Home Makala Magufuli: Chunga kila hatua ya Kagame

Magufuli: Chunga kila hatua ya Kagame

1098
0
SHARE

NA  M. MOHAMED

NIMEULIZWA swali kwamba naitazama vipi ziara ya Rais Paul Kagame wa Rwanda na urafiki wake na Rais  wa Tanzania, John Magufuli. Ni swali zuri, nami nimejiuliza nyongeza yake kwamba; nini msukumo wa urafiki huo? Kwani uhusiano mwema uliopo sasa ni tofauti na ilivyokuwa wakati wa mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete. Marais hawa walikuwa na msuguano kuanzia mapema mwaka 2013.

Tumesikia Rais magufuli akisema Rais Kagame anamshauri mambo mbalimbali na kwamba wamekuwa marafiki wazuri. Urafiki wa Rais wetu ina maana unalihusisha taifa letu. Unawahusisha wananchi waliomchagua. Kwa maana hiyo hapo ndipo wananchi tunatakiwa kutafakari juu ya urafiki huo na manufaa yake kwa nchi yetu.

Tunakumbuka Kagame aliwahi kutoa maneno mazito dhidi ya Kikwete, na uongozi mpya wa Magufuli unayafahamu fika tangu akiwa Waziri wa Ujenzi kipindi hicho.

Aidha, uongozi wake unafahamu kuwa tumepeleka Jeshi letu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupambana na kile kinachoitwa vibaraka wa Kagame wanaokwapua malighafi za nchi hiyo.

Urafiki wa Kagame na Magufuli naweza nikauweka pande mbili—ni urafiki usioleta mashaka.

Ni kweli tumekuwa na urafiki wa mashaka na wenzetu, hasa utawala wao, kiasi kikubwa ikihusisha suala la amani ya DRC, ushiriki wetu dhidi ya waasi wa M23 ambao sisi, jumuiya za kimataifa, na nchi kama Marekani wamethibitisha kuwa kuwa kundi hili, linapata msaada wa kivita kutoka Rwanda katika kile kinachoonekana kutafuta ushawishi katika nchi za Maziwa Makuu.

Lakini pia Rwanda chini ya Paul Kagame, inaaminika ndio watoroshaji wakubwa wa rasilimali za DRC, hasa madini, kupitia vita hivyo. Tanzania inaamini haya, lakini ili tufanikiwe kiuchumi zaidi katika eneo hili la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, ni lazima tushirikiane na majirani zetu kibiashara. Lakini ili kushirikiana vizuri, lazima tuweke mahusiano mazuri zaidi, kama yalikuwa na utata, basi tuyaboresha.

Tulipata kusikia dhamira ya serikali ya Rwanda ya kuacha kutumia Bandari ya Dar es salaam kwa madai ya huduma mbovu na kukithiri kwa rushwa, lakini wengi waliona kuwa ni kutokana na kutoelewana na Tanzania kwa wakati huo chini ya Kikwete. Hilo lilithibishwa na kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Hiari—Coalition of the Willing kati ya Kenya, Uganda na Rwanda na kuitenga Tanzania na kusababisha ikose fursa mbali mbali za kusaidia kukuza zaidi  kwa uchumi wake na kuleta maendelo. Katika hilo, tuliona Kagame akimkaribisha Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ili kujadili miradi ya kiuchumi.

Kwa hiyo, wasio na shaka, wanaona huu ukaribu ni mbinu nzuri ya kuhakikisha tunakuwa na mahusiano mazuri zaidi ya kibiashara, kiuchumi na kimaendeleo. Tukumbuke mshindani wetu mkubwa kwa sasa ni Kenya, na Coalition of the Willing (CoW) ilikuwa katika nafasi ya kuinufaisha zaidi Kenya, lakini sasa hali ni tofauti. Ni kama CoW imefutwa rasmi.

Aidha, ni urafiki unaoleta mashaka, pamoja na ukweli kwamba uhusiano mzuri unahitajika.  Hata wakati wa kipindi cha Jakaya Kikwete, pamoja na uhusiano kulega lega, lakini ushirikiano wa kiuchumi ulibaki pale pale.

Itakumbukwa kwamba Rais Kagame alikuja kutembela Bandari ya Dar es Salaam, na pia kuzindua reli wakati wa kipindi cha Kikwete. Kwa hiyo, ushirikiano wa kiuchumi upo tu siku zote, kinachotokea sasa kinatia shaka hata kwa kisingizio eti ni katika kuimarisha uhusiano kwa faida ya uchumi wan chi hizi mbili.

Rais Kagame anajulikana kuwa ana ndoto za kufanya kabila lake la Hima au kujenga Dola la Bahima kwa lengo la  kuitawala Afrika Mashariki kama alivyofanya litawale Rwanda kwa kuwakandamiza Wahutu waliowengi.

Watutsi ni kama Wayahudi wa Israeli, wanaaaminil, wanamini kuwa wanastahili kuwa watawala tu siyo watawaliwa. Rais Kagame  ni mtu mjanja sana. Anatumia mbinu za kiujanja unjana (manipulations). Kila hatua anayoifanya ni lazima kuingalia kwa makini sana. Siku zote anakuwa na mipango isiyo wazi.

Inashangaza mpaka Rais wetu anatutia fedheha kwa kutaka kuwaita wataalamu wa kutoka Rwanda waje kutuwekea mifumo ya kompyuta kwenye mamalaka zetu. Ni jambo la aibu kuzungumzwa jambo hili, tena na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania. Usalama wa nchi utaakuwaje?

Sasa hatujui kama Rais Kagame alitoa ofa kwa rais wetu au la, lakini pia hatujui mengi ambayo hayajazungumzwa hadharani. Inatia wasiwasi zaidi ukizingatia Rais wetu hana uzoefu wa masuala ya kijeshi na kijasusi.

Natambua kuwa tutasema wapo washauri, lakini anaonekana hata washauri hawasikilizi, au wanamuogopa. Kama tutakumbuka baada tu ya kuteuliwa, balozi wa kwanza kumtembelea Magufuli alikuwa ni balozi wa Rwanda nchini. Haikupita muda, kukatumwa jopo maalumu kutoka Rwanda kuja kuzungumza na Rais Magufuli.

Inafikirisha kwamba Rais Magufuli hakwenda Zanzibar kwenye sherehe ya Siku ya Mapinduzi, badala yake akaenda Rwanda!