Home Makala Kimataifa Mambo yanayotatanisha kuhusu ugaidi

Mambo yanayotatanisha kuhusu ugaidi

825
0
SHARE

Na William Shao

KATIKA toleo lililopita tulieleza kuwa utondoti wa matukio ya ‘kigaidi’ ya Septemba 11, 2001 unaweza kumwongoza anayetumia akili ya kawaida kung’amua kwamba hakukuwa na Al-Qaeda katika ndege zile kama inavyodaiwa, na wala hakukuwa na raia mwenye asili ya Kiarabu ambaye dunia ingeweza kuhisi kuwa alikuwa mtekaji, au gaidi, au mfuasi wa Al-Qaeda.

Tazama orodha ya waliotajwa kuwa magaidi waliohusika na tukio la Septemba 11, 2001, ambao wote walidaiwa kufa siku hiyo ya tukio. 1. Marwan Al-Shehhi, 2. Fayez Ahmed, 3. Mohald (Mohammed) al-Shehri, 4. Hamza al-Ghamdi, 5. Ahmed al- Ghamdi na 6. Waleed al-Shehri.

Wengine ni 7. Wail al-Shehri, 8. Mohamed Atta, 9. Abdulaziz Alomari (al-Omari), 10. Satam al-Suqami, 11. Khalid al-Midhar, 12. Majed Moqed, 13. Nawaq (au Nawaf) al-Hamzi, 14. Salem al-Hamzi 15. Hani Hanjour, 16. Ahmed Alhaznawi, 17. Ahmed Alnami, 18. Ziad Jarrahi na 19. Saeed Alghamdi. Upo hapo?

Hao tuliambiwa na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kuwa walikufa katika tukio lile. Lakini ilibainika kuwa baadhi yao hawakuwa katika tukio hilo. Hata kama waliotajwa inawezekana kuwa ni kweli walikuwa katika ndege zile, madai ya kwamba walikuwa katika ndege hizo yanatosha kutuambia kuwa walikuwa magaidi na kwamba ndio walioteka ndege hizo siku hiyo?

Kama baadhi ya waliotajwa kuwa katika ndege zile walibainika kuwa hawakuwapo kwa sababu walijitangaza wako hao, kwanini tuamini kuwa na wale wengine ambao hawakujitangaza kama wenzao walikuwa katika ndege hizo? Madai ya kwamba walikuwako katika ndege hizo yanatosha kutufanya tusadiki? Kabla hujaamua kusadiki, tafakari kwa makini sana.

Soma orodha ya waliotajwa kuwa magaidi lakini baadaye ikagundulika kuwa haikuwa kweli. Pamoja na kwamba walitajwa katika orodha ya FBI kuwa walikuwa katika tukio hilo, baadaye waliibuka na kutangaza kushangazwa kwao na taarifa za FBI.

Hao ni 1. Waleed al-Shehri, 2. Wail al-Shehri, 3. Abdulaziz al-Omari, 4. Mohand al-Shehri, 5. Salem al-Hamzi, 6. Saeed al-Ghamdi na 7. Ahmed al-Nami. Je, kwa kutazama hilo kuna sababu ya kuwa na imani kwamba hata wale wengine wanaodaiwa kuwa walifia katika ndege hizo ni kweli walikuwamo? Na kama walikuwamo je, ni kweli ndio waliziteka?

FBI walisema hawa ndio magaidi wa Septemba 11, 2001, lakini walipogundua kuwa karibu nusu yao wako hai na wanaweza kujitetea tofauti na wale waliodaiwa kufa, FBI wakasema vitambulisho vyao viliibwa na kwamba wao si magaidi.

Kama waliiba vitambulisho, FBI waliwatambuaje kama magaidi? Septemba 23, 2001 Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilitangaza kuwa ‘watekaji’ wanne kati ya 19 waliotajwa na FBI walikuwa hai.

muellerBBC ilipomhoji Mkurugenzi wa FBI, Robert Mueller, kuhusu kuwapo hai kwa wale aliowataja kuwa walifia katika tukio la kigaidi, alisema: “…utambulisho wa watuhumiwa kadhaa una mashaka.” Utambulisho una mashaka? Kwamba hawakuwa na hakika na walichokitangaza?

Anayedaiwa kuwa nyuma ya ugaidi huo ni Osama bin Mohammed bin Awad bin Laden, au Osama (Usama) bin Laden, aliyezaliwa Saudi Arabia Jumapili ya Machi 10, 1957. Lakini ni kweli alihusika?

Lakini madai ya kwamba Osama alihusika ni hadithi ambayo FBI iliamua kuitunga na kuusimulia ulimwengu na mkurugenzi wake, Robert Mueller, kulazimika—angalau mara mbili, Septemba 20 na 27, 2001—kuzungumza kwenye kituo cha televisheni cha CNN na kukiri kwamba “…hakuna ushahidi wa kisheria unaothibitisha kuwa hao waliotajwa kuwa magaidi ni watekaji.”

Akitoa hotuba yake Ijumaa ya Aprili 19, 2002 katika Klabu ya Jumuiya ya Madola mjini San Francisco, California, Mueller alikiri hivi:

“Katika upelelezi wetu, hatujaweza kugundua kipande chochote cha karatasi— iwe ni hapa Marekani au katika hazina yoyote ya habari iwe ni Afghanistan au mahali pengine popote—kinachomhusisha mshukiwa yeyote na njama za Septemba 11.”

Alisema kilichoifanya FBI kushindwa kupata ushahidi wowote ni kwamba “…watekaji hawakuwa na kompyuta, hawakuwa na chochote…” Kama hivyo ndivyo, walijuaje kuwa wale 19 ndio waliziteka zile ndege wakati “… hawakuwa na chochote…” kilichowafanya wawatambue?

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba upelelezi ambao Mwanasheria Mkuu wa Marekani, John Ashcroft, alikaririwa na gazeti The Washington Post la Septemba 13, 2001 akiutaja kama “…ni upelelezi wa hali ya juu na wa kina zaidi kuwahi kufanyika katika Amerika…” ndio ambao Mueller aliiambia dunia kuwa haukuweza kugundua hata kipande chochote cha karatasi kinachomhuhsisha mshukiwa yeyote na njama za Septemba 11.

Mueller alisema mawakala 4,000 maalumu na wasaidizi wengine 3,000 na kiasi cha asilimia 25 ya makachero bingwa wa FBI, walishirikishwa katika upelelezi huo wa “hali ya juu na wa kina zaidi”. Hiyo iliwahusisha pia wataalamu bingwa 400 wa uhalifu ambao walipelekwa maeneo yote ya matukio.

Kwa kuzingatia yote hayo, nakubaliana na Ashcroft aliposema kuwa huo ni upelelezi wa “hali ya juu na wa kina zaidi”. Lakini hali hiyo inazaa swali muhimu sana katika jambo hili: kwa nini walisema hawakuweza “…kugundua kipande chochote cha karatasi…” wakati awali walisema kuna pasipoti ya gaidi mmoja waliiokota eneo la tukio?

Ashcroft, kwa mujibu wa The Washington Post lililotajwa hapo juu, alisema wapelelezi wamepokea zaidi ya vidokezi 100,000 na Mueller akasema vilikuwapo zaidi ya 200,000 ambavyo walikuwa wakivichunguza.

Wakati kila mmoja akisema lake, ni vigumu kuwaelewa wote kwa wakati mmoja. Ni vidokezi 100,000 au ni zaidi ya 200,000? Vyovyote iwavyo, hata kama vilikuwako 20,000 au hata 5,000 au hata 2,000 au hata 1,000 au hata 500, kwanini upelelezi huu wa “hali ya juu na wa kina zaidi” haukuweza “…kugundua kipande chochote cha karatasi…”?

Labda hayo ndiyo matokeo ya upelelezi wa kina zaidi. Kwa nini kile walichotueleza awali kuwa wana uhakika nacho baadaye kimegeuka na kuwa ni jambo la kubahatisha? Kwamba waliotajwa na FBI kuwa wamekufa baadaye walijitokeza na kusema wako hai?

Kama FBI ilikuwa na uhakika na kila jambo wanalofanya—au angalau walilofanya wakati huo—kwanini sasa walituambia “… hakuna ushahidi wa kisheria unaothibitisha kuwa hao (waliotajwa) ni watekaji”?

Kulingana na habari ya The Washington Post, Mueller alibadili kauli yake. Alidai kuwa baadhi ya washukiwa wa ugaidi na washirika wao wana uhusiano na makundi kadhaa ya kigaidi. Lakini alipotakiwa na mwandishi wa gazeti hilo, Kamran Khan, kuelezea madai yake kinaganaga, hakufanya hivyo.

Orodha ya kwanza ya FBI ya ‘watekaji’ ilitolewa Ijumaa ya Septemba 14, 2001. Maswali ya kutia shaka yalipoanza kuwa mengi, na baada ya waliotajwa kuwa wamekufa kujitangaza kuwa wako hai, ndipo ikatolewa orodha nyingine Septemba 27 ambayo ilikuwa na tofauti kidogo kwenye tahajia.

Orodha ya pili ilikuwa na majina ya ziada pamoja na lakabu. Kiungo kimoja katika tovuti ya FBI, http://www.fbi.gov/pressrel/penttbom/penttbomb.htm, kilikuwa na habari hiyo, lakini sasa hakipatikani, na pengine tayari kimeondolewa ili kisionekane tena.

Katika orodha hiyo, sawasawa na ilivyokuwa orodha ya kwanza, raia wa Saudi Arabia ndio walioitawala ambao wanadaiwa kuwa walikuwa wakiongozwa na Mohamed Atta, ambaye ni raia wa Misri, kwa niaba ya Osama bin Laden, ambaye naye ni raia wa Saudi Arabia.

Ukiitazama vyema orodha hiyo, na ukachunguza wasifu wa kila mmoja wao, utagundua kuwa hakuna raia hata mmoja wa Afghanistan aliyeshiriki au kushirikishwa katika mpango huo. Huo ndio ukweli wenyewe. Ndio ukweli halisi. Hata kama ingekuwa kweli kwamba waliotajwa na FBI ni kweli ndio walioziteka ndege zile na kuteketea nazo, bado hakukuwa na jina hata moja la raia wa Afghanistan au Iraq.

Historia itakayosimama kama shahidi wa jambo hili itashuhudia kuwa hakuna raia hata mmoja wa Afghanistan aliyetajwa katika orodha yoyote ya FBI kwamba alihusika katika ‘ugaidi’ wa Septemba 11. Nasisitiza tena, kama tukio hilo lilifanywa na Waarabu wa kutoka Mashariki ya Kati, hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyetoka Afghanistan wala Iraq.

Kwa maneno mengine, hakuna raia hata mmoja wa Afghanistan wala Iraq aliyehusishwa kwa vyovyote, kwa namna yoyote na kwa wakati wowote na ugaidi uliofanyika Marekani Septemba 11, 2001. Lakini inashangaza kwamba kile kilichoitwa VITA DHIDI YA UGAIDI kilizushwa dhidi ya Afghanistan huku Saudi Arabia, ambako kunadaiwa kuwa ndiko walikotoka magaidi wengi, ikasimama nyuma ya Marekani kama mshirika wake katika vita hiyo.

Lakini Afghanistan na Iraq, ambako hakuna hata raia wake mmoja aliyetajwa kushiriki katika ugaidi huo, ndizo zilizovamiwa na Marekani kwa kisingizio cha VITA DHIDI YA UGAIDI. Ninapokuwa nikijadili mada kama hizi na kuhisi akili ikitekenywa ndipo ninapokosa mahali pa kuweka koma au nukta.