Home Habari Waliotumbuliwa waigharimu Serikali

Waliotumbuliwa waigharimu Serikali

851
0
SHARE

Rished BadeGABRIEL MUSHI NA MARKUS MPANGALA

WATENDAJI na watumishi wa umma waliosimamishwa na wengine kutenguliwa nafasi zao wanadaiwa kuigharimu serikali mamilioni ya fedha kutokana na kuendelea kulipwa mishahara. RAI limebaini.

Tangu Rais  John Magufuli aingie madarakani ameshawatumbua majipu zaidi ya watumishi 160, huku wengine akiahidi kuwapangia kazi nyingine, ambazo hajapangiwa hadi sasa.

Miongoni mwa watu waliowekwa pembeni kwa ahadi ya kupangiwa kazi nyingine ni Makatibu na Naibu Makatibu wakuu zaidi ya 20.

Uchunguzi wa RAI umebaini kuwa mshahara wa katibu mkuu na naibu wake ni kati ya Sh. milioni tatu au zaidi kwa mwezi.

Makadirio hayo yanaifanya Serikali kutumia kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 260 kuwalipa makatibu wake wanaosubiri kwa zaidi ya miezi minne sasa kupangiwa kazi nyingine.

Hali hiyo inatajwa kuondoa dhana ya Rais Magufuli ya kubana matumizi kwani hadi kufikia sasa ni makatibu wakuu wawili tu walioahidiwa kupangiwa kazi nyingine ndiyo wameipata nafasi hiyo.

Makatibu hao ni aliyekuwa Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Jumanne Sagini na aliyekuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donald Mmbando

Sagini ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu na Mmbando ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira katika Serikali ya awamu ya nne, Dk. Makongoro Mahanga, ameliambia RAI kuwa hakuna ubanaji wa matumizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano kwani ni dhahiri watumishi hao wamekuwa wakiitia hasara serikali.

“Kiutaratibu mtumishi wa serikali akisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi au akitenguliwa uteuzi wake na kusubiri kupangiwa kazi nyingine, huendelea kupokea mshahara wake wote kama ilivyokuwa awali.

“Kwa maana hiyo hawa makatibu wakuu na manaibu wao zaidi ya 22 wameendelea kupokea mishahara bila kufanya kazi yoyote kwa sababu wanasubiri uchunguzi ukamilike au kupangiwa kazi nyingine.

“Sasa ni miezi minne imekatika tangu wawekwe kando na Rais Magufuli na hakuna chochote kilichofanyika kuepuka gharama hizi zisizo za lazima, kwa sababu kwa taratibu za kazi kiongozi hatakiwi kukaimu nafasi kwa muda wa zaidi ya miezi sita ila hapa kwetu tunaona wanakaa hata zaidi ya miaka mitatu,” alisema.

Kaimu Msemaji wa Ikulu, Gerson Msigwa, akitoa ufafanuzi wa suala hilo, alisema uongozi ni gharama na kwamba walioahidiwa kupangiwa kazi nyingine si kama wamesahaulika bali wanapaswa kuendelea kusubiri uamuzi wa Rais.

“Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua, kutengua na kumfukuza kazi mtumishi yeyote.

“Lazima kutambua kuwa uongozi ni gharama, kwa maana hiyo hatuwezi kumharakisha Rais eti awapangie kazi hao aliotengua uteuzi wao kwa sababu wanaisababishia serikali hasara kwa kuendelea kupokea misharaha. Hili ni jambo ambalo haliwezekani.

“Rais ana taratibu zake kwani anachukua hatua kulingana na uchunguzi wa vyombo husika, kwa sababu hiyo maamuzi anayoyafanya yanatokana na kukamilika kwa mchakato wa hatua mbalimbali za kisheria kwani naye anafuata sheria kama ilivyomruhusu kutengua,” alisema.

Pamoja na kauli hiyo ya Msigwa, pia zipo taarifa kuwa Rais Magufuli hayuko tayari kufanya kazi na baadhi ya Makatibu Wakuu aliotengua uteuzi wao na katika kuhakikisha hilo linatimia tayari ameagiza wapewe barua za kustaafu kwa hiyari.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani Novemba 5, mwaka jana amekuwa kwenye mkakati mzito wa kuisafisha Serikali yake kwa kuwaweka pembeni watumishi wasioendana na kasi aliyokusudia kuitumia katika kipindi chote cha utawala wake.

Hatua yake hiyo imechagizwa na utumbuaji wa majipu ambayo imegawanyika katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni lile linalowajumuisha watumishi wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali na kundi la pili ni la wale wasioendana na kasi ya Rais.

WANAOENDELEA KULIPWA MSHAHARA

Baadhi ya watendaji wanaoendelea kulipwa mshahara na Serikali huku wakisubiri kupangiwa kazi nyingi ama kukamilika kwa uchunguzi ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Dk. Ramadhani Dau.

Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango-Malecela, aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Wilson Kabwe  na aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), George Nyatega, ambaye alitupwa nje na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kufuatia madai ya udhaifu wa kiutendaji usioridhisha katika taasisi hiyo.

Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji, Utoaji mikopo Onesmo Laizer.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Dk. Julieth Kairuki  ni mmoja wa watu wanaosubiri kupangiwa kazi nyingine baada ya Rais kutengua uteuzi wake kwa madai ya kutopokea mshahara wake tangu mwaka 2013 alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Dk. Ali Simba ni miongoni mwa watendaji waliokumbwa na fagio la Rais.

Aidha, vigogo 23 wa Mamlaka ya Bandari (TPA) walisimamishwa kazi sambamba na kutenguliwa kwa uteuzi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi Profesa Joseph Msambichaka pamoja na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe.

Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Gabriel Nderumaki  na kumteua  Tuma Abdallah kukaimu nafasi hiyo.

Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya taifa (NIDA) Dickson Mwaimu  ni miongoni mwa watu wanaosubiri uamuzi wa Rais.

Rungu la Magufuli kwa Mwaimu pia liliwakumba wasaidizi wake ambao ni Joseph Makani, Mkurugenzi wa TEHAMA, Rahel Mapande, Ofisa Ugavi Mkuu, Sabrina Nyoni,  Mkurugenzi wa Sheria na Ofisa Usafirishaji George Ntalima.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dk. Edward  Hosea naye uteuzi wake ulitenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Valentino Mlowoka.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Rished Bade ni mmoja wa wanaosubiri uamuzi wa Rais baada ya uteuzi wake kutenguliwa mara baada ya Rais Magufuli kukabidhiwa nchi.