Home Makala Serikali ndiye mchawi wa maisha ya wafanyakazi

Serikali ndiye mchawi wa maisha ya wafanyakazi

764
0
SHARE

NA JULIUS MTATIRO

NATAMBUA kuwa mjadala wa “fao la kujitoa” umepamba moto na ni jambo lisilokwepeka kujadilika kwa sababu linagusa maslahi ya ndani ya wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi hapa nchini.

Kila nikiwaza nia ya serikali yetu juu ya fao hili najiuliza maswali muhimu, kwa nini serikali inajaribu kufanya makosa yaleyale kwa mambo yaleyale ambayo ilijikwaa hapo nyuma? Lengo la serikali lina mantiki na nia ipi? Kabla serikali haijajaribu jambo hili ilitafakari madhara yake? Nani anaishauri serikali kuhusu masuala nyeti ya wafanyakazi na katika hili ameishauri nini serikali? Serikali imejifunza katika nchi nyingine zilizofanikiwa katika sekta ya ajira?

Kihistoria, mjadala wa fao la kujitoa (withdrawal benefit)  ulianza mwaka 2012 baada ya Sheria ya Udhibiti wa Mifuko ya Kijamii kupitishwa bungeni mwezi Aprili mwaka 2012 na kisha kusainiwa na Rais Kikwete. Sheria hiyo ndiyo ilianzisha mgogoro kwani ililiondoa (remove) fao hilo.

Kabla ya kuondolewa fao hilo lilikuwepo kisheria. Baada ya maumivu makali waliyopitia wafanyakazi, baadhi ya makampuni na wafanyakazi kujiendesha katika wakati mgumu n.k. suala hili liliibuliwa tena na mbunge wa jimbo la Kisarawe (CCM), Selemani Jafo ambaye alipeleka hoja binafsi bungeni ikajadiliwa na kupelekea serikali kuunda kamati maalum iliyozunguka kuchukua maoni ya wadau.

Baada ya kamati kumaliza kazi yake na kuwasilisha ripoti serikalini, serikali iligundua makosa yake makubwa katika sheria husika na hivyo waziri mwenye dhamana ya Kazi na Ajira wakati huo akatoa kauli bungeni kuwa serikali itaendelea kuhimiza uwepo wa fao hilo na kisha baadaye itapeleka muswada bungeni ili kurekebisha sheria hiyo na kuondoa kipengele cha kuondoa fao hilo. Baada ya ahadi hiyo ya serikali, Mifuko ya hifadhi ya Jamii iliendelea kuwapa fao hilo wafanyakazi na hali ikawa shwari.

Mgogoro mpya juu ya fao hili uliibuka tena tarehe 23 Mei 2015 ambapo mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF ulitangaza kusitisha utoaji wa fao husika (kule kule kulikolalamikiwa na kuwaumiza wafanyakazi miaka minne iliyopita).

PPF walitoa utetezi kuwa, hakuna sheria inayowalazimisha au kuwataka kuzingatia fao hilo. Wadau walishtushwa na tangazo la PPF na kuhaha kuupata ukweli kutoka PPF, SSRA, mawaziri wenye dhamana na SSRA na Mifuko ya hifadhi za jamii n.k. Huko kote waligonga mwamba, hakukuwa na majibu ya kueleweka.

Baadaye ndipo inatambulika kuwa serikali imo mbioni, kupitia katika muswada wa marakebisho ya sheria kurasimisha uondolewaji wa fao husika.

Ndiyo kusema kuwa, tangazo la PPF la kutozingatia tena fao hili muhimu ilikuwa ni “janja ya nyani”, hali halisi itakuwa kwamba, serikali ndiyo imepanga na ndiyo inalipatia nguvu, PPF imetumika kulitangaza tu ili serikali ianze kulitekeleza bila kelele sana.

Ikiwa utekelezaji wa kauli ya PPF ambao unaonekana kusukumwa na serikali utaanza, mtu anayeacha kazi akiwa na miaka 25 atapaswa kusubiri miaka 35 zaidi ili afikishe miaka 60 ndipo apate fedha zake.

Na yule anayeacha kazi akiwa na miaka 30 atasubiri miaka 30 mingine ndipo apate fedha zake kutoka kwenye mfuko wa hifadhi za jamii. Huu ni uchuro, uchuro wa karne! Ndiyo kusema, mtu akiacha kazi na miaka 30, 25, 40, 50 n.k kwa sababu yoyote ile binafsi na muhimu, hatakuwa na namna ya kuanza maisha yake huko aendako na itampasa asubiri hadi akiwa na miaka 60, kwamba maisha ya kila siku, uchumi mgumu n.k. vitakuwa vinamsubiri tu hadi afikishe miaka 60!

Mimi nimewahi kuishi na kufanya kazi zisizo rasmi katika mgodi wa Barrick Kakola. Nimejionea mwenyewe namna wafanyakazi wa migodini wanavyoacha kazi, mtu anafanya kazi miaka mitatu anaacha, anakwenda kwingine au anaondoka kabisa mgodini.

Wengine wanafanya kazi ardhini (underground) wanapata madhara makubwa ya kiafya na wanaacha kazi ili wakapambane kulinda afya zao. Najiuliza, anayepuuza fao la kujitoa anataka watu hawa wote wakajifie mbali baada ya kuacha kazi? Mtu huyo analo lengo gani?

Nchi hii kwa bahati nzuri inao viongozi, walioko madarakani na waliostaafu, waliokuwa na dhamana kubwa sana. Ni kwa nini viongozi hawa wao wana uhakika (assurance) ya maisha yao na familia zao wanapokuwa kazini na wanapostaafu? Na tena wanapostaafu wanaendelea kulipwa asilimia za juu za mishahara inayopokelewa na mtu aliyeko kwenye wadhifa huo kwa muda uliopo.

Haya yote yanafanyika kwanini? Kwa sababu ni lazima kulinda maisha ya watu waliolitumikia taifa, na ulinzi huo hauwezi kusubiri miaka 10 au 20 mbele, ulinzi huo lazima uzingatiwe mara tu (immediately after) baada ya mhusika kuacha kazi ili awe sawa na yule aliyestaafu.

Nimejiuliza kuwa, huenda serikali inachanganya dhana ya kuacha kazi ukiwa na miaka 30 na kustaafu kazi ukiwa na miaka 60. Kwa wanaofahamu Kiswahili wanajua kuwa kustaafu kazi na kuacha kazi kwa hiyari ni kitendo chenye lengo moja tu, kupumzika majukumu uliyokuwa unayafanya muda mrefu uliopita.

Hakika, mtu aliyeacha kazi serikalini, yeye mwenyewe, au kwenye sekta binafsi na akaamua kujikita kwenye biashara na asiajiriwe tena huwezi kumtofautisha hata kidogo na yule aliyestaafu.

Wote wamefanya kitendo kimoja, wameacha kazi, wanaangalia maisha mengine na wanatarajia fedha hizo ndizo ziwasaidie katika kupambana na maisha, unapoondoa fao la kujitoa ili mtu afikishe miaka 60 unamchuria mtu huyo “kifo cha mapema” kutokana na kushindwa kuhimili mikiki mikiki ya maisha.

Na tusisahau kuwa, vijana wengi sana hutumia fao la kujitoa kwa ajili ya kukusanya pesa za kujiongezea elimu (kujisomesha). Katika nchi nyingine, kila mfanyakazi anayetaka kujiongezea elimu hutumia pesa za mwajiri wake kwa ajili hiyo na hakuna urasimu katika kupata fedha hizo, Hapa Tanzania ni wafanyakazi wachache sana ndiyo hupata ruhusa na fedha za kujiongezea elimu na maarifa.

Wengi wa wafanyakazi hunyimwa ruhusa na fedha kwa ajili hiyo na wale wenye kiu kubwa hulazimika kuacha kazi ili wajipange. Wanapoacha kazi ni fedha za fao hilo pia huwa tegemeo lao muhimu. Leo zinapoondolewa kwa nguvu, tunategemea nini kitatokea?

Ni wazi kuwa tabia ya serikali yetu ya kujifungia na kufanya maamuzi kimya kimya bila kuwashirikisha wadau ndiyo inatugharimu.

Katika jambo hili kuna utatu unaobaguana na kutoshirikishana, serikali inao wajibu wa kulishirikisha Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) katika hatua na mipango yote inayolenga kuinua au kukwaza maisha na maslahi ya wafanyakazi.

Lakini pia serikali inapaswa itende mipango yake kwa kukiweka karibu Chama cha Waajiri Tanzania (ATE). TUCTA na ATE ni wadau wanaofungamana na serikali.

Ni masikitiko makubwa kuwa, niliposoma taarifa ya tamko la pamoja lililotolewa na Vyama vya wafanyakazi na asasi za kiraia nimegundua kuwa mchakato wa serikali katika kuliendea suala hili ulikuwa siri kuu, wadau muhimu ambao ni wafanyakazi (ndiyo hasa wamiliki wa mifuko ya jamii) wameshtukizwa serikali inaliendea jambo muhimu kama hili bila kuchukua maoni na ushauri wao.

Sote tunajua kuwa serikali hivi sasa inahaha usiku na mchana kusaka pesa kokote kule ziliko ili iziwekeze katika shughuli zake, lakini kuwanyonya wafanyakazi kikatili namna hii ni jambo lisilokubalika.

Tunafahamu kuwa mifuko ya hifadhi za kijamii inapokuwa na fedha nyingi na zinazokaa muda mrefu, serikali hutumia mwanya huo kuzikopa na kuzirudisha kwa mbinde. Ndiyo maana mwaka 2015, Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF liliripotiwa kukumbwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na serikali kushindwa kulilipa madeni yake makubwa.

Kwa hiyo, kwa wenye akili wanatambua kuwa hata hatua ya sasa ya serikali ya kutaka kurasimisha uondolewaji wa fao la kujitoa ni njia ya ujanja wa juu wa kulazimisha fedha za wafanyakazi walioacha kazi kwenye taasisi binafsi za umma ziendelee kukaa huko kwenye mifuko kwa muongo mmoja, miwili au mitatu na katika kipindi hicho fedha hizo zitumike kusimamia miradi ya serikali kwa kukopwa.

Ujanja huu wa kusikitisha sana unanifanya nihitimishe kuwa, anayechawia maisha ya wafanyakazi wa Tanzania ni serikali yenyewe. Ni muhimu wadau wote wa maendeleo nchini walikatae jambo hili, sote tuungane na kusema hapana kwa kuliondoa fao la kujitoa maana tutaua maisha ya nguvukazi ya nchi yetu, kwa mikono yetu wenyewe.