Home Latest News Wapiga ‘dili’ CCM wajiandae kutumbuliwa

Wapiga ‘dili’ CCM wajiandae kutumbuliwa

445
0
SHARE
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete akihutubiwa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho.

MALIMBILI MWAMLIMA,

WENGI wanashauku kuona Julai 23 inafika kwa kuwa ni siku ambayo Dk. John Magufuli atakabidhiwa uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tunategemea kuiona CCM mpya chini ya mwenyekiti mpya, hivyo tunaamini kuwa lazima utafumuliwa mtandao mbovu ndani ya chama hicho ambao ulikuwa unawafanya baadhi ya watu kuonekana ni miungu watu, kisha utajengwa mtandao mpya ambao utaifanya CCM kuonesha kuwa inataswira ya kutetea masilahi ya nchi, kwa kupiga vita rushwa, ufisadi na kila aina ya uovu nchini pasipo kujali cheo cha mtu, au mrengo wake kisiasa.

Wengi watafyekwa ndani ya chama hicho na kupoteza utukufu waliokuwa nao. Kwa sababu hiyo,  wapo vigogo ambao watainua vita kwa namna mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuhamia kwenye vyama vya upinzani. Hivyo kuufanya upinzani nchini dhidi ya CCM na serikali yake kuwa mkubwa zaidi ya uliopo sasa.

Lakini kwa upande mwingine, itamuongezea Dk. Magufuli na serikali yake uwezo wa kutekeleza mipango aliyonayo.

Watanzania wengi wanaimani sana na mipango aliyonayo Dk. Magufuli. Wanaamini anadhamira ya dhati katika kuleta maendeleo ya nchi. Imani hiyo inatokana historia ya utendaji wake wa kazi na mipango lukuki ambayo serikali yake imeiweka wazi mbele ya umma.

Hata hivyo, inaonekana vita ni kubwa kuliko uwezo wake na dhamira aliyonayo. Kwa maana hiyo, akili na nguvu zaidi vinahitajika katika kuhakisha ile neema ambayo wananchi wengi wanaitegemea kupitia uongozi wake inapatikana. Kwa kuwa nchi haiwezi kuendelea kwa serikali kupanga mipango tu.

Tumeona nchi hii tangu ipate uhuru mpaka leo, kumekuwa na mipango mingi kwa ajili kuleta maendeleo. Lakini hata hivyo, matokeo yake mara nyingi huwa ni tofauti kabisa na matarajio ya wengi.

Sisemi nchi yetu haina maendeleo, yapo, lakini hayaendani ni umri wa nchi, uwingi wa rasilimali zilizopo pamoja na idadi ya watu.

Nazungumzia idadi ya watu kwa kuwa mtaji mkuu wa nchi ni rasilimali watu yaani wananchi. Kwa maana hiyo, maendeleo yenye tija nchini, huletwa na wananchi. Bahati mbaya wananchi wengi hawatambui kuwa wao ndio wenye jukumu hilo la kuleta maendeleo nchini. Ndiyo maana kila kukicha wamekuwa wakiilaumu Serikali kuwa haileti maendeleo, huku ushiriki wao katika kuhakikisha nchi inapata maendeleo ukionekana ni mdogo. Si kwa wale ambao ni watendaji kazi serikalini, wala si kwa mwananchi wa kawaida. Kila mtu anawaza tumbo na mipango yake binafsi tu.

Dk. Magufuli alisema “Nimeamua Tanzania iende mbele, atakayejaribu kukwamisha atakwama mwenyewe” na kweli anaonekana anadhamira ya dhati kuhakikisha kwamba nchi inakwenda mbele, lakini pekee yake hataweza bila kutengeneza mazingira yatakayomlazimu  kila mwananchi kushiriki kwa dhati katika kuipeleka nchi mbele na kupambana na wanaojaribu kuikwamisha?

Kweli anamipango mingi, lakini mipango pekee na matamko havitaweza kuipeleka nchi mbali kimaendeleo.

Mfano, kuna mpango wa kuhakikisha kila shughuli iliyowekwa kwenye mpango wa kulipa kodi nchini, Serikali inapata kodi inayostahili. Katika kuhakikisha mpango huo unaleta matunda, Serikali imeamua kununua na kutoa mashine za kisasa za EFD kwa kila mfanyabiashara, huku baadhi ya wafanyabiashara wakipewa bure ingawa zinanunuliwa kwa gharama kubwa.

Mbali na hilo, Serikali imetafuta vyanzo vingine zaidi vya ukusanyaji wa mapato. Mfano, kila mwenye nyumba anapaswa kuilipa kodi ya nyumba.

Hiyo yote ni mipango ya kuhakikisha nchi inatoka kwenye kutegemea misaada. Ni jambo jema, lakini je, tatizo mpaka tunategemea misaada lilikuwa kukosa mashine za EFD pekee na wenye nyumba kutokuwa kwenye mpango wa kulipia kodi? Hapana si hivyo.

Tatizo kubwa lilikuwa ni ukusanyaji mapato, kwani ulikuwa ni mdogo ikilinganisha na vyanzo vilivyopo nchini, huku kidogo kilichokuwa kinakusanywa kilikuwa kinatumika vibaya.

Hata hivyo tunaweza kusema kwa sasa ukusanyaji wa mapato umeongezeka na matumizi mabaya yamepungua, lakini si kwa kiwango kinachostahili. Ukwepaji kodi bado upo, na matumizi mabaya ya hicho kidogo kinachopatikana bado yapo pia.

Nimegundua kuwa wafanyabiashara wengi wanapokwenda kuchukua mzigo kwa mfano Karikoo, hutembea na risiti moja hata kama wamenunua mzigo mara saba.

Huchukua mzigo kwenye duka hili mfano wa Sh 300,000 na kupewa risti. Wanaupeleka sehemu wanapotumia kwa ajili ya kukusanya mizigo yao. Wanarudi tena na kuchukua mzigo mwingine kwa mfano wa Sh 400,0000 wakitumia risiti ileile moja. Kitu ambacho kuna watu wanafunga mzigo hadi wa milioni moja na kuendelea, lakini risiti anayokuwa nayo ni ya Sh 300,000 ambayo anakuwa ameichukua kwenye duka moja tu. Anayefanya hivyo ni mwananchi wa Tanzania ambaye kila siku anailaumu Serikali yake kwa kutokuleta maendeleo.

Wenye dhamana ya kufuatilia, wanakaa ofisini, kwenye majengo ya kifahari, kwenye viti vya kuzunguka, huku wakipigwa na viyoyozi, wakisubiri mwisho wa mwezi ufike na mishara iingie kwenye akaunti zao.

Wakifuatilia basi ujue Rais ametoa tamko kali au siku kuu zimekaribia, wanatafuta fedha za siku kuu.

Tuliona wakati siku kuu ya Iddi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walikamatwa maeneo ya Kariakoo kwa sababu ya kutokuwa na risiti. Tulitegemea zoezi litakuwa endelevu, lakini baada ya siku kuu kupita, haijawa hivyo.

Mbali na hiyo, pia nimebaini juu ya risiti za kawaida ambazo hizo ndizo ambazo wafanyabiashara wengi wanazitumia.

Baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia risiti hizo, kwa mfano, mtu akinunua mzigo wa Sh 70,000, mteja wake akidai risiti huandika sh 7,000, kisha huchana na kuongezea sifuri nyingine baada ya kuchana ili kwenye kumbukumbu isomeke 7,000/- lakini kwenye risiti isome Sh 70,000. Kama mteja hajadai hawatoi kabisa.

Kifupi mambo mengi yanafanyika kwenye nchi yetu ambayo zisipofanyika jitihada za dhati na zikatumika mbinu mbadala katika kutokomeza mipango mingi mizuri ya Serikali ya awamu ya tano, itaishia kuandikwa kwenye makaratasi tu, kama ambavyo imekuwa ikifanyika tangu uhuru.

Kila la kheri CCM katika mchakato wa kukabidhi kijiti cha uongozi ndani ya chama kwa mwenyekiti mpya kama ilivyoutamaduni wenu. Tunaimani kupitia Dk. Magufuli CCM itakuwa mpya na nchi pia.

0764000383