Home kitaifa 2016 ILIKUWA KICHEKO KWA WALIMA KOROSHO

2016 ILIKUWA KICHEKO KWA WALIMA KOROSHO

1064
0
SHARE
Wakulima wakibangua korosho.

NA FLORENCE SANAWA, MTWARA

ZAO la korosho ni miongoni mwa mazao ya biashara hapa nchini huku mikoa ya Mtwara na Lindi ikiwa na uzalishaji mkubwa kuliko mikoa yote nchini hali ambayo inatoa nafasi kwa wakulima wa mikoa hiyo kuonyesha jinsi gani kilimo hicho kimewakwamua kiuchumi hasa katika msimu wa 2016/17.

Msimu huo utakuwa ni msimu wa kukumbukwa baada ya kupata pembejeo kwa wakati hali ambayo ilipelekea korosho kushamiri mashambani hivyo kupata mazao mavuno mengi kuliko misimu mingine huku wafanyabishara wengi wakifika mkoani hapa kununua korosho hivyo kuongeza ushindani sokoni.

Pamoja korosho hizo kuuzwa kwa bei kubwa lakini usafirishaji wa zao hilo ulipatwa na changamoto nyingi ikiwa ni sehemu ya ulinzi ili kuzuia usafirishaji haramu wa korosho ambazo katika misimu mingine nyingi zilisafirishwa bila ya kuwa na vibali stahiki.

Katika msimu huu mnada wa nane wa TANECU uliofanyikia Wilayani Tandahimba tani 100 ziliuzwa kwa Sh 4000 bei ambayo haijawahi kufikiwa hivyo kuingia katika hisitoria ambayo inawapa hamasa wakulima kuhudumia mashamba yao kwa hali na mali.

Asha Mbani  ni mkulima kutoka Halmashauri ya Mji wa Nanyamba anasema kuwa wameridhishwa na bei ya korosho kwa msimu huu hali ambayo itaongeza hamasa ya kuandaa mashamba mapema kwa msimu ujao hasa yale yaliyokuwa yameshindwa kuendelezwa kwa kipindi kirefu.

Anasema kuwa wakulima wengi waliyaacha  mashamba yao kutokana na kushindwa kuhudumia mashamba yao hali ambayo ilipelekea mashamba hayo kuungua moto na kushindwa kuyaendeleza.

Aidha, waliongeza kuwa hali ya bei sokoni imewapa hamasa tofauti na miaka mitatu iliyopita ambapo ulikuwa unapata 300,000 za malipo huku ukitakiwa kutumia zaidi ya 700,000 ili kukamilisha mahitaji ya shamba hali ambayo ilikuwa inaangusha wakulima wengi wa zao la korosho.

Hata hivyo, wakulima wilayani Tandahimba Jamardin Mussa anasema serikali kuwa inatakiwa kuangalia upya suala la vyama vikuu kuondolewa kwa Sh 20 ukizingatia vyama hivyo ndio wamepewa jukumu la kusimamia minada katika ununuzi huo.

“Vyama vikuu ndio vinajukumu kubwa la kujua korosho ya mkulima inauzwaje na wamewaondolea ile Sh 20 wakati wao ndio wanasimamia uunzaji wa korosho katika minada tunaiomba serikali yetu ni sikivu italiangalia upya suala hili.” anasema Mussa.

Kwa upande wake mkulima kutoka kijiji cha Msijute, Omary Msumba, anasema kuwa itakuwa aibu kubwa kwa mkulima wa zao la korosho kuishi miaka 50 katika makazi duni kutokana na serikali kutoa mazingira mazuri ya kuhakikisha wakulima wanapata bei mzuri  kwa msimu huu ili waweze kuboresha maisha yao.

“Sisi tunatoa changamoto kwa serikali bado watukazanie ili nchini hii iweze kubadilika haiwezekani watu waliotawala miaka ya 50 bado wanakuishi katika nyumba za nyasi hii aibu  kwa sababau katika nchi hii kuna mkulima na mfanyakazi mkulima kila siku asibaki kuwa duni hii sio kweli asiwe kama samaki aliyetemwa na samaki aina ya chewa jambo hili haiwezekani hii nchi ni ya kishirika ya wafanyakazi na wakulima.” anasisitiza Msumba

Aidha, mkulima huyo anasema Serikali imeweza kumpigania mkulima kuweza kupata bei nzuri kwa msimu huu katika kuboresha maisha yao huku akisisitiza kuwa wasiridhike kuwafikisha wakulima katika sehemu hiyo na badala yake waendelee kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha wanamkomboa mkulima wa zao hilo.

Katika hatua nyingine Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Masasi, Mtwara (MAMCU) anasema kuwa bei bado ni nzuri sokoni baada ya kampuni 31 zilijitokeza  kutenda ambapo kampuni saba ziliweza kushinda na kununuliwa tani 5700 ziliuzwa katika mnada huo.

Anasema korosho zinazotoka wilayani Masasi zimepungua bei baada ya kuchukuliwa kwa bei ya juu 3805 na bei ya chini 3760, huku  Mtwara zikichukuliwa kwa bei ya juu 3805 na bei ya chini 3785 tofauti na mnada wa kwanza ambao bei ya mnada huo korosho za Mtwara ziliuzwa kwa bei ya juu 3595 na bei ya chini 3585 kutokana na ubora.

“Awali wanunuzi walikuwa hawana imani na korosho za Mtwara kwakuwa zilikuwa hazikauki lakini msimu huu wameweza kukausha na kuwa na ubora mzuri ambao umepelekea bei yao kupanda wakulima wanapaswa kuendeleza ubora huu ili bei iendelee kuwa juu.

“Wakulima wanaowahisha korosho ghalani ili kuwahi bei wanaua bei ya soko kwakuwa korosho zao zinakuwa na unyevunyevu hali ambayo inapelekea ubora wa korosho kupungua anikeni korosho ili kuifanya bei iongezeke zaidi” anasema Rajab.

Lakini pia Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Hassan Jarufu, anasema korosho nyingi zimeshindwa kusafirishwa msimu wa mwaka 2016/17 kwa kukosa makasha hali ambayo italeta athari kubwa kwa wafanyabishara wengi baada ya korosho nyingi kuwekwa mitaani kwenye maghala.

Anasema ukosefu huo wa makasha umeifanya minada inayoendelea kushuka bei kutokana na korosho nyingi kuwepo mitaani na kushindwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi hadi bei kufikia 2610 katika mnada 10 ambao wafanyabiashara tisa kutenda hali ambayo inaonyesha wazi kuwa wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Katika msimu huu zaidi ya tani 216,275,324 zilitolewa vibali kwa ajili ya kusafirishwa tofauti kati ya hizo tani 57473.178 zilipelekwa nchini India na tani 67496.649 zilipelekwa nchini Vietnam,  wakati msimu wa mwaka 2015/16 Bodi ilitoa vibali kwa tani 124,969,827 pekee.

Jarufu anasema hali hiyo imekuwa ikiwaingizia gharama kubwa wafanyabiashara kutokana na kushindwa kusafirisha hivyo kuweka korosho nyingi kwenye maghala mtaani hatua ambayo haitoi fursa kwao kurudi mnadani.

“Unajua korosho nyingi ziko kwenye maghala mitaani ndio maana bei ya korosho imepungua laiti korosho zingesafirishwa kwa wakati basi tungeendelea kupata wafanyabiashara wengi kama ilivyokuwa mwanzo wa msimu huu ambapo zaidi ya makampuni 107 yalijitosa kwenye mnada.

“Kinachotakiwa ukinunua korosho lazima usafirishe biashara hii inatumia fedha nyingi kiasi ambacho hata wenye biashara huwa wanatoa pesa ya kununa korosho mara moja ambapo na kupakia kisha kupata hati ya kusafirishia mizigo ambayo humtumia mtu aliyemtumia pesa ambapo yeye huangalia mtandaoni juu ya meli iliyosafirisha mzigo  wake anapoona jina lake ndio anakuwa na nafasi nzuri ya kurudi mnadani tena isipofanyika hivyo mzigo unakwama kununuliwa  wafanyabishara wanashindwa kutuma pesa” anasema Jarufu

“Kama inaonekana kuwa na tatizo kwenye usafirishaji wa korosho vyombo vya ulinzi na usalama vipo kwanini visitumike ili mzigo ukiwa unasafirishwa na kuzifikisha salama kuliko korosho nyingi kuwepo bila kusafirishwa? Alihoji Jarufu

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo aliwashauri wakulima kufungua akaunti ili kuweka usalama katika fedha zao kuliko utaratibu uliofanyika mwaka huu ambapo wakulima wengi wamelipwa mkononi hivyo kuhatarisha maisha yao.

“Wakulima wengi hawaamini fedha zao kulipwa benki wanataka wapokee ndio wahakiki kisha wazipeleke benki wenyewe hii ni hatari ndio maana hawa wanaopewa taslimu wanachukua muda mrefu kupata malipo nawashauri kuwa na akaunti kwa usalama wao” alisema Jarufu.