Home Makala Zanzibar: Suluhu ni mazungumzo pekee

Zanzibar: Suluhu ni mazungumzo pekee

379
0
SHARE

NA HILAL K SUED

KAMA bado kulikuwapo na hata chembe ya uwezekano wa kuleta suluhu kwa mgogoro wa kisiasa huko Zanzibar, basi chembe hiyo iliyeyuka wiki iliyopita baada ya Rais John Magufuli kutembelea sehemu hiyo ya Muungano na kutoa hotuba.

Kilichobakia ni kuomba tu kwa Mwenyezi Mungu kwamba hali ya utulivu iliyopo sasa hivi Visiwani angalau ibakie kuwa hivyo hivyo.

Au pengine tutegemee tu kudhihirika ule usemi mmoja wa lugha ya Kiingereza kwamba ‘Time heals’ – yaani muda (mwingi) huponyesha vidonda.’

Na kusema kweli usemi huu ndiyo umekuwa ukitegemewa sana na watawala kule Visiwani – katika mitafaruku iliyokuwa ikijitokeza kila baada ya uchaguzi – tangu ule wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi kufanyika visiwani huko.

Na kila mara badala ya kutatua kwa njia za dhati, basi huachwa hivyo hivyo kwa matarajio watu watasahau, yataisha na hivyo amani na utulivu kuwapo kwa ahuweni ya watawala na hali ya maisha kuendelea kama kawaida.

Ni kweli hakuna anayeweza kuumaliza mgogoro wa kisiasa huko Zanzibar kwa sababu mtazamo wa watawala wa kule (na wa huku Bara pia) hautaki kuona au kukubali kuna mgogoro wowote isipokuwa kushikilia tu kwamba upande mmoja kati ya miwili wa kisiasa umedhamiria kuingiza chuki, kuvuruga amani, kumrudisha Sultani na kadhalika na kadhalika, bila ya hata kuthibitisha hoja zao.

Nitatoa mfano: Miaka kadha iliyopita, Mbunge mmoja wa Unguja na aliyewahi kushika nyadhifa katika Baraza la Mawaziri la Muungano, akiwahutubia wananchi wa jimbo lake wakati wa kampeni aliwaambia kuwa CUF ikishika nchi, watamrudisha Sultani Jamshid (yule aliyepinduliwa 1964)!

Huwezi kuamini kuwepo kwa kada mkuu wa CCM kuweza kusema kitu kama hicho huku akishika picha ya Jamshid juu kuonyesha wapigakura wake. Hii inaonyesha kitu kimoja tu – kukosa kabisa hoja ya kukubalika katika siasa za upinzani.

Yaani baada ya takriban nusu karne Zanzibar bado iko nyuma sana kimaendeleo ikilinganishwa hata na nchi nyingine za visiwa katika eneo la Bahari ya Hindi zilizojikomboa katika miaka kama ile ile ilivyojikomboa Zanzibar.

Sasa hivi huyo Jamshid ana umri wa miaka 96, yuko Uingereza na inasemekana hupoteza fahamu, achilia mbali kuwa na ari ya kutaka kurejeshwa madarakani Zanzibar!

Chimbuko kuu la mgogoro wa Visiwani ni la kijamii (ethnicity), na hata hivyo wanasiasa wakuu hawapendi kutaja hivyo waziwazi, ingawa baadhi ya wakereketwa wa chama tawala wamekuwa na ujasiri kidogo kulitaja.

Kada mmoja wa chama tawala kutoka Visiwani (sasa marehemu) alitamka katika kikao kimoja cha Bunge la Katiba mwaka juzi kwamba chama chake “kamwe hakiwawezi kuiachia nchi kwa wapinzani (CUF) kupitia vipande vya karatasi (yaani kwa sanduku la kura), na wakitaka labda watupindue.”

Hili, pamoja na lile tukio la bango la kibaguzi lililobebwa na vijana wa UVCCM kule Zanzibar wakati wa kampeni mwaka jana vinaonyesha hali halisi ilivyo siku zote, hali iliyokosa usuluhishi au hata kukemewa na wakuu wa nchi wenye dhamana ya kuliongoza taifa hili kwa amani. Ukimya wao unaonyesha kuafiki kwa kauli hizo.

Na wengi wanasema raundi hii ya mgogoro wa sasa hivi haukuanzia katika hali iliyozoeleka kuhusu namna chaguzi huko Visiwani zilivyokuwa zikizalisha migogoro kutokana na maamuzi ya Tume yake ya Uchaguzi (ZEC).

Ilishangaza katika uchaguzi wa mwaka jana kwanini Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishindwa kujihakikishia ushindi na kutangazwa hivyo hadi ikajikuta katika hali ya sintofahamu na mpinzani wake mkuu – Chama cha Wananchi – CUF.

Inaonekana safari hii ama CCM walisinzia au walijiamini mno kwamba chama hicho kinaweza tu ‘kufanya vitu vyake’ bila wasiwasi wowote kwani ndiyo chama kilichoshika dola pamoja na vyombo vyake, ikiwemo chombo hicho muhimu katika uchaguzi – ZEC?

Kwa maneno mengine kile kitu kiitwacho “kushindwa uchaguzi kwa kupungukiwa uungwaji mkono wa wananchi” huwa hakipo kabisa katika msamiati wa CCM kule Zanzibar – ingawa hiki hasa ndicho kilitokea mwaka jana.

Yumkini safari hii watawala wa Zanzibar walisinzia, au upinzani ulikuwa mkubwa mno kiasi kwamba ilikuwa vigumu CCM kufanya longo-longo kama kawaida katika chaguzi zile ziingine huko nyuma.

Hivyo walijikuta wanashindwa kutangazwa ushindi ile mara ya kwanza tu na ndiyo ukasukwa ule mpango wa ghafla wa kufuta matokeo na baadaye kutangaza uchaguzi mpya siku nyingine. Ajabu kubwa ni kwamba ule uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri haukufutwa.

Hadi leo hii hili suala hili halijapatiwa maelezo ya kuridhisha – yaani uchaguzi wa siku moja, daftari moja la wapigakura lakini matokeo ya Zanzibar yawe haramu na yale ya Bara yawe halali.

Na imekuwa ikielezwa kwamba sababu kuu ya “kukosa” (au “kukwepa”) suluhisho la aina yoyote kule Visiwani ni kwamba laweza kubadilisha hali ya kisiasa ya visiwa hivyo na kuvisalimisha kwa utawala mpya wa chama kikuu cha upinzani – CUF. Na hapo ndipo kilipo kiini cha mgogoro wenyewe. Hivyo basi watawala walikuwa wanahakikisha wanauonyesha mgogoro kwa namna ambayo ni vigumu kupata suluhisho.

Mfano wa ninayosema ulijitokeza wakati wa kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais wa Muungano aliyetangulia – Jakaya Kikwete alipotembelea Pemba mwaka 2006. Ingawa hotuba yake kule haikuwa ya kuukoroga zaidi mgogoro kama hii ya Magufuli miaka 10 baadaye, alisema mgogoro unakuzwa tu bila sababu kutokana na watawala pande mbili za Muungano “kutokutana mara kwa mara kuondoa kero za Muungano.”

Mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar hauhusu masuala ya Muungano kwani chaguzi zake husimamiwa na sheria na mamlaka za kule – ingawa ghasia zinapoibuka, au zinapotaka kuibuka watawala kule huutazama utawala wa Muungano kuwahakikishia vyombo vya dola kuthibiti hali na hasa kuuthibiti upande ule mwingine.

Siasa hizi za hovyo hovyo zinazoambatana na chuki za kibaguzi zisizokemewa vilivyo zimekuwa zikikwaza maendeleo ya Zanzibar. Inashangaza hadi sasa ‘mapinduzi’ bado ndiyo mbiu kuu ya watawala wa Zanzibar na bila shaka lengo ni kama nilivyosemahapo juu – kuwakumbusha wananchi kuna watu wanataka kurejesha watawala wa Kiarabu.

Linganisha Zanzibar na visiwa vingine katika eneo la Bahari ya Hindi – ambavyo ni Mauritius na Seychelles (Ushelisheli). Mauritius ina karibu idadi sawa ya wakazi kama Zanzibar (takriban wakazi 1.3 milioni) na ilipata uhuru wake miaka minne baada ya mapinduzi ya Zanzibar, yaani mwaka 1968.

Na visiwa vyote viwili vilikuwa na zao moja kubwa la uchumi, Zanzibar ni karafuu na Mauritius ni miwa. Leo hii ukilinganisha Mauritius ba Zanzibar utashangaa jinsi kisiwa hicho kilicho karibu na pwani ya Afrika ya Kusini kilivyopiga hatua kubwa mbele kimaendeleo wakati Zanzibar ikiachwa nyuma kabisa ikiimba wimbo wake ‘Mapinduzi daima.’ Sijitungii haya.

Mwaka juzi (2014) mfanyakazi mwenzangu mmoja alikwenda Mauritius katika Mkutano wa kampuni ya Multichoice ilipotimiza miaka 20 na aliporudi nilimuuliza tofauti ya kisiwa hicho na Zanzibar. Akasema “Mauritius ni sayari nyingine, ni muujiza (miracle) na Wanzibar wanacheza tu na maendeleo.”

Hakika wanacheza. Hakuna mtu asiyependa maendeleo ya kweli na kutaka kuyabeza. Na maendeleo si kitu kinachoweza kufichika, maendeleo hujionyesha yenyewe. Lakini kwa Zanzibar hayaonekani hivyo ni sharti kila mara watawala wayapigie debe. Kila rais wa Zanzibar, akipata tu jukwaa lazima aorodheshe maendeleo ya Zanzibar tangu mapinduzi.

Katika sherehe za miaka 52 ya mapinduzi mapema mwaka huu, Rais Ali Mohamed Shein alifanya hivyo – na kuongeza kwamba maendeleo ya Zanzibar yasibezwe. Yasibezwe kwani wananchi hawayaoni?

Wanasiasa wengi na watu wengine wamekuwa wakisema kwamba kilichokosekana Zanzibar ni Tume ya Maridhiano, mithili ile ya Afrika ya Kusini ya Askofu Desmond Tutu ilyoundwa baada ya ukombozi wa nchi hiyo. Lengo lake lilikuwa ni kujaribu kutibu vidonda na makovu ya kihistoria ya misuguano ya ubaguzi wa rangi wakati wa utawala wa Makaburu.

Wanasema Zanzibar ilipaswa kuunda Tume kama hiyo na pengine siyo kwamba hili limechelewa. Wakati wa utawala wa Dr Salmin Amour “komandoo,” aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof Haroub Othman (marehemu) alitoa wazo hilo.

Alisema watu wote walio hai ambao walifanya vitendo kinyume na sheria na kukiuka haki za binadamu wakati na baada ya Mapinduzi wajitokeze mbele ya Tume, wajieleze, wakiri na wapate msamaha. Aidha alisema hata wale walionyang’anywa mali zao au kuuawa ndugu zao au wale ‘waliopotea” kwa mazingira ya utatanishi watafutiwe fidia angalau kidogo walipwe.

Profesa Othman aliongeza pia kwamba ingetafutwa jioni moja mjini Zanzibar kufanyike maulidi kubwa ya kuombea maridhiano ya kudumu. Hayo yote yalipuuzwa na Dk. Salmin, na kilichoendelea ni siasa za chuki, kibabe na kama tunavyoona hadi sasa, za kibaguzi.

Masuala kama haya yamekuwa yakiiathiri sana taswira ya Jamhuri ya Muungano mbele ya jumuiya ya kimataifa kwani imekuwa inalazimika kubeba tuhuma na lawama mbali mbali kutokana na vitendo vinavyotokea kule Zanzibar, hasa katika masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Na serikali ya Muungano imekuwa ikifanya hivyo kwa ‘utiifu’ mkubwa, tena kimya kimya bila yenyewe kulalamika. Ni vigumu kujua iwapo serikali ya Muungano imekuwa ikiikaripia serikali ya Zanzibar kwa mwenendo wa namna hii unaoiweka Tanzania katika mwanga hasi kimataifa. Nitatoa mifano.

Wakati wa utawala wa Salmin Amour, hasa katika kipindi cha baada ya ujio wa mfumo wa vyama vingi (1992-2000) kulikuwapo vitendo kadha vya ukiukwaji wa misingi ya haki za kibinadamu na sheria nyingine za nchi vilivyokuwa vinafanywa na watawala vilivyotokana na shughuli za kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani, hususan wakati wa kampeni za uchaguzi na wakati wa uchaguzi wenyewe.

Zaidi ya mara moja au mbili katika kipindi hicho ripoti za kila mwaka za Shirika la Haki za Binadamu duniani (Amnesty International) zilikuwa zinaituhumu Tanzania (kwa maana ya Serikali ya Muungano) kwa ukiukwaji huu.

Nazo baadhi ya nchi za magharibi zinazotupatia misaada ya kiuchumi, kama vile Norway, zimewahi kuilalamikia Tanzania kwa uminywaji wa haki kule Visiwani, hasa wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 na nchi hiyo ilidiriki hata kutishia kusimamisha misaada yake.

Lakini hakuna tukio kubwa lilioitia doa Tanzania kama lile la mauaji ya makumi wa wafuasi wa chama cha upinzani – Chama cha Wananchi – (CUF) wasiokuwa na silaha kule Pemba tarehe 27 Januari 2001 baada ya kupigwa risasi na polisi.

Tukio hilo lilitokana na mwenendo wa uchaguzi wa mwaka 2000 na matokeo yake. Wafuasi hao walikuwa wakiandamana kudai, pamoja na mambo mengine, tume huru ya uchaguzi.

Itakumbukwa tukio hilo lilisababisha, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, wakimbizi kutoka nchi hii kwenda nchi ya jirani ya Kenya. Isisahauliwe kwamba kwa miaka mingi Tanzania ndiyo ilikuwa mpokeaji mkubwa wa wakimbizi kutoka jirani waliokuwa wanayakimbia machafuko nchini mwao.

Baadhi ya wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kwa upinzani kushika dola huko Zanzibar kunategemea kwa upinzani kushika dola Bara. Na ndiyo maana katika uchaguzi uliopita CUF, kwa msukumo wa Katibu Mkuu Maalim Seif alikumbatia sana UKAWA kwamba ingeleta ushindi Bara (Chadema) na Visiwani (CUF).

Hoja hii ilikuwa na mashiko kidogo na nitatoa mfano. Yaliyokuwa makoloni ya Ureno – Angola, Msumbiji na Guinea Bissau – yalichelewa kujikomboa kutokona na utawala wa kiimla ulikokuwapo Ureno kwenyewe chini ya Antonio Salazar na baadaye Marcelo Caetano. Nchi hizo zilikuja kupata uhuru baada tu ya mabadiliko ya utawala huko Ureno mwaka 1974.