Home Latest News 2016 ILIVYOZIDUWAZA NYANYA NA KUZISHANGAZA EMBE

2016 ILIVYOZIDUWAZA NYANYA NA KUZISHANGAZA EMBE

1311
0
SHARE
Wakulima wakipanga nyanya.

Na Mwandishi Wetu,

Mwaka 2016, unaelekea ukingoni. RAI lijalo litachapishwa katika mwaka mpya wa 2017. Kwa lugha nyingine makala hii ni ya mwisho kwa gazeti la mwaka huu. Mwaka umeenda na mengi lakini kubwa unaweza kufanya kuwa, ni hali ya kutokuwepo majibu ya moja kwa moja ya nini kinafanyika, nini kinatakiwa kufanyika na namna ya kukifikia hicho kinachohitajika.

Katika mwaka huu, kila sekta inaweza kujadiliwa kwa namna moja ama nyingine. Katika hali ya kutaka kujiongezea kipato wananchi wengi walijikuta wakikimbilia sekta ya kilimo kuwekeza huko. Nchi yetu haijawa na uwekezaji mkubwa katika sekta hii licha ya kuwa na ardhi kubwa inayofaa kutumika kwa kilimo.

Kutokana na hali hii, nchi yetu imekuwa haiwezi kuzalisha kwa ajili ya kuuza nje licha ya kuwa kuna fursa za kufanya hivyo. Eneo mojawapo la fursa hizo lipo katika matunda na mbogamboga. Lakini la kushangza ni kuwa hata matunda ya ndani yameanza kukabiliana na ushindani kutoka nje, au zile mbegu za asili kuanza kutoweka na hivyo kuibuka mbegu mpya ambazo pia hukabiliwa na ukinzani wa kimazingira, kijiografia na mwisho kimasoko.

Tunda aina ya tikitimaji limejipatia umaarufu kwa siku za hivi karibuni na hivyo kufanya wananchi wengi kujishughulisha katika ulimaji wake. Tunda hili kwa mwaka unaomalizika limejikuta likianguka sokoni kutokana na uzalishaji mkubwa kuliko uwezo wa hitaji la soko. Wengi waliowekeza katika kulima tunda hili ni ama wamepata hasara au wamejikuta wakibakia kufikiria namna mpya ya kurejesha gharama zao za uzalishaji baada ya kupata mavuno ya kutosha lakini soko kukabiliana na ushindani mkubwa.

Wakati hali hiyo ikiyakabili matikitimaji, miezi kadhaa baadaye likaja anguko kubwa la kukosekana kwa soko la nyanya. Ikumbukwe kuwa nyanya ni zao linalolimwa kwa msimu na kwamba uhifadhi wake unahitaji utaalam wa juu na pia uwekezaji mkubwa ili ziweze kuhifadhiwa kwa siku nyingi. Wakulima wa nyanya katika maeneo mengi ya nchi wakajikuta wakiziacha ziliwe na wadudu na ndege. Hata ndege nao hawakuweza kuzimaliza.

Kwa majiji kama Dar es Salaam ambako huko ndipo lililopo soko kubwa la nyanya na mazao mengine, nako kukatokea hali ya kushuka kwa bei ya zao hilo. Kwa lugha nyingine, wakulima wakabakia kutazama hasara kubwa iliyowafata. Ikumbukwe pia kuwa hali ya mwaka 2016 kiuchumi imefanya hata wananchi nao kubadili tabia na aina ya maisha. Wale wenye makazi yao wakaanza kupanda mazao ya mbogamboga badala ya kurutubisha maua. Hali hii nayo ikachangia kupunguza soko maana zao kama nyanya linaweza kuzalishwa katika eneo dogo na likazaa vema kwa kipindi kama tu litalimwa vema.

Kwa lugha nyingine ni kuwa, kukosekana kwa soko la nyanya kuliathiri wakulima wake walioko mikoa ya Iringa, Morogoro na kwingine ambako zao hilo linastawi kama Arusha na Kilimanjaro. Swali lililobakia katika anguko la soko la nyanya likawa, je, kama nchi hatuna uwezo wa kuhifadhi hata nyanya? Je, hatuna uwezo hata wa kuzibadili hadhi ili ziweze kukaa kwa siku nyingi na kupata soko katika namna nyingine baada ya ile ya awali kushindikana? Na je, nini mikakati yetu baada ya kuangalia anguko hilo ambayo tumeichukua kama funzo? Na mwisho, je, tumejutia hali hiyo na kuamua kwa makusudi kuwa isitokee tena?

Maswali hayo yote ni ya kimkakati. Ni dhahiri nadharia ya Tanzania ya viwanda ambayo haina tofauti na ile ya Elimu kwanza au ile nyingine ya Kilimo kwanza, ipo ipo tu kama wimbo. Waziri mwenye mamlaka ya Wizara hiyo anasema kazi yake ni ‘kupiga sound.’ Hii ni lugha ya mtaani ambayo ikitolewa na kiongozi anayetakiwa kuibadili nchi iweze kukabiliana na majanga ya ndani ama kutafuta majibu ya masuala ya ndani, bila shaka unabakia kinywa wazi. Unabakia hivyo kwa kuwa inakupa picha ya namna kauli mbiu hii itakavyobakia kuwa kama zile zilizotangulia na kwamba inawezekana ikawa imeshindwa hata kabla ya kuanza.

Ndio maana tena wakulima walioko kanda ya Ziwa na maeneo mengine ambao wanamiliki miti ya miembe nao wamekumbwa na jambo lilelile walilokabiliana nalo wakulima wa nyanya. Embe zinazoea kwenye miti ilhali tunda hilo lina soko kubwa nje. Tena embe nyingi za kwetu ni zile za asili ambazo hazijaathirika na mifumo ya kimaabara inayolenga kuongeza uzalishaji ilhali ikileta aina ya matunda ambayo ubora wake unabakia katika maswali.

Kabla ya miti ya miembe haijaweka maua bila shaka inaonekana. Na kwa kuwa tulishakuwa na somo la kukosekana kwa soko la nyanya na tikitimaji, tungeshajifunza ili kukabiliana na madhara ya kukosekana kwa soko. Ili kukabiliana na hali hiyo ilitakiwa kutafuta wawekezaji katika kuhifadhi mazao ya aina hiyo ili yaweze kukaa kwa muda mrefu na yaweze kupata soko siku zijazo.

Tunazo embe kutoka Mombasa na maeneo mengine nje ya Tanzania. Za kwetu zinazoea chini unabakia na maswali yale yale yaliyojitokeza katika nyanya. Inaelezwa kuwepo kwa njaa katika maeneo kadhaa ya nchi mwakani. Bila shaka embe hizi zingekuwa mkombozi kwa wakazi wa maeneo mengi nchini kama tungekuwa na mkakati wa kuzihifadhi ili zikae muda mrefu na pia ziweze kupata soko la ndani na la nje.

Kwa kuwa hatukufanya, tutabakia kuuona mwaka huu ukiwa hauna funzo. Utabakia kuwa mwaka wa matukio makubwa kama nilivyoyabainisha hapo. Tumeduwazwa na kuporokoka kwa soko la nyanya hadi kufanya wakulima kuzitelekeza katika mashamba. Kwa kuwa hatujifunzi kutokana na makosa yetu sasa tunashangazwa na kuoza kwa embe katika miti. Kupanga ni kuchagua na ukichagua fungu baya utavuna hilo hilo.