Home Makala JPM, Ndugai haya si ya kuyapuuza

JPM, Ndugai haya si ya kuyapuuza

520
0
SHARE

NA RACHEL MRISHO

NI vigumu kubashiri nini kitajiri katika Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unatarajia kuanza Septemba 6, mwaka huu.

Matarajio ya Watanzania ni kuona chombo hicho muhimu kinafanya kazi yake kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Hawatarajii kuona Bunge la maigizo lililojaa vijembe, mipasho, kejeli au kususia kila mara.

Watanzania wasio na itikadi ya vyama vya siasa na mashabiki wa vyama wenye nia njema na taifa lao wanaamini kwamba kurejea kwa Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye alikuwa nchini India takribani miezi miwili kwa matibabu, kunaweza kuleta mabadiliko makubwa ndani ya Bunge hilo.

Kama ilivyoshuhudiwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge lililopita ulioongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, wa kujadili na kupitisha Bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2016/2017, ulikuwa na maigizo ya kutosha yenye sura isiyofurahisha machoni mwa watu hususan waliotumia muda wao mwingi kwenye foleni ya kuwapigia kura wawakilishi hao.

Minyukano na mivutano katika mkutano ule uliokuwa na viashiria vya ubabe katika ya makundi mawili, ulionyesha wazi kuwa kulikuwa na kitu kimepungua ambacho ni busara kwa pande hizo mbili.

Kwa mtazamo finyu yaliyojiri hayakuwa ya lazima, ni mambo yaliyokuwa na uwanda mkubwa wa kuzungumza bila kuathiri shughuli za Bunge.

Kususia vikao vya Bunge ni sehemu tu ndogo ya namna ya kushinikiza suala fulani lipewe kipaumbele ama lisikubalike, hivyo hapakuhitaji elimu ya ziada wala kutunishiana misuli zaidi ya kutafuta mwafaka kwa jambo husika.

Hoja ya wapinzani kususia Bunge ilikuwa ni kutokuwa na imani na Naibu Spika Dk. Tulia katika uendeshaji wa chombo hicho muhimu, wakidai kuwa alikuwa anapendelea upande mmoja ambao ni wa chama tawala na kukiuka baadhi ya kanuni. Kilichotakiwa hapo ni kuangalia uzito wa hoja zao na kuangalia namna bora na yenye tija ya kumaliza mvutano kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

Ni wazi kabisa kuwa misuguano na mivutano kati ya Dk. Tulia na wapinzani iliondoa ladha ya ufuatiliaji wa shughuli za Bunge, itoshe tu kusema kwamba, hata baadhi ya wapiga kura walikata tamaa kwa kukosa wawakilishi wao wakati wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali ambayo kimsingi huainisha vyanzo vya mapato ya Serikali ikiwamo makusanyo ya kodi, pia hutoa dira ya maendeleo ya nchi.

Yaliyojiri katika mkutano wa tatu, yanabaki kuwa historia na darasa bora kwa wanaohitaji kujifunza.

Kama nilivyoeleza awali Bunge linatarajia kuanza siku chache zijayo. Kwa upande wa siasa nchini hali si shwari. Wabunge wa upinzani hivi sasa wako katika harakati za kutetea demokrasia wanayodai kuwa inaelekea kuminywa na Serikali.

Makala haya naangalia mambo mawili yaliyo mbele yetu; Mosi ni kuanza Bunge. Pili harakati za Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema za kuanzisha Operesheni iitwayo Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania-Ukuta ambayo inatarajia kuanza Septemba Mosi mwaka huu, siku chache kabla ya Bunge kuanza.

Mambo haya yanapaswa kuangaliwa kwa jicho pana kwanza Serikali kujitathimini katika msimamo wake wa kupambana na upinzani katika wakati huu ambao Watanzania wanasubiri kuona ahadi zilizotolewa na Chama tawala zinatekelezwa.

Pia; ifahamike kuwa washiriki wakuu kwa upande wa upinzani bungeni ndio hao hao wanaohamasisha kufanyika kwa operesheni  Ukuta.

Hoja hapa ni kwamba kama wapinzani watapata maumivu ya aina yoyote wakati wa kutetea demokrasia ni wazi kwamba Septemba 6 wakati Bunge litakapoanza yawezekana hali ikaendelea kuwa mbaya ndani ya Bunge letu.

Spika Ndugai ameahidi kurejesha maridhiano ndani ya Bunge hilo kwa kushirikisha maspika wastaafu. Kinachosubiriwa nu kuona utekelezaji wa jambo hilo unafanyika ili hadhi ya Bunge irejee.

Uimara wa Bunge unaweza kupunguza mihemko ya kisiasa na kuondoa chuki baina ya wabunge wenyewe kwa wenyewe pamoja na kiongozi wao wa Bunge.

Spika, Naibu Spika na Wabunge wakiheshimu kanuni na sheria zilizopo na kupingana kwa hoja matukio ya kulishushia hadhi Bunge letu yatapungua ama kukoma kabisa.

Wakati tunatarajia kuona usuluhishi wa nguvu ya Spika wa Bunge ni umuhimu pia Rais John Magufuli auangazia uamuzi wake wa kuzuia shughuli za kisiasa zisifanyike hadi mwaka 2020. Rais atazame maslahi ya taifa na si mtazamo wa kisiasa.

Hakuna asiyefahamu kwamba John Magufuli ndiye Rais wa Tanzania, tena mwenye nguvu na mamlaka makubwa katika uamuzi wa jambo lolote. Kwa kutambua hilo kama itampendeza Rais wetu basi asimamie misingi ya  Katiba yetu katika kulinda maslahi ya Taifa.

Hulka ya Watanzania ni watu wanaopenda amani na ni waoga wa machafuko. Hilo halina ubishi. Angalizo ni kwamba lisitokee jambo litakalo wasukuma kutoka kwenye amani na woga na kuingia kwenye vurugu na ujasiri, mambo hayo yakiingia damuni ni vigumu kuyaondoa.

Taifa lenye watu wenye usugu wa kusikia milipuko ya mabomu, risasi za moto na umwagaji damu ni taifa hatari sana.

Kwa muktadha huo hakuna sababu yoyote ya msingi ya kulazimisha kuliweka Taifa letu reheni.

Ni vema viongozi warejea katika viapo vyao ambavyo ni pamoja na kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa sababu wanaoucheza mchezo wa tishio la amani ni viongozi wetu na ni hao hao watakaoucheza mchezo wa kurejesha maridhiano na amani.

Uzalendo na busara vinahitajika ili kuepusha vurugu, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na aina yoyote ya umwagaji damu.

Hofu ya hali ya usalama imeenea kila kona ya nchi ndio maana baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa akiwamo Mwenyekiti wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa na kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi –CCM Steven Wasira wametoa angalizo kuhusu suala hilo.

Ili kudumisha amani ulinzi wa taifa hili uanzie kwa viongozi wakuu wa Serikali na Bunge letu tukufu.

Mungu Ibariki Tanzania

0713 241234