Home Latest News MSUGUANO WA KISIASA ZANZIBAR:

MSUGUANO WA KISIASA ZANZIBAR:

638
0
SHARE

Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Maalim Seif Sharif HamadNi Upemba na Uunguja au uCUF na uCCM?

NA GRACE SHITUNDU

JUHUDI za kutatua mgogoro wa uchaguzi Zanzibar zimeendelea kwa mazungumzo mbalimbali yanayofanyika ili kunusuru hali ya amani visiwani humo, ingawa kwa upande mwingine mgogoro huo ni muendelezo wa historia ya madhara ya uchaguzi yanayovikumbua kisiwa hicho.

Mgogoro wa sasa unatokana nauamuzi wa   Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi uliohusu Zanzibar pekee na kutangaza kurudiwa, uamuzi ambao unaitesa Zanzibar na Taifa kwa ujumla.

 

Katika madai yake Jecha anasema uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu visiwani humo ulikuwa na kasoro nyingi zikiwamo kutokuwepo kwa maelewano kati ya wajumbe wa ZEC ahli iliyochangiwa na baadhi yao kupigana kwenye chumba cha kutangazia matokeo. Kura zilizopigwa kutofautina na idadi ya wapiga kura hasa katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi kisiwani Pemba, kubwa zaidi likidaiwa ni hatua ya  Maalim Seif Sharif Hamad kujitangazia ushindi.

 

Tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo kumetolewa matamko mbalimbali ya kupinga hatua hiyo huku vyama vikuu vilivyo na upinzani mkubwa Zanzibar Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vikiwa na msimamo tofauti, ambapo CCM wameridhia kurudiwa uchaguzi na CUF wamegomea.

 

Msigano huo umesababisha Tanzania kusitishiwa msaada wa Sh. trilion 1.5 zilizokuwa zitolewe na Marekani katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo CCM inapinga uamuzi na kwa upande wa CUF kimeunga mkono uamuzi huo na kutaka mshindi wa Urais wa Zanzibar atangazwe na kuapishwa ili kuondoa vikwazo vya kiuchumi.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari – CUF, Ismail Jussa Ladhu anadai kuwa hakuna njia ya kunusuru Tanzania kuwekewa vikwazo vya kiuchumi ikiwemo kunyimwa misaada zaidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar kukubali kukamilisha uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu.
Anadai  kuwa kuna kikundi cha watu wachache Zanzibar ambao hawataki kuona mabadiliko yakitokea ya kiutawala Zanzibar licha ya CCM kushindwa kufikia malengo ya uchaguzi mkuu mwaka huu kutokana na masilahi yao binafsi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, anasema haikuwa mwafaka kwa Marekani kuzuia msaada huo wakati Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilikuwa na hoja za msingi za kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 Mwaka huu.
Anasema ufumbuzi wa migogoro sio kuzuia misaada kwa sababu unawaumiza hadi watu wasiokuwa na hatia, cha muhimu ni  kutafuta njia ya mufaka za kuondoa matatizo.

Tayari Rais Dk. John  Magufuli amekutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambaye pia alikua ni  mgombea urais wa Zanzibar wa CUF Maalim Seif Sharrif Hamad Desemba 21 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo ya viongozi hao ambayo pia yalihudhuriwa na Makamu wa Rais  Samia Suluhu Hassan ambapo kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar ambapo Maalim Seif alieleza hali na anavyoielewa na Rais Magufuli akamshukuru Makamu huyo wa Kwanza na kumsihi waendelee na mazungumzo hadi suluhisho muafaka lipatikane.

Wakati suala hilo linatafutiwa ufumbuzi ni vyema wahusika wajihoji wenyewe je, mvutano huo ni “Uccm na Ucuf au Upemba na Uunguja?

Katika mitandao mbalimbali kumbukumbu za siasa Zanzibar zinaonyesha mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar unaonekana kuwa ni wa kihistoria  tangu enzi za harakati za kudai uhuru mwaka 1957 hadi Mapinduzi ya 1964, katika chaguzi zote za mfumo wa vyama vingi na hata kufikia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010.
Inaelezwa kuwa Mwaka 1958, wakati uhasama kati ya vyama vya ukombozi visiwani – Afro-Shirazi Party (ASP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP) ulipofikia kilele na kutishia umoja na hivyo kuathiri harakati za ukombozi.

 

Rais wa kwanza wa Ghana, hayati Dk. Kwame Nkrumah, aliwaita na kuwakalisha chini mjini Accra, viongozi wa vyama hivyo, Abeid Amani Karume (ASP) na Ali Muhsin (ZNP) na kufikia mwafaka wa kwanza wa kudumisha umoja, uliojulikana kama “The Accra Accord”, lakini mwafaka huu ulivunjika baada ya mwaka mmoja tu wakati harakati zikiendelea na uhasama kurejea kama mwanzo.

Chaguzi zote zilizofanyika kati ya mwaka 1959 na 1963 zilitawaliwa na mizengwe dhidi ya ASP, na kwa ZNP kulelewa na kukingiwa mbawa na Serikali ya Sultani chini ya udhamini wa Wakoloni wa Kiingereza walioitawala Zanzibar tangu mwaka 1890.
Imeelezwa kuwa baadhi ya njama zilizofanywa na serikali dhidi ya ASP ni pamoja na wafuasi wa chama hicho kutishwa na kukamatwa ovyo ili kutia hofu miongoni mwao; kuongezwa kwa majimbo ya uchaguzi kwenye maeneo yenye wafuasi wengi wa ZNP ili kuongeza viti vya ushindi; wizi wa kura na mara nyingine kufutwa kwa matokeo pale ASP ilipoonekana kupata ushindi mkubwa.
Lengo la yote haya lilikuwa ni kukihakikishia ushindi Chama cha ZNP ambacho baadaye na Zanzibar and Pemba Peoples’ Party (ZPPP) kilichodai uhuru kwa madhumuni ya nchi kubakia chini ya himaya ya Sultani kama zilivyo Canada, Australia na nchi zingine, ambazo licha ya kuwa nchi huru, lakini zinabakia kuwa chini ya Himaya ya Malkia wa Uingereza Kikatiba.
Kumbukumbu hizo zinaonyesha kuwa kwa chaguzi zote kuelekea uhuru, mara nyingi ASP kilishinda kwa wingi wa kura lakini kilihujumiwa, Vivyo hivyo, katika uchaguzi wa mwisho uliofanyika Julai 1963, ASP kilishinda kwa wingi wa kura zilizopigwa lakini kikashindwa kwa viti vya Bunge kwa kupata viti 11, na Muungano wa ZNP/ZPPP  ukapata viti 13 na kukabidhiwa serikali, Desemba 10, 1963, chini ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte wa ZPPP kutoka Pemba.
Serikali ya Shamte, iliyoonekana kutowakilisha wala kukidhi matakwa halisi ya Wazanzibari, ilidumu kwa mwezi mmoja tu hadi Januari 12, 1964, pale ilipopinduliwa na wanaharakati wa ASP na wenzao wa Chama cha Umma Party (UP) cha Abdulrahman Babu.
Kufuatia Mapinduzi hayo, Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, alitangaza kwamba kusingekuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 50 mfululizo hadi 2014 kwa madai kwamba dhana ya uchaguzi ni jambo la kikoloni.

 

Pia inaelezwa iliazimiwa  kwamba chini ya utawala wa ASP, wote waliokuwa wafuasi wa ZNP na ZPPP na ndugu zao hadi vizazi, na hasa wenyejiwa Visiwa vya Pemba alikotoka Shamte na Othman Sharrif, wasipewe kamwe nafasi za uongozi katika Serikali ya Mapinduzi ikiwa ni njia ya kuwakomoa kwa kuipinga ASP.

 

Mtafaruku wa kisiasa Zanzibar umewatesa kwa takribani karne ambapo wenyeji wa Unguja na Pemba walikuwa hawazikani na hawashirikiani katika jambo lolote hadi pale ilipoundwa serikali ya Umoja.
Hata hivyo, hali na historia ya uhasama wa kisiasa Visiwani vinaonekana kujirudia kwa misingi na kwa mbinu zile zile za miaka ya 1960 kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 nchini na hivyo kufumua upya vidonda/majeraha ya kale.
Katika chaguzi kuu zote za mwaka 1995, 2000 na 2005, na hata huu wa 2015, Chama cha Wananchi (CUF) ambacho ni Chama Kikuu cha Upinzani Visiwani, kimedai kila mara kupokonywa ushindi kwa hila na CCM kama ilivyokuwa kwa ASP dhidi ya  ZNP/ZPPP miaka ya 1950 – 1960.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 30, 2000, kama yalivyokuwa matokeo ya Januari 1961, yalifuatiwa na vurugu na machafuko ya kisiasa ambapo watu 30 waliuawa na vyombo vya dola; wakati mwaka 1961 watu 69 waliuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa; bila kuhesabu walioikimbia Zanzibar.
Hali kama hii ndiyo iliyoshinikiza kuundwa kwa tume ya pamoja ya Rais, mwaka 2001 ili kupendekeza mwafaka wa Kitaifa, kama ilivyokuwa mwaka 1958 kwa kutiwa sahihi Mwafaka wa Accra – “Accra Accord”.
Hata hivyo, kufikiwa kwa Mwafaka mpya kwa njia ya kuunda serikali ya mseto ya SUK mwaka 2010 halikuwa jambo rahisi wapo walikuwa wakipinga na wapo waliounga mkono kutokana na mizozo ya mara kwa mara kila baada ya uchaguzi.

 

Baraza la Wawakilishi lililokutana Machi 2010, lilipitisha Azimio lililoweka msingi wa SUK na upatikanaji wake kwa njia ya kura ya maoni na kura hiyo ilipigwa Julai 31, 2010 ambapo asilimia 71.7 ya Wazanzibari wenye haki ya kupiga kura walishiriki.
Matokeo yalikuwa kwamba, asilimia 64.4 ya kura zilikubali kuundwa kwa SUK kuashiria kwamba Wazanzibari walikuwa wamechoshwa na ubaguzi na uhasama wa kijinga wa enzi za kale.
Oktoba 31, 2010, uchaguzi wa Rais ulifanyika katika hali ya amani na utulivu kuliko chaguzi zote katika historia ya Zanzibar. Uchaguzi huo ndio uliozaa Serikali ya Mseto ambapo mshindi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyepata kura nyingi zaidi aliteuliwa kuwa Rais, na aliyefuata kwa vyama vya upinzani, Maalim Seif Sharrif Hamad wa CUF, aliteuliwa Makamu wa kwanza wa Rais.
Katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu matokeo yamefutwa na kila mmoja akitoa kauli na tamko lake lakini je, kiini cha msuguano huo ni CCM na CUF au Upemba na Uunguja ni vyama suluhu ikapatikana na kuachana historia ambayo inendeleza utengano wa kitaifa.

 

Kuna usemi unasema Umoja ni Nguvu Utengano ni Udhaifu na Vita vya Panzi Furaha ya Kunguru.