Home kitaifa Wakulima wa zao la muhogo Kisarawe kuanza kunufaika

Wakulima wa zao la muhogo Kisarawe kuanza kunufaika

1597
0
SHARE
Wana kikundi wa Green Voices wa kitanga wakiangalia namna mashine yakusagia muhogo inavyofanya kazi.

Na Sidi Mgumia, Kisarawe

Wakulima wa zao la muhogo wa kijiji cha Kisanga wilayani Kisarawe wanataraji kufaidika na soko jipya la muhogo baada ya kupatikana kwa ufadhili wa Taasisi ya Wanawake wa Afrika ya Uhispania.

Kutokana na ufadhili huo wakulima hao wataweza kuuokoa muhogo ambao umekuwa ukipotea kwa asilimia kubwa kutokana na kutokufahamu matumizi mengine mengi ya muhogo.

Hili linathibitika katika jamii mbalimbali nchini kwani wengi wamekuwa kwa muda mrefu wakiliona zao la muhogo ni zao duni na hata wakulima wa mihigo kuwa masikini hali inayotokana na kuiuza kwa bei ndogo pia kukosekana kwa masoko.

Vile vile, kama ilivyozoeleka kwa wengi kuwa muhogo una matumizi machace ambayo ni pamoja na kuuchemsha, kuuchoma na kuutafuna mbichi.

Zaidi na hapo wengine hutumia katika mapishi ya uji na ugali, majani yake kama mboga ya kisamvu lakini pia miti yake kama kuni.

Taasisi ya Wanawake wa Afrika ya Hispania ambayo inawafadhili wanawake wa Kijiji cha Kitanga, Wilayani Kisarawe, mkoa wa Pwani nchini Tanzania kupitia mradi wa Green Voices wenye lengo lakukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, imejitoa kuwapatia fursa wanawake hao kuimarisha uzalishaji pia masoko.

Kwa mujibu wa Abiah Maghembe ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mradi wa huo, tangu alipotoka Madrid, Uhispania alipopata mafunzo ya namna yakupambana na mabadiliko ya tabia nchi, amerudi nyumbani na kuwahamasisha wawake wa Kitanga wapatao 30 na namna watavyofaidika na kuboresha matumizi ya muhogo pia kujipatia fursa ya masoko ya uhakika.

“Hii ni habari njema zaidi kwani swala hilo limepokelewa kwa mikono miwili na wanawake hao na kuahidi kuwa wako tayari kufanya ujasiriliamali huo ili kujikomboa kiuchumi kama ilivyo kwa akina mama wengine wenye miradi kama hiyo ulimwenguni kote,” alisema Maghembe

Akizungumzia faida za muhogo na namna ambavyo mtu anaweza akautumia na kujipatia kipato licha yakupata chakula tu, anasema kuwa maganda ya mihogo pia hutumika kama chakula cha mifugo yakikaushwa au mabichi.

Vile vile, muhogo ukisagwa mbichi kupitia mashine maalumu ambayo inachuja maji yake kutoa na kupunguza sumu iliyopo  kwenye muhogo hivyoo kuuacha salama kabisa.

Kwa upande wa teknolojia, njia bora za usindikaji ni  kwa kutumia mashine aina ya Grater. Hii hutoa chembechembe laini za muhogo, ambazo baadae hukamuliwa kwa kutumia kifaa kingine kiitwacho “presser” ili kuondo sumu iliyoko kwenye muhogo. Mashine hii hutumika hususani kwa muhogo mchungu pia kwa kutumia mashine aina ya chipper ambayo hutoa vipande vidogo vidogo (chips). Mashine hii hutumika hasa hasa kwa ajili ya mihogo mitamu au ile ya baridi.

Chakufurahisha zaidi ni kwamba zao la muhogo lina matumizi makubwa na mengi zaidi ya ambavyo wengi wamezoea ama wanafahamu, na hii ina maana ya kwamba kwa kutumia muhogo huo huo unaweza ukatengeneza vyakula lukuki kama ambavyo wakina mama wa kijiji cha Kitanga wanavyofanya sasa.

Ni faraja kubwa kuona kwamba akina mama hao wamekuwa wabunifu na kuhakikisha kuwa wanautumia muhogo vilivyo kutengneza vyakula bora kama vile cassava chop, chips, chapati, maandazi, biskuti, tambi, katlesi, keki na vingine vingi.

Juhudi hizo ni baada yakupatiwa mafunzo kupitia mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na taasisi hiyo ya Uhispania iliyoko chini ya Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega Sanz.

Abiah anasisitiza kuwa kuanzishwa kwa mradi huo wa kusindika muhogo pamoja na bidhaa zake kuna manufaa makubwa kwa jamii na matarajio yao nikufika mbali haswa kiuchumi.

Anaongeza kuwa wameamua kutilia mkazo zao la muhogo kwani ni zao linalookoa jamii nyingi nchini hasa nyakati za ukame.

Lakini pia Barani Africa, Tanzania inashika nafasi ya nne baada ya Kongo DRC, Ghana na Nigeria kwa uzalishaji wa muhogo ambapo inasemekana kuzalisha tani milioni tano kwa mwaka ambazo ni sawa na tani 8 kwa ekari moja.

Muhogo hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye maeneo ya mita 0 – 1500 kutoka usawa wa bahari. Vile vile muhogo hustawi vizuri kwenye maeneo yanayopata mvua ya wastani wa mm 750  – mm1200 kwa mwaka. Muhogo hustawi vizuri kwenye ardhi ya kichanga. Vili vile zao la muhogo ni maarufu sana kwa uvumilivu wa hali ya ukame.

“Ni jambo la msingi sana kwetu kwani kwa sasa muhogo hautaozea tena shambani kwakua matumizi lukuki yanafahamika na kupitia kikundi chetu hiki cha wakinamama wa Kitanga cha Green Voices nilichokianzisha miezi mitatu iliyopita,  tutajitahidi kulitumia zao hili ipasvyo,” alisisitiza Maghembe

Kwa upande wake Silvera Mujuni, Ofisa Chakula na Lishe wa Wilaya ya Kisarawe, anasema kwamba wilaya hiyo ina fursa kubwa ya kusindika na kuchakata mazao mengi yatokanayo na muhogo kwa kuwa zao hilo ndilo kuu kwa chakula na biashara.

Mujuni anasema kuwa juhudi za wakina mama wa Kitanga zitaleta faida kubwa kiuchumi kijijini hapo kutokana na kwamba ardhi yao inastawisha muhogo kwa wingi.

“Akina mama hawa fursa wameshaipata sasa ni kazi kwao kuitumia ili waweze kunufaika kiafya na kiuchumi katika jamii zao na hasa kupitia mshikamano walionao katika kikundi chao cha Wanawake wa Green Voices Kitanga,” alisisitiza Mujuni

Akitoa pongezi zake Anna Sallado ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanawake wa Africa ya Hispania anawashukuru wanawake kwa kuupokea mradi, lakini pia kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya na ni tegemeo lake kuwa kutakuwa na mafaniko makubwa zaidi ya hapo kwani kikubwa ni kujihakikishia usalama wa chakula, kujipatia kipato lakini pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tumefurahishwa na juhudi za akina mam wa KItanga ambazo zimeonyesha mafanikio ndani ya miezi mitatau tangu kuanzishwa kwake na kwa hilo tunaangalia namna ambavyo tutaingia katika awamu ya pili ya mradi na kuwa na mipango endelevu katika swala zima la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Sallado

Kwa upande wake, Secelela Balisidya ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, anasema kwamba inatia moyo sana kuona namna wakina mama walivyohamasika kushiriki katika miradi hiyo ya Green Voices ambayo ipo pia katika mikoa sita nchini ambayo ina malengo ya kumkomboa mwanamke kupitia ujasiriamali lakini pia kupambana kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Akinamama 10 wanaofanya miradi mbalimbali ya ujasirimali kupitia mradi wa Green Voices wanatoka mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro, Morogoro, Kigoma, Pwani na Dar es Salaam.

Naye Mtendaji wa Kijiji hicho, Wazir Yakoub Wazir, aliwataka akinamama hao wasiishie hapo bali wajitahidi na kuhakikisha wanasajili kikundi chao ili kiwe rasmi na waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali na taasisi nyingine za binafsi.

“Hili litaleta tija sana na kwa upande wetu tuko tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika ili kuwawezesha ninyi mfanikishe malengo yenu,” alisisitiza Wazir

Pamoja na mambo mengine, Diwani wa Kata ya Msimbu, Anna Lilomo, amesema atajitahidi kwa kushirikiana na madiwani wenzake ili kuhakikisha kuwa mambo Kisarawe yanakwenda sawa na mradi unazaa matunda kwani anaamini kuwa kufanukiwa kwa mradi ni kfanikiwa kwa wana Kitanga na Kisarawe kwa ujumla.

Na ukweli ni kwamba leo hii watu wanapohamasishwa kulima muhogo kwa sababu ya kustahimili ukame, bado wengi wanasuasua, lakini watakapoambiwa kwamba unga wa muhogo unatoa bidhaa nyingi zenye faida kubwa, huenda wengi wakaligeukia zao hilo na kulima kibiashara.

Akisisitiza hilo hilo Diwani wa viti maalum Mossy Sultan Kufurumbaya anasema kuwa wao wako tayari kuwasaidia akina mama kupitia  vikao vya Baraza la Madiwani ili waweze kupatiwa misaada na mikopo hata kupitia katika asilimia 10 ya bajeti ya halmashauri ambayo hulenga kuwasaidia wanawake na vijana.

Akinamama wa Kijiji cha Kitanga wanaweza kuwa mabalozi wazuri wa zao hilo, kwa sababu tayari wameanza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo hata wananchi wa kijiji hicho wameshangazwa nazo baada ya kuzionja na kuona ubora wake.

Wakiongea kwa nyakati tofauti akina mama wana kikundi wa hicho katika kijiji cha Kitanga wamesema kuwa kilimo cha muhogo siyo tu kitasaidia kukuza pato lao kama wakulima, lakini kinaweza pia kuokoa mazingira pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu mabilioni ya pesa zitumikazo kuagiza chakula nje, jukumu ambalo kikundi cha Kitanga Green Voices kimeamua kulibeba.

Kiujumla muhogo ni zao mojawapo ambalo linaweza kuiepusha jamii na baa la njaa huku katika baadhi ya mataifa likitumika kama chanzo cha nishati ili kukabiliana na bei ya mafuta na nishati nyinginezo.