Home Latest News Dk.Magufuli akawe Sultani Kenya

Dk.Magufuli akawe Sultani Kenya

597
0
SHARE

UHUSIANO wa Rais wa John Magufuli na Kiongozi wa
Upinzani nchini Kenya, Raila Odinga,unaathiri kwa kiwango
kikubwa harakati za Muungano wa Jubilee kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017.
Muungano huo wa Jubilee, unaoongozwa na Rais wa sasa wa Kenya, Uhuru Kenyata na Naibu wake, William Ruto, ulikuwa ukiomba
Magufuli asiingie Ikulu Oktoba mwaka jana. Hata alipoingia, habari kutoka mitandao ya kijamii Kenya, zinasema Jubilee walimuunga mkono kimya kimya, aliyekuwa mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa.

Jubilee, walianza kuinamisha vichwa chini, pindi Dk. Magufuli
alipoteuliwa kuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, akimpiga kumbo Waziri
Mkuu wa zamani Edward Lowassa, ambaye hatimaye alijiunga na Umoja wa
Katiba ya Wananchi—UKAWA mwaka jana.

Dk. Magufuli alipopenya katika msitu wa wagombea wenzake 38 katika
Chama Cha Mapinduzi (CCM), siasa za Kenya zilielekea kuwatupa mkono
akina Uhuru kuelekea 2017.

Kuelekea mwakani 2017, siku ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta
na William Ruto, wakijulikana  sana kama ‘Uhuruto’  wachambuzi wa
siasa za Kenya wanaona Muungano wa Jubilee ukikumbwa na upinzani mkali
ambao haujawahi kutokea safari hii kuelekea 2017.
Wakati rushwa miongoni mwa vigogo wa serikali ya Kenya na hatua dhalili zinazodaiwa kuchukuliwa na Rais Kenyatta dhidi ya ufisadi, hapa
Tanzania Magufuli akisikika kubana matumizi na kuwawajibisha watumishi wala rushwa huku watumishi ‘Mizuka’ wakiondolewa. Hayo yameifanya serikali hii ya Awamu ya Tano yenye kauli mbiu, ‘HAPA KAZI TU,’ kuufanya Muungano wa Jubilee kuwa na changamoto kali katika uchaguzi mkuu wa mwakani.
Rais Dk.John Magufuli, amejipatia umaarufu mkubwa miongoni mwa raia kwa
kuwatimua  kazi vigogo  wengi bila kuwatazama usoni, maarufu “Kutumbua
Majipu” kwa lengo la kurejesha heshima na uwajibikaji serikalini, kitu
ambacho Wakenya wanamlilia  Rais kenyatta angefanya pia.

Kufuatia hali hiyo, Dk. Magufuli anasifiwa sana katika mitandao ya
kijamii ya Kenya, kwamba uongozi wake unalenga kuleta mabadiliko ya
kweli ya kiuchumi katika nchi, tofauti na Kenya ambako wananchi
wanaomkosoa Kenyatta, wanasema serikali yake inafumbia macho kashfa za
za kifisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma. Mtindo wake wa kubana matumizi ya serikali umelikumba hata Shirikisho la Afrika Mashariki(EAC),ambapo fedha zilizokuwa zikitumika kufanya sherehe na maadhimisho yasiyo na tija,sasa zinalengwa kupelekwa katika miradi ya maendeleo na Huduma za Jamii.

Urafiki wa Magufuli na Raila Odinga ni wa muda mrefu. Magufuli alikwenda Kenya kuhudhuria maziko ya ya mtoto wa Raila, Marehemu Fidel Castro Makarios, maarufu kama Obange, akimwakilisha Rais Kikwete wakati huo.

Wakati Magufuli anaapishwa kuwa Rais wa Tanzania Novemba mwaka jana,
Ikulu ya Nairobi ilipatwa tashtiti. Hii ni kwa mujibu wa Kenya Today.
Kiongozi wa Chama cha Cord, Raila Odinga, Aprili Pili mwaka huu 2016
alitua kwa ‘Chopper’ huko Kilimani, Chato Mkoani Geita, mahali ambapo ni
nyumbani kwa Rais Magufuli.
Marafiki hawa wawili, wakiwa na wake zao, Ida Odinga na Janet
Magufuli, walitumia mapumziko yao huko Kilimani kuzungumza mambo ambayo
hayako bayana sana. Hata hivyo, ziara hii ya ‘Babu’ Raila Odinga, haikutazamwa
vizuri na Muungano wa Jubilee unaoongoza nchi huko Jamhuri ya Kenya.

Inawezekana, urafiki huu wa Dk. Magufuli na Raila, ambaye hupenda
kujinasibisha kama ‘Mtanzania’ kwa kuwa aliwahi kupewa ‘Scholarship’
na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  kwenda kusoma
Ujerumani, unaathiri kwa kiwango kikubwa, juhudi za ‘Uhuruto’ kusalia
mamlakani Kenya baada ya Julai 2017.
Raila alisema, alikwenda kamtembelea rafiki yake Magufuli. Alifika Tanzania wakati Magufuli akiapishwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alikaribishwa kama vile ‘Rais’ wa nchi na kutia wasiwasi na ‘maswali yasiyo na majibu’ kitu ambacho kulingana na mitandao ya Kenya, Ikulu ya ‘Uhuruto’ ilikosa usingizi, kufuatia kitendo hicho!

Inasemwa kwamba, kuna vitu haviwezi kujificha, kama ujauzito wa mwanamke
na Ukweli. Inasemwa kwamba ushawishi wa Raila ulimsaidia Magufuli kuibuka
mshindi katika Uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka 2015.
Hivyo, Dk.Magufuli katika Ikulu ya Dar es salaam ni kitisho kikubwa
katika Uchaguzi wa Kenya unaoelekea kuwa mgumu kwa Uhuru na William
Ruto kuliko ilivyokuwa uchaguzi uliopita. Wakati CCM wakisemwa kusaidiwa na Odinga, mtu wa karibu wa Uhuru, Mutahi Ngunyi, anasemwa kusalia katika hoteli za fahari Arusha kulimsaidia Lowassa katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Baadhi ya Wakenya walikamatwa wakijihusisha na kampeni chafu katika
mitandao ya kijamii.
CCM wanadaiwa kumwambia hivi Odinga: “Ndugu yetu Bwana Waziri Mkuu, sisi kama CCM tungependa kutoa shukrani zetu za dhati kwake yeye na jamii yake pamoja na timu yake kwa mchango wao wa kimaarifa uliotuwezesha kuushinda uchaguzi huu. Isingalikuwa yeye na na kikundi chake stadi, pengine hatungeweza hii race. Mwenyezi
Mungu ambariki Mheshimiwa Raila”  Maneno haya yanadaiwa kutolewa na
CCM kumpongeza Raila.
Kufuatia hali hiyo, Serikali ya Kenya kudaiwa kuunga mkono upinzani wa
Tanzania, na Wapinzani wa Kenya kumsaidia Magufuli, kinachosubiriwa
sasa huenda Magufuli na serikali yake wakaendeleza uswahiba na kumpa
nguvu Raila Odinga katika uchaguzi ujao.
Hata hivyo, wapinzani wa Tanzania chini ya mwavuli wa UKAWA, wamekuwa wakimwandama Magufuli kwa sababu serikali yake imebinya sana uhuru wa kujieleza na Demokrasia nchini.

Kama ilivyokuwa zama za utawala wa Kikwete, Bunge halionyeshwi ‘Live’(papo); watu wanangoja kuona usiku. Wabunge wa Ukawa wameonekana wameziba midomo kwa karatasi wakati mmoja wakiingia Bungeni katika kikao kilichopita.
Inasemwa mikutano hususani ya upinzani imepigwa marufuku hadi wakati wa
Kampeni za 2020. Yapo matamshi lukuki ya Rais Magufuli yanayoonekana kuukera upinzani. Kwa ujumla, wanaounga mkono upinzani hapa Tanzania, wanamwona Rais Dk. Magufuli kama mtawala wa kiimla, aliyeondoa demokrasia katika kipindi
cha miezi michache tu ya utawala wake.

Mabaya ya utawala uliopita:

Ufisadi, watumishi hewa, safari nyingi za
nje n.k vinaelekea kusahaulika kwa kasi huku wengine wakianza
kumkumbuka Kikwete kwamba alilea demokrasia na uhuru wa kujieleza!
Kutokana na sababu hizi chache sana, nabaini hapa kwamba Magufuli
anakubalika kwa wapinzani wa Kenya, wakati Muungano wa Jubilee
ukiingiwa hofu kuweza kuanguka 2017.
Hata hivyo, Dk. Magufuli anasemwa na wapinzani kwamba ni
‘dikteta’ anayesigina Katiba ya nchi, hata wanatamani ashitakiwe The
Hague, Uholanzi! Kwa vyovyote vile, wapinzani wa Tanzania wakiwemo Ukawa, wanamuunga mkono sasa Uhuru Kenyatta na William Ruto, kwa kuwa ‘mpinzani  mwenzao’ Babu Raila ni ‘rafiki’ wa adui yao, Magufuli.
Kama Raila angekuwa adui wa adui yao Magufuli, basi angekuwa rafiki
yao, maana adui wa adui yako ni rafiki! Raila amechagua kuwa rafiki wa Magufuli huyu asiyependwa na wapinzani, kiasi cha kuhataraisha utawala wa Jubilee kusalia mamlakani Kenya baada ya 2017.
Kwa kuwa Ukawa hawampendi Magufuli kwa makosa wanayodai kufanya hapa, na kwa kuwa Ukawa wangependa Magufuli aanguke 2020 wakati wapinzani wa Kenya-akina Babu Odinga-wakimwombea atawale japo mpaka 2025, nadhani sasa Ukawa wanawapenda Ruto na Kenyatta.
Ni kwa sababu hii napatwa tashtiti kusema: “Je, Magufuli aende kuwa Rais Kenya, kisha Kenyatta anayebatizwa jina la Vasco Da Gama kwa kuzunguka-zunguka duniani kote kwa kodi za Wakenya, halafu kashindwa kupambana na rushwa na Rutto waje hapa kwetu watutawale kwa kuwa ni adui ya adui wa wapinzani wa Tanzania?

Halafu, utawala wa Magufuli ni kila kitu kutozwa kodi! Afadhali, Vasco
Da Gama, Kenyatta kuliko Kaisari Magufuli na kodi kila mahali eti?
Ukienda hotelini dai risiti(kodi), ukipanda daladala dai
risiti …. Inatukera Watanzania hadi tunatamani utawala
unaofumbia macho ufisadi na rushwa?
Tashtiti!