Home kitaifa Askofu Gwajima: Nashambuliwa

Askofu Gwajima: Nashambuliwa

431
0
SHARE
Josephat Gwajima

NA GABRIEL MUSHI,

HATIMAYE Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amefunguka kwa mara ya kwanza kuelezea kile kinachosababisha kanisa lake kuzushiwa taarifa za uongo kuwa limefungiwa na serikali.

Taarifa za kufungiwa kwa kanisa hilo lilipo Ubungo Tanecso jijini Dar es Salaam, zilianza kusambazwa wiki iliyopita na mapema wiki hii zilidi kushika kasi hali iliyoibua taharuki miongoni mwa waumini wake ambao wapo zaidi ya 70,000 nchini.

Kufuatia taarifa hizo, RAI lilizungumza na Askofu Gwajima ambaye alibainisha kuwa taarifa hizo za uzushi zimekuwa zikisambazwa na wale aliodai ‘kuwachapa’.

“Hizo ni taarifa za uongo, hakuna kitu kama hicho… hii inaonesha dhahiri kuwa wale niliowachapa wapo kazini kunishughulikia lakini wameshindwa.

“Wanachokifanya kwenye mitandao ya kijamii ni vurugu zao tu kwani hamna ukweli wowote, na sasa tumeandaa waraka kukanusha taarifa hizi ambao tutausambaza kwenye vyombo vya habari,” alisema.

Pamoja na mambo mengine Askofu Gwajima alisita kuzungumzia taarifa za kuhojiwa na jeshi la Polisi ambazo ziliripotiwa mapema wiki hii na vyombo mbalimbali vya habari.

“Wewe si umeona wanasema Gwajima ahojiwa lakini hata picha hawakupata, hivyo kwa hali ilivyo sasa siwezi kuzungumzia suala hilom, tusubiri kwanza hali itengamae ndipo tumjibu mtu kwani kama ilivyo kawaida yetu wakizidi kusema sana lazima tuwajibu,” alisema

Askofu Gwajima alikuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa siku kadhaa na kukamatwa mapema wiki hii katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) alipowasili akitokea Japan.

Baada ya kukamatwa na Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa JNIA alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi uliopita.

Akizungumzia na vyombo vya habari kuhusu kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi Uwanja wa JNIA, Martin Otieno alisema askofu huyo aliwasili saa 2.45 asubuhi akitokea Japan kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Otieno alisema mara baada ya kukamatwa alipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

“Ni kweli tulimkamata Askofu Gwajima hapa uwanja wa ndege wa JNIA baada ya kuwasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya na tulipomuhoji alidai kuwa alikuwa nchini Japan,” alisema Otieno.

Mwanasheria wake Peter Kibatala alinukuliwa na vyombo vya habari akisema Gwajima alifika Kituo Kikuu cha Polisi saa 4.45 asubuhi kwa mahojiano mafupi na aliruhusiwa kuondoka baada ya kujidhamini yeye mwenyewe.

“Askofu Gwajima amehojiwa leo (Jumatatu) na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu na amejidhamini yeye mwenyewe, ameruhusiwa kuondoka hivyo tunasubiri chochote kitakachoendelea,” alisema Kibatala bila kueleza mahojiano yalivyokuwa.

Askofu Gwajima alikuwa anatafutwa na polisi tangu mwezi uliopita baada ya kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya kijamii unaodhaniwa una sauti yake akipendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kufikishwa mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo sasa Rais John Magufuli anayashughulikia kwa mtindo wa kutumbua majipu.

Katika mkanda huo, sauti hiyo inadai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Rais Magufuli asipewe uongozi wa chama hicho kwa sasa kama ilivyo utaratibu wa chama hicho na kwamba hilo likifanyika basi Rais abadili katiba ili mstaafu huyo aweze kufikishwa kortini.

Tangu ulipotolewa mkanda huo, makachero wa polisi wamekuwa wakipiga kambi nyumbani kwa Askofu Gwajima kwa lengo la kumkamata lakini hawakumpata.

Baadaye ilikuja kufahamika kwamba askofu huyo alikuwa amekwenda nje ya nchi lakini haikujulikana ni nchi gani.

Hata hivyo, baada ya kutafutwa na polisi, Gwajima kupitia wakili wake Kibatala alisema atakaporejea nchini atakwenda moja kwa moja polisi kwa ajili ya mahojiano.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amekuwa akisisitiza kwamba jeshi litaendelea kumtafuta askofu huyo kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa, Interpol.