Home Makala Uingereza ni Tai aliyechoka kuwinda ndege wa Afrika

Uingereza ni Tai aliyechoka kuwinda ndege wa Afrika

407
0
SHARE

NA IGAMANYWA LAITON

SEHEMU ya kwanza ya makala haya tulieleza namna serikali ya Uingereza chini ya chama cha Labour na Waziri Mkuu Tony Blair ilivyobadili sera zake juu yabara la Afrika. Aidha, tulieleza namna nishati na madini zinavyowindwa na mataifa makubwa ya Ulaya. Endelee kusoma sehemu ya pili…

Mashirika ya kuuza silaha kama BAE yamewekeza kwa kiasi kikubwa katika bara la Afrika yakiuza na kusambaza silaha kubwa na ndogo barani Afrika, mashirika haya barani Afrika ni mboni na uti wa mgongo kwa uchumi wa Muingereza.

Afrika kusini ndiyo nchi inayoongoza Afrika kuwa Soko kubwa la bidhaa za Muingereza ikifuatiwa na Nigeria. Mwaka 2005 pekee bidhaa za Muingereza zilizouzwa Afrika Kusini zilifikia mauzo ya takribani paundi bilioni 3.2, huku uwekezaji ulifanywa na makampuni ya Muingereza nchini Afrika kusini ukifikia paundi bilioni 30 na zaidi.

Nchini Nigeria peke yake tuliona Uingereza iliuza bidhaa zinazokadiriwa kufikia kiasi cha paundi milioni 535 mwaka 2000 na zikipanda hadi kufikia paundi milioni 818 mwaka 2005.

Umoja wa Ulaya ulikuwa kikwazo kwa Muingereza kufanya atakavyo barani Afrika (kama vile Tai aonavyo kuwinda na ndege wengine kuwa kikwazo) kwa nini?

Umoja wa Ulaya ilikuwa mfadhili mkubwa wa miradi mbalimbali barani Afrika. Uhusiano wake na Afrika uliimarika zaidi na kurasimishwa na Mkataba wa Cotonou uliofanyika mwaka 2000, baada ya ule wa Lome uliokuwa kati ya Uingereza na mataifa ya Afrika, Karibeani na Pasifiki.

Tofauti na Lome mkutano na makubaliano ya Cotonou yalihusu bara la Afrika tu, ripoti zinaonesha kuwa Uingereza ilitoa takribani asilimia 25 hadi 31 ya misaada kupitia EU, lakini uhusiano wa Umoja wa Ulaya na bara la Afrika ulikuwa na matatizo ambayo yalianzia katika maamuzi ukichangiwa na sera za umoja huo juu ya Afrika.

Tukumbuke uUmoja wa Ulaya una idadi ya wanachama 27 hii ina maana jambo lolote lile kuelekea aina, kiasi na wapi msaada uende ilitegemea kwanza mawazo na kukubaliana kwa wanachama wote 27.

Hii ilichukuwa muda mrefu na mara nyingi kulikuwa na kutoelewana katika maamuzi. Udhaifu wa Umoja wa Ulaya uliathiri mahusiano yake na bara la Afrika hivyo kupunguza lengo mahususi la misaada. Kutoelewana pia kulichangiwa na uhusiano wa kinafiki uliokuwako kati ya Ufaransa na Uingereza mataifa ya kibepari yote yakisaka namna kushindana na kuwa na nguvu ya kisiasa na kiuchumi zaidi ya mwingine.

Ikumbukwe kuwa Ufaransa na Uingereza zimekuwa katika ushindani karne na karne, kila moja ikitaka kumpiku mwenzake. Mfaransa na Muingereza kuiva chungu kimoja ni hadithi ya Tony Blair na Jacques Chirac waliposhindwa kuiva katika mtizamo juu ya vita ya Iraki, Tony akiunga na Jacques akipinga.

Kuundwa kwa DFID (Taasisi ya Muingereza inayohusiana na Misaada) kulikuwa njia sahihi aliyoiona Muingereza kuatamia maslahi na malengo ya kile akitoacho kama misaada, kuliko kutumia mlango wa Umoja wa Ulaya ambamo hakuwa na uwezo wa kuishikia rimoti na kuongoza.

Muingereza aliona DFID kuwa njia sahihi zaidi kwa maslhai yake barani Afrika, kama vila mvuvi aliyeacha kutumia ndoano ya kijiji na kuamua kutumia ndoano yake binafsi kuamua kiasi na aina ya chambo atakayotumia kuvua samaki kulingana na aina ya samaki amtakaye.

Uingereza akaigeukia DFID kama ndoano yake kuvua samaki barani Afrika. Kuanzia mwaka 1997, Taasisi ya DFID ilikuja kuwa ‘kiendesha sera mjenzi’ wa Muingereza barani Afrika.

Misaada ya Muingereza iliyokuwa ikipitia DFID ikiongezeka kutoka Pauni milioni 300 kwa msimu wa 1997 na 1998 hadi pauni bilioni 1.25 mwaka 2006na 2007.

Asiliamia 55 ya bajeti ya DFID ilitengwa maalumu kwa ajili ya Afrika, baadhi ya nchi zilizokuwa katika orodha ya kupokea misaada hiyo zilikuwa ni pamoja na Ghana, Nigeria, Sierra Leone, Sudan, Ethiopia, DR Congo, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania, Zambia, Malawi, Mozambique, Zimbabwe, Lesotho na Afrika kusini.

KUIBUKA KWA CHINA BARANI AFRIKA

China imekuwa ikitumia misaada barani Afrika kama chambo cha kuatamia rasilimali muhimu za madini, mafuta na masoko. China imejifunga mkanda na kuwekeza zaidi ya Paundi bilioni 7 katika sekta ya miundombinu barani Afrika pekee.

Novemba mwaka 2006, viongozi wa Afrika takribani 48 walihudhuria katika kile walichokiita Kongamano la kibiashara kati ya China na Afrika lilofanywa Beijing ambapo serikali iliahidi kuzidisha mara mbili ya misaada yake na kupanua soko la bidhaa za Afrika nchini China.

Kwa mujibu wa kitabu cha Congo Masquerade kilichoandikwa na mwandishi Theodore Trejorn, kwenye ukurasa wa 55 wa kitabu hicho anasema, “China imekuwa muuzaji mzuri wa silaha nchini Sudan  na kwingine kwa miaka,

“China pia imewekeza katika sekta ya Mafuta na Gesi barani Afrika. Kwa mfano China imewekeza nchini DR Congo katika miradi ya kujenga barabara yenye thamani dola bilioni 3 kwa mabadilishano na madini, kwa kujenga viwanja vya ndege, kujenga vyuo, hospitali na zahanati na shule china imepata dili kwa kupewa ruhusa ya kuchimba bure tani milioni 8 za madini ya Copper,  tani 200,000 za madini ya Cobelt na tani 372 za madini ya dhahabu.”

Faida anazovuna China barani Afrika zimeyashitua mataifa ya Ulaya na Amerika, kila moja likijikusanya kutumia kila aina ya mbinu kuhakikisha linakuwa na uwezo pekee wa kuwa na sauti na nguvu barani Afrika iwe kwa kutumia misaada au namna nyingine.

HITIMISHO

Kuzorota kwa Umoja wa Ulaya na mkutano wa Berlini uliofanyika karne ya 19 ni kama kichwa cha sarafu chenye sura mbili, tofauti ikiwa katika mkutano huo mataifa ya Ulaya yaliungana na kukaa pamoja ili kuwinda rasilimali za Afrika, wakati katika kuzorota na kubomoka kwa Umoja wa Ulaya mataifa yanazozana ili kila mmoja awe huru kuatamia rasilimali za Afrika.

Kutoka siasa za Tony Blair, umuhimu wa Afrika katika uchumi wa Uingereza,kutokalika chungu kimoja kwa mabepari katika boti moja ya uvuvi, kuibuka kwa viwanda barani Asia kukichagizwa na kiu ya Uchina kusaka masilahi na nguvu barani Afrika kunaibua sababu zilizofichika zilizochagiza kudhoofika kwa umoja wa ulaya.

Kama vile Tai wasivyoweza kuwinda pamoja na ndege wengine ndivyo mataifa ya kibepari yalivyoamua kuparangana katika boti ya Umoja wa Afrika, sera ya ubepari inataka ushindani na unafiki, kila mmoja akitanguliza masilahi ya nchi yake mbele kuliko ya mataifa mengine, kuwepo katika meza moja ya chakula kulikuwa kikwazo na manung`uniko kwa Muingereza.

Sasa Muingereza amechoka kukaidi kanuni ya Tai (Ubepari) na kuamua kuwinda peke yake japo umri ni kama umemtupa mkono kule kutaka kuamua kujitoa Umoja wa Ulaya hata kama kutasababisha maumivu kiasi gani Uingereza imeamua kuchukua zoezi la kujitoa mabawa na kunoa kucha na mdomo wake katika jiwe ili iwe rahisi kuwinda rasilimali kwa ufanisi na kwa kujiachia barani Afrika huku akiachana na Kunguru kama Ugiriki na ndege wengine kama vile Ufaransa,vyovyote itakavyokuwa Uingereza imeamua kuwa Tai atakayewinda peke yake kwa lolote lile.