Home Makala SIASA ITAENDELEA KUUA WAKINA LIPUMBA

SIASA ITAENDELEA KUUA WAKINA LIPUMBA

482
0
SHARE

NA FRANK BANKA

KWENYE sakata la Chama cha CUF, namtazama Profesa Ibrahim Lipumba kwa jicho la udadisi. Naitafakari Elimu yetu na bara zima la Afrika. Nawatafakari zaidi watanzania waliomo kwenye dunia hii ya sayansi na teknolojia.

Hivi ndio jinsi ninavyoona namna matumizi ya elimu kwa hiki kizazi chetu yalivyoharibiki. Unaweza kua na fikra yakinifu na pembuzi Ila zisiwe na faida kwa jamii iliyokuzunguka.

Profesa Lipumba ni moja ya wasomi wakubwa waliobahatika kuipata elimu ya Kikoloni. Namaanisha kwa wakati ambao alizaliwa na kusoma bado taifa hili lilikuwa linaimba nyimbo za kupigania kupata uhuru.

Hivyo yuko kwenye elimu  ile ambayo waliitumia vizuri mababu zetu kama William Dubois ambaye ni mwafrika wa kwanza kupata PHD. Dubois hakujali kiwango cha elimu akichokipata na kupewa sifa kama mwafrika wa kwanza kupata PHD bali aliitumia elimu yake kudai haki za mtu mweusi huko Marekani katika kampeni ya “Back To Africa” ambayo kuna wamarekani weusi walirudi kutafuta asili zao wengine wakabaki Marekani.

Hii ndio namna ya nzuri ya Elimu, Tunapaswa kuitumia Elimu kwa faida ya kizazi hiki na kizazi kinachokuja. Kwa mfano Makamu wa Rais mstaafu Dk. Ghalib Bilal ni mtalamu wa Nyuklia aliesomeshwa na serikali ila mpaka sasa Tanzania ina kiwango kikubwa cha upatikanaji wa madini ya Uranium ambayo hayachimbwa.

Najiuliza kama  huyu mtalamu kamaliza muda wake kwenye siasa lakini katika kipindi chote hakuwahi kushika hata chaki na kutoa elimu aliyonayo kwa hiki kizazi. Inawezekana Leo watu kama yeye wangekuwa wakutosha nchini. Lakini pia ni nini maandalizi ya serikali kama inajua nchini kuna Uranium huku hakuna Chuo chochote kinachozalisha wataalamu wa Nyuklia?

Mwalimu Nyerere alipata kusema nchi hii inazo rasilimali lakini ni vizuri tukazitumia baadaye kipindi ambacho watanzania watakuwa na elimu ya kutosha yenye uwezo wa kugundua fursa na namna ya kuleta tija kwa Taifa . Hii ndio namna ya nzuri ya kuwa na uzalendo kwa taifa sio kuwa na utalamu wa aina fulani lakini utaalamu huo usitumike kuwasaidia wengine.

Hesabu zangu za haraka haraka karibu kwa kila mwanasiasa mmoja msomi  nchini kazalisha wapumbavu milioni moja ambao wanaishi kwa kumtukuza kwa kiwango cha elimu yake kisicho na faida kwa jamii iliyomzunguka.

Hesabu inaweza kuwa hivi kila mwanasiasa msomi aliyetumia vibaya elimu yake bila faida kwa jamii kachangia kuzalisha wafuasi wapumbavu kwa kiwango hiki.  Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 kuna Watanzania milioni 45 hivyo mchango wa kuzalisha wapumbavu kwa wanasiasa wasomi wakubwa wanaotumia siasa kujinufaisha uwe 1%. Hivyo unapata watanzania laki nne na nusu ambao watakuwa wakifuata maneno yake wakiamini yeye ndio mungu mtu.

Hakuna hasara kubwa kama hii kwa taifa letu ,maisha ya siasa yanachangia kupoteza wasomi wakubwa ambao wangekuwa watendaji ila wanaishia kupiga kelele kwenye majukwaa na elimu zao hazitumiki kama chachu ya kuwakomboa watanzania.

Kuna kila sababu hawa wanasiasa wasomi wakapewa vipindi vya kufundisha kwenye vyuo vikuu vilivyoko nchini nadhani hili lingekuwa  jambo kubwa zaidi maana lingesaidia kuzalisha watanzania makini kuliko Ilivyo sasa nguvu ya elimu yao inavyotumika kama vibaya.

Nchi yetu ina wasomi wachache lakini wengi wao ni wachumia tumbo kila mmoja anawaza kuwa na gari na nyumba nzuri kwa kuiba mali ya umma. Jambo hilo sio geni kwangu katika siasa kama ambavyo limetokea hivi karibuni Mkutano wa CUF kufuatia malumbano makali ya kumrudisha au kutomrudisha Profesa Lipumba kwenye nafasi ya uenyekiti.

Kilichotokea ndicho sura halisi ya wanasiasa na wafuasi wa vyama ambao wana maneno mengi  yasiyoweza kujenga taifa hili. Najiuliza hiki kinachoendelea CUF inamaana hawakujifunza kipindi kile cha sakata la Zitto Kabwe, Samson Mwigamba na Kitila Mkumbo   wakati ule walipofukuzwa Chadema?

Kuna matatizo mengi kwenye fikra za watanzania juu ya viongozi wa vyama vyetu vya kisiasa  kutokana na mafunzo ya elimu mbovu waliyoipata kutoka kwa viongozi wetu kwani badala ya kuzitumikia fani zao kuzalisha wataalamu wao wameishia kwenye fitina za siasa.

Ukada kuna muda unatawala kwenye Vichwa vyetu kuliko uhalisia na namna tunavyopaswa kufikiri juu ya matukio yanayotokea kwenye maisha ya kila siku hasa yanayohusu siasa.

Tunapaswa kuwa na mawazo huru kama vile kelele zetu za kila siku za kudai demokrasia. Haiwezekani tuwe na fikra huru za kidemokrasia lakini tukajivisha ukada ambao muda mwingine tunapingana na ukweli ambao unatuumiza ndani kwa ndani.

Haya matatizo ya watanzania yangemalizwa kama tungefahamu  umuhimu wa elimu na utashi wa kupambanua mambo lakini matokeo yake tunafundishwa utii wa vyama vyetu na kulalamika kiitikadi za vyama vyetu. Elimu sio lazima tuipate darasani hata hizi changamoto tunazokutana nazo kila siku ilitosha kutufundisha kuwa wanasiasa hawapendi tuwe na uelewa ila wanatufundisha utii wa vyama vyao.

Dunia ya kidemokrasia sio dunia ya kufia vyama bali ni ile ya kufungua uelewa na muda mwingine kupingana hata na Chama chako au mwenyekiti wa Chama chako au kauli zozote za viongozi wetu pale tunapoona hakuna usahihi kwa wanachokisema.

Kila serikali duniani huwa inaogopa wananchi wanapokuwa na elimu ya kutosha, tofauti yake na Afrika wenye elimu wamefungwa mdomo lakini wasiyo nayo wanapiga kelele kwenye majukwaa.

Tuwe na macho ya kuona kwani tofauti kwenye siasa za Afrika ni kwamba kila mmoja anawaza kushika madaraka fulani, ilimchukua muda mrefu Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF  lakini  hakujua ipo siku muda wake utakwisha na atakuja mtu mwingine kwenye nafasi yake. Tusimalize akili zetu kwenye siasa za kijinga zilizojaa ukada na uelewa kidogo. Tuutumie utashi wetu vizuri kujitofautisha na wanyama wengine.