Home Latest News Gonzalez: Umeya si kazi rahisi

Gonzalez: Umeya si kazi rahisi

610
0
SHARE

MartaNa Sidi Mgumia, aliyekuwa Madrid

KATIKA mataifa yaliyoendelea, nafasi ya Meya hupewa thamani kubwa kutokana na umuhimu wa mtu huyo katika jiji au Manispaa.

Hata hivyo huenda kwa Tanzania nafasi hiyo isiwe na mashiko sana kutokana na msingi wa nafasi hiyo kutokuwa imara.

Ukweli wa umuhimu wa Meya unaelezwa na mwanasiasa kijana nchini Spain,  Marta De Las Mercedes Perez Gonzalez.

Gonzalez  ni Meya wa Manispaa ya Raduena, jijini Madrid, umri wake ni miaka 31 hali inayomfanya kuwa kiongozi mwananamke mdogo tofauti na mameya wenzake wa manispaa 175 za jiji la Madrid.

Pamoja na majukumu mazito ya kisiasa na kiuongozi aliyonayo, bado Gonzalez ni mama wa mtoto mmoja.

RAI lilifanya mahojiano maalum na binti huyu ili kujua anawezaje kuimudu nafasi yake hiyo sanjari na familia yake.

RAI: Jukumu lako hasa ni lipi katika nafasi yako ya umeya?

Gonzalez: Zipo kazi nyingi na asikwambie mtu, kazi ya umeya ni nzito na si rahisi kama watu wengi wanavyodhani.

Katika kujibu swali lako, labda niseme kuwa kazi yangu kubwa ni kuhakikisha nasimamia rasilimali chache tulizonazo hapa kwenye Manispaa yetu ili kuhakikisha zinawanufaisha wakazi wote wa Raduena, bila kujali itaikadi zao.

RAI: Kuna shughuli nyingine zaidi ya umeya unafanya?

Gonzalez: Ndio, zipo shughuli nyingi tu, lakini kubwa najihusisha na mtandao wa TERRAE, mimi ni rais wa mtandao huo na kazi yetu kubwa ni kuendesha mradi wa udhibiti wa takataka wenye lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kazi hii nayo ni ngumu lakini tunafanikiwa kuifanya kwa ufanisi kwa msaada wa wataalamu.

RAI: Kazi ya kutunza mazingira mnaifanya nyie tu au zipo taasisi nyingine mnasaidiana?

Gonzalez: Kuna watu wengi wanafanya kazi ya kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa ipasavyo na zote lengo lao ni  kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

RAI: Mnapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wakazi wa eneo unaloliongoza?

Gonzalez: Ndio. Wakazi wa manispaa ya Raduena ambayo ipo Kaskazini mwa mji wa Madrid wanashirikiana nasi kikamilifu, wanachofanya ni kutunza udongo, lengo kuu la kufanya hivi ni kukwepa matumizi ya mbolea za viwandani.

RAI: Manispaa yako ina jumla ya wakaazi wangapi?

Gonzalez: Tupo wakazi takribani laki mbili.

RAI: Shughuli kubwa inayowaingizia kipato ni ipi?

Gonzalez: Wengi wetu ni wakulima wa mboga mboga na tunalima kwa ustadi wa hali ya juu huku tukitumia mabaki ya chakula kulisha kuku pamoja na kutengeneza mbolea ya mboji.

RAI: Unakutana na changamoto gani katika majukumu yako?

Gonzalez: Zipo changamoto nyingi, kama jinsia yangu na umri wangu, wapo wanaoniona ni mdogo hivyo siwezi kuamua mambo mazito, lakini siwalaumu kwani ni jambo la kawaida, kikubwa ninachokifanya ni kuhakikisha nafanya mambo makubwa ili wao washangae.

RAI: Umekuwa Meya kwa muda gani sasa?

Gonzalez: Huu ni mwaka wa tano, hiki ni kipindi changu cha pili cha miaka minne minne na imani ya watu wangu ndio imenisaidia kuendelea kuwaongoza.

Nimeahidi kuwatumikia wakazi wa mji wa Raduena na dhamira yangu ni kutaka  kuuonesha umma kuwa bado wanawake wanaweza katika siasa na pia wana umuhimu sawa na wanaume na siko kwenye kiti hiki kwa uzuri wangu bali kwa kujitoa kwangu na uwezo wangu  mkubwaa wa kufanya kazi kwa bidii huku nikiwa makini na mwenye kujali sana maslahi ya watu wangu walionipa dhamana.

RAI: Unajivunia nini katika awamu yako ya kwanza ya utawala?

Gonzalez: Katika awamu ya kwanza nimeweza kupata mafanikio makubwa kama Meya wa Raduena.

Nimejitahidi kuhamasisha kwa vitendo kazi za maendeleo na sasa wakazi wengi wa mji huu wanajibidiisha kwenye kilimo cha mboga mboga na shughuli nyingine.

RAI: Umesema moja ya changamoto ni umri wako, je, kwako hicho ni kikwazo?

Gonzalez: Hapana. Kwangu kuwa mdogo katika nafasi hizi sio tatizo, tumepatiwa mafunzo ya kutosha ya uongozi, vilevile ni ukweli usiopingika kuwa wakati mwingine mtu unaweza ukawa huna uzoefu wa kazi lakini ukisha kuwa kazini na ukiwa makini unazoea na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Lakini pia elimu yangu ya darasani inatosha kunipa maarifa na uelewa wa mambo, hata unapokosea inakuwa rahisi kujisahihisha na kutorudia kosa lile.

RAI: Unajua lolote kuhusu siasa za Afrika hasa Tanzania?

Gonzalez: Nisiwe mwongo sizijui sana siasa za Afrika na hata Tanzania siijui, nimefurahi kukutana nawe Mtanzania, bila shaka utanieleza machache kuihusu nchi hiyo.

Hata hivyo navutiwa na namna sera za mambo ya jinsia yanavyopewa nafasi Afrika hii nimekuwa nikiisikia kidogo, nasikia wanawake wanaongoza nchi na wengine wana nafasi kubwa za uongozi, hili ni jambo zuri sana.

RAI: Kwa maelezo yako inaonekana unatumia muda mwingi kuitumikia jamii yako, je, unapata nafasi ya kuitazama familia yako?

Gonzalezi: Ndio napata, si kwa kiwango kikubwa, lakini naijali sana familia yangu, kila ninapokuwa na muda naihudumia.

Nafasi yangu ya Umeya pamoja na kazi yangu ya Katibu Tawala katika Chuo cha Manesi vinanibana kiasi, lakini nakuwa na muda kidogo wa kupumzika na familia yangu.

RAI: Wito wako ni upi kwa wanawake duniani kote?

Gonzalez: Wanawake hasa vijana wanapaswa kujua kuwa hakuna kinachoshindikana katika siasa, muhimu ni kuwa wajasiri na wavumilivu.

Wasiwaogope wale wazee waliogoma kuachana na  siasa, jamii hii ya wazee ni sawa na madudu makubwa ya kale yaliyojulikana kama Madainasozi.

Ili ufanikiwe ni vyema mtu ukawa mwerevu na shupavu kwani hiyo ndiyo siri ya mafanikio, hupaswi kuogopa mtu bali kujituma na kutumia busara zako.

Hispania ni moja ya nchi zilizotoa nafasi kubwa kwa wanawake kushikilia nyadhifa za kisiasa.