Home Habari kuu Kinana kubaki CCM?

Kinana kubaki CCM?

435
0
SHARE

* Uwezo na uzoefu wa kukiunganisha chama wambeba

NA MWANDISHI WETU

PAMOJA NA Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutangaza kustaafu wadhifa huo mara baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa chama hicho mwishoni mwa wiki hii, bado anayo nafasi kubwa ya kuendelea kusalia kwenye nafasi za uongozi za chama hicho. RAI linachambua.

Pamoja na ukweli huo, Kinana anaweza kusimamia uamuzi wake ili kutimiza ahadi yake aliyoitoa mwaka 2012 ya kung’atuka mara baada ya kukitumikia chama hicho kwa miaka 25.

Hata hivyo uamuzi wake huu wa kutangaza kujiuzulu nafasi zake za uongozi ndani ya CCM si mara ya kwanza, alishafanya hivyo mwezi Septemba, 2012 kwa kujivua nafasi zake za ujumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu kwa hoja ya kuachana na siasa uchwara.

Uamuzi wake huo hakuutekeleza kwa madai kuwa viongozi wastaafu walimwomba na kumsihi aendelee kukitumikia chama katika wadhifa wa Katibu Mkuu hadi baada ya uchaguzi mkuu uliopita.

Kwa kauli yake Kinana alisema maombi ya wazee pamoja na yale ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete yalimfanya kukubali kurejea kundini na kubeba dhamana ya kukitumikia chama hicho.

Baada ya kulikubali jukumu hilo na kukivusha chama kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Kinana sasa anaiona haja ya kung’atuka na kuwapa nafasi makada wengine ili waweze kukisaidia chama katika nafasi za juu.

“Uchaguzi ukimalizika nitapumzika, mwanasiasa ni lazima ujue wakati wa kuingia kwenye uongozi na kutoka,”alisema alipohojiwa na moja ya magazeti ya kila siku nchini.

Kinana alikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa ndani ya CCM, wapo vijana na wenye rika la kati wenye sifa na uwezo wa kukiongoza chama katika ngazi mbalimbali, kutokana na kulelewa vizuri na kuwa na mapenzi makubwa na chama.

Mwanasiasa huyo aliyekitumikia chama kwa miaka mitatu akiwa Katibu Mkuu alinukuliwa akisema kuwa atachukua uamuzi huo mara baada ya kuchaguliwa kwa Mwenyekiti mpya, ambapo ataandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo ili kumpa nafasi ya kuteua sekretarieti mpya.

Pamoja na kauli hiyo ya Kinana inayoonesha kudhamiria kujiweka kando ya uongozi ndani ya CCM, duru za habari zimebainisha kuwa mwanasiasa huyo mwenye mbinu na mikakati ya hali ya juu ya kiutendaji, bado anayo nafasi kubwa ya kusalia kwenye nafasi yake ya sasa ama ya juu zaidi.

Wanaobeba hoja hiyo wanasema mchango wake mkubwa ndani ya chama kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake pamoja na uzoefu alionao vinamfanya kuwa mtu muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na ushindani mkubwa wa kisiasa.

Katika kuhakikisha Kinana anaendelea kusalia ndani ya uongozi zipo taarifa za kuwepo kwa baadhi ya makada wenye ushawishi kujipanga kwa ajili ya kumshawishi yeye mwenyewe au Rais Magufuli ili asimwache katika sekretarieti yake.

Kinana anaonekana kama mtu pekee aliyeweza kukiunganisha chama katika kipindi kigumu ambacho CCM ilikuwa imeparaganyika kutokana na baadhi ya wanachama wake kuhusishwa na kashfa mbalimbali.

Ukweli wa hilo aliudhibitisha mwenyewe kwa kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake amekumbana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kukikuta kikiwa hakina mshikamano baina ya viongozi na wanachama pamoja na kutamalaki kwa uhasama ndani ya chama.

Katika kuhakikisha chama kinarejea katika hali ya kawaida, Kinana alisema alihakikiisha anapunguza uhasama miongoni mwa wanachama na viongozi, kuimarisha umoja ndani ya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu.

Kabla ya Kinana kuanza kazi ya kukifufua na kukiimarisha chama hicho, hali ilikuwa tete kwani CCM, kilishuhudia kutokuelewana kwa baadhi ya viongozi wake huku pia kikiwa mbali na wananchi hasa wale wa vijijini.

Mbali na hilo, lakini pia Kinana anatajwa kuwa msaada mkubwa kutokana na uamuzi wake wa kuongoza harakati za kukinusuru chama wakati wa uteuzi wa majina ya wagombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kwamba alikuwa kinara wa kuhakikisha wanachama wote waliokuwa na nguvu ya ushawishi ndani ya CCM, majina yao yanakatwa jambo ambalo mbali ya kumpa nafasi Rais Magufuli kuibuka kidedea, lakini pia limekinusuru chama.

Kama hiyo haitoshi Kinana pia anatajwa kuwa  msaada mkubwa ndani ya CCM, hata kabla ya kuwa Katibu Mkuu kwani katika uchaguzi wa mwaka 2000 na ule wa  2005 ndiye alikuwa meneja wa kampeni na  kinara wa kuusaka ushindi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Umahiri, uhodari na uzoefu  huo wa Kinana katika kukifufua na kukiimarisha chama, unasababisha kupewa nafasi kubwa ya kuwa msaidizi wa karibu wa Mwenyekiti ajaye ambaye anatajwa kutokuwa na uzoefu wa kutosha ndani ya chama.

“Si rahisi kwa chama kuruhusu Kinana aondoke kirahisi namna hiyo, ni mtu muhimu sana kwa sasa, katika kipindi kifupi cha uongozi wake, amekifanyia makubwa, uwapo wake una maana kubwa sana hasa ukizingatia mwenyekiti wetu ajaye hana uzoefu mkubwa ndani ya chama,”alisema mmoja wa makada waandimizi wa CCM.

Wanaotaka Kinana aendelee kubaki kwenye safu ya uongozi wanaweka wazi kuwa si lazima mwanasiasa huyo asalie kwenye ukatibu mkuu, badala yake anaweza kukabidhiwa kiti cha Makamu Mwenyekiti Bara, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Philip Mangula.

Hoja ya Kinana ambaye anatajwa kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya CCM, kustahili kushika nafasi ya Mangula inaangaliwa kwa mtazamo tofauti kutokana na sifa ya kuuchukia ufisadi kwa vitendo aliyonayo  Makamu mwenyekiti huyo.

Nia ya kutaka Kinana aendelee kusalia madarakani ni kuhakikisha nyuma ya Rais Magufuli ndani ya chama kunakuwa na mtu mwenye uwezo wa kumshauri bila woga wala unafiki kwa masilahi ya CCM.

“Kinana ni mtu makini sana, hana woga wala unafiki, kwenye ukweli anausimamia na kuutetea bila kujali, sasa chama kinahitaji mtu wa namna hiyo, hasa ukizingatia Mwenyekiti mtarajiwa ni mgeni kabisa kwenye uongozi wa chama, tunajua Rais wetu ni kiongozi mahiri na makini katika kufuatilia na kutekeleza mambo, kwa umakini huo huo anapaswa kuwa na mtu wa aina yake ili watuimarishie chama,”alisema.

Umuhimu wa Kinana unakuja katika kipindi ambacho tayari ipo orodha ya wanachama mbalimbali wa chama hicho wanaotajwa kustahili kushika nafasi yake.

Wanaotajwa ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Abdallah Bullembo, George Mkuchika, Spika wa zamani wa Bunge la tisa, Sumuel Sitta, Mhadhiri wa chuo Kikuu, Bashiru Ally na mbunge  wa zamani wa Songea mjini, Emmanuel Nchimbi.