu hiyo wanaweza wakasema kuwa ili Rais aonekane na kuzungumzia na kwenda kutoa mahali pole basi janga linapaswa kuwa kubwa sana na lenye vifo vingi sana; kwamba vifo 16 kwenye tukio hili si vya kushtusha sana kwani Watanzania tayari wameshazoea kupata habari za ajali zenye kuua watu wengi.

Wenye kutoa sababu hii wanaweza kuendelea na kusema kuwa tayari ajali za magari zinaua watu wengi sana na si mara zote au hata mara moja Rais hajaenda kutembelea maeneo ya ajali. Kwamba, kuna ajali zimeua watu thelathini au ishirini lakini Rais anaishia kutoa pole na rambirambi tu.

Tatizo la sababu hii ni kuwa suala la tetemeko la ardhi ni zaidi ya ajali; ni mojawapo ya matukio makubwa ya nguvu za asili za ulimwengu (natural occurring event) ambayo mwanadamu hajaweza kuyapatia majibu ya kutosha kujiandaa nayo. Kwa maneno mengine, tukio la tetemeko la ardhi siyo “ajali” kwa maana ya ajali bali ni “baa” ni “janga”. Matukio mengine yanatokana na nguvu hizi za asili za ulimwengu ni kimbunga, mafuriko, moto, n.k

Hivyo, kuchukulia janga la tetemeko la ardhi kama ni ajali tu mojawapo ni kutokuwa makini na kutoonyesha kujua uzito wa tukio hili. Tetemeko hilo lingepiga hadi kufikiria hata kiasi cha alama namba 7 kwenye kipimo cha Richter basi hadi Mwanza, Mara na inawezekana hata Kigoma kungesikika kilio kama siyo mpaka Dodoma! Hivyo, mshtuko wa tukio hili peke yake kwa eneo kubwa la nchi yetu na lenye watu wengi ingemlazimu Rais mwenyewe kuhakikisha anajitokeza mara moja kuwatuliza wananchi na kuwapa moyo watu waliokuwa kwenye juhudi za kufanya uokoaji.

Pia kuna sababu nyingine ambazo hata zikitolewa bado watu wataona zina shida. Kwa mfano, ni vigumu kuwafanya watu waamini kuwa Rais alikuwa ‘busy’ sana na mambo mengine ya kitaifa – kama kufanya teuzi mbalimbali na kuwaapisha watu mbalimbali – kiasi kwamba hakuwa na muda wa yeye mwenyewe kujionesha kuwa anajali kilichowatokea watu wake. Hivi, watoto wa Kitanzania wanapolala nje, wananchi kukosa makazi ya kudumu, watoto (kwa maelfu) kuwa katika hali ya mshtuko wasijue wazazi wao watafanya nini kuwahakikisha malazi, makazi na vyakula siyo sababu ya Rais mwenyewe kujionesha na kuwatuliza moyo wananchi hawa na familia zao? Siwezi kuona ‘ubusy’ wowote ule ambao unaweza ukawa sababu au kisingizio cha kwanini Rais hajatokea kuzungumza na taifa na kutembelea Bukoba.

Sasa inawezekana akaamua kwenda huko punde na kuwaona wananchi na kuwapa pole. Hata hivyo, wiki moja baadaye au mwezi mmoja baadaye akiamua kwenda huko ni bora aende na maelezo mazuri. Angalau hivyo ndivyo watu wanaweza kufikiria.

Binafsi naamini kuwa akiamua kwenda huko wakati wowote ule sababu pekee kubwa ambayo haimpi udhuru wa kutokwenda huko mara moja baada ya tukio – hasa baada ya kupita kwa shughuli za uokoaji – ni mwitikio wake kuhusiana na taifa letu lilivyo linapokuja suala la majanga.

Itoshe kusema hapa kuwa Rais Magufuli muda wote wa kampeni na hata baadaye amekuwa akizungumzia kuwa yeye hatowaangusha “wanyonge” na “maskini” wa Tanzania. Kwamba, atafanya kazi kujali maslahi yao na kujali utu wao na kuwafanya wajisikie na kuwa wao siyo watu tu bali pia wao ni binadamu.

Ni matumaini yangu popote alipo atajiuliza kama mwitikio wake yeye binafsi – siyo serikalia au watu wengine – umemfanya aonekene kama mtu anayejali wanyonge, maskini, walioathirika na waliowekwa pembezoni sababu ya tetemeko hili. Je, wananchi hawa wote wanaweza kusema kweli Rais wao anawajali katika hali na saa ya unyonge wao?

Kati ya vitu ambavyo binafsi nimekuwa nikiviandika kwa uchungu mkubwa kwa sababu naamini vinapaswa kuwa sehemu kubwa ya taifa la kisasa ni kujiandaa na majanga. Tunaweza kuwa na magari mazuri, majengo mazuri, ndege nzuri na hata silaha nzuri na tukaonesha takwimu zote za jinsi gani taifa letu linapiga hatua ya haraka ya maendeleo lakini bila kuonekana tunaweza na tumejipanga kukabiliana na majanga mbalimbali hayo mengine yote ni mbwembwe tu.

Kuna furaha gani kutamba kuwa ‘tunaweza’ kama tunajionesha hatuwezi kushughulikia shughuli za uokoaji katika janga kama hili. Nina uhakika – wa imani zaidi – kuwa wengi waliokufa katika tukio hili wamekufa kwa sababu walikosa huduma ya kwanza ya uokoaji kuliko kitu kingine chochote.

Hili ni kweli hata kwenye ajali zetu nyingi za mabasi au magari; watu wetu wengi wanakufa kwa sababu hakuna huduma ya kwanza au mfumo mzuri wa kutoa huduma ya kwanza (paramedic) kwa karibu nchi nzima. Mtu anaweza akaumia kidogo lakini kwa vile hatuna watu wa kujali kuangalia hali ya mtu, kuzuia kupoteza damu na kuwahisha wagonjwa kwenye vituo vya huduma za ajali (trauma centers) basi tunapoteza watu wetu wengi. Wenyewe tunaamini “yote ni mipango ya Mungu” na hivyo tumegoma kujipanga!

Kuhusiana na tetemeko la ardhi wengi leo wanashtuka na kuzungumzia; lakini binafsi nilishawahi kuandika kwa kirefu juu ya hili na kutoa maoni yangu – ambayo naamini yanakaribiana na kuwa bora kuliko ya mtu mwingine yeyote kuhusiana na suala hili – na kuelezea kuwa kwa taifa kama la kwetu kutojiandaa na tetemeko kubwa la ardhi ni kujiandaa na maafa. Hivi inawezekana vipi watu ambao tunajua tunaishi kwenye eneo la Bonde la Ufa (Mashariki na Magharibi) na tunajua nchi yetu ina maeneo mengi ambapo kuna nguvu za Volcano zinafanya kazi lakini tunakaa na kuombea kuwa “ati tetemeko lisitokee” au likitokea wote tushangae na kujiuliza “Mungu imekuwaje”; kwani Mungu alitupa vichwa vya kufikiri siasa wakati wote?

Niliandika mada kama hii Machi 2, 2010 kwa sababu ilikuwa ni miaka mia moja tangu tetemeko kubwa zaidi kuwahi kutokea katika ardhi yetu katika rekodi inayokumbukwa.  Ndani ya mada ile niliweka pia mojawapo ya nyaraka ambazo nina uhakika zingeweza kuwa kichochea cha mijadala ya kujiandaa na majanga siyo tu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu bali pia sehemu nyingine.

Ni matumaini yangu kuwa binafsi nitaelewa ukimya na kutoonekana kwa Magufuli kwa sababu ya kile alichokisema katika taarifa yake ya kuahirisha kwenda Zambia. Kwamba, aliahirisha kufanya vile ili kufuatilia shughuli za uokoaji kufuatia tetemeko la ardhi. Ni matumaini yangu kuwa atakaposimama kuzungumzia hili:

  1. Ataelezea nia yake ya kufumua mfumo wetu wa kukabiliana na majanga na shughuli za uokoaji na kuondoa kitengo cha Uokoaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na kukifanya kiwe mamlaka huru na chenye kutengewa bajeti ya kutosha.
  2. Kuchangia ni jinsi gani Kikosi cha Uokoaji chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kinaweza kufanyiwa mabadiliko au maboresho ili kiweze kukabiliana na majanga mbalimbali.
  3. Kuangalia ni jinsi gani shughuli za uokoaji zinaweza kuletwa kwenye Halmashauri na Miji mbalimbali badala ya kusubiri hadi maamuzi yatoke Ikulu au Dar er Salaam. Kwa mfano, Kamati za Ulinzi na Usalama kwanini zisiwe pia kuwa ni Kamati za Majanga na kuweza kufanya maamuzi mbalimbali huko huko mikoani au Wilayani?
  4. Kuangalia ni jinsi gani JWTZ linaweza kutumika kama mwitikiaji wa mwanzo linapotokea janga kubwa (first responders) kwa sababu wana vifaa, wanajua kukabiliana na majanga na wana nidhamu ya kuweza kusimamia suala hili toka Mwanzo. Tumewaona jinsi gani walivyokuwa wanafanya mazoezi nchi nzima kuelekea ile Septemba Mosi – Siku ya Majeshi. Je, linapotokea janga kama hili inachukua muda gani kwa vikosi vya jeshi kufika mahali na kusimamia shughuli za uokoaji? Je, Rais ameridhika na mwitiko wa vyombo hivi vya usalama?

Baadhi ya hoja nyingine naamini nilivyoandika mwaka 2010 bado zina nguvu leo hii.

www.zamampya.com