Home Makala Ma DC chapeni kazi siasa hadi 2020  

Ma DC chapeni kazi siasa hadi 2020  

408
0
SHARE

NA ABRAHAM GWANDU ARUSHA.

SAFU ya uongozi katika serikali ya awamu ya tano inaendelea kuimarishwa. Baada ya Mawaziri, Makatibu wakuu,Wakuu wa idara na taasisi mbalimbali, wakuu wa mikoa, tayari wakuu wapya wa wilaya wametangazwa.

Kutokana na uteuzi huo, maana yake ni kwamba sasa jicho la Rais linaona kila kinachoendelea katika kona zote za nchi. Na kwa Rais huyu ambaye kila anapopata nafasi haachi kuchomekea kauli mbiu ya serikali anayoongoza ya Hapa Kazi Tu, ni matarajio ya wengi hawa Ma DC walioteuliwa watakwenda sambamba naye.

Wengi wanahoji sababu za nafasi hizi kuendelea kuwepo katika mfumo wa utawala wa nchi. Miongoni mwa sababu wanazotoa ni kuwepo kwa gharama kubwa za kuwalipa mishahara, magari, nyumba, wasaidizi nakadhalika hivyo wanapendekeza nafasi hizo zifutwe kwani hazina faida kwa taifa.

Wanaenda mbali zaidi wakihusisha nafasi hizo na zawadi wanayopewa wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kufanya kazi nzuri ya kukiletea chama heshima au ushindi baada ya uchaguzi.

Sijui ukweli wa madai haya, ninachoamini ni kwamba Rais John Magufuli anateuwa watu kulingana na vile anavyoamini kuwa watamsaidia kufanya kazi za kuwaletea wananchi wote maendeleo bila ya kuwabagua kwa misingi yoyote ile.

Huenda wengine kwa kutojua wakatumia vibaya kule kuwa kwao wanachama wa CCM kukitumikia chama hicho badala ya kuwatumikia wananchi wote. Wakifanya hivyo watakuwa wamefanya makosa makubwa na itakuwa halali yao kutumbuliwa.

Kimsingi kazi hasa za wakuu wa wilaya hazielewiki vizuri kwa wananchi walio wengi, wapo walioaminishwa kuwa ni makada wa CCM wanaofanya kazi za kudhibiti upinzani katika maeneo yao, lakini tukubaliane kwamba hawa ni wawakilishi wa Rais na ni jicho lake katika kipande hicho cha nchi  kama nilivyosema hapo juu.

Pamoja na hisia za ukada, jambo la kufurahisha ni msimamo usioyumba wa Rais Magufuli kuhusu kuwatumikia Watanzania wote bila ubaguzi.

Hii maana yake ni kwamba kila Mtanzania anapaswa kusahau itikadi yake ya kisiasa kwa muda wa miaka minne na ushei ijayo kwani tumeshatangaziwa siasa zisikwamishe ahadi ambazo viongozi walitoa wakati wakiomba kura kwa wananchi .

Kila Mtanzania anatakiwa kufahamu kwamba sasa ilani inayotekelezwa ni ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020. Kwa maana hiyo Ma DC walioteuliwa hawana wajibu mwingine wowote zaidi ya kusimamia maendeleo ya wananchi katika maeneo yao kama ambavyo aliyewateuwa anavyotuambia kila wakati.

Haitarajiwi akajitokeza DC anayetumia madaraka yake vibaya mathalani kwa kuwakamata viongozi wa vyama vya upinzani walio katika maeneo yao bila sababu. Serikali hii inajiapisha kuwa ni ya wananchi wote tutashangaa tukishuhudia DC akipendelea wana CCM kwa namna yoyote ile.

Zipo changamoto nyingi katika Wilaya ambazo zinawakabili wanachi, nyingine sugu, nyingine zipo katika uwezo wa mamlaka waliyonayo wanaweza kuzitatua bila kusubiri mamalaka nyingine zilizoko juu.

Migogoro ya ardhi  ni miongoni mwa changamoto hizo, katika maeneo mengine migogoro hiyo imesababisha mapigano katika makundi ya kijamii. Mapigano ya wakulima na wafugaji, kabila moja na kabila lingine, ukoo moja na ukoo mwingine  wanapigana hadi kusababisha vifo.

Badala ya kukimbizana na wanasiasa Ma Dc wanaweza kujikita katika kutatua migogoro hiyo. Katika maeneo ya miji, manispaa na majiji Ma DC mbali na suala la kufuatilia na kusuluhisha migogoro ya ardhi ambayo nayo ipo katika maeneo hayo lakini wanakabiliwa na changamoto za ziada zinazotokana na mazingira ya kuwa mjini.

Afya , elimu na upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa changamoto ambazo wakuu wa wilaya wakishirikiana na viongozi waliochaguliwa na wananchi mbunge na diwani kwa pamoja  wakiweka msukumo wao basi kero hizo zinapungua ama kwisha kabisa.

Itakuwa ni jambo la ajabu kama utatuzi wa kero za wananchi utasubiri mpaka pale rais, makamu rais au waziri mkuu anapotembelea mkoa au wilaya wakati yupo mwakilishi wa viongozi hao katika eneo husika.

Bahati mbaya kwao walioteuliwa ni utandawazi . Siku hizi wanachi wanatuma ujumbe wa simu , barua pepe, au mitandao mingine ya kijamii moja kwa moja kwenda kwa Rais wa nchi naye anausoma na kutoa maelekezo. Je huyo mwakilishi wake nini kitafuatia kama sio kutumbuliwa!

Zamani ilikuwa mpaka chombo cha habari kifichue udhaifu au uzembe wa kiongozi, siku hizi ni tofauti. Kasi ya dunia ni kubwa mno. Taarifa za kila kona ya nchi Rais anaweza kuzipata hata kabla hajapelekewa kwa mfumo rasmi wa kiutawala.

Zile zama za DC kupiga watu makofi akiwa baa huku amelewa hazipo tena, zile zama za kuwatisha watu wenye asili ya kiasia zimepita. Wakuu wa wilaya wachape kazi za kuwatumikia wananchi maana ndilo jukumu pekee walilokabidhiwa na Rais si kuzungukia maduka ya wahindi kuwatisha kwa vyeo ili mpate kaunda suti!.

Tumetangaziwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kwamba wakuu wapya wengi ni vijana wasomi. Hatutarajii vioja kutoka kwa wasomi hawa. Sifa za kijana zinajulikana.

Vijana wana nguvu, wanaakili ambazo hazijachoka, ni wepesi wa kufikiri na kuamua kwa hiyo tutarajie nchi ikienda mchakamchaka kwenda kwenye maendeleo kama alivyowahi kusema Waziri wa zamani na aliyekuwa mgombea nafasi ya Rais kupitia Chadema katika uchaguzi mkuu uliopita  Edward Lowassa.

Nguvu, ari, wepesi vikichangamana na elimu nzuri tuliyotangaziwa kuwa wanayo, hakika baada ya miaka mitano ijayo Tanzania ikiendelea kuwa katika hali hii ya kutambaa kiuchumi badala ya kusimama na kukimbia, basi tujue aliyetuloga kafa!