Home Latest News Kulindana wakubwa kumekwaza vita dhidi ya ufisadi

Kulindana wakubwa kumekwaza vita dhidi ya ufisadi

619
0
SHARE

badnariNA HILAL SUED

UKICHUNGUZA kwa makini historia ya vita dhidi ya ufisadi iliyokuwa ikiendeshwa na watawala hapa nchini kabla ya ujio wa Rais John Magufuli, huwezi kuacha kugundua vita hiyo ilikuwa imejaa ukosefu wa ari, unafiki, uongo, ghilba, kiini macho, upotoshaji, dhihaka na kila aina ya sifa hasi utakayofikiria.

Na lengo kubwa ya haya ni kulindana kwa wakubwa katika chama na serikali. Lakini sasa hivi hali hii inaanza kubadilika iwapo kutakuwapo jitihada za nguvu za kutenganisha chama (CCM) na serikali.

Kasi, na hasa muelekeo ya Rais John Magufuli katika azma yake ya kusafisha ufisadi na uozo uliokuwapo na kushamiri katika utawala wa awamu ya mtangulizi wake  huenda ni sababu moja kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukawia kumpongeza kwa anachokifanya.

Ni kweli kuna viongozi mmoja mmoja wa chama hicho wametoa kauli za kumpongeza kwa nyakati tofauti lakini kichama ilichukua muda mrefu hadi mapema wiki hii hii.

Na sababu kubwa ni kwamba ‘tingatinga’ linaushambulia kwa kasi mfumo wa ufisadi uliokuwa unavumiliwa, kama siyo kulelewa na uongozi wa juu wa chama hicho.

Nasema hivi kwa sababu hata siku moja, kwa mfano, hatukuwahi kusikia viongozi wa  chama hicho wakitoa kauli za kukemea ufisadi, ukwepaji kodi na wizi uliokuwa unafanyika kupitia bandari ya Dar es Salaam kwa muda mrefu sana.

Baadhi ya viongozi wa juu wa CCM kama vile Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nauye walikuwa wakifanya ziara kadha mikoani ambako walikuwa wakikemea uzembe wa watendaji wa serikali, ubadhirifu na ufisadi wao, kutosikiliza migogoro ya ardhi na hata kutoa wito kwa rais kwamba baadhi ya mawaziri wake walikuwa ‘mizigo’ tu na awafute kazi.

Lakini wawili hao waliojitambulisha kwamba wanakerwa na uozo ndani ya utawala wao hata siku moja hatukusikia wamekwenda bandari ya Dar es Salaam na kukemea madudu makubwa makubwa ya pale yaliyokuwa yanaikosesha nchi matrilioni ya mapato. Inawezekana walikuwa hawajui?

Na Kinana na Nauye wanashindwa kujiuliza hili swali: kwa nini Magufuli kaanza na bandari? Ameanza eneo ambalo wao walikuwa kimakusudi wanalikwepa – kulinda masilahi ya wakubwa?

Lakini Kinana na Nape hawakuwa peke yao katika unafiki wa namna huii. Wako wengi, hasa katika mamlaka na idara za serikali ambao walikaa kimya huku wachache walikuwa wakiikamua nchi kama vile ng’ombe wa maziwa kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mfano kulikuwa Waziri wa Fedha na Naibu wake. Naomba nizungumzie kidogo naibu wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba ambaye kama mwaka mmoja tu uliopita wakati wa sakata la mashine za EFD limepamba moto, alionekana katika TV akimhenyesha mmiliki mmoja wa duka Kariakoo mwenye asili ya Kiasia kwa kosa la kukutwa akitumia mashine ya EFD ambayo ilikuwa haipeleki taarifa za mauzo kule Mamlaka ya Mapato (TRA).

Hiyo ilileta picha ya waziri huyo kutaka kuonekana ni mchapakazi na mfuatiliaji wa kodi za serikali. Lakini hivi kweli Mwigulu alikuwa hajui kabisa ukwepaji mkubwa wa kodi uliokuwa ukiendelea pale bandarini, na badala yake akaamua tu kukomaa na huyu ‘dagaa’ wa ukwepaji kodi?

Na achilia mbali suala la kuikoseha nchi mapato yake muhimu, kuna suala la usalama wa nchi. Vyombo vya ulinzi na usalama — kama vile jeshi la polisi na Usalama wa Taifa vilikuwa havioni kwamba ilikuwa ni hatari ‘kiusalama’ kwa taifa kwa makontena kuibiwa kutoka bandarini au kutolewa bila kukaguliwa? Je iwapo mengine yangekuwa yamesheheni madawa ya kulevya au silaha?

Lakini hakuna taasisi ya serikali ambayo imeonekana ‘imevuliwa nguo’ kutokana na anayofanya Magufuli sasa hivi kama ile ya kupambana na kuzuia rushwa – TAKUKURU.

Taasisi hii ambayo ndiyo hasa yenye jukumu la kupambana na vitendo vya ufisadi ilikuwa usingizini wakati maafisa wa umma (TRA na TPA) wakishirikiana na wafanyabiashara wachache wakila njama kuikosesha serikali matrilioni ya mapato.

Na bila shaka udhaifu wa TAKUKURU Magufuli anaubaini kwa sababu kwa muda wa siku chache tu tangu kuibuliwa kwa tuhuma dhidi ya maagfisa wakuu wa TRA, walitinga mahakamani bila ya TAKUKURU kushirikishwa.

Kikawaida, taasisi hii ingechukuwa muda kufanya uchunguzi, na baada ya hapo huja kile kipindi cha kutupiana mpira kati ya taasisi hiyo na ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa serikali (DPP).

Utupianaji huu wa mpira mara nyingi huleta tafsiri kwamba lao ni moja tu – kulinda wakubwa katika tuhuma za ufisadi. Lakini cha kujiuliza ni kwamba hawa watendaji si wana mkuu wao aliyowateua, mbona huwa kimya?

Mara kwa mara TAKUKURU imekuwa inaumbuka katika kashfa kadha, kama vile ile ya Wizara ya Maliasili ya utoroshaji wa twiga, ya ufisadi katika Wizara ya Nishati na Madini iliyomhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wake David Jairo, ile ya ufisadi iliyotetemesha Bunge hadi ikapelekea mawaziri kadha kuondolewa katika nafasi zao, akiwemo Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo na pia ya ununuzi wa mafuta ya Tanesco.

Kashfa zote hizi hazikugunduliwa na Takukuru, bali na taasisi au watu wengine hususan Wabunge. Inashangaza kuona Mbunge tu wa kawaida akipeperusha Bungeni nyaraka (barua) iliyoonyesha ufisadi katika Wizara ya Nishati na Madini miaka mitatu iliyopita.

Barua hiyo iliandikwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo David Jairo ikiomba ‘michango’ ya fedha (yaani milungula) kutoka taasisi zilizokuwa chini yake kwa ajili ya ‘kuwalainisha’ Wabunge ili wapitishe bajeti ya Wizara yake bila dodosa nyingi. TAKUKURU ilikuwa haina barua hiyo, pamoja na kwamba taasisi hiyo ilikuwa na bajeti yake mahsusi, wachunguzi kila wilaya, na maafisa wengine na ‘manusanusa’ kila kona na katika ofisi za umma walishindwa kuipata hati kama hiyo na kuifanyia kazi.

Isitoshe Takukuru inawezeshwa na sheria, ambapo maafisa wake wana uwezo wa kuomba na kupewa mara moja nyaraka yoyote wanayotaka kutoka wizara na ofisi za serikali.

Lakini hakuna wakati ambapo kauli ile ya Dk. Hosea ya kusema taasisi yake ilikuwa ‘huru’ katika shughuli zake ilipokuja kumsuta sana mwenyewe kama wakati mtandao wa Wikileaks ulipomnukuu yeye mwenyewe akimwambia afisa mmoja wa ngazi ya juu kutoka Ubalozi wa Marekani hapa nchini kwamba alikuwa anapata vizingiti kutoka juu kuhusu azma yake ya kuwapeleka mahakamani watuhumiwa wa ufisadi ambao ni vigogo wa serikali.

Hakuna haja ya kutaja hapa kwamba katika kimbiza kimbiza yake hii dhidi ya mafisadi, Magufuli anayafahamu yote haya na hivyo atakuwa anachukua hatua stahiki, tofauti na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.