Home Makala ‘Tumekuwa kama fisi anayesubiri mkono udondoke’

‘Tumekuwa kama fisi anayesubiri mkono udondoke’

596
0
SHARE

Na Gabriel Mwang’onda

Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter MuhongoMIONGONI  mwa mbinu zinazotumika kukwepa kodi ni uanzishwaji wa kampuni nchi moja kama Tanzania na kuifanya nchi hiyo kuwa msambazaji wa madini ghafi.

Hili linathitishwa nchini mwetu kwa kutokuwa na refinery ya madini. Matokeo yake tunauza madini ghafi kwa bei ya kutupwa.

Yapo mambo mawili yatazuka kwa wakati mmoja ambayoni transfer pricing and mis-invoicing.

Inafahamika kwamba soko kubwa la madini ghafi toka Tanzania ni Afrikia Kusini, sababu kubwa ni kwamba Afrika Kusini imeingia makubaliano ya kodi (Double Taxation Agreements) maarufu kama DTA’s na Mauritius kisiwa ambacho corporate tax ni asilimia 3, no capital gain taxes, no withholding taxes on dividends kwa kifupi hiki kisiwa kimekuwa tax haven.

Kuna wafanyabiashara kadhaa wakubwa nchini wamesajili kampuni zao huko, Kwa leo ambalo leo sitaongelea. Afrika Kusini kuingia makubaliano hayo na Mauritius imekuwa ni rahisi watu kusajili kampuni zao Mauritius na kuziendesha shughuli zao Afrika kusini maana ya kuchakata madini ili wayaongezea thamani zaidi na kuyauza. Mifano hai ipo nadhani kila mtu anajua.

Nini maana ya hayo sasa? Kampuni hiyohiyo iliyosajiliwa Tanzania itatoa ripoti ya hasara kwakuwa inauza madini ghafi kwa bei ya kutupwa, na mteja wao mkubwa anakuwa mmoja tu ambaye yupo Afrika Kusini lakini ni kampuni hiyohiyo bali ni tanzu yake. Kama haitoshi ile kampuni ya Afrika Kusini itakuwa imetokea Mauritius.

Kwakuwa kuna makubaliano kati ya Afrika Kusini na Mauritius basi kodi itaenda kutozwa Mauritius ambako hata hivyo hawatozwi kodi kwakuwa Mauritius ni pepo ya kodi. Mwishowe watatoa ripoti ya faida katika soko la hisa la London (London stock exchange market) ambako wameorodhesha hisa zao huku kwetu tunabaki kuwaona kwenye taarifa za kibiashara za Bloomberg kwamba wametoa gawio kwa wanahisa wao.

Kwa mtiririko wa maelezo hayo hapo juu basi unaweza kuona ni jinsi gani Tanzania inaporwa mali zake iwe kwa makusudi ya watangulizi walioingia mikataba hiyo au kwa kutokujua.

Hata hivyo kampuni hizo haziishii hapo kama ambavyo Glencore inavyoiba kodi kwenye madini ya kopa hapo kwa wadogo zetu Zambia na kuwaorodheshwa kwenye masoko makubwa ya mitaji kama London Stock Exchange ndivyo vivyo hivyo makampuni yanayochimba dhahabu nchini kwetu yameweza kujiorodhesha kwenye masoko ya mitaji huko London na wengine hapa nyumbani. Na kuripoti faida kubwa kabisa huko na kugawana gawio huku Tanzania ikipewa ripoti inayoonyesha hasara tangu waanze kuchimba madini. Inasikitisha lakini ndiyo hali halisi ambayo unaweza kuitazama kupitia televisheni ya biashara ya Bloomberg.

Nchi kubwa zenyewe zinamiliki baadhi ya visiwa ambavyo ni pepo ya kodi,vipo takribani 80 duniani kwa sasa. Hili ni jambo linawasumbua hata wao wenyewe (The establishments) . kashfa ya Panama papers zimeonyesha ni jinsi gani vita imekuwa ngumu kwa sababu hata viongozi wakubwa duniani wanaoaminiwa wamekuwa vinara wa kukwepa kodi. Kampuni makubwa kama Apple, Starbucks zimekuwa vinara kwa kukwepa kodi.

Leo nimezungumzia hivyo kwa sababu kuna bajeti inasomwa bungeni na kuna ongezeko la kodi, maeneo ya ongezeko la kodi mengi ni kwa raia wa kawaida tofauti nilivyotegemea kuwa sekta ya madini  itaguswa ili Watanzania waanze kufaidi uwepo wa Madini waliyopewa na Mungu.

Suluhu ambayo ningeomba iwe ni ya msingi ni mabadiliko ya ITA (Income Tax Act ) kuna vipengele vingi ambavyo nitavianisha mbeleni ili kuhakikisha tunakuwa na matunda yatakayofaidiwa na Watanzania wote. Kama hatua za awali.

Ninapoandika makala haya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wamefungua kesi lukuki kudai kodi kutoka kwenye kampuni hizo, lakini sheria ya ITA haiwapi ushindi, ni wakati sahihi sasa kuangalia kesi hizo ili kuweza kuziba mianya.

Inagharimu dola milioni 60 kujenga kiwanda cha kuchakata madini, na hii huongeza ajira pia mapato. Yafaa tutumie ili tupate.

Kwa mfano tumetumia dola milioni 136 kujenga Daraja la Kigamboni huku tumeshindwa kuona kama ‘refinery’ ni kipaumbele ambacho kwa muda mfupi kingekuja kujenga hilo daraja. Hapa unaweza kuona jinsi tunavyokosea kupanga vipaumbele. Achana na faida za Daraja la Kigamboni maana itachukua miaka mingi kurudisha faida.

Narudia tena sipingi ujenzi wa daraja hilo bali nimeonyesha ni jinsi gani kupanga vipaumbele vyetu kulivyo na umuhimu kwa kuzingatia mahitaji ya nchi husika. Nasubiri ikifika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, tutaona wabunge wetu wataendelea kuimba wimbo wetu ule usio na kiitikio kwamba tuna nchi tajiri yenye watu maskini. Huu ni wimbo tumeanza kuusikia tangu tuzaliwe wengine hauna mwisho, tuchukue hatua na tuache kuimba wimbo huo.

Hakuna kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini  hadi aonyeshe hata nia ya kujenga ‘refinery’. Ukiwauliza watakwambia tunasubiri wawekezaji watoke nje. Huu nao ni ugonjwa mwingine unaofaa kutibiwa utasubiri mwekezaji  hadi lini? Yaani tunakuwa kama fisi anayesubiri mkono wa mtu udondoke. Ni wazi kwamba makampuni makubwa hayataruhusu hilo kutokea kwa gharama yeyote.

Kwa umuhimu wa kiwanda cha aina hiyo serikali haina budi  kuwa mmliki au mbia mkubwa ili kuweza kudhibiti mapato yake vizuri. Ukimweka mtu mwingine ni hasara kubwa kwa serikali kwa sababu sasa hivi tuna TMAA ( Tanzania Mineral Audit Agency) lakini ni nini walichofanikiwa mpaka leo.

Katika kanuni bora za usimamizi wa kodi mojawapo kuwa, gharama za kukusanya kodi zisizidi kodi yenyewe. Sasa tunataka tuanze kuingia gharama kubwa ya kuanza kufukuzana mitaani kukusanya kodi kufungana na kufungiana biashara, kufilisiana huku wazungu wakituona kama maboya, ama tumelaaniwa au tumerogwa.

Kama wabunge watasimama pamoja kuhakikisha sekta ya madini inatoa mchango stahiki basi hatutasumbuana tena mitaani. Mimi siwatetei wakwepa kodi ila naumia kuona mali zinaibiwa tena na wageni huku mangi mwenye ‘kiosk’ anayeishi kwa kudra anakabwa mpaka anashindwa kuishi kwa amani.

Katika kila dola moja inayotolewa kama msaada Afrika, basi Afrika hupoteza zaidi ya dola 30. Sasa wengine tumeamua kuhakikisha hiyo dola 30 inabaki na hiyo dola moja waondoke nayo. Ni jambo la kusikitisha kuona hata wabunge wanasahau kabisa dola 30 na wanaililia dola moja sababu inaonekana kirahisi zaidi ya ile dola 30 iliyofichika sana. Hebu  tuamke basi. Yafaa waaanze kutafuta taarifa ili kuliokoa na madini yaonekane kuwa ni neema si laana.