Home Latest News Demokrasi ya Marekani funzo kwa Afrika

Demokrasi ya Marekani funzo kwa Afrika

1123
0
SHARE

Donald TrumpNa Franklin Victor

WAKATI siasa katika baadhi ya nchi 54 mwanachama wa Umoja wa Afrika – AU imekuwa vita hatari ya kubaki madarakani au kupata mamlaka kwa namna zilizo nje ya uwezo wa kura na demokrasia; funzo kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini Marekani 2016 lazima liwaingie Waafrika ili siku zijazo wawe vinara katika uga wa demokrasia ya uchaguzi.

Siasa na demokrasia kuuelekea Uchaguzi  Kuu huo vimeshika kasi baada ya Jumanne kuu  ya Machi 01, 2016 – Super Tuesday ya mchujo wa wagombea wa vyama mahiri vya Democrat na Republican kushuhudia ushindi kwa Hillary Clinton (Democrat) na bilionea machachari Donald Trump (Republican).

Wagombea hawa wawili hadi sasa ndiyo wanaopewa nafasi ya kukutana katika kinyang’anyiro cha urais wa Marekani na hatimaye mmojawao yawezekana (kama hakutakuwa na mabadiliko ya ghafla) akamrithi Rais Barack Obama anayemaliza muda wake wa kuwahudumia Wamarekani.

Dhima ya makala haya si kuwatazama Hillary Clinton na mpinzani wake Seneta Ben Sanders bali bilionea Donald Trump na njia aipitayo kuuelekea urais wa Marekani kama itapitika ama itawekwa vikwazo ili kusudi asiyafikie malengo yake kisiasa, na nafasi yake kupewa mgombea mwingine hasa Marco Rubio anayepigiwa chapuo au Ted Cruz aliye nyuma ya Trump katika ushindani.

Katika Uchaguzi Mkuu 2016 Wamarekani wengi wanapima kwa kuzingatia mgombea gani akiwa rais anaweza kuwaboresha zaidi ndani ya nchi yao, kuongeza manufaa kwa kila Mmarekani ndani ya Marekani ili kukidhi stahili ya kuwa taifa kubwa lenye nguvu duniani.

Sera za ndani ndizo zenye turufu ya wapiga kura wengi wa Marekani tofauti na ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita ambapo sera za kimataifa zilitawala na kuamua mgombea yupi aingie ikulu kuiongoza Marekani na dunia.

Mpaka sasa mgombea mwenye hatua kubwa kuuelekea uteuzi wa chama cha Republican na hata urais wa Marekani ni bilionea Trump asiyeuogopa ukweli, anayewapa jinamizi vigogo wa chama chake, asiyemung’unya maneno hasa yale ya kuchoma mioyo myepesi. Kigogo huyu ana kila sababu ya kumfanya kuwa rais wa taifa hilo kubwa la Marekani, mzee makini anayeitanguliza Marekani mbele kupitia kauli mbiu yake ya kuifanya Marekani kuwa taifa bora tena – Make America great again.

Kwa hatua aliyoifikia bilionea Trump, baadhi ya wachambuzi na wapiga kura wa Marekani wanamuhesabu kama mshindi, mgombea wa Republican. Kitu pekee, tena cha ajabu kinachoweza kumnyima nafasi Trump kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Republican ni ‘kukatwa’, yaani chama kutozingatia matakwa ya wapiga kura wala kukubalika kwa mgombea.

Hii maana yake nini? Maana yake ni kucheza kamari ya kisiasa yenye kila dalili ya kukipa ushindi chama tawala cha Democrat kupitia mgombea yeyote atakayepitishwa nacho. Vigogo na wakongwe wa Republican hawamuamini sana Trump, wako katika taharuki juu ya mafanikio na weupe wa njia aipitayo kuelekea kuwa rais wa Marekani. Baadhi yao wanampinga hadharani na kutangaza rasmi kusuka mipango ya kuhakikisha jina lake linakatwa na kuwekwa jina jingine hasa la Rubio au ikiwa ngumu afadhali apate Ted Cruz.

Vigogo hawa wanahofia mengi ikiwemo kuporomoka umaarufu wao kisiasa na kuwa wanajua hawataweza kumdhibiti watakavyo Trump endapo ataachwa awe mgombea kisha rais. Marco Rubio anapendwa na wakongwe wa Republican wakitumai mambo mawili kati ya mengi. Kwanza, Rubio ni mpole, anadhibitika na pili, wanahisi Rubio huyu atashindwa kirahisi na mgombea yeyote wa Democrat hivyo mambo mengi hayatabadilika sana hivyo kuwapa nafasi ya kumpandisha mgombea wamtakaye atakayeshinda 2020.

Kwa jinsi Trump alivyojipanga, kikwazo pekee cha kufanikiwa kwake ni kuruhusu baadhi ya vigogo na maveterani wa Republican kukalia demokrasia na matakwa ya wengi na kuamua Trump huyu ‘akatwe tu’. Jambo hili linawezekana kama na endapo Republican wanahisi ni bora urais ubaki Democrat kuliko kuja Republican katika himaya yake Donald Trump wasiyemuamini, wanayemhofia, asiyeogopa. Kupanga ni kuchagua.

Wachambuzi kadhaa wa siasa za Marekani wanadai Republican wamechelewa kutengeneza ‘fitina’ au ‘jipu’ kumkata Trump ingawa wakilazimisha inawezekana lakini kwa gharama ya kuutoa bure urais kwa Democrat, kitu ambacho ni nadra kutokea katika siasa na demokrasia maridhawa.

Binafsi nahisi harakati za ‘kumkata’ Trump zina mikono ya ushawishi ya watu wengi nje kuliko ndani ya Republican. Kati ya wasiopenda Trump apate nafasi anayoistahili wamo baadhi ya watu maarufu, wafanyabiashara matata wa Mexico na wajuzi wa mambo wa Democrat wanaojua dhahiri endapo Trump atapata uteuzi basi ataweza kumshinda mgombea yeyote wa Democrat na kutinga ikulu.

Pia, wahafidhina wasiomtaka Trump na wenzao wa namna zao ndani ya Democrat wako radhi Seneta Sanders autwae uteuzi badala ya Clinton katika Democrat ili mipango yao ya muda mrefu itimie bila kuumiza kichwa. Suala la vigogo kumtaka Rubio ikulu lina mengi linaonyesha vichwa vyao vitakuwa na raha. Ila utamu wa siasa safi na demokrasia huru ya ushindani inayoheshimu nguvu ya kura na ‘akili nyingi’ za wana mipango walio nyuma, kati na mbele ya wagombea watarajiwa na mifumo-nchi husika ni kushuhudia mshindi akipatikana kupitia sanduku la kura.

Tatizo la siasa safi kidemokrasia ni kwamba ‘kukatwa’ lazima kuwe na sababu mahsusi zenye mantiki, si ‘kumkata’ mgombea kirahisi tu kisa kuna watu binafsi wametaka! Sababu yenye mantiki ndiyo wanaitafuta vigogo wa Republican ili kushawishi ‘ukataji’ wa jina Donald Trump.

Majimbo aliyoshinda bilionea Trump katika Super Tuesday kati ya mengi yanayompa nafasi ya kuwa mgombea wa Republican katika uchaguzi mkuu wa rais wa Marekani 2016 ni Alabama, Arkansas, Georgia, Massachusetts, Tennessee na Virginia; huku washindani wake Ted Cruz akishinda nyumbani kwake Texas, Alaska na Oklahoma; na chaguo la vigogo wasiopenda mabadiliko makubwa katika sera za uongozi wa nchi, Marco Rubio akishinda jimbo moja pekee la Minnesota.

 

Sms 0772 066 667.