Home Makala Kimataifa WAPIGAKURA UCHAGUZI MAREKANI: Wasiofanya maamuzi hadi sasa ndiyo watampitisha mshindi

WAPIGAKURA UCHAGUZI MAREKANI: Wasiofanya maamuzi hadi sasa ndiyo watampitisha mshindi

815
0
SHARE

Trump__ClintonNA HILAL K SUED

Jumatatu iliyopita wagombea wawili wa urais wa Marekani walishiriki katika mdahalo wao wa kwanza wa kampeni, mdahalo ambao ulitarajiwa kuangaliwa na wananchi wengi zaidi katika historia ya midahalo ya kampeni nchini humo.

Mmoja wao ni mke wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, na aliyewahi kuwa Seneta na Waziri wa Nchi za Nje, Bi Hillary Clinton. Mwingine, Donald Trump, hajawahi kuchaguliwa kwa kura katika nyadhifa yoyote, na hadi mwaka jana alikuwa ni mtu maarufu tu nchini humo kutokana na utajiri wake mkubwa.

Lakini yote haya si jambo muhimu sana kuhusu uchaguzi wa Urais wa Marekani. Kitu kinachoshangaza ni kwamba kura za maoni sasa hivi zinaonyesha kwamba wagombea hawa wawili wamejifunga kwa ukaribu sana kuliko wananchi wengi wanavyofikiria katika hatua hii ya kampeni.

Baada ya Mkutano Mkuu wa chama cha Democratic mwisho mwa mwezi Julai, masoko ya  kamari yalimpa Donald Trump asilimia 20 tu ya nafasi ya kuwa Rais wa 45 wa Marekani. Mashambulizi yake dhidi ya wazaazi wa askari ambaye aliuawa Iraq ndicho kilichomfanya avuke mstari wa kudidimia.

 Na wiki chache zilizofuata uzito wa kauli zake hazikulainishwa kwa kiasi cha kuwa za kawaida. Alimsifia Putin ambaye alitoa kauli ya kumsifia yeye, au kusema kwamba Hillary Clinton alikuwa amejiondoa kwenye kampeni baada ya lile tukio la kuishiwa nguvu katika hafla moja ya kuadhimisha miaka 15 ya ulipuaji mabomu jijini New York, au kwamba walinzi wa huyo mpinzani wake wanyang’anywe silaha. Wananchi walionekana kuzipuuza kauli kama hizi.

Kwa upande wake, Clinton alilazimika kutoweka kwa kipindi kifupi baada ya tukio la afya yake. Lakini ulipuaji wa mabomu huko New York na New Jersey ulionekana kumsaidia mama huyo ambaye alitoa wito wa kuweka ulinzi zaidi wa mipaka na kuwachunguza zaidi Waisilamu nchini.

Ingawa kura za maoni za ngazi ya kitaifa zimekuwa zikikaribiana sana jinsi siku za kampeni zinavyokwenda, kitu kinachojitokeza dhahiri ni jinsi kura za moni ki-majimbo zinavyozidi kukaribiana kwa karibu sana, kitu ambacho kimepelekea watabiri kukarabati tabiri zao.

Bi Clinton bado ni mgombea anayekubalika zaidi, lakini Trump bado hajafikisha zaidi ya asilimia 40 katika kura za maoni kitaifa. Lakini hii si kwa sababu ya upenzi wa halisi kwa mgombea wa chama cha Democratic, ambaye amekiri yeye mwenyewe kwamba siyo mpiganaji mzuri katika kampeni na kukabiliana na mtiririko wa maswali kuhusu uaminifu wake.

Sehemu kubwa ya wapigakura hawavutiwi na wagombea wote wawili, na hili linakuja kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi wa urais wa mwaka 1992, pale ambapo mgombea wa ‘chama cha tatu’ Ross Perot aliweza kunyakua asilimia 19 za kura zote.

Safari hii si umaarufu wa ‘chama cha tatu’ ambao ujio wake unatishia kunyonya makumi ya mamilioni ya wapigakura kutoka kwa wagombea wote hawa wawili, bali ni ari kubwa uliyoko ya kutovutiwa na wagaombea hawa kiasi cha kukataa kushiriki hata katika kupiga kura za maoni.

Wananchi wengi wa Marekani wangependa kuanza upya na wagombea wawili wengine wapya, kitu ambacho hakipo. Baada ya kampeni hizi ambazo ni chafu zaidi kuwahi kutokea kwa kipindi cha robo karne, takriban asilimia 20 ya wapigakura wanasema bado hawajaamua watampigia kura mgombea yupi – yule wa Republican au wa Democrat.

Maamuzi ya hawa katika wiki sita zijazo ndiyo yataweza kutoa mwanga wa matokeo wa uchaguzi wa mwaka huu. Na kwa wale – wakiwamo wafuasi wakereketwa wa chama cha Republican – ambao wanashangazwa na kupanda chati kwa Trump katika kura za maoni za hivi karibuni, mdahalo wa kwanza ulitarajiwa kumpa nafasi nzuri kwa Bi Clinton kuwanasa wapigakura hawa ambao bado hawajawa na maamuzi.

Lakini hiyo inaweza ikawa ni ndoto tu. Katika muda wote wa kampeni wagombea hawa wawili wamekuwa wanahukumiwa kwa vipimo tofauti. Lakini kutokana na uzoefu wake katika siasa, Bi Clinton anatarajiwa kufanya vyema katika midahalo.

Naye Donald Trump anaweza kushangaza wengi iwapo hatawatukana watu wengi au kupandwa na hasira au jazba. Kumhoji Trump ni sawasa na kujaribu kumkamata samaki kwa mikono yako miwili kutoka kwenye mto unaokwenda kasi. Na kumpinga katika mdahalo ni vigumu zaidi.

Aidha, wakati ambapo Wamarekani wengi wanachoshwa na wanasiasa, Bi Clinton ni nembo halisi katika vitu vyote ambavyo hawavipendi katika siasa. Na hata kama Trump amekuwa katika kinyang’anyiro kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na kupokea jumla ya Dola 166 million kama michango, na ameajiri mwendesha kura za maoni kama mkuu wa kampeni zake, bado mgombea huyo ameshindwa kabisa kutazamwa na wananchi wa Marekani kama ni mwanasiasa.

Na pengine katika midahalo ijayo, wapigakura watabadili mitazamo yao kuhusu wagombea hawa na kuangalia zaidi sera zao.

Na huenda ni kutokana na shaka zao kuhusu wagombea wawili hawa, ndiyo maana wote wanaonekana kama vile hawafai. Lakini si hivyo. Wengi wanasema uchaguzi wa mwaka huu siyo unatafuta nani aingie Ikulu ya Marekani jijini Washington, bali ni namna Marekani yenyewe inavyotakiwa iwe.

Na wadadisi wa mambo wanasema kwa Wamarekani ambao hupigia kura ‘chama cha tatu’ ambao wanaoamua kutokwenda vituoni kupiga kura, hufikiri siasa ni kitu ambacho hutokea kwingine, mbali sana na maisha yao ya kila siku, basi safari hii wajitayarishe kupata mshangao.