Home Makala Kwanini Serikali inatishwa?

Kwanini Serikali inatishwa?

434
0
SHARE

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa, Jumanne MaghembeKAMPUNI ya uwindaji wa kitalii ya Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Limited imeamua kutangaza vita na serikali ya Tanzania ili kuhakikisha kwamba inarejeshewa kitalu cha uwindaji cha Lake Natron Game Controlled Area (East) kwa njia yoyote ile.

Ni mpambano mkali ambao kampuni hiyo yenye vinasaba vya Marekani kwa kiasi kikubwa lakini sura ya Kitanzania kwa uchache sana imeamua kwamba itauendeleza kwa kutumia njia zozote zile halali na haramu.

Chimbuko la mgogoro wote huu ambao kila uchao unapewa sura mpya na Wengert ni kitendo cha kampuni ya Green Miles Safaris Limited ambayo ilipokwa kitalu hicho cha Lake Natron East baada ya kutuhumiwa kwamba ilikuwa ikifanya utalii wa kuwinda bila ya kufuata sheria.

Uchunguzi umeonyesha na kuthibitisha kwamba uamuzi uliofanyika wa kuipoka kampuni ya Green Mile Safaris kitalu hicho haukuwa sahihi kwa sababu tuhuma zilizoelekezwa kwa kampuni hiyo kama mmiliki wa leseni ya uwindaji wa kitalii katika kitalu hicho hazikuwa sahihi.

Tuhuma zilizoelekezwa kwa mmiliki wa leseni zilikuwa zinatakiwa zielekezwe kwa wasimamizi wa uwindaji wa kitalii, ambao ni watumishi wa umma na muwindaji bingwa   na si kwa mmiliki wa leseni.

Mmiliki wa leseni shughuli yake kubwa ni kutafuta biashara, kuwezesha watalii kufika katika kitalu cha uwindaji na kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa mahali pake kufanya mtalii afurahie mapumziko yake.

Suala la uwindaji ikimaanisha kuhakikisha uwapo wa vibali vyote, aina ya mnyama, silaha zinazotumika na watu wanaoruhusiwa kufanya uwindaji huo ni shughuli ya askari wanyamapori ambaye ni mwajiriwa wa wizara na muwindaji bingwa (professional hunter).

Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha uamuzi uliofikiwa ni kumwadhibu mmiliki wa leseni kwa kumnyang’anya kitalu jambo ambalo lilimlazimisha mmiliki huyo kukata rufaa kwa waziri wa maliasili na utalii.

Kampuni ya Green Mile Safaris ilifanikiwa kurejeshewa kibali chake baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii kujiridhisha kuwa kulikuwa na makosa katika kuifungia kampuni hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mmiliki wa kampuni hahusiki na wageni wanapokuwa wakiwinda.

Ni uamuzi huo wa kuirejeshea leseni Green Mile ndio unaichanganya kampuni ya Wengert Windrose Safaris na hadi kujikuta wakifanya mambo ambayo yanawafanya watu kujiuliza kulikoni? Kwanini kampuni hii inang’ang’ania umiliki wa kitalu hicho cha Lake Natron kama vile hakuna tena vitalu vingine hapa nchini?

Katika kujitahidi kukipata kitalu hicho Wengert walilazimika kuongea na Green Mile Safaris na kuomba iwauzie hicho kitalu jambo ambalo kampuni hiyo ilikataa. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni kwamba Green Mile ilieleza kuwa itakuwa tayari kuwauzia safari kwa maana ya biashara na si kitalu.

Kitendo cha Green Miles kukataa kukubali ombi la Wingert la kuiuzia kitalu hicho ndipo uhasama wa wazi ukaanza. Zipo taarifa kwamba ilifikia hatua watu wanaodaiwa kuwa ni wakala wa Wingert walikwenda kuchimba mitaro katika barabara za kurushia ndege ili kusababisha ajali. Tuhuma hizo zilifika hadi serikalini.

Hiyo ni baada ya kuwapo pia tuhuma kwamba Wingert waliwatishia nyau Green Mile na kuwaambia kwamba watahakikisha wanashindwa kufanya biashara. Kuna nini katika kitalu hicho?

Katika vurugu hizo za kutaka kuihamisha kwa nguvu Green Mile kutoka huko Lake Natron wakati wa ziara ya Marekani huko Revo-Nevada katika maonesho ya kuuza safari za utalii wa kuwinda inadaiwa mawakala wa Wengert waliwafanyia fujo maofisa na mawakala wa Green Mile kiasi cha asasi ya Safari Club International kuingilia katika na kutafuta suluhu.

Wingert baada ya kuona kwamba uwezekano wa kupata kitalu hicho cha Lake Natron East unazidi kufifia ikaamua kutoa tuhuma kwamba vitalu vya Lake Natron vimebadilishwa majina makusudi ili kitalu chao apewe Green Miles. Hata hivyo, ukweli ni kwamba majina hayo yalibadilishwa ili kuendana na majina ya maeneo halisi kijiografia vilipo vitalu vyenyewe.

Tuhuma hiyo Wingert waliitoa kama njia ya kuonesha kwamba kitalu wanachomiliki wao kihalali ni kile ambacho kilikuwa Lake Natron East ambacho kiuhalisia ndicho kitalu cha Green Mile. Inaelekea kwamba Wingert wapo tayari kufanya lolote ili kupata hicho kitalu cha Lake Natron East. Swali ni kwamba kwa ninny kitalu hicho? Kuna nini katika eneo hilo ambalo kampuni hiyo imeamua hadi kwenda ndani ya serikali ya Marekani kutaka iingilie kati ili warejeshewe?

Kisheria Wengert walitakiwa kuwa wameondoka katika kitalu cha Lake Natron (North) Machi 31, 2013 baada ya msimu wa uwindaji kuwa umemalizika. Hata hivyo, kama vile kutaka kuendeleza ujeuri wao waliamua kutoondoka na kukimbilia mahakamani baada ya kutokuridhika na majibu ya rufaa waliyowasilisha kwa Waziri wa Utalii. Hata pamoja na kushindwa katika rufaa kampuni hiyo iliamua kukalia kitalu hicho kwa mabavu.

Mmiliki wa kitalu hicho Green Mile alilalamika kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori kwamba anataka kuanza ujenzi wa miundombinu katika kitalu hicho kujiandaa kwa biashara jambo ambalo lilimfanya ofisa huyo kuwaandikia Wengert barua ya kuwataka kuondoka katika muda wa siku tatu kuanzia Mei 20, 2013.

Pamoja na amri hiyo ya Mkurugenzi wa Wanyamapori Wengert badala ya kuitekeleza kama ilivyoagizwa waliamua kukata rufaa Mei 23, 2013 kwa kumuandikia Waziri.

Katika barua hiyo Wengert waliomba kitalu ambacho kinaitwa Lake Natron  North ambacho kimebadilishwa jina na kuwa Lake Natron East wapatiwe wao. Sanjari na hilo walitaka pia waziri asitishe amri ya Mkurugenzi wa Wanyamapori kuwataka wawe wameondoka katika kitalu hicho katika muda wa siku tatu tangu kupata barua.

Pamoja na waziri wa utalii kumwagiza Mkurugenzi wa Wanyamapori kuitisha kikao ili kutafuta suluhu, pamoja na kufanyika lakini kampuni ya Wengert katika mazingira ya kutatanisha ilisema kwamba yenyewe haipo tayari kusikia lolote isipokuwa kuachiwa kufanya biashara katika kitalu kile.

Katika utendaji wa shughuli zake Wengert imekuwa kila wakati ikiingia katika vikao na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na za masjala ya siri na ambazo si rasmi lakini kutoka katika ofisi za serikali jambo ambalo linaashiria kutumia njia za panya kutafuta namna ya kupata ushindi.

Kampuni ya Wengert imekuwa ikifanya kila njia kutaka kumilikishwa hicho kitalu hata pamoja na kushindwa kesi zote ambazo imezifungua kwa ajili ya kufanikisha azma yao hiyo.

Taarifa ya vitendo vya hujuma na uhuni uliofanywa na maofisa na mawakala wa Wingert katika kitalu hicho ni nyingi.

Hata hivyo pengine ni vyema kukariri vile ambavyo vimetolewa taarifa rasmi kama Julai 5,2013 Wingert ilipozuwia uwindaji kufanyika huku wafanyakazi wa kampuni hiyo walipojaribu kuwagonga na gari wageni wa Green Mile na kudaiwa pia kuchimba mahandaki kwenye barabara ya ndege ili ndege zisitue. Aidha, walifunga barabara za kuingia kwenye kitalu kwa kutumia magogo.

Katika jitihada hizo za kuwafanya Green Mile washindwe kufanya biashara katika kitalu hicho cha Lake Natron East Wengert waliwachochea wanavijiji kuwafanyia Green Mile vurugu, jambo ambalo lilimlazimisha Mkuu wa Wilaya ya Longido kuitisha kikao na wawekezaji wote na kutoa onyo dhidi ya mwekezaji ye yote yule atakayewachochea wananchi kufanya vurugu kwa kisingizio chochote kile.

Wengert wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba inarejeshewa kitalu cha Lake Natron East. Swali ni kwamba kuna nini katika kitalu hicho cha uwindaji kiasi cha kuifanya kampuni hiyo kuhaha hadi kukimbilia kwa Rais Barack Obama?