Home kitaifa Watendaji, mawaziri jifunzeni kwa CAG

Watendaji, mawaziri jifunzeni kwa CAG

565
0
SHARE

raiPAMOJA na ukweli kwamba Rais John Magufuli, anajitengenezea taswira ya kuogopwa na watendaji, mawaziri wake lakini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad amejitoa katika mtego huo wa kuwa mwoga.

Mtendaji huyo amejitoa katika kundi la viongozi na watendaji wanaotii kila amri inayotolewa na Rais Magufuli hata kama haina mashiko kwa mustakabali wa taifa.

Sababu kubwa ya CAG kutokubalina na kila kitu imechangiwa kwa kiasi kikubwa na wengi kuwa waoga wa kuhofia kutumbuliwa endapo watabainika kwenda kinyume na mkuu huyo wa nchi hata kama atakuwa amepotoka.

CAG amekuwa tofauti na watendaji wengine kwa sababu amegoma kufanya kazi kwa woga, amekataa katakata kuwa kokoro linalotumiwa na wavuvi kuvulia samaki likizoa kila aina ya uchafu unaokuwa baharini.

Profesa Assad amegoma kukubali kufanya mambo kwa kwa woga badala yake amesimama kuangalia majukumu yake ya kazi yanasemaje bila ya kujali kama atapewa sifa na Dk. Magufuli.

Uwezo wake, uwazi, kujiamini na kusimamia majukumu yake kiufasaha kumemuwezesha kuzungumza ukweli bila kujali kama ataumizwa kwa kiasi gani na ukweli atakaokuwa ameusema.

CAG pamoja na kutambua kuwa Rais ndiye anayefanyia kazi kila ripoti anayotoa, lakini amegoma kuwa daraja la kuficha uchafu uliowahi kufanyika kwenye wizara aliyopitia Rais wakati akiwa waziri wa ujenzi katika serikali iliyopita.

Ninachoamini ni kwamba kama Pofesa Assad angekuwa kama watendaji wengine wenye woga wa kunguru wa kuogopa mbawa zao, angeficha uozo na madudu yaliyofanyika wakati Rais Magufuli akiwa katika wizara hiyo, akipania kupalilia kibarua chake.

Katika ripoti yake aliyoitoa hivi karibuni na kumkabidhi rais, CAG ameonyesha kuwepo kwa madudu kadhaa katika taasisi mbalimbali za serikali.

Pamoja na kuonyesha madudu hayo hakupepesa macho kutaja wizara na taasisi zilizokuwa chini ya Rais  Magufuli zilizofanya madudu hayo wakati zikiwa chini yake.

Katika makala haya nitaelezea maeneo yaliyoguswa na ripoti ya CAG, Assad yakimgusa mkuu wa kaya, Rais Magufuli wakati akiwa waziri wa Ujenzi ni utendaji wa Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (Temesa).

Taasisi nyingine iliyoguswa iliyokuwa chini ya wizara hiyo ni Wakala wa Barabara (Tanroads).

Katika taarifa yake, CAG alisema Temesa imenunua kivuko chenye kasi ndogo kuliko ilivyotarajiwa na hadi ulipokuwa unafanyika ukaguzi Agosti 2015, chombo hicho kilikuwa hakifanyi kazi kwa zaidi ya mwaka.

CAG anakwenda mbali katika ripoti yake hiyo na kutaja dosari katika ununuzi wa kivuko hicho kutumia thamani ya Sh. 7,916,955,000 ambazo ziliridhiwa na Wizara ya Ujenzi iliyokuwa chini ya Dk. Magufuli kupitia Temesa.

Mkataba huo wa manunuzi ya kivuko hicho uliingiwa na kampuni ya M/s Johs.Gram-Hanssen Bergensgade 10, DK 2100 Copenhagen Oe Denmark cha Dar es Salaam kwenda Bagamoyo.

CAG hakujali kama Dk. Magufuli ndiye alikuwa waziri wa wizara hiyo, kama ndiye aliyewaaminisha Watanzania kwamba ni kivuko chenye ubora na cha kisasa wakati wa usainishaji wa mpango huo.

Profesa Assad ameamua kuweka mambo wazi kwa kusema dosari zilizobainika katika manunuzi hayo kuwa ni kasi ya kivuko hicho kutozingatia matakwa ya mnunuzi.

Ripoti hiyo imebaini kwamba Watanzania walielezwa na ofisi ya zamani ya Dk. Magufuli wakati wa usainishaji wa mikataba kwamba kivuko hicho kingekuwa na kasi ya kiwango cha knots 20, hali hiyo imekuwa tofauti na kuwa knots 17.25.

Tatizo jingine alilobaini kufanyika ni kivuko kukabidhiwa bila hati ya makabidhiano Novemba 17, 2014 baada ya ucheleweshwaji wa siku 16, na pia akabaini hadi wakati wa ukaguzi, Agosti 2015, hati ya makabidhiano ilikuwa haijatolewa na mzabuni.

Ununuzi wa feri hiyo umewahi kuzua sakata bungeni huku wabunge wa upinzani wakilalamika kwamba lilikuwa bomu kwani kinatumia zaidi ya saa tatu kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo badala ya dakika 45 za gari za kwenda eneo hilo.

Eneo jingine alilogusa CAG, Assad ni malipo yaliyofanywa na Tanroads kwa makandarasi waliomaliza kazi zao, kwa madai kwamba taasisi hiyo ilionesha matatizo makubwa ya udhaifu katika menejimenti.

Assad bila woga wala kujali rais Magufuli atamchukuliaje ameamua kuonesha namna ambavyo Tanroads, imeingia mikataba mbalimbali ya ujenzi wa barabara na madaraja wakati ikiwa chini ya rais.

Anaonyesha kwamba wakati wa ukaguzi amebaini kwamba baadhi ya mikataba haikukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na kuchelewa kwa ulipaji wa fedha kati ya mikataba 16 hivyo kusababisha ulipaji wa riba kupaa na kufikia Sh. 5,616,652,022 na dola za Marekani 686,174.86.

Jambo jingie la kupigiwa mfano wa kuigwa ni kwamba mtendaji huyo ndiye pekee amefungua mdomo na kukosoa hatua ya Rais Magufuli kuwanyima wafanyakazi wa ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NOAT), kutopewa ruhusa ya kwenda nje ya nchi kuhudhuria mikutano ya kupeana ujuzi.

Assad alipinga wafanyakazi wake kunyimwa kibali hicho katika mkutano wa ufunguzi wa Baraza la kwanza la Wafanyakazi hao, ambapo alisema pamoja na hali ya fedha serikalini kuwa mbaya lakini kuruhusiwa kwa wafanyakazi hao kwenda nje ya nchi kuhudhuria mikutano nje ya kupeana uzoefi ni jambo jema kwao na nchi kwa ujumla.

Wakati wakuu wa taasisi nyingine wakilalamikia chini kwa chini bila kuibuka yeye ameibuka na kusema kwa mfano hivi karibuni baadhi ya taasisi zimekuwa zikilalamikiwa wakurugenzi wake kupeana mishahara minono tofauti na ukweli lakini hakuna aliyethubutu kuibuka na kukanusha taarifa hizo waziwazi na badala yake wamekuwa wakisema chini chini.