Home Habari Bajeti 2016/2017 ngumu

Bajeti 2016/2017 ngumu

557
0
SHARE

MAGUFULI1NA SHABANI MATUTU,

BAJETI ya mwaka wa fedha 2016/17 ya kiasi cha shilingi trilioni 21, inadaiwa kuwa ngumu kutekelezeka. RAI linaripoti.

Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya uchumi wamebainisha kuwa upunguaji wa mizigo bandarini na  hatua ya wafanyabiashara wengi kupunguza kasi ya uingizaji na utoaji wa bidhaa nje ya nchi na  kufungiwa kwa kampuni 210 za uwakala vinaweza kuwa chanzo cha kupunguza kasi ya ukusanyaji wa kodi.

Kwamba hali ikiendelea ilivyo sasa upo uwezekano mkubwa wa kushuka kwa makusanyo ya kodi hali inayosababisha kutofikiwa kwa lengo la bajeti ya mwaka huu wa fedha kutegemea pato la ndani.

Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) inatarajiwa kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 19 kwa mwaka, lakini tayari zipo taarifa kwa kutofikiwa kwa kiwango hicho.

Wataalamu mbalimbali wa uchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, kwa nyakati tofauti wameliambia RAI  kuwa hali ya mambo ikiendelea hivi ilivyo sasa upo uwezekano mkubwa wa kukusanya kiasi cha Sh trilioni 14.5 na ikizidi sana ni Sh. trilioni 15.

Taarifa za TRA zinaonyesha kuwa  makusanya ya kodi kwa  mwaka 2015/2016 yamefikia kiwango cha Sh. trilioni 12.363.

Taarifa zinasema kwamba mara baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani na kuweka msisitizo kwenye ukusanyaji wa kodi, hali ya ukusanyaji ilibadilika kwa makusanyo ya mwezi kuongezeka, lakini kwa mwenendo wa sasa mambo yamekuwa tofauti kwani makusanyo yameanza kudorora kutokana na kukosekana kwa vyanzo vya uhakika vya mapato.

Watoa taarifa wetu walibainisha kuwa kwa mwezi Disemba mwaka jana lengo la ukusanyaji wa kodi lilikuwa ni Sh. trilioni 1.346.

Hata hivyo walkifanikiwa kuvuka lengo la kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 1.403.

Mafanikio hayo yanadaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na mipango kazi iliyokuwa imeachwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Inadaiwa kuwa mwezi Januari lengo lilikuwa kukusanya Sh. trilioni 1.059,  ambalo lilivukwa na kukusanya Sh. trilioni 1.079.

Mwezi Februari lengo lilikuwa kukusanya Sh. trilioni 1.028, TRA ikafanikiwa kukusanya Sh. trilioni 1.040.

Machi mwaka huu lengo lilikuwa ni kukusanya Sh. trilioni 1.302 lakini fedha zilizopatikana hazikupanda wala kushuka kwa kuwa zilisalia pale pale pa mwezi Februari.

Katika kipindi cha Aprili 2016 ilipunguza kiwango cha makadilio ya ukusanyaji na kuwa Sh. trilioni 1.040, hata hivyo lengo halikufikiwa kwani walikusanya Sh. trilioni 1.030.

Hali hiyo inatafsiriwa kama dalili ya kuporomoka kabisa kwa makusanyo kama hakutakuwa na jitihada za makusudi za kuwajengea wafanyabiashara mazingira mazuri ya biashara  yasiyo na vitisho.

Akielezea baadhi ya sababu zinazoweza kushusha ukusanyaji wa mapato mfanyabiashara, Golfanil Kamilly, ameliambia RAI kwamba hofu iliyowatawala wawekezaji inaweza kuwa sbabu kwani wengi wao hawaingizi mizigo mipya, badala yake wanauza iliyopo na wale waliomaliza wanatafuta namna nyingine.

Suala la kuporomoka kwa uchumi limewahi kuonywa na Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe alisema uchumi wa nchi unaweza kushuka kwa uamuzi wa kutenga wafadhili na kuporomoka kwa makusanyo ya ndani.

Hadi sasa inaelezwa kwamba wafadhili waliotangaza kuunga mkono bajeti ya Tanzania wamejielekeza kufadhili miradi midogomidogo ya maendeleo.

Hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka jana, mifuko sita ya hifadhi ya jamii ilikuwa ikiidai Serikali kiasi cha Sh. trilioni 7.134 ambazo ni mikopo pamoja na riba.

Mifuko hiyo ni Mfuko wa Akiba wa Watumishi Serikalini (GEPF), Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Jamii kwa Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSPF), na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Kiasi ambacho mifuko ya jamii inaidai Serikali kwenye mabano ni PSPF (Sh. trilioni 4.828), NSSF (Sh. trilioni 1.334), NHIF (Sh. bilioni 458.6), PPF (Sh. bilioni 288.6), LAPF (Sh. bilioni 207.7) na GEPF (Sh. bilioni 18).

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa George Shumbusho anasema kwamba suala la kushuka kwa mapato linachangiwa na wafanyabishara wa kampuni za uwakala wa upakuaji na upakiaji wa mizigo kusimama kufanya kazi hiyo.

“Wengi wameachana na biashara wakiogopa kubanwa kwa kutoa rushwa ili kuruhusu mizigo yao ipite, lakini kwa sasa wanaofanyakazi ni wafanyabiashara wachache ambao ni waaminifu wanaolipa kodi kama inavyostahili huku wale wengi wasikuwa waaminifu wakisubiri kama serikali italegeza kamba na kuwaachia waendelee kufanyakazi katika taratibu za kutoa rushwa,” alisema Shumbusho.

Profesa ambaye pia ni Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho  alisema hali hiyo imechangia kushuka kwa mapato hali inayofanya serikali kukusanya mapato kwa hao wachache waaminifu wanaofuata taratibu kwa mujibu wa sheria.