Home Makala ATCL wamefufuka, wengine wanatikisika

ATCL wamefufuka, wengine wanatikisika

615
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

NYOTA njema huonekana asubuhi, hivi ndivyo tunavyoweza kusema baada ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) kuanza kuonesha dalili za kuamka kutoka katika usingizi uliosababisha Taifa letu kukumbwa na fedheha ya kutokuwa na ndege hata moja iliyoweza kuruka.

Ilikuwa ni aibu kwa Tanzania, nchi iliyojaliwa rasilimali za kutosha zenye kuvutia watalii na watu wengine dunia. Lakini katika kipindi cha miaka mingi shirika letu la ndege lilikuwa mithili ya mgonjwa asiyetaka tiba. Shirika hili linaelezwa kuwa lilitafunwa na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Hali hii ilisababisha nchi kama za Kenya, Rwanda, Zimbabwe, Afrika Kusini na Ethiopia kupiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta ya usafiri wa anga.

Ikumbukwe kuwa Shirika hili la ndege (ATCL) lililoanzishwa Machi, 1977, baada ya kuvunjika kwa lililokuwa Shirika la Usafiri wa Anga la Afrika ya Mashariki (East African Airways) kwa kipindi kirefu lilidorora na kutokuleta matumaini yoyote kama ilivyotarajiwa.

Katika miaka ile ya 1980, shirika hili lilikuwa katika kipindi kizuri na cha kusifiwa na kutegemewa; likiendesha safari kadhaa za kimataifa kama vile kutoka Dar es Salaam kwenda Athens (Ugiriki), London (Uingereza), Bujumbura (Burundi), Kigali (Rwanda), Maputo (Msumbiji), Cairo (Misri) na kwingineko.

Pia safari za ndani zilikuwa si haba. Kulikuwa na safari za kutoka Dar es Salaam kwenda Iringa, Dodoma, Mwanza, Zanzibar, Lindi, Mafia, Masasi, Mbeya, Njombe, Nachingwea, Songea, Pemba, Tabora na Mafia.

Shirika hili lilipita katika mapito mbalimbali ikiwamo ubinafsishaji, na kuingia katika soko huria lililoambatana na ushindani mkubwa pia kutoka katika mashirika mengine ya kimataifa.

Pamoja na juhudi mbalimbali za kuikwamua ATCL, ni wazi kuwa  watendaji wa serikali walishindwa kuzuia ubadhirifu katika shirika hilo ambao pia katika kaguzi kadhaa za Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), ulibainishwa.

Kwa mfano katika ripoti hiyo ya CAG mwaka huu ilibainisha wazi kuwa menejimenti ya Shirika hilo haikuwa na mipango madhubuti ya kulifufua shirika hilo licha ya serikali kuweka mipango kadhaa ya kulifufua.

Ujio wa Bombadier

Pamoja na mapito hayo ni wazi kuwa Rais John Magufuli ametimiza moja ya ahadi zake. Ameitendea haki ahadi ya kulifufua shirika hilo kwa kufanikisha kununua ndege mbili kutoka kampuni ya Kampuni ya Bombadier Inc ya nchini Canada.

Ndege hizo zenye uwezo wa kubeba abiri 70 zinatarajiwa kufanya safari za ndani na nje ya nchi hususani katika Visiwa vya Comoro.

Aidha, Magufuli katika hotuba yake pindi alipokuwa akizindua ndege hizo alibainisha wazi kuwa katika awamu yake amedhamiria kuongeza ndege nyingine kubwa mbili zitakazokuwa na uwezo wa kubeba abiri kuanzia 160 hadi 240.

Ujio wa ndege hizo utaimarisha huduma za usafiri wa anga na kuongeza ushindani katika utoaji wa huduma za anga hapa nchini kati yake na kampuni binafsi za ndege zinazotoa huduma hiyo kwa sasa.

Pamoja na kuimarisha huduma za usafiri lakini pia Taifa letu litafanikiwa kuongeza mapato katika sekta ya usafiri na utalii kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa jirani zetu Wakenya, shirika lao la Kenya airways lililoanzishwa kipindi kile kile cha mwaka 1977 (baada ya kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika Mashariki) limepiga hatua kubwa na kuwa lango la kuingiza watalii nchini mwao huku wale wanaosalia ndio wanaokuja Tanzania.

Licha ya baadhi ya watalii kulenga kuja Tanzania, wamekuwa wakisalia Kenya na kuja kutembelea Tanzania hali inayodhihirisha namna Taifa letu lilivyokuwa limeshindwa kutumia fursa zilizopo.

Hivi sasa jirani zetu wengine, Rwanda, shirika lao linakua kwa kasi kubwa; hivi karibuni limeweza kuanzisha na kupata wateja wa safari za Afrika Kusini kwenda Dar es Salaam, kwa kupitia Kigali (Rwanda) na Kilimanjaro (Tanzania). Katika hili, shirika hili linatumia ‘mbinu ya biashara’ kwamba linapeleka watu Kilimajaro! Na hivyo utajiri wetu (Mlima Kilimanjaro) unaendelea kuwanufaisha wengine.

Changamoto mpya kwa ATCL

Ni dhahiri kuwa menejimenti mpya ya ATCL inazo changamoto kubwa kadhaa, kwanza ya kuhakikisha Shirika hilo linafufuka na kuwapa matumaini Watanzania kama Rais Magufuli alivyodhamiria lakini pili kuendana na ushindani uliopo sasa katika sekta ya usafiri wa anga hasa ikizingatiwa zipo kampuni mbalimbali kutoka nje ya nchi ambazo zinatoa huduma hiyo kama vile Fastjet na Precision Air.

Baadhi ya kampuni hizo ikiwamo Fastjet zimeanza kulalamika mdororo katika sekta hiyo na kuanza kupunguza wafanyakazi, hii ni mojawapo ya changamoto ambayo ATCL inakabiliwa nayo licha ya kutakiwa kupunguza wafanyakazi pia shirika hili limefufuka katika kipindi ambacho mashirika mengine nchini yako taabani.

Lakini pia changamoto nyingine ni kutekeleza agizo la Rais Magufuli kuwa hataki kusikia suala la mawakala katika kukatisha tiketi. Hili ni jambo ambalo linaelekea kuleta ugumu kwa shirika hili katika kurudi mfumo sahihi wa soko hasa ikizingatiwa katika zama hizi mawakala hawakwepeki pindi shirika linapohitaji kuboresha huduma zake.

Hii inatokana na ukweli kuwa hiki si kile kipindi cha kupanga foleni kusubiri tiketi, ndio maana baadhi ya wanazuoni akiwamo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uchumi anashauri kuwa kuwakwepa mawakala kutaongeza gharama za uendeshaji.

Profesa Ngowi anabainisha kuwa watu wananunua tiketi wakiwa nyumbani kutoka katika mashirika mengi duniani kupitia mawakala kwa mantiki hiyo kuondoa huduma hiyo kutachangia kupunguza wateja kwa sababu hakuna atakayekubali kupoteza muda wa kupanga foleni ya kukata tiketi wakati anaweza kununua popte alipo.

Hoja hiyo ya Profesa Ngowi pia inaungwa mkono Mchambuzi wa masuala ya usafiri, Erick Tendega ambaye anabainisha kuwa kwa sasa ATCL haipaswi kuwaondoa mawakala katika uendeshaji.

Kwa maana hiyo ni dhahiri kuwa ATCL inatakiwa kutafuta mawakala kutoka kila pembe ya dunia ili ipate wateja wengi, kuondoa usumbufu wa kupanga foleni kukata tiketi na kupunguza gharama ya kuajiri wafanyakazi wengi ambao mzigo wa kuwalipa utarudi kwa wananchi.

Lakini pia katika kupunguza gharama za uendeshaji ambao huongeza mzigo kwa mlaji, inapaswa wawepo wafanyakazi wachache na watalaamu wa ndege na biashara ambao watakuwa na majibu ya soko linachotaka.

ATCL inarudi wakati waliopo kwenye soko ni wazoefu, wana utalaamu wa muda mrefu, hivyo ni vema sasa ATCL kuangalia changamoto zilizopo sokoni na kuzifanyia kazi kabla ya kuingia kazini.