Home Makala Vyama vimejaa wapambe kuliko makada

Vyama vimejaa wapambe kuliko makada

344
0
SHARE

Na Markus Mpangala

YAPO mambo ambayo mara zote nashangzwa na namna yanavyofanywa na wanasiasa wetu pamoja na vyama vyao vya siasa. tunavyo vyama vya siasa takribani 22 ambavyo vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria iliyoruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Kazi ya vyama vya siasa ni muhimu na kubwa mno katika maisha ya Watanzania. Tunaelewa vyama hivi vinakuwa na madhumuni ya kukuza na kujenga demokrasia. Tunafahamu kuwa vyama hivi vinafanya kazi ya kuelimisha raia kupitia haki na ushinikizwaji wa masuala ya msingi.

Bahati mbaya iko dhana inahodhiwa nyakati hizi kwamba wanasiasa wanatakiwa kuwa watu wanaoweza kuvisaliti vyama vyao, kwamba wawe tayari kuungana na wapinzani wao na wasivipiganie vyama vyao kwa sababu ya kutafuta kupendwa .

Wanahodhi fikra kwamba mwanasiasa anatakiwa kukikana chama chake ili asifiwe na wapinzani wa chama hicho. Fikra hizi zimejikita zaidi kwa wanasiasa vijana na ambao wanathubutu kujiaminisha kwamba ili mwanasiasa bora inakulazimu ukane cheo chochote unachoweza kupewa.

Ninapata tabu kuelewa ukada wa wanasiasa wetu wa kizazi kipya. Wengi wao wanashindwa kufafanua na hata kuchanganua zaidi sifa za kada wa chama. Hawachanganui itikadi ya chama cha siasa. wanachama wanajiunga na vyama ili kujisifu kuwa wanamiliki kadi ya chama fulani kinachopendwa kuliko itikadi yake.

Wengine hushindwa kueleza itikadi na kada wa chama zinahusu nini. Mathalani hivi karibuni kulikuwa na uteuzi wa wakuu wa wilaya uliofanywa na Rais John Magufuli. Uteuzi huo umetajwa kwa namna tofauti kwamba unakibeba Chama Cha Mapinduzi-CCM. Ninaungana na wale wanaosema kuwa nafasi ya ukuu wa wilaya inapaswa au inatakiwa kufutwa.

Lakini ninatofautina na wapingaji wa uteuzi huo eti kwamba wapo makada wa CCM wamepewa vyeo hivyo kama fadhila ama walikuwa wakifanya juhudi ili wapata vyeo.

Nimejiuliza swali moja kuu; hivi ni mwanasiasa gani ambaye hatafuti cheo katika dunia tangu uanzishwe mfumo wa siasa za uwakilishi uliokuwa umetongolewa kule Ugiriki ya zamani?

Miongoni mwa wanaojaribu kujenga hoja kwamba makada walioteuliwa hawakupaswa kukubaliana na vyeo walivyopewa. Binafsi ninashindwa kuelewa mantiki hii inatokana na nini.

Nimebutwaishwa na fikra hizo na kujiuliza kama hao waliteuliwa hawatakiwi kukubali, je kadi za CCM zina kazi gani kwao? Ni kwanini tunawashambulia baadhi ya wanasiasa waliokubali uteuzi huo ilhali tunatambua kuwa wao ni wanachama wa CCM?

Ikumbukwe sifa ya kwanza kabisa kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya au mkoa ni lazima uwe kada wa CCM (kulingana na chama kinachotutawala kwa sasa)

Katika muktadha huo tulitarajia kuona kwamba kada wa chama akatae cheo anachopewa na chama chake eti kwakuwa wapinzani wake wamekuwa wakimshauri asikubali ndipo atapewa sifa? Sidhani.

Ninaamini huo ni mtazamo finyu kiasi na ambao unatudhihirishia kuwa tumekuwa wapambe zaidi kuliko kuzibeba itikadi za chama na ukada.

Kada wa chama anapaswa kwanza kuelewa chama chake kinasimama katika misingi ipi? Kada wa chama anatakiwa kufahamu pia nini falsafa ya chama hicho.

Ni lazima kada wa chama ajue taratibu, kanuni na sheria zinazokiongoza chama hicho. Kada analazimika kufahamu kuwa kwa kujua hayo, ndipo anaweza kuitetea itikadi na anakuwa kada halisi.

Aidha, kada wa chama akielewa maana ya ukada na itikadi anaweza kusimamia maslahi ya chama chake pale anapoona maslahi hayo yanatetereka au yapo katika hatarini.

Vilevile kada wa chama anatakiwa kukishauri chama, kwa misingi, falsafa, taratibu, kanuni na sheria zake zinazounda hicho chama. Ni lazima kada huyu azitambue miiko, mipaka, mamlaka, na ajenda za chama chake.

Sasa tujijadili, hivi kazi ya kada wa chama ni nini kama siyo kutetea chama chake na itikadi yake? Kuna mwanasiasa gani asiyetaka au kutafuta cheo hapa duniani? Tunajiunga na vyama vya siasa bila kukubali kutetea itikadi ya chama? Au hatujui kada ni nani kwenye chama cha siasa? Kama mwanasiasa hutafuti cheo kwenye siasa unatafuta nini huko ndani ya chama?

Mathalani, unapokata rufaa kupinga uamuzi wa kamati kuu za chama au uongozi wa juu kukuengua kwenye ugombea wa nafasi fulani ya uongozi huwa unatafuta haki ili ufanye nini?

Unapochukua kadi ya chama huwa unafikiria uzito wa kada wa Chama.? Kama wewe hutafuti cheo ya nini uwanange wanaotafuta cheo kwenye siasa wakati ndiyo msingi wenyewe na mzunguko mzima wa demokrasia?

Nijuavyo kada wa chama hutetea chama chake na itikadi yake kwa njia sahihi na halali. Ukiwa kada hupaswi kuwa “katikati” dhidi ya wapinzani wako. Mwanasiasa au mwanachama wa kawaida unaweza kuongea lolote au chochote dhidi yao kisiasa, kiitikadi na ukada halisi.

Hivyo basi wewe unapomwona mgombea fulani ana taswira hasi lakini wapo wanaompigania na kumwona ni msafi. Ni ukada wa chama. Ni utetezi wa itikadi na ajenda ya chama. Na vilevile unapodhani wanasiasa fulani wanatafuta cheo fulani kwa njia zao sahihi na halali ndo siasa hizo.  Ndiyo ukada. Ndiyo itikadi.

Kulingana na muktadha huo, wale wanasiasa au makada wanaojitapa kwamba hawatafuti vyeo kwenye vyama vyao au siasa mara nyingi hujikita kwenye dhana ya ‘Meritocracy’, kwmaba unapewa majukumu kulingana na uhodari au uwezo uliona na kwamba viongozi au wanachama wanajua unaweza.

Waama, vyeo hivyo huja kutokana na Meritocracy hata kama hutafuti lakini utapavipata na wengine hawajapata hivyo hutumia njia nyingine.

Bahati mbaya sana tuliyonayo nyakati hizi kwenye siasa zetu Makada tulio nao wengi ni wapambe wa kiongozi, mwanasiasa au wanachama wa mwanachama fulani. Akihama mwanachama huyo nao huhama bila kujali itikadi ya chama alichojiunga.

Sijui ni lini wanasiasa watamudu kutushawishi baadhi yetu tushiriki siasa za majukwaani mbali na shuleni. Inafka wakati tunataka adui au mpinzani wako afanye unavyotaka wewe. Wapambe ni wengi kuliko makada wa vyama.