Home Makala Kama Magufuli, Chadema wana makosa waambiwe

Kama Magufuli, Chadema wana makosa waambiwe

396
0
SHARE

NA OVERCOMER DANIEL

WIKI iliyopita niliandika Makala yenye kichwa kilichosomeka “Ukuta wa Chadema na msimamo wa Magufuli; watumishi wa Mungu majaribu”. Hii ni sehemu tu ya mwendelezo wa mada niliyoianzisha wiki iliyopita. Kwa kuweka kumbukumbu vizuri nieleze japo kwa muhtasari kile nilichokiandika katika sehemu ya kwanza ya Makala hii.

Nilikuwa nazungumzia juu ya msuguano uliokuwapo baina ya serikali na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu kile ambacho wao walidai kuwa wangeandaa maandamano na mikutano ya nchi nzima kupinga kile walichokiita kupinga ‘udikteta’ unainyemelea Tanzania.

Chadema walituhumu kwamba kuna kila dalili kwamba nchi yetu sasa inanyemelewa na chembechembe za udikteta, kwa hiyo wanachokifanya ni kujenga ukuta ili kuzuia hali hiyo, wanasisitiza kwamba nchi hii ibaki ikiongozwa au kuendeshwa kwa mujibu wa sheria huku Katiba ambayo ndio sheria mama ikiheshimiwa!

Baada ya tangazo hilo la Chadema  tukasikia na kuona serikali ikitunisha misuli, rais wetu alitangaza kuwa anayetaka kuandamana aandamane akione cha moto, na akapigilia msumari kuwa yeye huwa hajaribiwi. Tena tukashuhudia serikali yetu ikipiga jaramba kupitia jeshi lake la polisi kama salamu kwa wale wote ambao waliokuwa wamekusudia kuandamana na “kujenga ukuta’ Septemba Mosi!

Wapo waliokuwa wakiunga  mkono kwa hoja au kishabiki wazo hilo la Chadema na kupinga msimamo wa serikali, lakini tena wapo ambao walipinga hilo la CHADEMA na kuiunga mkono serikali kwa hoja au kishabiki tu. Na ninapozungumzia hoja hapo juu sio lazima ziwe za maana au za hovyo, lakini ni ngumu kuzuia mtu kufikiri au kusema au kuandika katika dunia hii ambayo inaenda kasi ikichajizwa na maendeleo ya kutisha na kushangaza ya teknolojia habari mawasiliano.

Katika ujumla wa hayo yote, baadhi ya wananchi waliingiwa hofu kuu, mimi ni mmoja wa wengi hao ambao walijawa na hofu kubwa. Kwa upande wangu hofu ilisababishwa na ukweli kwamba kama kila upande ungetunisha misuli, na wanaondamana ni raia, na tayari jeshi la polisi lilionekana kujipanga, kwa kweli sikuwa naiona amani siku hiyo.

Na niwe mkweli, kama zile silaha ambazo tuliziona kwenye picha za mazoezi ya jeshi la polisi ndizo ambazo zingetumika kuwadhibiti waandamanaji siku hiyo, moyo wangu uliugua kwa maumivu yanayosababishwa na hofu!

Nikawaza hivi, kama risasi zingerindima, zikavunja viuno na miguu ya waandamanaji au hata kuua, je tulipaswa kufanya nini? Majibu yaliyonijia kichwani yaliniongezea ugumu wa kufikiri. Je, ili watu wasijeruhiwa au kuuawa siku hiyo tungemshauri Rais Magufuli na serikali kwa jumla iwaachie Chadema watimize haki yao ya kikatiba? Au tuwaambie Chadema waachane na mpango wao wa ‘kujenga ukuta’ ili kutii amri ya Rais Magufuli?

Nikauliza nani yuko tayari kati ya ‘miamba’ hii miwili hapa kumuacha mwenzake apate akitakacho? Au kila mmoja hataki kuonekana ameshindwa? Lakini kushindwa huku ni kwa manufaa ya nani? Kama kushindwa kwa mmoja wapo kutalinda masilahi mapana ya Taifa na raia wake, kuna ubaya gani?

Ndipo sasa kila mmoja akawa anatoa maoni yake kuhusu hili, mitaani, kwenye vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii. Watoa maoni hawa ni pamoja na raia wa kawaida na watumishi mbalimbali wa Mungu katika nafasi za kidini.

Niliona kwenye mitandao watumishi wa Mungu hasa Wachungaji na Wainjilisti wakitoa maoni ya na kujadili sakata hili. Hapa ninapozungumzia ‘sakata’ nalenga kusema msimamo wa rais na msimamo wa serikali kuhusu Ukuta!

Baada ya kufuatilia hoja za baadhi yao ndipo nikadiriki kusema kwamba wako majaribuni kwa sababu wengi wamefeli kabisa kuacha kuwa na upande katika hilo. Wanatoa maoni na ushauri huku wakionekana kabisa kuwa na upande kati ya serikali na CHADEMA.

Lakini mbaya zaidi ni pale ambapo tunajikuta tunaitumikia hofu ya rais tukidhani tunadumisha amani katika nchi huku tukiacha makovu katika mioyo ya wale ambao tunawaongoza, na wakati mwingine tunaunga mkono Chadema tukidhani tumesimamia haki kumbe tunajiingiza matatizoni kwa kuwa hatuna hoja za maana tukipimwa!

Nikasema hivi, kama watumishi wa Mungu wanajipa jukumu la kuleta utatuzi katika nchi hii au kusuluhisha migogoro ya kisiasa hapa nchini wahakikishe kwamba dhamiri zao zinawashuhudia kwamba hawana upande katika pande mbili zinazopingana. Wahakikishe mioyoni mwao wanamuogopa Mungu peke yake na sio rais, viongozi wa vyama siasa au wananchi.

Kama katika sakata hili rais ana makosa aambiwe, ashauriwe, arekebishwe, kwa sababu ni mwanadamu, anaweza kughafilika. Kumpigia makofi hata anapoteleza na kuteleza kwake kukatishia amani ya nchi, hatumtendei haki rais, hatulitendei haki taifa wala hatuzitendei haki huduma na dhamana alizotupa Mungu!

Katika kusuluhisha au kupendekeza njia za utatuzi tusifanye hivyo kwa kujipendekeza kwa rais au idara zingine za ulinzi na usalama wa nchi yetu. Tusijipendekeze kwao, hata wao wanapenda watu watakaowashauri ukweli kwa upendo na unyenyekevu, wanapenda kupata njia bora za kulitunza taifa ili lidumu katika amani. Wao sio miungu kwamba hawakosei na kughafilika, ndio maana wanahitaji kushauriwa lakini sio kubezwa au kutukanwa.

Viongozi wa dini kwa ujumla tunapoishauri serikali tusiishauri kwa kutaka sifa, tunapomshauri rais au waziri mkuu tusifanye hivyo kwa hila, tufanye hivyo kwa masilahi ya nchi. Wanapoteleza na kughafilika kama wanadamu wasaidiwe, na ukweli peke yake ndio utakaowasaidia viongozi wetu kudumu katika njia salama ya kutupeleka kule tunakotaka. Tusiwaharibu viongozi wetu kwa kuwapamba na kuwasifia hata wanapokosea, tujitofautishe!

Na zaidi ya yote tunapaswa kutafakari na kuzipima kauli zetu, iwe tunapingana na misimamo ya serikali au misimamo wapinzani katika nchi hii, tuseme ukweli, tusiingie kwenye mkumbo wa ushabiki badala ya kutengeneza, tusjipendekeze kwa yeyote kati yao, nafasi zetu hazituruhusu kufanya hivyo, ni hatari tena sio kidogo.

Nitatoa mfano hapa, Wapinzani walitaka au wanataka kuandamana, rais anawakataza au amewakataza, tujadili. Nilisema rais ndiye kiongozi mkuu wa nchi yetu, amewekwa pale alipo kwa mujibu wa Katiba ya nchi hii, na katiba ndio sharia mama, hakuna mtu yeyote awe kiongozi serikalini, bungeni au kwenye vyama vya siasa ambaye yuko juu ya sharia, Katiba hii inaweka mwanzo na mwisho wa mipaka ya rais wetu Rais wetu na viongozi wengine, rais wetu aliapa kuilinda Katiba., alipo apa kuilinda maana yake aliapa kuishi na kutenda ndani ya mipaka aliyopewa na Katiba.

Chadema wanadai kuwa ni katiba hiihii inayowapa wananchi haki ya kuandamana, vyama vya siasa vina haki pia ya kikatiba ya kufanya mikutano na bila shaka hata maandamano. Rais amewakataza, Chadema wanasema kukataza huku ni kinyume cha matakwa ya Katiba.

Unatokea msuguano hapo, serikali inatunisha misuli, na wapinzani vivyo hivyo wakidai kulindwa na katiba ambayo kila mmoja anapaswa kuiheshimu kwa ustawi wa taifa letu. Wananchi wanaingiwa hofu, wanaishi kwa mashaka!

Kama ndivyo ilivyo, na kama katiba inaruhusu maandamano, watumishi wa Mungu wasiite maandamano kuwa ni ushetani kwa ajili tu ya kumfurahisha rais wetu, kama Katiba imeruhusu maandamano (haijalishi ni mabaya au mazuri), wanapoyapinga ili kumpamba rais wao pia wanashiriki katika kiuhalifu Katiba. Hawapaswi kuwapinga wapinzani mpaka itakapothibitishwa kuwa amri ya rais ya kukataza maandamano na mikutano ya kisiasa haijaathiri wala kwenda kinyume na katiba ya nchi yetu.

Na ikithibitika kuwa aliteleza na kwamba katazo lake linakwenda kinyume na Katiba, ashauriwe kwa upendo wa dhati kabisa kwamba “Mheshimiwa Rais, pale ulighafilika” Sio kumuunga mkono ili kujipendekeza kwake, kujiweka karibu na yeye, sio vizuri kwa masilahi ya nchi yetu. Mimi nadhani hata Rais Magufuli mwenyewe asingependa aina hii ya viongozi wa dini kulingana na dhamira njema aliyonayo kuisongesha mbele nchi hii!

Badala yake tungeweza kumshauri rais kwamba ili kusiwepo mikutano ya kisiasa nchini mpaka wakati wa uchaguzi mwingine, basi angeweza kuandaa muswada na kuupeleka Bungeni utakaopendekeza jambo hili na litungiwe sheria. Na sharia ikitungwa, ikapitishwa na Bunge, halafu bado wapinzani wakang’ang’ana ndipo watumishi wa Mungu wawageukie wapinzani na kuwashauri na kuwakemea bila hofu kwamba wanavunja sharia za nchi!

Kuna ubaya gani kumshauri rais namna hii kuliko kumuunga mkono kwa uongo ili ionekane kuwa mko upande wake, narudia tena, nadhani hata rais wetu mwenyewe asingefurahia aina hii ya washauri, vinginevyo tunyamaze, tumsaidie kwa kumuombea tu! Tumsaidie rais wetu kwa kumshauri na kumkosoa bila hila au nia ovu ndani ya nafsi zetu. Tumuombee hekima na uthabiti usiokwenda kinyume na matakwa ya Katiba inayotambulikana hivi sasa.

Kwa upande wa pili kwa wale wanaopingana na  misimamo ya rais kama tunataka kushauri na kuleta suluhu, badala ya kubeza kauli za rais, hata kama kweli amekosea, kwa nini kama tunashindwa kumkabili rais tusiende kuzungumza na viongozi wa UKUTA ikiwezekana waahirishe kwa muda au watafute namna nyingine ya kufikisha wao kwa serikali na dunia kwa ujumla?

Kama ni rais anakosea, na tunapingana na msimamo wake tusifanye hivyo kwa kujipendekeza kwa wanasiasa wa kambi ya upinzani.

Kama ni wao ndio wanakosea kuratibu maandamano na mikutano ya kisiasa licha ya katazo la rais twende tuwaambie ukweli kwamba wanakosea kufanya maandamano, lakini tuwaambie hivyo kama tu ikithibitika kuwa wana haki ya kikatiba, tuwashauri kama ninavyopendekeza hapo juu.

Kuwabeza, kuwatukana na kuwakejeli ili kufurahisha upande mwingine hakuwezi kuleta matokeo tarajiwa ambayo ni amani na utulivu, wao wanasema wana haki, ni sawa, lakini waangalie, kwa ajili usalama wa Watanzania watiifu kwao walitazame hili mara mbili na kuona kuwa pengine kuahirisha mpango wao ni salama zaidi kuliko kuendelea nao.

Hoja yangu ni hii hapa: Watumishi wa Mungu linapokuja sula la kisiasa katika nchi hii wawe makini, wasiwe na upande, wasikandamize mmoja na kumuinua mwingine kwa masilahi binafsi. Hatupaswi kuogopa kusimamia ukweli kama kweli tunaka kuendelea kusimamia maadali ya nafasi tulizo nazo. Tuna nafasi kubwa sana kuangamiza taifa hili kwa kalamu au vinywa vyetu tusipokuwa makini.

Misikiti na makanisa tunayoyaongoza yana watu wenye vyama na wasio na vyama, lakini wote wanatusikiliza sisi, tena ikumbukwe kwamba kitendo cha wao kuwa wafuasi wetu haina maana kwamba wao ni mazuzu, wajinga na mataahira wasioelewa haki na wajibu wao. Tusimamie haki, tusiwagawe, ni hatari!

Tutakaposimamia haki, hata wao watajua kuwa tuko kwenye mstari wa haki, na hata Mungu atajua, na tunapofanya mambo kwa upendeleo, wao watajua, wanaweza wasiseme, lakini tutapoteza nafasi zetu ndani ya mioyo yao, na tutakapopotea mioyoni mwao ni ngumu kwa wao kupokea vitu vya Mungu tulivyoagizwa na Mungu, na huo ni mwanzo wa kuwapoteza!

Tusimamie haki, bila kumuonea mtu. Tusipendelee serikali wala wapinzani!

 

MCHUNGAJI OVERCOMER DANIEL

EAGT – DAR ES SALAAM

SIMU: 0672 663482