Home Makala Demokrasia na vyama vya siasa Tanzania

Demokrasia na vyama vya siasa Tanzania

793
0
SHARE

cc9NA WAANDISHI WETU

TANZANIA ina vyama vya siasa 21 vyenye usajili wa kudumu huku kikiwepo kimoja ambacho kina usajili wa muda. Vyama hivi vimepatikana baada ya mabadiliko madogo ya Katiba yaliyotoa fursa ya kurejesha mfumo wa vyama vingi katika nchi yetu mwaka 1992.

Kufuatia mabadiliko haya, Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilichokuwa cha kwanza kupata usajili wa kudumu mwaka 1992, huku kikifuatiwa na vyama vipya vya CUF, CHADEMA,UMD, NCCR, NLD, UPDP, NRA, TADEA NA TLP vilivyopata usajili wa kudumu mwaka 1993.

Vyama vingine na usajili wao kwenye mabano ni:  UDP (1994), Demokrasia Makini (2001), CHAUSTA (2001), DP (2002), APPT(2003), Jahazi Asilia (2004), SAU (2005), AFP (2009), CCK (2012), ADC (2012), CHAUMMA (2013) na ACT (2014). RNP ni chama pekee kilichopo katika orodha ya vyama visivyo na usajili wa kudumu.

Mwandishi Henry Mwangonde Aprili 23, 2014 katika gazeti la The Citizen, alimnukuu Dk. Benson Banna Katika makala yake ya “Vyama vingi vimeisaidia Tanzania” na kuandika; “vyama vya siasa nchini Tanzania havina nguvu katika kutanua mianya ya demokrasia kutokana na kukosa sera nzuri, mikakati pamoja na tabia ya viongozi wa vyama hivi kutokutumia mtaji wa wanachama wao kuviendeleza badala yake kuwatumia kwa masilahi binafsi.” Kwa mujibu wa Dk. Bana katika makala hiyo; vyama hivi vimeshindwa kutanua miaya ya demokrasia kwa kuwa havina demokrasia ndani yake.

Dai la Dk. Bana limekuwa likitumika na wachambuzi wa siasa hapa nchini hasa pale wanapozungumzia suala la kutokuwepo mabadiliko ya viongozi katika vyama vya siasa. Dai hili mara nyingi limejikita katika kutoangalia umri wa vyama hivi lakini pia uimara na intelejensia katika vyama hivyo.

Mfano tangu kuanzishwa kwake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kwa sasa ni chama kikuu cha upinzani Tanzania Bara, kimekuwa chini ya wenyeviti watatu. Katika kipindi hicho hicho yaani kuanzia 1992, CCM nayo imekuwa na Wenyeviti watatu hadi sasa, huku NCCR Mageuzi ikiwa na wenyeviti watatu tangu kuanzishwa kwake. Inawezekana hoja kubwa ikawa namna wanavyopatikana viongozi wa vyama hivi kwa maana ya mfumo wa uchaguzi, lakini dai hili pia linagusa hata CCM ambacho ni kikongwe kabisa. CCM humpa Uenyekiti kwa kigezo cha kuwa Rais wa nchi.

Ukitazama pia, vyama vingi vya siasa vilisajiliwa miaka ya 1990 na hii inaelezwa kuwa ilitokana na serikali kutoa ruzuku kwa vyama vya siasa, ruzuku ambayo imekuwa ikiwekewa masharti mengine kama, kuwa na idadi ya kura katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Hitajiko hili, limefanya vyama vingi kubakia katika orodha ya vyama, lakini uhalisia wake katika uwanja wa demokrasia unabaki na maswali mengi. Moja ya maswali hayo ni kutokuwa na makao maalumu. Kutofanya chaguzi pamoja na kubakia na waanzilishi wa vyama hivyo hata kutumia makazi yao kuwa ofisi za vyama vyao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa yeye anaelezea kuwa,  vyama vya siasa nchini vinapiga hatua licha ya kukabiliwa na mazingira magumu ya kutekeleza majukumu yake.

Kwa mujibu wa Dk. Kahangwa, mazingira hayo magumu yalianzia wakati wa kuanzishwa vyama vingi hapa nchini na ulitokana na nafasi ya chama tawala kushiriki katika mchakato mzima wa kutengeneza sheria ya vyama vingi hapa nchini. Sababu nyingine anayoizungumzia ni kutokuwepo kwa Katiba inayotoa mfumo sawa kwa vyama vya siasa, hasa suala la rasilimali, ilhali chama tawala kikiwa na rasilimali nyingi ambazo kimezirithi wakati nchi ikiwa katika mfumo wa chama kimoja.

Hashimu Rungwe ni Mwenyekiti wa CHAUMMA, yeye anafafanua kuwa, tangu mfumo wa vyana vingi urejee hapa nchini, baadhi ya vyama vinakuwa kwa mwendo wa Kinyonga na hali hii inasababishwa na kutokuwepo mazingira sawa katika kufanya siasa. Kwa mujibu wake, bado chama tawala kwa namna moja ama nyingine, kinaviminya vyama vingine kwa lengo la kuhitaji kubakia madarakani.

“Ila niseme kuwa demokrasia imekua kwa sababu wabunge wameongezeka, halmashauri zimechukuliwa na upinzani ila tungeweza kukua zaidi ya hapa iwapo viongozi wetu wangetoa nafasi ya ushindani wa kweli,” anaelezea Rungwe.

Kwa upande wake Profesa Mwesiga Baregu, Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine na mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa hapa nchini, yeye anafafanua kuwa, vyama vya siasa vinakabiliwa na tatizo la mfumo ambao vimeurithi.  “Jaji Nyalali alisema mfumo wa vyama vingi hauwezi kustawi chini ya Katiba ambayo ni ya chama kimoja. Kwa hiyo suala zima la Katiba ambalo linaweza kujenga demokrasia na vyama kustawi ni dhahiri Tanzania bado tuna nakisi ya Katiba ambayo  misingi yake ni ya kujenga demokrasia.

Kwa upande wake, Dk. Azaveli Lwaitama anasema hali ya ukuaji wa demokrasia katika vyama vyetu inatia moyo japokuwa viongozi waliopo madarakani wanatafuta njia mbalimbali za kuzuia matokeo ya demokrasia.

“Ili kutimiza matakwa ya demokrasia, busara inatakiwa zaidi badala ya kutumia mabavu kuhalalisha mifumo ya utawala katika kipindi cha uchaguzi ambayo haitupatii picha halali ya demokrasia. Kwa mfano tukiangalia kilichotokea Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka jana kwamba aliyekuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi akafuta matokeo ya uchaguzi ni jambo ambalo halikutakiwa kwa sababu Tume kazi yake ni kusimamia uchaguzi,” anasema Dk. Lwaitama.

Kwa mujibu wa wachambuzi mbalimbali wa siasa hapa nchini, vyama vya siasa kwa namna moja ama nyingine vimekuwa vikikabiliwa na migogoro ambayo chanzo chake kinaweza kuwa ni ugumu katika kusimamia rasilimali fedha na pia namna ya kuwa na fedha za kutosha ili kuviendesha. Kutokana na hali hiyo na hasa siku za hivi karibuni, imeonekana wazi kuwa viongozi wa vyama hivi huenda wamo katika vyama kwa kazi nyingine na sio kukuza demokrasia au itikadi wanayoiamini.

Mgogoro katika Chadema ulisababisha kuzaliwa kwa chama cha SAU, na ule wa NCCR-mageuzi ulisaidia kukua kwa chama cha TLP. Pia mgogoro ndani ya CUF, umezaa vyama kama ADC na CHAUSTA. Hata hivyo vyama ambavyo vimeanzishwa kutokana na migogoro vingi vimeshindwa kutamba zaidi ya ACT-ambacho kilimonyoka kutoka CHADEMA na sasa kinaongoza Halmshauri moja na kina kiti kimoja cha ubunge.

Lipo dai la kutaka vyama vya siasa kuungana ili kuweza kuongeza mtaji wa kuchagulika. Dai hili linakabiliwa na ugumu unaotoka na uwezo wa kiintelejensia ambao chama tawala kinao, na pia udhaifu wa kutoweza kudhibiti masuala ya ndani ya vyama vya siasa.

Kwa upande wa wananchi, bado wanayo imani kuhusu uwepo wa vyama vya siasa lakini nia yao ni kuona kunakuwa na vyama vyenye nguvu na vinavyoweza kuwa na agenda mbadala ya kusukuma maendeleo ya nchi.