Home Habari Ukosefu wa chanjo waibua maswali

Ukosefu wa chanjo waibua maswali

494
0
SHARE

NA WAANDISHI WETU

KUWAPO kwa uhaba wa chanjo mbalimbali nchini kumeibua maswali ya namna ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko endapo yatatokea.

Wiki iliyopita Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alilitangazia Bunge kuhusu ukosefu na uhaba wa chanjo mbalimbali nchini.

Ummy alilitangazia Bunge kuwa nchi inakabiliwa na ukosefu wa chanjo za Ndui, Pepo Punda, Homa ya Manjano, Kuhara na Homa ya Ini na uhaba wa chanjo ya Kichaa cha Mbwa.

Baada ya taarifa hiyo kutolewa na kufuatia kuwepo malalamiko kadhaa, imebainika kuwa taifa linaweza kuwa hatarini kutokana na uchelewaji wa baadhi ya chanjo hizo na kama yatatokea magonjwa ya mlipuko, taifa linaweza kuingia katika hatari ya kupoteza mamia ya watoto na akina mama wajawazito ambao wengi ndio walengwa wa chanjo hizo.

RAI lilizungumza na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto, Catherine Mung’ong’o ambaye alithibitisha uwepo wa ukosefu na uhaba wa chanjo hizo na kisha kufafanua kitaaluma madhara ya kutokuwepo kwa chanjo hizo sasa na siku zijazo.

“Ni kweli kuna uhaba wa chanjo ambao utasababisha wananchi wetu kuwa katika hatari kubwa pale patakapoibuka magonjwa ya milipuko,” alisema Dk. Mung’ong’o.

Dk. Isack Maro, alisema athari za ukosefu wa chanjo zimedhihirika hivi karibuni mara baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa Surua maeneo ya Mbagala jijini Dar es Salaam.

Ugonjwa huo unadaiwa kuwaathiri watoto wengi waliokuwa wamekosa chanjo ya ugonjwa huo.

Alisema kukosekana kwa chanjo kunailazmisha serikali kuingia gharama kubwa ya kuwatibu watoto waliokosa chanjo hasa magonjwa ya milipuko yanapoibuka.

MAGONJWA YANAYOHITAJI CHANJO

Homa ya ini

Madhara ambayo gazeti hili imeyabaini kutokana na ukosefu wa chanjo ya homa ya ini ni pamoja na kansa ya ini au hata kusababisha ini kushindwa kufanya kazi.

Kuhara

Kutokana na ongezeko la vifo vya watoto sehemu mbalimbali duniani Shirika la Afya Duniani (WHO), limetoa chanjo dhidi ya kuhara ambayo hata hivyo bado haipo nchini hivyo kuhatarisha maisha ya watoto wengi.
Madhara ya kuhara ambayo yanaweza kusababisha watoto kuhara damu inaweza kusababisha kifo kutokana na kupoteza maji mengi mwilini.

Pepopunda

Kwa mujibu wa wataalamu hao madhara ya kukosekana kwa chanjo ya Pepopunda, vifo na ulemavu usiotarajiwa hususani kwa wajawazito, watoto wachanga na majeruhi wa ajali.
Homa ya manjano

Watalaamu wanaeleza kuwa Homa ya manjano ni ugonjwa unaowashika watoto wachanga baada ya masaa machache kuzaliwa. Manjano kawaida huonyesha rangi ya manjano kwenye macho, paji la uso, nyayo za miguu, kifuani na tumboni, ukimkagua mtoto vizuri hasa kwenye mwanga wa jua utaona njano hiyo kwa urahisi. Homa ya manjano huwaandama watoto na watu wazima pia.

Wanaeleza kuwa madhara ya ukosefu wa chanjo ya homa ya manjano ni pamoja na kuongezeka kwa kemikali ya ‘bilirubin’ ambayo ikiongezeka sana kwenye damu huathiri ubongo. Aidha ukosefu wa chanjo hiyo husababisha matatizo ya kutosikia, kutoona, kushindwa kuongea na kutembea vizuri; ulemavu wa kudumu na hata kifo.

Kichaa cha mbwa

Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa umeonekana kuwa hatari zaidi kwa maisha ya binadamu na mifugo kutokana na baadhi ya watu waliojeruhiwa kwa kung’atwa na mbwa kupoteza maisha hasa kwa kuchelewa kufika katika hospitali kwa matibabu ya haraka.

Rai lilielezwa kuwa madhara ya ukosefu wa chanjo ya kichaa cha mbwa ni kifo kutokana na sumu ya ugonjwa hupo kuenea kwa haraka mwilini.

Kutokana na tatizo la ukosefu wa baadhi ya chanjo nchini Serikali imeagiza chanjo kutoka shirika la kimataifa la kuhudumia watoto UNICEF, huku hazina ikiwa imeshatoa zaidi ya shiling 6.4 bilioni kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.