Home Latest News Tafadhali Wenger usimtumie tena Ospina

Tafadhali Wenger usimtumie tena Ospina

454
0
SHARE
ospina na wenger
Wenger akiwa na Ospina

KELVIN LYAMUYA NA MITANDAO

WAKATI orodha za vikosi viwili vya Arsenal na West Ham zilipotoka kabla ya kuanza kwa pambano la Ligi Kuu ya England baina ya klabu hizo wikiendi iliyopita, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, aligundua kosa kubwa alilolifanya katika upangaji wa kikosi.

Aliweka wazi mshangao wake katika mkutano na waandishi wa habari kwa kusema kuwa hakutegemea kama angeliona jina la Andy Carroll katika orodha ya West Ham tena katika wakati ambao aliamua kumpumzisha mlinzi wake mwenye umbo refu, Per Mertesacker pamoja na mlinda mlango, Petr Cech.

Wakati jambo hilo linatokea, safu ya ulinzi ya Arsenal iliyokuwa ikiongozwa na mlinda mlango, David Ospina, ilishindwa kabisa kuendana na nguvu aliyonayo Carroll hasa pale walipokuwa wakipigiwa mipira ya juu kwani urefu pamoja na umbo kubwa alilonalo Mwingereza huyo vilipelekea awafunge mabao yote matatu.

Na kwa sababu hiyo basi mlinda mlango namba moja wa klabu hiyo, Petr Cech, kwa namna moja au nyingine hana budi kurudishwa katika kikosi cha kwanza cha ‘Gunners’ hao kwenye mchezo ujao wa ligi.

Labda katika fikra za Wenger bado alikuwa na hofu kwamba Cech atakuwa hajapona vizuri majeraha ya goti aliyoyapata dhidi ya Swansea mwezi Machi, hilo lipo juu yake.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Arsenal wanahoji kuwa kama Cech ni mzima kiasi cha jina lake kuwemo kwenye orodha siku hiyo dhidi ya wagonga nyundo hao, kwanini hakucheza?

Inaonekana bado Wenger amelikalia kimya hili suala la hali ya kiafya ya mlinda mlango huyo huku Arsenal ikiwa katika wakati mgumu hasa baada ya kuzidi kuachwa mbali kwenye mbio za kuwania ubingwa wa England na alipoulizwa kuhusu maamuzi yake ya kumwanzisha Ospina katika mchezo huo, alisisitiza uamuzi wake uliegemea zaidi kiwango cha mchezaji.

Katika michezo minne ya mwisho kabla ya kuwavaa West Ham, Ospina amekuwa na kiwango cha kuridhisha ambapo dhidi ya Barcelona na Tottenham alifanya kazi nzuri, kabla ya kucheza dhidi ya Everton na Watford na kutoruhusu nyavu zake zitikiswe.

Kiwango chake katika mchezo dhidi ya Everton hakikuwa kibaya sana licha ya majeraha aliyoyapata katika kipindi cha pili cha mchezo, lakini alijitahidi kuzuia michomo ya hatari iliyoelekezwa langoni mwake na Romelu Lukaku na wenzake.

Hata hivyo, kumwanzisha Ospina langoni dhidi ya kikosi kigumu msimu huu cha West Ham tena katika wakati ambao wanahitaji kuikimbiza Leicester inayokaribia kunyakua ubingwa, huku akimuacha Cech katika benchi ni moja ya maamuzi mabovu ambayo kocha huyo amekuwa akiyafanya na kuigharimu timu.

Na kwa inavyoonekana Wenger ameamua kumpanga Ospina katika mfululizo wa mechi hizo ili kuwasahihisha wale waliokuwa wakimponda mwanzoni mwa msimu.

Ni jambo linalochanganya na lisiloeleweka kwanini hasa mlinda mlando mwenye kiwango cha dunia kama, Petr Cech, anaachwa nje, alipofika klabuni hapo kila mtu alitegemea kuona tatizo la kutokuwa na chaguo la kwanza la kipa linakwisha na kuwa namba moja klabuni hapo.

Lakini bado katika michezo saba ya mwanzo ya ligi, Wenger aliamua kumpanga Ospina mbele ya Cech. Katika michezo ya awali ya hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na ule wa West Ham ambayo Ospina alianza, yote aliigharimu timu.

Petr-Cech-REUT
Petr Cech

Wenger anajitetea kwamba tatizo la kushindwa kucheza mipira ya juu lipo tangu mwanzoni mwa msimu lakini Cech angeweza kulitatua kutokana na upungufu alionao Ospina wa kuganda kwenye mstari wake golini pindi mipira ya juu inapotua kwenye eneo lake la hatari.

Kutokana na upungufu wake huo, ni mara chache sana amekuwa akiruka na kuzuia mipira ya juu. Cech yeye anajiamini zaidi kiasi cha kujiingiza katika msitu wa wachezaji na kuidaka mipira yote inayokuja kwa juu na huwa haruhusu kuipangua kutokana na uchu wa washambuliaji wanaosubiri mipira ya kurudi.

Inawezekana Ospina alikuwa na uwezekano mdogo sana wa kuokoa bao la kwanza la Carroll, lakini kama Cech angekuwepo sidhani kama mshambuliaji huyo angepata nafasi za kutingisha safu ya ulinzi ya Arsenal.

Mchango wa mlinda mlango awapo golini ni namna anavyozuia mipira mbalimbali ya hatari na Cech angeweza kutumia uzoefu wake kuiongoza safu ya ulinzi ya Arsenal au umbo lake kubwa lingeweza kumzuia Carroll asilete madhara zaidi.

Hebu vuta picha kama Cech angeunasa ule mpira wa kwanza ambao West Ham waliuchonga kuelekea lango la Arsenal, je, wagonga nyundo hao wangeweza kutumia mipira ya juu tena kwa kasi ile waliyoitumia kuisumbua Arsenal?

Wikiendi hii, Arsenal wataialika Crystal Palace katika mwendelezo wa Ligi Kuu na watakutana na safu yenye mshambuliaji kama Carroll, si mwingine ni Emmanuel Adebayor, hapa Wenger usimtumie tena Ospina tafadhali.